NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, November 27, 2010

MIJIBABA LAIVU IKILANA DENDA HADHARANI. KAZI NI KUWAELEWESHA WATOTO !!!

 • Sina tatizo na tabia na mapendeleo ya kingono ya mtu ye yote na ninaamini kwamba kila mtu anao uhuru wa kuserebuka kivyake kama anavyoona inafaa. Pamoja na ukweli huu ni lazima nikiri kwamba huwa napatwa na ukakasi fulani hivi ninapoona mijibaba ikikukurushana kimahaba mchana kweupe. Pengine hii inatokana na ukweli kwamba hii si tabia yetu Waafrika ambako mambo ya kimahaba (hata kati ya mwanamke na mwanaume) yalitendeka kwa siri sana kiasi kwamba katika makabila mengi (mf. Wasukuma) hata wapenzi kushikana mikono tu hadharani ilitosha kuwashangaza watu.
 • Alhamisi ya wiki hii nikawa nimepeleka watoto Mc Donald. Ile tunatoka tu na kukata kona kuingia barabara kuu chini ya mti mkubwa karibu na supamaketi moja hivi, kukawa na mijibaba miwili yenye miili iliyokakawana kwa ushupavu ikiwa inatembea huku imeshikana mikono. Nilijaribu kuongeza mwendo kidogo ili watoto wasione lakini nikawa nimechelewa. Binti wa kati (miaka 7) ndiye alikuwa wa kwanza kupiga makelele "Dad, look, look. Those men are kissing". Nilipogeuza kichwa kweli jibaba moja lilikuwa limegeuka na kusimama tisti mbele ya jenzake na nyuso zao zilikuwa zimeshonana. Baadaye nilisikia magari yaliyokuwa nyuma yakipiga honi fulani hivi pengine kuunga mkono (au kupinga) kitendo cha mijibaba ile.
 • Pengine hiki si kisa cha kushangaza kwani kwa wenzetu hawa mambo haya ni ya kawaida. Tatizo ni ugumu na kigugumizi nilichokipata kujibu mvua ya maswali kutoka kwa mabinti hawa wachanga wasioelewa cho chote bado. Nilijaribu kuwaambia kwamba nitayajibu maswali yao yote tukifika nyumbani nikiamini kwamba tutakapofika nyumbani watakuwa wamesahau. Tena niliwaahidi kwamba tukifika nyumbani basi wanaweza kucheza michezo yao ya video waipendayo. 
 • Pamoja na juhudi zote hizi, tulipofika nyumbani tu kitu cha kwanza walichokifanya ni kumsimulia mama yao kisa kile na hapo tena mvua ya maswali ikaanza kunyesha upya. Tulijaribu kuyajibu maswali yao "kistaarabu" kwa kadri tulivyoweza. Tuliwaambia kwamba ile mijibaba ilikuwa hai"mushi mushi" kama walivyodhani lakini pengine ilikuwa inacheza mchezo fulani hivi wa kivita, mchezo ambao unawataka washiriki wake kusogeleana kabisa huku wakiwa ana kwa ana. Yule mdogo (miaka mitano) alionekana kuridhika lakini yule mkubwa (miaka 7) alikuwa na mashaka na maelezo haya ingawa naye mwishoni alikubali - japo kwa shingo upande.
 • Ati, ungekuwa ni wewe ungewapa maelezo gani watoto wa miaka saba na mitano kuhusu jambo hili. Ungewaambia ukweli au "ungewadanganya" kama tulivyofanya? Watu wa Saikolojia na utambuzi mnasemaje? 
  • Ni wazi kwamba mambo ya malezi hayana fomyula ati! Siku moja wataugundua ukweli na kama watakuwa hawajasau kuhusu kisa hiki si ajabu watatunyeshea tena mvua ya maswali kwa nini tuliwadanganya.

  No comments:

  Post a Comment

  JIANDIKISHE HAPA

  Enter your email address:

  Delivered by FeedBurner

  VITAMBULISHO VYETU