NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, December 27, 2010

ATI, MILA HII NI UNYANYASAJI WA KIJINSIA? WANAWAKE MNASEMAJE?

 • Katika makabila mengi ya Kiafrika wanawake kupiga magoti wanaposalimiana na wanaume na watu wanaowazidi umri ni jambo la kawaida. Upigaji huu wa magoti hutofautiana kutoka kabila moja hadi jingine. Kwa Wanyantuzu (Wasukuma wa kule Bariadi), kwa mfano, mwanamke alitegemewa kupiga magoti mpaka chini kabisa hasa anaposalimiana na wazee; na upigaji huu wa magoti ulikuwa (na bado) ni ishara mojawapo kuonyesha kwamba binti amelelewa vyema na ana sifa za kuoleka!
 • Picha hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Bi. Etta Banda akipiga magoti wakati wa kusalimiana na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete imezua maswali kuhusu mila hii kongwe. Ni heshima au udhalilishaji?
 • Inabidi tukumbuke pia kwamba wanaopigiwa magoti si wanaume pekee bali mwanamke anaweza kumpigia magoti mwanamke mwenzake anayemzidi umri au anayetaka kumwonyesha kwamba anamheshimu. Na katika jamii nyingine, wavulana na hata wanaume ndiyo hupiga magoti. Nakumbuka wakati nikisoma katika shule ya Sekondari ya Kahororo kule Bukoba, vijana wa Kihaya ndiyo walikuwa wakipiga magoti walipokuwa wakiwapa watu wazima vitu na jambo hili lilikuwa likitushangaza sana sisi "Banyamahanga" wa kutoka mikoa ya Shinyanga na Mara.
 • Kuna njia nyingi za kuonyesha heshima kwa watu wazima au watu wenye wadhifa katika jamii mbalimbali duniani. Ndiyo maana Rais Obama aliwasha moto hapa Marekani alipopigwa picha huku akiinamisha kichwa wakati akisalimiana  na Mfalme Hirohito wa Japan. Hii ilionwa kama dalili ya udhaifu na kutojiamini wakati ni jambo la kawaida katika utamaduni wa Kijapani.
 • Mimi nadhani kinachohitajika ni maelewano na utangamano wa kitamaduni. Kwa wakati huu wa dot.com, wakati wa usasa na utandawazi ni rahisi sana kutupilia mbali mila zetu kwa kudai kwamba zimepitwa na wakati. Na wakati mwingine tunaweza kushangaa baadaye tunapokuja kugundua kwamba hata hao "wakubwa zetu" tunaojaribu kuwaiga kumbe nao wana mila zinazofananafanana na zetu tunazojaribu kuzitupilia mbali. Umeshawahi kujiuliza, kwa mfano, ni kwa nini, wafalme wachache waliobakia Afrika wanapigwa vita sana na nchi za Kimagharibi wakati huo huo Ulaya nzima imejaa wafalme na malkia? Au pengine kwa vile Wafalme waliobakia Afrika (mf. Mswati wa Swaziland) ni "madikteta?" na wengi walioko Ulaya wapo "kiishara" tu?
 • Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba ni lazima tuwe waangalifu kwani si kila mila yetu ni mbovu na si kila mila ya Kimagharibi ni nzuri !!! Mila ikionekana ni potofu (mf. ukeketaji, au hata hii ya wanawake kupiga magoti) basi ni lazima tuitupilie mbali na kama ni nzuri, ni lazima tuishikilie. Vinginevyo tutapoteza utambulisho wetu na kuwa watu wasio na chao hapa duniani! Kama kupiga magoti kwa lengo la kuonyesha heshima ni unyanyasaji (na hapa simwongelei J.K. wala picha hii), basi inabidi tutafute njia nyingine ya kuonyesha heshima hiyo. Au pengine hata hakuna haja ya kuonyesha heshima!
 • Na kwa hili la kupiga magoti, ningeomba hasa wanawake watupe maoni yao (ili tusije tukawa kama huyu jamaa). Wanajisikiaje wanapofanya hivyo. Ni kweli wanahisi kuwa wananyanyaswa? Dada Yasinta, Koero, Da Mija na wengineo tuambieni.
 • Soma maoni ya Profesa Mbele - bingwa wa maswala ya kitamaduni na Mwl. Mhango wa Blogu ya Mpayukaji hapa.

10 comments:

 1. Kupiga magoti ni utamaduni na si kwamba kwa kupiga magoti ndo unaheshima sana. Mimi ni mnyamwezi na nilizaliwa Kilimanjaro ambako hakuna kupiga magoti. Wazazi wangu walikuwa ni wafanyakazi waliohama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine lakini nilipowasiliana nao aidha kwa kuwaamkia ama kutoa au kupokea kitu nilifanya hivyo nikiwa wima na kwa unyenyekevu.

  Sasa nimeolewa kwenye kabila ambalo kupiga magoti ni sehemu ya utamaduni (Mbeya) siku ya shereke za harusi kwaweli nililazimika kupiga goti na kila mtu alijua huyu ni wakuja. Jinsi maisha yanavyoendelea unajikutaunapiga kwa kiasi.

  Muingiliano wa tamaduni either kwasababu ya ndoa ama kuhamia mijini kunafanya baadhi ya mila, tamaduni na desturi kupotea. Ni mara chache utawaona watu mijini wakisalimiana kwa kupiga magoti kama ambavyo ukiwakuta huko ndani usukumani au unyakyusani.

  Sioni kama ni udhalilishaji ikiwa utasalimu ama kutoa au kupokea kitu kwa kupiga magoti au ukiyafanya hayo bila kupiga magoti haina maana kwamba una dharau.

  Vipi hao warembo (bintizo) wanapiga magoti wanapokusalimu? Au ndo wameshaiga ya wamarekani?

  ReplyDelete
 2. Inaelekea dada anabembeleza cheo hajiamini, sijaipenda kabisa kati ya mila potofu za kufutwa ni pamoja na hii. Foreign Minister hawezi kufanya hivyo

  ReplyDelete
 3. Hii habari/mila kwangu sio ngeni kabisa na wala sioni kama ni unyanyasaji. Kule kwetu ungonini tunapiga magoti kwa waliotuzidi umri, wakwe nk. nakumbuka mara ya kwanza kabisa bibi yangu mzaa mama alikuwa akimwona baba anampigia magoti na ukapulya wangu nikamuuliza kwanibni anafanya hivyo? akasema ni mila na pia ni heshima tu.
  Na baada ya miaka nikahamia ubenani hapa ndo nilipoona jinsi upigajimagoti ulivyo yaani we acha tu yaani wabena wana jua kupiga magoti bwana wewe. Lakini mimi sioni ni kitu cha unyanyasaji ni mila na ni utamaduni. Kumbuka huku kupiga magoti hata wenzeti hapa kale walikuwa wanapiga magoti na sasa kunaanza ku├ąpotea na kuanza kukumbatiana. Na sasa naona kama kawaida yetu nasi tunajifanya kuiga kuacha kupiga magoti.

  ReplyDelete
 4. Mdau wa December 27, 2010 7:32 PM punguza jazba! Hahahahahahaaaaa! Mimi sina shida kabisa na kupiga goti, japokua kwetu (Tanga) hatuna hiyo mila, lakini huwa binafsi nina 'adjust' kulingana na mahali nilipo, provided najua "maana iliyobebwa" katika hicho nnachofanya/iga! Kupiga goti, kwangu mimi HAKUNA SHIDA KABISA! Ila huyo aliyempigia mama Kikwete...hiyo siyo heshima, ila naona ni kama bwana na mtumwa kabisaaaaaaa! Hiyo siyo!!! Arrah

  ReplyDelete
 5. Hakuna udhalilishaji wowote katika kumpigia magoti mtu unayemuheshimu, suala la udhalilishaji linaweza kuja kama magoti hayo yatakuwa ni ya kulazimishwa kwa sababu tu mpigiwa magoti ni jinsia inayopewa kipaumbele na jamii inayomzunguka...

  ReplyDelete
 6. Hata mimi naungana na dada Yasinta. Sioni ubaya wowote katika kupiga magoti ili kuonyesha heshima. Tusiwe wajinga kwa kudhani kwamba kila kitu that is ours ni cha kijinga na kinastahili kupigwa vita. Haya basi tuanzeni kubend kama huyo Kenyan boy hapo juu au alama zinginezo.

  Mimi ni Mnyakyusa and I bend ili kuonyesha heshima kwa watu wote wenye utamaduni huu na sioni ubaya wo wote. Huyu mama wa Malawi must be praised kwa kuenzi mila zake and this is not gender discrimination. Jamani tuamkeni. Not everything African is bad and not everything ya mzungu is good. Trust me, many wazungus would wish to have what we have e.g. discipline to our kids. Hakuna issue hapa

  ReplyDelete
 7. Hii ni mila nzuri. We have to show respects to our seniors ingawa sina uhakika hapo juu. Hakuna unyanyasaji wo wote wa kijinsia hapa and you modernizers, acheni kuiga na kuchafua kila kitu that is African!!! Kama kupiga magoti ni udhalilishaji, kwa nini kubend kichwa is not???

  ReplyDelete
 8. duhu wanawake kwa kupiga magoti naona na nafuu kwao hata kuchuchumaa na ndio maana kwenye haja ndogo pia hupiga magoti!

  ReplyDelete
 9. Hahahahaaaaaaaaa
  Suala la KUDHARAULIKA ama KUNYANYASIKA KIJINSIA halijawahi kutokana na KITENDO, bali TAFSIRI na HISIA ya kile kitendekacho.
  Lakini suala la HESHIMA ama NIA ya kufanya ufanyalo yaweza kuwa kigezo ha HESHIMA ama DHARAU. Kuna wakati ambao kumheshimu asiyestahili (hata kama unadhani ni sahihi) kunaweza kutafsiriwa kama dhalilisho.
  Sina hakika kama huyu Mama alifanya haya akifuata tamaduni ama akiamini kuwa Rais Kikwete anastahili HESHIMA HIYO.
  Unadhani wanaosema wanadhalilishwa "kupigishwa" magoti hawapi(ga)gi nyakati nyingine wapendazo wakifanya wapendayo?
  WANAFANYA
  Je! pale WAHITAJIKAPO kupiga magoti (kama kwenye kuchota maji nk) unadhani wanahisi kunyanyasika?
  LA HASHA!!
  Si kwenu ukimpiga mkeo unamnyanyasa kijinsia? Huku nje ya nchi je? Lakini kwa yale makabila ama sehemu waaminio kuwa hicho ndio kigezo cha wivu unaoakisi kiasi cha upendo...SI WANAONA NI BARAKA KWAO?
  Kwani hatuoni kuwa kuonesha alama ya dole gumba ni ishara kuwa kila kitu kiko swafi, je nchi za Iraki na Irani wanalichukuliaje?
  Ama hujaona wanaosalimiana kwa kuoneshana "kidole cha kati" (japo kwa mizaha) ilhali ukiwatendea wewe msiyetaniana mnaweza kutoana ngeu.
  Amaaaaaaaaaaa...Si kote ni KUPIGA MAGOTI ama ni KUMPIGA MWANAMKE ama ni KUMNYOOSHEA KIDOLE CHA KATI?
  Kwanini basi tafsiri ya KUONEA ama KUDHALILISHA ama KUNYANYASA isiwaguse wengine ama walewale kwa namna moja na iwaguse kwa namna nyingine?
  Ni kwa kuwa NAMNA TUONAVYO TATIZO NDILO TATIZO.
  Kuna mengi (hasa yafanyikayo nyuma ya pazia na zaidi kwa wanandoa) ambayo kwa hakika yakitendeka kwingine ama yakisemeka utendekaji wake ni KUNYANYASIKA, lakini yakitendwa kwa yatendwavyo na kubaki kwa watendayo, ni chachandu ya mapenzi

  NAACHA...Tuonane NEXT IJAYO

  ReplyDelete
 10. Utumwa uliopitiliza,wakupigiwa magoti ni Mungu peke yake.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU