NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, November 18, 2010

WANAHISABATI MPO? TUSAIDIANE KUKOKOTOA UPYA HAYA "MAFUMBO" YA KIDATO CHA PILI ENZI ZILE

 • Ni kule shule ya Sekondari ya Kahororo mjini Bukoba. Tulikuwa kidato cha pili; ndiyo tu tumekaramka na kuanza kuwakaramsha "form one" wetu. 
 • Tulizoea kupeana mafumbo haya kama utani tu bila kujua kwamba kwa kufanya hivyo tulikuwa tukijifunza (tena kwa lugha tunayoielewa vizuri na katika mazingira yetu wenyewe) baadhi ya misingi muhimu ya hisabati - somo linaloogopwa na kuchukiwa sana kutokana na udhahnia wake na jinsi lifundishwavyo
 • Tatizo ni kwamba, sina uhakika kama nakumbuka tulikuwa tunapataje majibu. Kwa wanamahesabu wakokotoaji, hebu tukumbushane tena.
***************

Fumbo la kwanza
 • Jumamosi iliyopita, Speciosa alinunua ndoo ya maembe na akala theluthi moja (1/3) ya maembe yote. Siku ya Jumapili alikula nusu ya maembe yaliyobakia. Siku ya Jumatatu na Jumanne alikula embe moja moja kila siku. Siku ya Jumatano alikula nusu ya maembe aliyokuwa amebakiza. Siku ya Alhamisi alipoangalia katika ndoo aligundua kwamba alikuwa amebakiza embe moja tu. Je, Speciosa alinunua maembe mangapi siku ya Jumamosi?
Fumbo la pili.
 • Babu alikuwa anapita msituni siku moja alipoona kundi kubwa la ndege mtini. "Shikamooni ndege mia" Babu aliwasalimia wale ndege "Sisi siyo ndege mia" Ndege wale walijibu halafu wakaendelea. "Sisi sote ukiongeza na wenzetu kama sisi, ongeza na nusu yetu, halafu uongeze robo yetu pamoja na wewe mwenyewe ndipo tutafikia ndege mia" Je, babu aliona ndege wangapi?

11 comments:

 1. Kweli mwalimu ni mwalimu! Hata hivyo, nadhani fumbo lapili inabidi lirekebishwe kidogo, ndio tupate jibu "tulilokariri sawa na nyie mlivyokua mnakariri mafumbo (lakini na "njia" itaonyeshwa. Fumbo lilikua hivi:

  Babu alikuwa anapita msituni siku moja alipoona kundi kubwa la ndege mtini. "Shikamooni ndege mia" Babu aliwasalimia wale ndege "Sisi siyo ndege mia" Ndege wale walijibu halafu wakaendelea. "Sisi sote, ukiongeza na nusu yetu, halafu uongeze robo yetu pamoja na wewe mwenyewe ndipo tutafikia ndege mia" Je, babu aliona ndege wangapi?

  Nadhani inabidi liwe, "SISI WOTE, UKIONGEZA NA WENZETU KAMA SISI... (kwingine kuendelee kama ulivyoandik).

  NJIA: Nadege hao tuite ni Y. So, y+y+1/2y+1/4y+1=100 Then tunatafyta KDS, ambayo hapa ni 4. So, inakua (8y+2y+y)/4=100-1

  Tunapata 11y/4=99
  Then: 11y=99x4
  11y=396
  y=396/11
  y=36
  PROOF:
  36+36+18+9+1=100
  NAOMBA KU SUBMIT ASSIGNMENT!!!

  ReplyDelete
 2. wewe,labda alipewa bure baaadhi ya maembe ila tukitaka kujua basi tumuulize mhusika, hata hivyo ya nini kujua siri zake?

  au ndege sijui kama babu alitaka kujua idadi au salamu, labda mia ni aina ya ndege na sio idadi au ni jina jipya la ndege hao kutoka kwa babu!

  ReplyDelete
 3. @Mdau wa kwanza: Asante sana kwa sahihisho na jinsi ulivyokokotoa hili swali. KDS ni Kigawe Kidogo cha Shirika? Umenikumbusha mbali sana. Shukrani!

  @Kamala: Hesabu zinakupa shida nini? Hata kama zinakupa shida mbona usiombe msaada kwa mtaalamu mwenyewe (Shemeji?). Hebu mwambie atusaidie kukokotoa hayo maembe hapo juu. Wakora!

  ReplyDelete
 4. Matondo umenikumbusha Ubayani Beach na mwalimu wa hesabu aliyesomea Urusi aitwaye Karuka na samaki wake wa Mbojo! Nashukuru umefuta comment yangu moja. Maana ukibishana na juha umma hautajua juha ni nani.

  ReplyDelete
 5. Mwalimu NN Mhango: Mwalimu Karuka (aka Mbojo) hata sisi tulimkuta japo hakutufundisha hesabu. Alikuwa makamu mkuu wa shule wakati ule. Mimi nilikuwa Kahororo wakati ule UKIMWI ndiyo umepamba moto na ilikuwa patashika nguo kuchanika. Walimu zaidi ya saba waliteketea, wapishi, na hata classmates waliokaramka kupita kupita kiasi kidato cha pili. Nasikia hata Mkuu wetu wa shule tuliyekuwa tunampenda sana (Mr. Ishengoma - mwalimu mzuri sana wa Kemia) naye alifariki muda mfupi tu baada ya sisi kuondoka Kahororo. Ilikuwa hali ya kusikitisha sana!

  Samahani kwa kuifuta comment yako na yule anony. Mjadala ule ulikuwa hauendi vizuri na hasa ulipoanza kuhusisha wanablogu wengine ambao hawamo. Huwa sipendi kubania wala kufuta maoni ya mtu isipokuwa tu pale ninapoona kuna faida ya kufanya hivyo. Samahani tena!

  ReplyDelete
 6. Masangu ndugu yangu usijali. Kuna watu wana tabia ya kudandia mambo na kuwa na ushabiki wa ajabu wa mambo hata ya hovyo.
  Inaonekana ulikuja pale Ubayani baada ya mie kuondokia. Mie niliondoka pale mwaka 1985 na nilikuwa nakaa kwenye cubicle ya British Caledonia pale kwenye bweni la ujamaa.
  Ni masikitiko kusikia kuwa kumbe mdudu alimaliza walimu wengi pale.

  ReplyDelete
 7. Mwalimu NN Mhango:

  Kumbe nilikukuta basi. Mimi niliingia kidato cha kwanza pale mwaka 1985 na nilikuwa bweni la Maji Maji. Pengine wewe ulikuwa mwaka mmoja na akina Lubambangozi - jamaa mmoja mkorofi sana kwa kutesa "wageni" aliyekuwa anakaa bweni la Maji Maji pia.

  Ndiyo hali ilikuja kuchafuka sana pale baada ya ugonjwa wa "Juliana" kucharuka. Kuna walimu pale ambao walikuwa wazuri sana na tulisikitika kweli walipoanza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Walimu na wafanyakazi kama vile Kaijage (mwalimu wa Kemia), Ntamakurilo (Bayolojia), Mr. na Mrs Mushaija (Hesabu na Fizikia), Nguma (hesabu), yule mhasibu kijana mweupe akiitwa Gama na wengineo wengi tu. Mungu Awapumzishe salama waelimishaji wale.

  Halafu hali ilizidi kuchafuka zaidi walipotuletea wasichana na vijana wengi kuzindi kuchanganyikiwa zaidi. Na kuanzia hapo Kahororo ikaacha kutamba katika matokeo ya kidato cha nne. Mwaka wetu nadhani ndiyo tulimalizia kwa kupata divisheni wani nyingi sana hata kuwashinda washindani wetu wakubwa wa Ihungo.

  ReplyDelete
 8. Mwalimu Matondo umenikumbusha mbali. Huyu jamaa Ngozi, nakumbuka aliwahi kunitembelea nyumbani kwangu Dar na alikuwa rafiki yangu pia. Kusema ukweli niko nyuma ya wakati kuhusiana na yaliyojiri Ubayani baada ya mie kuishia.

  Hao walimu wote uliowataja nawakumbuka sana. Mushaija nakumbuka, alikuwa maarufu kama mwalimu aliyesomea Marekani akiongea kiingereza kwa mbwembwe na mkewe mtulivu. Kaijage alinifundisha kemia na Ntamakuliro Biolojia. Namkumbuka mwalimu Agricola tuliyezoea kumuita Galileo,Makoye,Tumbu, Ruta na Bayona na maraizoni yao bila kumsahau Soter Byarugaba gwiji la historia.

  Kidyagama yule mhasibu namkumbuka sana akisakata kabumbumbu huku wapishi Michaelna Shadrack Lugiko wakivuta sigara kama hawana akili nzuri.

  Fidelis (mleta chakula) naye namkumbuka kwa unoko wake wakati ule.Anyway inasikitisha sana.
  Inaonekana sikukumbuki kutokana na ukweli kuwa form four na form one zama zile walikuwa mbali sana. Sijisifii, nilikuwa bingwa wa debate na kifaransa wakiniita shehu Shaghari na mwaka huo niliondoka na A ya Kifaransa.

  ReplyDelete
 9. Mwalimu NN Mhango;

  Umenikumbusha hata walimu na wafanyakazi wengine ambao nilikuwa nimeshawasahau. Agricola alikuwa rafiki yangu mkubwa. Alikuwa anapenda mwandiko wangu sana kiasi kwamba alijitolea kuwa ananipa madaftari kila mwaka huku akiwasimulia watu shule nzima kwamba hajawahi ona mtu akiandika vile!

  Byarugaba - pengine mwalimu bora kabisa wa Historia. Niliwekeana naye miadi kwamba ni lazima nipate A ya Historia kidato cha nne. Na kweli nikaipata + zingine tano!

  Ndiyo - Kiingereza cha Mushaija kilikuwa kimetulia na fomu wani wala tulikuwa hatumwelewi anasema nini. Alikuja kufariki yeye na mkewe ingawa mkewe ndiye alitangulia. Yaani nakumbuka laivu kabisa. Maisha!

  Enzi zile maingiliano ya fomu wani na wazee wa kidato cha nne yalikuwa hayapo na hata huyo Lubambangozi nilimfahamu tu kwa sababu ya ukorofi wake wa kutesa watoto wa kidato cha kwanza. Nasikia baadaye alijiunga na vijana wa FFU!

  Kifaransa mimi nilifundishwa na mwalimu mmoja aliyekuwa anaitwa Isaya. Nadhani nyinyi ndiyo mlifundishwa na yule mama wa kizungu. Aliondoka tukiwa fomu wani na nadhani kuanzia hapo Kifaransa nacho kikaanza kudorora. Basi tukashikwa na Eliphas K. Bengesi - mzee wa falsafa na nadharia zisizoeleweka, tukakamatwa hasa kwenye Kiswahili kiasi kwamba hata Kifaransa wengine tukakiachia. Ni aibu kwamba sasa nimeshasahau karibu kila kitu. Itabidi nijipige msasa mtandaoni nijikumbushe angalau cha kuombea maji ili siku nikipita mitaa ya Paris nisiaibike!

  Asante kwa kumbukumbu hizi!

  ReplyDelete
 10. Asante nawe pia kwa kunirejesha kwenye enzi hizo. Ngozi alizaliwa hivyo. Hivyo, kujiunga na FFU kulimfaa zaidi.

  Je toujours parle Francais comme Anglais. Parceque elle est langue internationale. Ici au Canada nous la parlons comme la secondiemme langue nationale.
  Mon ami, merci et au revoir.
  Nimeona lau nikuchokoze na kukulingishia japo kidogo lau upate usongo wa kuanza kujinoa kwenye lugha hii tamu japo ya kikoloni.
  Kila la heri mwana wakwa.

  ReplyDelete
 11. Fumbo la kwanza majibu yake.fanya x=maembe yaliyonunuliwa.alipotumia 1/3x alibakiwa na 2/3×.alipokula nusu ya maembe alibakiwa na 1/3×.alipokula maembe mawli kwa siku mbili alibakiwa na 1/3-2 alipokula nusu ya maembe yaliyobakia alibiki na 1/6×-1 Hivyo ukichukua 1/6×-1=1,moja ni embe lililobaki.1/6×-1=1 1/6×=1+1 1/6x*6=2*6 x=12. Hivyo jumla ya maembe yote ni 12.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU