NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, November 10, 2010

HONGERENI WANABLOGU KWA KAZI NZURI MLIYOIFANYA WAKATI WA UCHAGUZI !!!

 • Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa tofauti sana na chaguzi zilizotangulia. Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia umma wa Watanzania ukiamka kutoka katika usingizi wa pono wa miaka mingi na kuanza kuhoji mambo. Mbali na mambo mengine, umma huu sasa unahoji ni kwa nini ungali ukiishi katika lindi la umasikini wa kutisha wakati nchi imejaliwa raslimali za kutosha? Raslimali hizi zinamnufaisha nani? Umma huu nao sasa unataka kuionja keki ya taifa!
 • Kutokana na msisimko huu tumeshuhudia majina makubwa (na kongwe) katika medani ya siasa na uongozi yakitupwa nje katika kura za maoni na hata katika uchaguzi wenyewe. Na hili ni jambo jema katika deokrasia yetu changa kwani, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, nchi yetu ilishaachana na mambo ya usultani na watu wachache kuhodhi madaraka miaka nenda miaka rudi si kitu cha kujivunia!
Ni nini kilicholeta mabadiliko haya?
 • Mbali na mambo mengine, naamini kwamba vyombo vya habari vimechangia sana katika kuwaamsha wananchi. Mambo ambayo zamani yalikuwa yakiogopwa kusailiwa sasa yanajadiliwa waziwazi. Na blogu zenu hizi zimekuwa mstari wa mbele katika harakati hizi kwa kuwahabarisha wapiga kura na kutetea ukweli bila kujali kama ukweli huo unawaudhi au unawafurahisha baadhi ya watu. Wakiwa wamejificha katika kunguku la u-anonymous, wadau wengi wa blogu hizi wamekuwa wakitoa mawazo yao ya ndani kabisa bila woga wo wote.
 • Hata wakati wa kupiga kura na wakati wa kusubiri matokeo, blogu nyingi zilikuwa mstari wa mbele kuripoti kilichokuwa kinaendelea ikiwemo kurusha matokeo kutoka vituoni laivu. Naamini kwamba hili limesaidia katika kupunguza visa visivyothibitishwa vya "uchakachuaji" wa kura.
 • Bila kutaja majina, napenda kuchukua nafasi hii kuwahongeresha wanablogu wote - hata wale "waliotuhumiwa" kuegemea upande mmoja na kupuuza upande wa pili. Nyote mmetoa mchango mkubwa sana katika kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Na uzuri ni kwamba kila kitu kimefanyika kwa amani na utulivu ukiachilia mbali visa vya fujo za hapa na pale.
 • Natumaini kwamba uchaguzi wa mwaka 2015 utakapofika Inshallah blogu zenu zitakuwa zimejiimarisha zaidi na zitatoa mchango wa uhakika zaidi. Hebu basi msichoke na kuliacha pigano. Kazi yenu wanablogu si bure katika kujenga "Civil Society" imara nchini Tanzania. Hongereni sana!

4 comments:

 1. Kweli blogs sasa hivi ni sehemu muhimu katika jamii, kwani ni sehemu amabyo mtu unaweza kuandika maoni yako, ushauri nk. Na hasa katika uchaguzi wengi walielezea kile cha muhimu.
  Tatizo kama nchi yetu hii, vitu kama internet bado ni kwa wachache, na hasa waliopo maofisini!
  TUHONGERENI SOTE!

  ReplyDelete
 2. Labda nianze kukuhongeresha wewe ambaye umefanya mengi magumu, muhimu lakini yasiyoonekana.
  Kupanga blogu hapa pembeni kwa kulingana na UHITAJI wa wasomaji ni jambo gumu saana na lahitaji umakini. Huwezi kuzipanga kama huzijui na huwezi kuzijua kama huzisomi.
  HONGERA KWA KUZISOMA
  Kisha hongera kwa kujichanganya nasi kina nanilii. Kwa muelimika ambaye anajua kuwa hatahitimu (kama ulivyosema hapo pembeni kuwa "THE TRULY EDUCATED NEVER GRADUATE", basi nasi tunaosaka ku-graduate tunashukuru kuwa u-nasi
  Mwisho ni kwa makala na fikirisho zako motomoto ambazo ni CHANGAMOTO kwa wengi juu ya uandishi "mfupi" lakini utufaao.
  Kuhusu uchaguzi, hapa nina tafsiri tofauti kidogo. Ni kweli tumeonesha kile tulichokuwa tunaweza kunasa lakini ni wachache saana walioweza kutoa tafsiri ama tathmini halisi ya kilichokuwa kikitokea.
  Hakuna walioweza kubainisha kinachoendelea na kilichostahili kuendeleaili kuleta maendeleo na mabadiliko halisi. Niliandika mapema mwaka huu kuhusu YATAKAYOWAANGUSHA WAPINZANI (http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/02/yatakachowaangusha-wapinzani-kwenye.html) na japo nilionekana "kudamka" katika hili, leo hii naamini wengi wakirejea makala wataona nilichozungumza. Lakini ukweli unabaki kuwa uleule kwamba KAZI YA KUONESHA ILIFANIKIWA, SASA TUHAMIE KWENYE KUELIMISHA.
  Nilikerwa na PICHA zisizo na maandishi wala maelezo ya kuridhisha na kutosha. Wakiandika kuwa fulani amekusanya watu wengi ilhali tulikuwa tukiona kuwa wapo wengi. Lakini nisiifanye mada hapa kwani nilishaiandika hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/10/nani-anayetafsiri-hizi-taswira-sawasawa.html

  ReplyDelete
 3. Asanteni nyote.

  @emu-three: Japo ni watu wachache ambao wanaweza kusoma hizi blogs, hata hao wachache wanaozisoma wanatosha. Ni mwanzo mzuri!

  @ Yasinta: Kweli Da Yasinta. Sisi sote ni ndugu.

  @ Mzee wa Changamoto: Angalizo zuri na asante sana kwa shukrani zako. Eti unanishukuru kwa kujichanganya nanyi. Hapa hata sielewi unasema nini? Mimi si mmoja wa wale wanaodhani kwamba kwa vile wamepata Ph.D katika kauwanja kao kadogo walikosomea basi wanajua kila kitu. Katika hali ya kawaida watu hawa wanaweza kugeuka na kuwa "majuha" kabisa, wakalewa "usomi" wao na kujiona wako juu ya kila kitu. Tazama hapa kupata fununu zaidi (http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2724)

  Kipindi cha uchaguzi ni kipindi cha jazba sana na ushabiki wa kisiasa unaweza kugubika maamuzi ya watu hata wale tunaowaamini na kuwategemea. Mbali na kwamba baadhi ya blogu ziliingia katika mkumbo wa kupiga kampeni (hili halipaswi kuwa jambo la kushangaza), bado naamini kwamba mchango zilioutoa ni mkubwa. Matukio mengi katika kampeni yalikuwa yanaripotiwa mara moja - yakiwemo matokeo ya uchaguzi. Huu ni mwanzo mzuri na natumaini kwamba tutaona mabadiliko makubwa katika uchaguzi ujao.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU