NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, October 7, 2010

WACHINA WATATUMALIZA: HII "REMOTE CONTROL" KIDOGO IUNGUZE CHUMBA.

 • Nilikutana na hii "remote control" ya kiyoyozi katika hoteli moja jijini Dar es salaam mwezi wa sita mwaka huu.
 • Kwa vile maelekezo yote yalikuwa katika Kichina basi ilinitoa ushamba (kumbuka mimi ni Msukuma!). Nilikuwa nimetoka kunyosha miguu nje na kulikuwa na joto ile mbaya; na nilihitaji sana hewa ya baridi.
 • Basi nilianza kubonyeza mishale ambayo nilidhani kwamba ilikuwa inaonyesha jinsi ya kuongeza au kupunguza joto lakini sikufanikiwa kuipata hewa ya baridi. Niliendelea kubonyeza bonyeza mpaka kiyoyozi kikaanza kutoa sauti za mkoromo na baadaye nikaona cheche zinaanza kutoka. 
 • Basi ilibidi nitoke nje kwenda kuwatafuta wahudumu. Bahati mbaya mhudumu niliyempata naye naona Kichina kinampiga chenga kwani alianza kubonyeza bonyeza hovyo tu kama mimi. Yeye nadhani badala ya kuweka hewa ya baridi basi aliweka joto kwani chumba kilipata moto vibaya sana.
 • Baadaye mhudumu mwenye "utaalamu" zaidi alikuja na kukizima kiyoyozi kile kwa kuchomoa kabisa waya uliokuwa umekiunganisha na umeme ukutani. Kesho yake nilipatiwa maelekezo kwa Kiswahili jinsi ya kutumia "remote control" ile kwani niliwaambia kwamba hata kimombo kwangu kilikuwa hakipandi. Bahati mbaya nimeyapoteza maelekezo ya Kiswahili vinginevyo ningeyaweka hapa.
 • Ni haki kweli kuweka mitambo ya viyoyozi vya kisasa katika hoteli kama ile yenye hadhi katika lugha ambayo naamini Watanzania (na hata watalii) wengi hawaifahamu?
 • Kama mambo ndiyo haya, pengine Mheshimiwa Lowassa alikuwa "sahihi" alipopendekeza mwaka 2007 kwamba Kichina kianze kufundishwa katika mashule yote ya Tanzania (japo Kiingereza kimeshatushinda!)

4 comments:

 1. Kesho tutaagiza bidhaa toka Ujerumani nazo zimeandikwa kijerumani, wakatyi huo tumeamua kujifunza Kichina, yatakuwa yaleyale...labda kwa wenye mahoteli hayo waatafute watu wakutafsri kwa kiswahili, au watu wakiagiza wapitishie kwa TBS, au Baraza la kiswahili wapewe tafsiri sahihi.
  Ni vyema kuifunza lugha za kimataifa, lakini je Watanzania wote tutaweza? Na je tujifunze lugha gani, kwa vile sisi huku ni dampo, au soko la kuuziwa bidhaa za wenzetu?

  ReplyDelete
 2. emu-three, kesho tukeshamaliza kuagiza za Ujerumani, keshokutwa tunaagiza za Iran na Uturuki... mwe!

  ReplyDelete
 3. Tatizo hapa si kiyoyozi bali mafisi wetu waliopewa jukumu la kuidhinisha ni bidhaa gani ziingizwe nchini. Sisi si dampo tu bali nchi ya vichaa inayoweza kulisha kila uchafu na ikatembea kifua mbele.

  Hivi unategemea nini toka kwenye nchi ambayo uchumi wake unaendeshwa na mafisi kama Jeetu Patel, Rostam Aziz na mbweha wengine wa kiuchumi waliotamalaki wakiwatumia watawala wetu kama vyangudoa kwa mshiko wa pipi?

  Hata hiyo nyumba isingeunguzwa na remote control, kesho itadondoka yenyewe kama ni ghorofa kutokana na watu kujijengea baada ya kuwahonga vyangudoa wa city.

  ReplyDelete
 4. Haya watu wa kukagua bidhaa wako wapi kifaa kimeandikwa kichina hamna mtu anajua hiyo lugha hata mwenye hoteli sidhani anazungumza hiyo lugha.Haya mambo ya aibu tupu unafikiri ukipeleka biashara yako imeandikwa kiswahili katika ulimwengu huu bila tafsiri hamna hata mtu mmoja ataiangalia bidhaa yako.Lazima nchi yetu ijifunze kutokana na mifano inayotokea sehemu mbali mbali za dunia hawa wachina wanauza bidhaa ambazo sina mchanganyiko wa madawa ya kudhuru afya ya binadamu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU