NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, October 20, 2010

"VIONGOZI" WALIOLEWA MADARAKA KAMA HUYU HUWA WANANIKERA !!!

 • Tarehe 13/6/2010 nilisafiri kutoka Dar es salaam kwenda Arusha na ndege ya Precision. Mbele yangu kulikuwa na mwanamke mmoja ambaye nadhani ni "kiongozi" mwenye cheo kikubwa serikalini au katika chama kimojawapo cha kisiasa.
 • Karibu safari nzima "kiongozi" huyu alikuwa akiongea kwa sauti kubwa na abiria mwenzake waliyekuwa wamekaa naye karibu. Akiwa ametawala maongezi yale, "kiongozi" huyu alikuwa anaelezea hasa juu ya safari zake za mara kwa mara kwa kutumia usafiri wa ndege. "Wiki jana nilikuwa Zanzibar kikazi, mwezi uliopita nilitumwa Nairobi halafu nikaenda Norway. Norway sikupenda baridi na hoteli waliyoniweka sikuipenda. Wiki kesho nitakuwa Rwanda halafu nitarudi Kigoma kikazi..." alikuwa akitamba kiongozi huyu kwa sauti kubwa kabisa na bila aibu yo yote.
 • Japo safari ya kutoka Dar es salaam kwenda Arusha inachukua chini ya saa moja, "kiongozi" huyu alianza kulalamika kwa sauti kwamba alikuwa amechoshwa na safari ile na alikuwa anasubiri kwa hamu kubwa ndege itue ili akapumzike japo kidogo katika chumba cha VIP katika uwanja wa ndege wa Arusha
 • Tabia hii ilinikera na sikutaka hata kuulizia alikuwa na cheo gani japo baadaye niliambiwa kwamba alikuwa ni mbunge mwenye cheo kikubwa katika kamati mojawapo muhimu. Mimi niliitafsiri tabia hii kama dalili za ubinafsi, ulimbukeni tu na kulewa madaraka. Pengine mimi ndiyo nina makosa lakini nina wasiwasi na kiongozi mwenye tabia kama hii.  
 • Pengine wanasaikolojia na watu wa utambuzi wanaweza kutoa maelezo ya kitaalamu kuhusu watu wenye tabia za aina hii. Na pengine si vibaya kujidai kwa mafanikio ambayo mtu umeyafikia. 

   7 comments:

   1. Kama ni mbunge basi ni mwanasiasa na kama ni mwanasiasa kuongea ni hulka yao. Na muongeaji sana ana aina ya `kupenda kusikilizwa'.
    Hilo tunaliona hata kwenye madaladala, watu wengine wanaongea kiasi kwamba inakuwa kero...kuna wataalamu wa kuanzisha mada. Kwa tunaosafiri kutoka Msasani hadi Gongolambotoo tunawajua hawa jamaa. Wakati mwingine inasaidia kupoteza mawazo, kwasababu safari hii ya kutoka Msasani hadi Gongolamboto inazidi ya kutoka Dar hadi Morogoro!
    Ukiwawapata hawa waongeaji ndani ya daladala kama ulikuwa na yako kichwani yanaweza kuyeyuka,...ni hulka na tabia ya waongeai, na watu kama hawo `uongo, na ubinafsi haukwepeki ndani ya nafsi zao'

    ReplyDelete
   2. Nanukuu``Mimi niliitafsiri tabia hii kama dalili za ubinafsi, ulimbukeni tu na kulewa madaraka.´´´-mwisho wa nukuu.

    Hapo umemaliza kabisa nilichofikiria baada ya kukusoma!

    ReplyDelete
   3. Jamani si kosa lake bali ni katika jitihada zake za kujipatia umaarufu kwa bei rahisi.

    ReplyDelete
   4. Alichokuwa anakitaka kumbe alikipata, ANGEKUWA KIMYA USINGEMJUA KAMA NI MBUNGE NA ANASAFIRI NCHI NYINGI. Inakera sana. Ungemuomba ahamie kiti cha karibu na shoga yake, UNGEKUWA UMEMPA ADHABU KUBWA.

    ReplyDelete
   5. Mmmesahau kuwa usupa staa wa Bongo ni dili? Jamii yetu kutokana na kuwa nyuma kiustaarabu imejenga tabia ya kuabudia umaarufu njiwa.

    Hamjawaona masupa staa uchwara mitaani wakiwaghasi wenzao kisa kaonekana kwenye video?
    Tatizo la mwenzetu huyu nadhani ni kutojiamini na ulimbukeni wa kawaida ambayo yaweza kuwa hulka ya mtu binafsi.

    Jamii yetu inapenda sifa na utukufu kiasi cha kujiruhusu haa kuridhia watu kughushi shahada au kutumia shahada za heshima kama za kuhenyea.

    Tatizo jingine laweza kuwa malezi. Maana kwa mtu aliyelelewa vilivyo, maisha yake si gazeti wala mkutano wa hadhara.

    ReplyDelete

   JIANDIKISHE HAPA

   Enter your email address:

   Delivered by FeedBurner

   VITAMBULISHO VYETU