NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, November 25, 2010

TAMADUNI ZINAPOGONGANA: SUALA LA KUCHOKONOA PUA BARABARANI NA KWENYE DALADALA

Tangazo hili liko hapa
 • Juzi juzi hapa nilikuwa naongea na mwanafunzi wa kike Mmarekani ambaye alikuwa anafanya utafiti wa shahada yake ya uzamivu jijini Dar es salaam na kisiwani Zanzibar. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kwenda Tanzania.
 • Nilipomuuliza kama aliipenda Tanzania alisema bila kusita kwamba ni nchi nzuri sana, yenye amani na kwa muda wa miezi yote mitatu aliyokaa huko hana jambo baya la kulalamika. Aliniambia kuwa mambo yaliyomvutia ni pamoja na ustaarabu wa watu, upole, wema, mazingira mazuri, maliasili kibao na kuambiwa "Mzungu, I love you" mara kwa mara barabarani na kwenye daladala.
 • Nilipomuomba anitajie jambo angalau moja ambalo hakulipenda jijini Dar es salaam mara moja alitaja tabia iliyomkera ya watu kuchokonoa pua zao kwa kutumia vidole vyao tena kweupe mabarabarani na hata kwenye daladala. Alisema kwamba ni kawaida jijini Dar kuona mtu amevalia vizuri akikatiza barabara na huku yuko bize akichokonoa pua yake bila wasiwasi wo wote. Hakuna cha kitambaa, maji wala nini
 • Sikujua kama hili ni tatizo kwani kusema kweli sisi hatujali sana kuhusu jambo hili. Nilijaribu kujitetea kwamba pengine ni kwa sababu ya vumbi, hali ya hewa vuguvugu na joto kali ndivyo hufanya pengine pua zitekenyeke na hivyo kuwalazimu watu kujisafisha. Basi alicheka tu na mjadala wetu ukaishia pale. Katika utamaduni wa kizungu, kuchokonoa pua hadharani kwa kutumia vidole ni jambo ambalo halikubaliki.
 • Ati, wewe una maoni gani kuhusu watu kusafisha pua zao kwa kutumia vidole na kisha haooo wakaendelea na hamsini zao kufukuzia maisha bila wasiwasi. Ulishawahi kufikiria kwamba ni jambo linalotia kinyaa na kwamba watu inabidi wajirekebishe kwa kununua vitambaa au kufanya hivyo kwa siri?

Huyu mchezaji aliwasha moto hapa Marekani baada ya kunaswa laivu na kamera akichokonoa pua yake

14 comments:

 1. Nulishalifikiria sana hilo! Sikujua kuwa linawakera wengi!!! Kweli ni vema katika hili tukajirekebisha. Lingine ambalo mimi na uafrika wangu linanikera sana. Sidhani kua Ulaya ama Marekani hilo lipo...Ni suala la kaka zetu, kiukweli sio ajabu kabisa kuona mwanamme akichepuka kidogo tu barabarani, na kutoa "maungo yake" na kujisaidia (haja ndogo). Akitoka hapo, hajali kua "amejishika maungoni" huko, hakuna cha maji ya kunawa mikono wala nini, na si ajabu dakika hiyohiyo akaja na kuoa mkono huo huo, pengie anasalimiana na mtu, anakushika mkono, etc! Mimi hua nshindwa kusema tu, ILA HILO NALO LINANITIA KINYAA SANA! Sidhani kama kwa wenzetu (ulaya, marekani) mambo hayo yapo, kwani suala la kujisaidia ovyo halipo, na kwenye vyoo kuna masink ya kunawia, sabuni, pamoja na karatasi za kufutia mikono!
  Hatuna hayo ya masinki huko barabarani, lakini pengine tujitahidi kuwa na kaustaarabu jamani!!!!!

  ReplyDelete
 2. Nilishalifikiria sana hilo! Sikujua kuwa linawakera wengi!!! Kweli ni vema katika hili tukajirekebisha. Lingine ambalo mimi na uafrika wangu linanikera sana. Sidhani kua Ulaya ama Marekani hilo lipo...Ni suala la kaka zetu, kiukweli sio ajabu kabisa kuona mwanamme akichepuka kidogo tu barabarani, na kutoa "maungo yake" na kujisaidia (haja ndogo). Akitoka hapo, hajali kua "amejishika maungoni" huko, hakuna cha maji ya kunawa mikono wala nini, na si ajabu dakika hiyohiyo akaja na kutoa mkono huo huo, pengie anasalimiana na mtu, anakushika mkono, etc! Mimi hua nshindwa kusema tu, ILA HILO NALO LINANITIA KINYAA SANA! Sidhani kama kwa wenzetu (ulaya, marekani) mambo hayo yapo, kwani suala la kujisaidia ovyo halipo, na kwenye vyoo kuna masink ya kunawia, sabuni, pamoja na karatasi za kufutia mikono!
  Hatuna hayo ya masinki huko barabarani, lakini pengine tujitahidi kuwa na kaustaarabu jamani!!!!!

  ReplyDelete
 3. Nafikiri kwa kibano cha BONGO kufikiria mpaka hili swala kwa wengi ni Luxury.  Ni sawasawa na nilivyowahi kusikia MSICHANA mmoja wa Kiswisi akilalamika kuwa Bongo kuna Bonge ya wavulana mahendsamu ila yeye kinachom- ``turn off´´ ni kukuta vijana wengi kwa muonekano wanavutia ila wananuka KIKWAPA kitu kimfanyacho kuhitimisha ni wachafu.:-(

  ReplyDelete
 4. Mazingira = Utamaduni= Maisha
  Nafikili mazingira tuliyonayo au ambayo tumekulia ndiyo yanatufanya tujenge utamaduni wa jambo fulani katika maisha.
  Unaweza kuona mtoto kutwa nzima anatoka makamasi na hakuna mtu wa kumfuta na kama wazazi au watu wakubwa watamfuta mara nyingi wanatumia vidole bila kitambaa kwa sababu ama kitambaa hakuna au hakuna msukumo wa kutafuta kitambaa, na hii imezaa utamaduni kama kufanya hivyo ni swala la kawaida, hakuna anayeona kama ni jambo la ajabu.
  Kutokana na hili, swala la kushika pua linakuwa si swala la ajabu katika jamii. Kwa mfano halisi, wakati nikiwa kijana, nilikuwa ninapeleka mifugo machungani ambapo ni mbali na nyumbani, nikipatwa na haja ya kujisaidia, nilikuwa tu ninatafuta kichaka na kujisaidia halafu ninatumia mchanga au majani kujisafisha. Haja ndogo ndo usiseme, popote pale kama hakuna wanawake wananiangalia, hii yote ni kwa sababu hakukuwa na choo karibu na karatasi zilikuwa ni bidhaa adimu. Huo ndo ukawa ni utamaduni ambao mpaka sasa sioni kama ni swala la ajabu sana nikimuona mtu anajisaidia haja ndogo barabani pamoja na kuishi katika nchi za ''Dunia ya kwanza'' miaka mingi achilia mbali kutumia vidole puani.
  Mazingira ya Nchi za ''dunia ya kwanza'' yanawafanya wananchi wake waone kama swala hili la kutumia vidole nila ajabu kwa vile nyenzo za kukabiliana na swala hili(kitambaa, karatasi nyepesi)zinapatikana kwa urahisi. Mtu akitumia vidole watu wanajiuliza kwa nini anafanya hivi wakati kuna nyenzo. Mazingira haya yamejenga utamaduni kama mtu akitumia vidole watu watamuona sio tu mchafu bali pia siyo mustaarabu.

  ReplyDelete
 5. Kuna baadhi ya mambo nakubaliana na mdau aliyepita na mengine kwakweli mimi hapana. Kama huko numa tuliondoa makamasi kwa mikono, haimaanishi tusibadilike! Na siamini kama huo ni utamaduni, bali ni uchafu tu. Kwani kakitambaa kakitumika, na baadae kakafuliwa na kuanikwa na kuendelea kutumika, hilo nalo linahitaji nini jamani? Mbona kuna mambo tunasingizia utamaduni, na wakati mwingine umaskini, hata kama kuna njia mbadala na rahisi sana? Kuna mambo ni lazima tubadilike jamani!!!
  Hebu fikiria, juzijuzi nilienda likizo hapo bongo. Nikaona mahindi ya kuchomwa, nikapenda, nikanunua. Then kuna mtu akanipigia simu akinitaka nimsubiri hapo nilipokua na angenipitia twende mahali flani. Basi nikala mhindi wangu. Baada ya hapo nilipata shida sana kutupa gunzi! Mazingira ya pale, wala hakuna ambaye angeshangaa kama ningetupa popote tu, kwani tayari palikua pamechafuka mno, magunzi, maganda ya miwa, maganda ya ndizi, nk, Nafsi yangu ilinisuta, nikavuka barabara kumfuata muuza mahindi, na aliniuliza kama nataka hindi lingine, nikamwambia "nimekuja kutupa gunzi mahali ulipoandaa pa kutupia takataka" Alishangaa. Lakini, kuna shida gani kufanua hivyo? Ama hata kuweka gunzi lako vizuri na kwenda kulitupia kwenye sehemu husika?
  Ninalotaka kusema hapa ni kwamba haimaanishi kwamba kwakua jambo flani tumelifanya kwa muda mrefu, sasa hatuhitaji mabadiliko! Jamani, mbona yapo mengi tunayoiga toka kwa wenzetu, hata kama hayana maana? Mbona tunaiga vimini, tunaiga...vitu vingine vya ajabu tu! Tunaiga hata "kula denda!" mbele za watu! Kwanini la usafi tunasingizia umaskini na tamaduni zetu??? Kwakweli katika hili mimi ah ah!!!!

  ReplyDelete
 6. Huyo mama angetembelea Kenya angekata roho. Maana alichoona kinakera Bongo kwa Kenya cha mtoto. Wakenya kupenga makamasi au kupiga chafya mtu anakula ni jambo la kawaida. Kuchokora pua ndiyo usiseme. Mliowahi kuikaa au hata kuijua Kenya mtakuwa mashahidi wangu.

  ReplyDelete
 7. KUna anayejua chemical composition ya kamasi atuambie? Mbona nasikia ni protini na antibodies kibao? Sasa tatizo liko wapi? Acheni watu wafaidi kamasi lao na msituletee mambo ya kizungu hapa. Kuna raha sana kulichokonoa kamasi hasa lile zito linalokaribia kuganda na ambalo limeanza kubadilika rangi kuwa yellow!

  ReplyDelete
 8. A-aaaaa! Tunakula mdau! Tukishindwa huu msosi lazima tuuposti uule!!! Unatuchefua bwanaaaa!!!!! (hasa ukizingatia msosi wenyewe tunaokula unakaribia karibia hicho unachotaja taja....bamia na....!!!! Acha bwanaaaa!!!!

  ReplyDelete
 9. naomba kuuliza...hivi kitendo hicho kina maana gani hasa kwa mila za huko? Uchafu ama maana nyingine? manake kwa mila za jamii fulani ukishika pua mbele ya mama/msichana manake unamtongoza :-(

  ReplyDelete
 10. @anony wa kwanza: Kumbe nawe unakerwa na hili tatizo la kuchokonoa pua. Pole. Kuhusu suala la kukojoa vichochoroni, nilishawahi kuulizwa pia na mwanafunzi wangu aliyekuwa anafanya utafiti wa vazi la kanga kule Tanga. Tazama link hapa chini.

  http://matondo.blogspot.com/2009/09/ili-kupambana-na-uchafu-inabidi-tuwe.html

  @Mtakatifu. Kama mdau wa November 25, 2010 2:43 PM alivyosema, tukianza kulaumu umasikini kwa kila kitu hata kutafuta kitambaa au karatasi ukailainisha basi hatutafika popote. Nadhani kwamba hili si suala la umasikini bali utamaduni zaidi na wachokonoa pua wala hawajui kama jambo wanalofanya linawakera watu wengine - kama huyo mdau hapo juu.

  @Ng'wanaMwamapalala. Usinikumbushe maisha ya utoto kule kijijini Usukumani. Maisha ya kuchunga ng'ombe siku nzima juani (huku watakwambia eti ni lazima utumie "sunscreen" kujikinga na kansa ya ngozi!). Maisha ya kutokuwa na wasiwasi.

  Kama nilivyosema hapo juu mimi siegemei upande wo wote katika suala hili ingawa pengine ningependelea tutumie vitambaa au karatasi kuchokonoa pua zetu hasa ukizingatia kwamba mtu anaweza kuwa na mafua au homa, akachezea kamasi lake halafu akaja kukushika mkono. Sijui kama kuna magonjwa ambayo yanaweza kuenezwa kwa njia hii. Utamaduni upi ni bora? Jibu ni hakuna ingawa kutokana na kutawaliwa kisaikolojia na watawala wetu tumekuja kuaminishwa kwamba kila kitu cha Kimagharibi ni bora kuliko chetu. Na mdau wa November 25, 2010 2:43 PM ameibua maswali mazuri. Mbona tunaiga tabia mbovu tu na kuacha zile nzuri? Mbona tuige vimini, kulana denda hadharani, kujichubua ngozi na mengineyo lakini tusiige hili la kushughulikia kamasi hadharani? Ati, tunaiga mabaya zaidi kuliko mazuri?

  Mdau wa November 25, 2010 4:53 PM, kusema kweli sijui chemical composition ya kamasi. Pengine madaktari na wakemia watuambie; na kama kuna madhara yo yote ya kuchezea kamasi kwa mikono.

  Mdau wa November 25, 2010 3:41 PM - kama Kenya mambo ni mabaya zaidi si jambo la kushangaza. Lakini hili la kukohoa na kutema makohozi wakati watu wanakula linahitaji "common sense" tu. Nimeshaona katika migahawa mingi ya Bongo wameweka onyo pale mahali pa kuoshea mikono kabla na baada ya kula kwamba haparuhusiwi kutema mate wala kusukutua.

  Kwa mdau unayekula bamia, pole. Ukiuchunguza mwili wa binadamu na mambo uliyoficha utashangaa. Huko tumboni ndiko kuna kizungumkuti. Usione kinyaa bali faudu bamia lako bila wasiwasi.

  @Ng'wanambiti: Nadhani kwa hawa jamaa kitendo hiki kinaashiria uchafu. Ni kitendo kibaya sana na miaka kumi niliyokaa hapa sijawahi ona mtu akichokonoa pua lake hadharani!

  ReplyDelete
 11. Unajua, suala, kwa mfano la kuchokonoa pua, au makamasi, nk, huko wetu lipo sana...na nakumbuka mie mwenyewe ni baada ya kutoka toka kidogo, labda ndio kidogo nimejifunza toka kwa wenzetu. Siwezi kuwanyanyapaa watu ambao bado hawajabadilika toka kwenye jambo hilo, kwa sababu naamini na mie yapo nnayofanya ambayo yanawaboa watu, ila nnachosema ni kwamba wakati mwingine tujitahidi kuiga mambo ya wezetu ambayo yana msingi, na kwakweli kwa mfano la kuchokonoa pua, halihitaji utajiri ndio mtu usichokonoe pua. Labda ni mazoea tu.

  Ila kama nilivyosema, siwanyanyapai wanaofanya hivyo, kwani na mie yapo ya kwangu pengine wala sijui lakini nawaboa sana watu.
  Na kwa upande wa watoto kwa mfano (kuna mdau aliongelea watoto kushinda na makamasi), nadhani mtoto kama mtoto hana tatizo, isipokua walezi wake.

  Mambo ya kuiga tamaduni za wenzetu, hiyo nayo ni kasheshe nyingine! Tazama wasichana kule Tanzania siku hizi wanavyoacha matiti nje-ni kama chuchu tu ndio inafichwa! Hayo tunaweza kuiga, na wala hatusemi "si utamaduni wetu", ama "sisi ni maskini!" Angalia milegezo ya suruali, angalia ...mambo mengi tu!

  Wacha nisiwachoshe.

  Siku nyingine.

  ReplyDelete
 12. Amani, Heshima na Upendo kwenu nyote.
  Binafsi sitasema lipi lililo sahihi wala sitataja lipi lenye KINYAA ZAIDI. Ila nilishaelezana na kueleweshana na kijana mmoja hapa Marekani kuwa KINYAA, AMA KERO inaweza kutokana na sababu nyingi ikiwemu suala la UMEKULIA WAPI, UMEKUZWA NA NANI, ALIPENDA NINI NA KWANINI NA ALIKUELEZA NINI KUHUSU MAISHA NA MATENDO YETU.
  Ni kweli kuwa hapa Marekani ni ajabu na kinyaa kwa mtu kuweka kidole puani (hata kama akitoka hapo ataenda kunawa), lakini ni UTAMU wa ajabu kwa mtu kuweka ULIMI KWENYE "MATUNDU" MBALIMBALI KATIKA KILE WAITACHO "CHACHANDU YA MAPENZI" a.k.a ROMANCE (hata kama akitoka hapo hatasuuza ulimi wake).
  Nilishaeleza kuhusu rafiki yangu ambaye kwa kisingizio cha KINYAA, asingeweza kuosha kikombe cha chai kwenye sinki la bafuni (japo alikuwa anaweka chai ya moto saaaaana) lakini HAKUWA NA SHAKA KUPIGA MSWAKI NA KUSUKUTUA KWENYE SINKI HILOHILO (hata kama maji hayo ya baridi yanaingia mdomoni na kubaki humo).
  Hapa ndipo ninapowaza ni nani wa kuona kinyaa????
  Awekae ulimi na kulamba vile ambavyo nyumbani (Tanzania) twaona havilambiki (japo tumeanza kuiga sasa), ama kuweka kidole puani?
  Je ni kinyaa kuosha kikombe kwa maji ya bafuni lakini si kusukutua mdomo?

  LABDA HAKUNA KINYAA NDIO MAANA KUNA KINYAA...

  Turejee kwenye jina la blogu kuwa "The Way You See The Problem Is The Problem"

  ReplyDelete
 13. Baada ya kutoa maoni hapa, nikaendelea kusoma blogu za wapendwa wengine nikakutana na HII...http://bashir-nkoromo.blogspot.com/2010/11/mahafali-ya-45-ya-cbe-dar-es-salaam.html

  Huyo mMarekani angeona hiyo picha ya tatu angefanyaje?
  Lakini kuna UBAYA WA MTU KUFANYA AFANYAVYO HUYO DADA?
  Tena anafanya kwa kujivunia saana (nami ningejivunia) japo hapa wanatengewa vyumba kwenye Mall ili wajifiche wanaponyonyesha. Unakumbuka yule mama aliyetolewa Mall kwa kuwa hakuwa akimnyonyesha mtoto kwenye "restroom"?
  Rejea hapa http://www.easterniowanewsnow.com/2010/05/04/c-r-mother-upset-after-breast-feeding-incident-at-mall/

  Swali langu bado labaki kuwa japo ni kinyaa na vibaya kumnyonyesha mtoto hadharani kwa hapa Marekani na si tatizo kuvaa ama kuwa uchi karibu 90% ya mwili wako, ni kipi kinyaashicho zaidi?
  BADO NAWAZA KWA SAUTI TUUUU KATIKA KUUENDELEZA NA KUUPANUA NA KUUNYAMBUA MJADALA

  ReplyDelete
 14. Mzee wa Changamoto: Pengine ni kweli kwamba "The Way we See The Problem Is The Problem"

  Tamaduni zina mambo yake na mimi nadhani kinachotakiwa ni heshima kwa kila utamaduni. Kinachoshangaza ni kwamba wapo watu ambao daima hudhani kwamba tamaduni zao ni bora kuliko za wengine na hawa huwa hawachelewi kubatiza tamaduni za wenzao kuwa za "kishenzi"! Lakini hata ukiangalia tamaduni zao pia zimejaa "ushenzi" mwingi tu - umerejelea mifano michache hapa.

  Kila utamaduni una mazuri na mabaya yake na yote haya yanategemea na utamaduni wa afanyaye tathmini. Na kwa vile tamaduni hizi ni lazima ziingiliane na kuathiriana, ingefurahisha sana kama mambo mazuri kutoka utamaduni huu kwenda ule ndiyo yangeigwa. Lakini kama alivyobainisha shangazi kutoka Norway, inavyoonekana ni rahisi kuiga mambo "mabaya" kuliko mazuri; na pengine hii ndiyo asili yetu binadamu.

  Ngoja niache na wengine waendelee....

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU