NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, October 27, 2010

“KAKA, TUNAOMBA NA SIE UTUMULIKIE…”

 • Hii ilikuwa sauti ya vitoto viwili vya kike (miaka 6–9) majira ya saa 2 usiku kule Mbagala Kongowe Mzinga mwezi wa sita mwaka huu.
 • Nilikuwa naelekea barabarani kununua vibua (aina ya samaki) wa kukaanga. Kwa vile kulikuwa na giza totoro, nilikuwa natumia kurunzi kujimulikia njia zile za vichochoro.
 • Nilipoviuliza vitoto vile vilikokuwa vikienda, vilinijibu kwamba vilikuwa vimetumwa kwenda kununua samaki wa kukaanga pale barabarani. Basi tulimulikiana njia mpaka tukafika barabarani. Kwa vile kulikuwa na maduka pia, nilivinunulia tochi moja ya sh. 3,500, nikaviwekea na betri kabisa kabla ya  kuachana navyo. “Asante sana kaka. Asante sana!” Vitoto vile vilinishukuru kisha nikaagana navyo.
 • Nimelikumbuka jambo hili kwa sababu ni mojawapo ya mambo machache ambayo bado yanaonyesha na kuakisi kwa usahihi Uafrika wetu. Kwa hapa Marekani na hasa sehemu za mijini ni nadra sana kuona mtoto (wa jinsia yo yote ile) akitembea peke yake iwe mchana au usiku.
 • Ipo majitu hapa yenye ulafi wa fisi ambayo ipo tayari kuvikamata vitoto visivyo na hatia (bila kujali jinsia) na kisha kuvibaka, kuvilawiti na hatimaye kuviua. Kwa hali hiyo hapa huwezi kuona watoto wakienda shuleni au kutembeatembea peke yao bila kusindikizwa na wazazi.
 • Hali ni mbaya kiasi kwamba majimbo mengi yamepitisha sheria zinazoyataka majitu haya kujiandikisha ili wazazi (na jamii kwa ujumla ) wajue yanakokaa na ikibidi waweze kuchukua tahadhari.
 • Katika jimbo la Florida, kwa mfano, unaweza kuweka anuani yako katika tovuti hii, kisha unabofya ili kuona kama unaishi karibu na majitu haya yenye kunajisi, kulawiti na hatimaye kuua vitoto visivyo na hatia.
 • Jana, kwa mfano, nilishtuka nilipoweka anuani yangu, nikabofya na kukuta kwamba kuna majitu haya hatari 12 katika eneo la maili 5 kutoka hapa ninapoishi. Kati ya haya 12, mawili yana cheo cha “sexual predator”, cheo ambacho ni hatari zaidi.
 • Pamoja na utandawazi unaotuandama, natumaini kwamba hatutakaa tufikie hatua hii ya kusikitisha. Ndiyo maana inabidi tupambane na majitu yanayoua maalbino na kubaka vitoto kwa imani za kishirikina (na zinginezo) kwa nguvu zote kabla mambo hayajatuharibikia zaidi.
 • Na kwa sisi tunaobeba maboksi huku nje, ile kuona tu watoto wakienda shule peke yao kule nyumbani ni jambo la kufurahisha sana. Ndiyo maana bado navikumbuka vitoto vile vichangamfu usiku ule kule “Uswahilini” Mbagala Kongowe Mzinga!

3 comments:

 1. Ahsante sana mkuu kwa kisa hiki na wema wako kwa watoto hawo, watukushukuru sana hadi ukubwani mwao.
  Ni kweli kama tutawalea watoto wetu na kuwalinda ni faida kwa taifa la kesho, ni faida kwa maisha yetu na usalama wetu, lakini kama tutawatelekeza na kuwaachia hawo watu waliolaaniwa, taifa litaharabika na vizazi vijavyo vitatulaumu!

  ReplyDelete
 2. Kusema ukweli umenifungua sana macho. Nilikuwa nafikiri wazazi wa wenzetu wanawapenda sana watoto wao, kwani nilikuwa naona kila mtoto anasindikizwa na mtu mzima, kumbeeee....
  Kwa kujitangaza kwa hiyo mijitu, je, tabia zao inaacha??
  Kuhusu suala la albino, Mizengo Pinda alisema kwa jazba, kuwa kama wao wanaua, kwa nini na wao wasiuwawe... lakini weeeeeeee, watu walipiga kelele, mpaka akaomba radhi bungeni.

  ReplyDelete
 3. @ Emu-three: Ni kweli. Mustakabali wa jamii yetu unategemea malezi na elimu tunayowapa watoto wetu. Ni wajibu mkubwa mno kuleta kiumbe cha Mungu hapa duniani na kisha kukipa malezi mema.

  Chib: Upendo pia upo sana hapa lakini pia kuna hiyo hofu ya haya majitu. Ukizubaa tu basi mtoto wako ananyakuliwa na ataokotwa baadaye akiwa ameuawa.

  Majitu haya inabidi yajitangaze ili yajulikane. Pia huwa hayaruhusiwi kusogelea sehemu zenye misongamano ya watoto kama vile shule, viwanja vya michezo na sehemu za kupumzikia. Yale yenye cheo cha Predator, hutakiwa kuvaa kifaa maalumu chenye GPS ambacho huwawezesha polisi kujua yaliko kwa masaa yote.

  Wanasaikolojia wanasema kwamba majitu haya ni magonjwa na kujitangaza namna hii ni hatua ya tahadhari tu na haisaidii cho chote katika kuyabadili tabia.

  Kizungumkuti kinakuja pale unapogundua kwamba jirani yako ni mmojawapo wa majitu haya na huku una vitoto vidogo. Sijui itabidi uhame au ufanyeje. Shida tupu unaambiwa.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU