NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, November 29, 2010

ATI, KWA NINI SHULE IFUNGULIWE KABLA HAIJAKAMILIKA? NI KUWAKOMOA WANAFUNZI, WAZAZI AU JAMII???

 
Mashujaa wa Kidato cha Sita - HGK Sengerema High School.
Hapa kuna maprofesa, maofisa wa jeshi na polisi, watawala, waalimu, wakaguzi wa fedha, wanasheria, wahasibu, watangazaji, wabunge n.k
***************
 • Ni nani anayeruhusu shule ya Sekondari ifunguliwe huku akijua kuwa bado haijakamilika? Utatoaje ruhusa shule ifunguliwe wakati unajua kabisa kwamba haina waalimu (wa kutosha), haina vitabu, haina maabara, haina vifaa vya michezo, haina vyoo, haina mesi, haina nyumba wala ofisi za waalimu na mambo mengine ya msingi?
 • Ni kweli mtoa ruhusa huyu angetoa ruhusa hii kama angejua kwamba watoto wake au ndugu zake wa karibu wangeenda kusoma katika shule ya aina hii? Au anafanya hivi kwa kutojali kwa sababu anajua kwamba watoto watakaosoma katika shule hii ni watoto wa wakulima na hawana la kufanya, na hivyo ni bora elimu badala ya elimu bora?
 • Hivi ndivyo ilivyotokea kwetu tulipopelekwa na kubwagwa Sengerema High School kusomea "combination" mpya ya HGK iliyokuwa imeanzishwa pale. Pamoja nasi walikuweko wenzetu wa PCB na PCM. Hawa wenzetu walichachamaa mpaka mtoa ruhusa akaamua kuwahamishia Shule za Sekondari za Shinyanga (Shy Bush) na Tosamaganga. Hata sisi watu wa HGK, wengi waliokuwa na uwezo na uamuzi wa kuhamia shule nzuri kama vile Mzumbe, Musoma Alliance na Tabora Boys walifanya hivyo. Tuliobakia pale ni "vichwa ngumu" na kusema kweli tulisoma kwa kutegemea"madesa" kutoka shule zingine. Na mtihani wa kidato cha sita ulipofika hivyo hivyo tulijikongoja na wachache wetu tuliweza hata kupata hiyo inayoitwa "divisheni wani"
 • Inashangaza sana kuona jinsi uzembe na kutojali kwa hawa wamiliki wa mfumo unavyoweza kuathiri na kudunisha maisha ya watu. Ati, ingekuwaje kama nasi tungepelekwa katika shule yenye walimu na vitabu vya kutosha nasi tukasoma na kufundishwa kama wenzetu wa Mzumbe, Musoma Alliance na Tabora Boys? Ni wangapi kati yetu ambao tulishindwa mitihani ya kidato cha sita kutokana na ukosefu wa waalimu na vitabu? Kuna hata anayejali? Kuna hata ambaye nafsi yake inamsuta kwamba pengine aliharibu maisha ya watu kwa kuwapeleka katika shule ambayo ilikuwa haijakamilika?
 • Inashangaza na kusikitisha sana kuona watu wanavyocheza na maisha ya watu namna hii. Na mchezo huu ndiyo sasa umeshika kasi katika haya "majengo ya kata" (a.k.a. shule za kata) yaliyotapakaa nchi nzima. Mengi yana upungufu mkubwa wa waalimu, hakuna vitabu wala maabara, hakuna nyumba wala ofisi za walimu, hakuna vyoo, hakuna mesi, hakuna...na bado majengo haya yanarundikiwa wanafunzi mamia kwa mamia kila mwaka. Kwa mtindo huu jamani, tunaanda taifa la aina gani? Unakuta shule ina wanafunzi 300 lakini walimu watatu au wanne. Kweli kuna elimu inayoendelea hapo? Halafu watoto hawa wakipata divisheni ziro tunawalaumu kwamba ni mbumbumbu na kwamba hawajui umuhimu wa elimu. Halafu nasi, kama vile wenye chongo mbele ya vipofu, tunasimama majukwaani na kujipiga kifua kwamba tumeboresha sekta ya elimu kwa kuongeza idadi ya mashule ya sekondari na idadi ya wanafunzi. Na vipofu wetu, pengine kwa kuona maluweluwe hafifu wanatushangilia. Kweli?
 • Ukweli unabakia pale pale kwamba bila elimu bora na kombozi hatutakaa tuendelee kwani Historia ndivyo inavyotuambia. Sijui ni kitu gani kinachotufanya sisi tufikirie kwamba tunaweza kuwa kighairi (exception) katika kanuni hii ya jumla. Inashangaza sana!

2 comments:

 1. Elimi bora kwa watotoo wao na bora elimu kwa watoto wa wenzao! Twaiona hii,

  ReplyDelete
 2. Who cares? Watoto wao wanasoma Uingereza na Marekani na wakirudi ajira zinawasubiri. Nyie hata mkifika varsity, ajira ziko wapi wakati elimu yenyewe ni ya vitabuni tu and doesn't prepare you to face the world.

  Majengo ya kata...I like that!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU