NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, November 2, 2010

NINI KIMEMWANGUSHA LAWRENCE MASHA NYAMAGANA?

 • Kuangushwa kwa Lawrence Masha ni mojwapo ya matokeo ambayo yamenishangaza sana. Mpaka wiki chache tu zilizopita mbunge huyu wa jimbo la Nyamagana (CCM) na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa hana mpinzani jimboni mwake. Halafu, tena kimchezo mchezo tu, mgombea wa CHADEMA akajitokeza kupambana na Mheshimiwa huyu aliyetukuka. Yaliyobaki ni historia!
 • Ni nini kimemwangusha kijana huyu machachari? Ni kushindwa kusoma alama za nyakati? Ni kujiamini kupita kiasi? Ni kulewa madaraka? Ni nini?
Ni wazi tatizo si kutonyanyuliwa mikono!

Msikilize hapa akifurahia "Kupita Bila Kupingwa!"


 • Siasa za Tanzania sasa zinaingia katika kipindi kipya. Heri asomaye alama za nyakati na kuzielewa! Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
 ******....****** 

NYONGEZA
 • Inasemekana eti Masha alipata mshtuko, akaanguka na kupoteza fahamu baada ya kubainika kwamba alikuwa amepigwa chini. Madaraka matamu ati! 

 • Kama habari hizi ni za kweli basi ni za kusikitisha sana na tunamtakia Mheshimiwa huyu uponaji wa haraka. Angali bado kijana na mchango wake kwa jamii yetu bado ni mkubwa. Isitoshe, si ajabu akapewa ukuu wa mkoa/wilaya au cheo kingine kizuri tu. Huu ni wakati wa kujipanga upya na kurudi kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi mwaka 2015. Kwa habari zaidi bofya hapa.

 • Mgombea mwingine aliyezirai baada ya kugundua kwamba amepigwa chini ni Mwita Mwikwabe wa Tarime (CHADEMA). Waheshimiwa wote hawa tunawatakia afya njema. Wakumbuke tu kwamba kuvunjika kwa koleo siyo mwisho wa uhunzi! Ila kama walikuwa wamekopa mamilioni ya kupigia kampeni wakitegemea kuyarudisha baada ya kuingia mjengoni Chimwaga ndiyo kasheshe sasa!
 Mwikwabe akiwa amezirai. Huduma ya kwanza vipi jamani?

18 comments:

 1. Prof., hii inanikumbusha neno katika kitabu kimoja cha maandiko matakatifu cha Wakristo "Ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke" ndiyo yale yale ya "Abiria chunga mzigo wako" aliimba Rose Mhando, "Mteule uwe macho" namalizia na "shika sana ulicho nacho asije mtu akakupokonya" (ipo huko huko maandikoni...).

  ReplyDelete
 2. Asante sana kwa yote mliyonifanyia wewe na mke wako mubarikiwe sana. Mke wako ni mwanamke mwema sana na mzuri sana. Umebarikiwa sana kuwa na mke kama mama Kija. Asante sana profesa. Haya mambo ya siasa jamani yanazidi kutushangaza.

  ReplyDelete
 3. Kuanguka kwa Masha ni ushindi dhidi ya kujuana na ufisadi wa kimfumo. Masha alipewa uwaziri wa mambo ya ndani bila hata uzoefu ukiachia mbali ukaribu wake na mtoto wa bosi. Amekuwa mbunge ambaye alidhani ukaribu wake na Ridhiwani ungeendelea kumweka kwenye utukufu asijue msingi wa utukufu wake ni ubunge utokanao na kura za wale aliowaona kama wadudu. Thank Lord Masha has been kicked out. Kuanguka kwa Masha hata Mogella, Mramba na vigogo wengine watakaoanguka ni somo kuwa wananchi si wapumbavu kama wanavyodhaniwa na wenye madaraka wasiojua kuwa si yao bali dhamana tu.

  ReplyDelete
 4. Mhhh, wananchi wanajua zaidi, na ukweli umedhihiri!
  'Hamjambo, nimkuja kuwaoana' halafu unaingia ndani ya shangingi lako, bomba, unaonekana baada ya mwaka, au zaidi...' utakumbukwa kweli!
  Nawaza tu, ila kweli huyu jamaa ni `kijana machachari' sijui kwanini kaanguka!

  ReplyDelete
 5. Kilichomwangusha ni imani ya watanzania waliyonayo kwa damu changa yenye uchungu na nchi yao na usongo wa maendeleo ya kweli. Ni vijana waliochoka kuona wanaishia kwenye kuvuta bangi na madawa ya kulevya huku hawajui watapata wapi tonge la ugali. Ni vijana waliochoka wimbo wa umaskini wakati tumekalia madini na raslimali za kumwaga. Ni vijana wasomi ambao hawaoni thamani yao

  ReplyDelete
 6. Kiukweli inashangaza sana! unajua matendo waliyoyafanya mwanza! Ni tembo alikutana na sisimizi akasema huyu sisimizi hafurukuti kwangu akataka kupita sisimizi akasema hupiti mara tembo kamwagwa na sisimizi. Hongera sana kaka WENJE

  ReplyDelete
 7. Hiyo video imenifurahisha. The boy looks arrogant! Dah, what a fall!!!

  ReplyDelete
 8. duhu sijui mimi wanajifanya wanajua sana kumbe waungua jua

  ReplyDelete
 9. ukisikiliza hio video kaulizwa swali kuwa umepita bila kupingwa ccm tu au na vyama vingine, jibu lake halikueleweka nafikiri alidhani ni wakati wa chama kimoja na kasema hakuwahi kufanya kazi serikalini kabla ya hapo ina maana alihisi hana uzoefu, wana mwanza mmefanya kufuru mlindwe kama mlivyoandamana kulinda kura, alipewaje uwaziri mtu alikuwa na kazi yake binafsi ya uhakika, halafu kina magufuli wakaambulia majina kuongezwa na wino, labda sasa mawaziri watapewa kazi kutokana na taaluma badala ya dakitari wabinadamu anapewa wizara ya ulinzi au mkemia anakuwa bwana samaki, egineer anapewa kilimo nk nk tubadilike

  ReplyDelete
 10. Matondo, hebu nami nifundishe jinsi ya kusoma alama za nyakati ili yasije yakanikumbuka yaliyomkumba huyu kijana wako unayemwita machachari kumbe ni zero. If you listen carefully kwenye hiyo video yake basi utaona ni kwa nini nchi hii hatuendelei. Hata hawezi kutaja angalau kitu kimoja ambacho amewafanyia watu wa Nyamagana. Badala yake anaeleza jinsi ambavyo hakua na experience lakini bado akaukwaa uwaziri tena wa wizara nyeti namna ile. At the end anachojali ni mategemeo yake ya kupata cheo kingine. Husikii anything to develop watu wa Nyamagana.

  Good Riddance watu wa Nyamagana. By the way akipewa Ukuu wa Mkoa au Wilaya tutaandamana tena. Hatutaki mchezo sasa. Nchi yetu sote hii jamani. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:

  "Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumedharauliwa kiasi cha kutosha...SASA BASI!!!"

  ReplyDelete
 11. aliyosema anony hapo juu ni haki, mtu hajui amefanya nini kwenye jimbo na anakiri kaukwaa uwaziri bila kuwa na uzoefu wa kazi, watu kama hao wakichaguliwa sehemu yoyote nyeti wanyonge ni kuandamana tu ni dawa

  ReplyDelete
 12. "Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumedharauliwa kiasi cha kutosha...SASA BASI!!!"

  Mwalimu Nyerere bwana kwa mistari alikuwa kiboko. I will always Love and cherish this guy!

  Masha upo? Ushatoka hospitalini???? Pole bro. Ndo maisha hayo. Lakini maelezo yako kwenye hiyo video dah! Mbumbumbu 100%

  ReplyDelete
 13. Bongo kweli tambarare. Mgombea kafleti lakini jamaa wanaendelea na shughuli zao tu. Kazi kweli kweli!!!

  ReplyDelete
 14. Mimi nasema, habari ndiyo hiyo.
  Hata Mongella kuporomoshwa Ukerewe imewashangaza watu pia

  ReplyDelete
 15. Simwonei Masha huruma hata kidogo. Wananchi wa Mwanza wameamka na hii ndo njia nzuri walioichukua kumtoa haraka. Namwonea huruma huyo wa Tarime na nahisi kuna kuchakachuliwa hapo. Wananchi wa Tarime walishaweka wazi kabla hata ya uchaguzi kuwa hawataki chama cha mafisadi na viongozi wasiotanguliza wananchi kabla ya matumbo yao hususani kwenye machimbo ya Nyamongo wanavyonyanyaswa na mazingira kuchafuliwa wanaishia kubadilika rangi za ngozi zao,kupata cancer na kufa. Ipo siku tuu, kila mwananchi wa Tanzania hususani wale ambao kila kukicha bora ya jana watasema hapana, tunataka hiki na ni lazima kitendeke kwa maslahi yao. Siasa za kuburuzwa zinaelekea ukingoni na wasipojirekebisha watapuputika zaidi kutoka kwenye madaraka ya kujuana yasiyo na tija kwa wananchi walio wengi.

  ReplyDelete
 16. Kuna ushahidi kabisa kwamba jimbo la Tarime limechakachuliwa na huyu mtunga vitabu vya kudesa Nyambari Nyangwine hakushinda kihalali. Sasa huyu mgombea mwenzake akifa baada ya kufleti huyu mfalme wa madesa Nyangwine si ndiyo atakuwa ameua au! Siasa kweli mchezo mchafu jamani!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU