NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, December 30, 2010

BIBLIA, SINEMA YA MAISHA YA YESU NA REKODI MBALIMBALI ZA DINI KATIKA LUGHA ZETU ZA KIASILI.

Picha hii inapatikana hapa.
 • Wamishenari wa mwanzo katika miaka ya 1900 walitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha zetu za kiasili. Mbali na kuitafsiri Biblia Takatifu katika lugha zetu, wao pia ndiyo waliandika sarufi na kamusi za mwanzo za lugha hizi, pamoja na kwamba wengi wao hawakuwa wanaisimu wala wataalamu wa mambo ya lugha. Cha kushangaza (au pengine niseme cha kusikitisha) ni kwamba hata baada ya miaka mingi ya uhuru, lugha zetu nyingi bado hazijashughulikiwa ipasavyo kwa kuandikiwa sarufi za kina na machapisho mengine; na badala yake zimeendelea kudharauliwa na nyingi zipo katika hatihati ya kutozungumzwa na pengine hatimaye kuweza kutoweka kabisa.
 • Wamishenari na watu wanaojishughulisha na mambo ya dini bado wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha na hata kuhifadhi lugha zetu kupitia azima yao isiyotetereka ya kueneza neno la Mungu. Ndiyo maana kama Mwanaisimu, nimefurahi sana kugundua kwamba Sinema ya Maisha ya Yesu sasa inapatikana mtandoni katika Lugha mbalimbali za Kitanzania kama Kibena, Kidigo, Kigogo, Kihaya, Kihehe, Kimasai, Kimeru, Kimoshi (Kichaga), Kimakonde, Kimakua, Kinyakyusa, Kinyilamba, Kimasai, Kinyamwezi, Kinyakyusa (cha Ngonde), Kishambala, Kisukuma, Kiswahili na Kiyao. Sinema hii pia inapatikana katika lugha nyingine za Afrika. Ukitaka kuisikiliza na kuitazama, tembelea tovuti ifuatayo na chagua lugha unayotaka.
 • Pia unaweza kusoma Biblia Takatifu, kusikiliza na kutazama filamu ya Yesu pamoja na rekodi mbalimbali za Kikristo katika lugha kadhaa za Tanzania kupitia tovuti ya Joshua Project (chagua Tanzania, halafu languages). Mungu Atubariki tunapouanza mwaka mpya wa 2011.    
 • Swali: Hivi Kurani Tukufu inapatikana katika lugha nyingine yo yote ya Tanzania mbali na Kiswahili? Au hairuhusiwi kuitafsiri hovyo hovyo kama ilivyo kwa Biblia Takatifu? 

   7 comments:

   1. Nimefurahi sana sana kuona kuna lugha nyingiii kiasi hiki za asili safi sana. Ila nasikitika sijapata lugha yangu.

    ReplyDelete
   2. Dada Yasinta;

    Ingawa sinema ya Yesu haipo katika Kingoni, ukienda hapa http://www.joshuaproject.net/countries.php, halafu weka Tanzania na baadaye bofya Languages utaona kwamba kuna Biblia ya Kingoni pamoja na hadithi na masimulizi ya dini katika Kingoni.

    Sijui walikuwa wanatumia vigezo gani katika kuchagua lugha za kufanyia tafsiri. Nimefurahi sana kuitazama na kuisikiliza tena sinema hii ya Maisha ya Yesu katika Kisukuma.

    ReplyDelete
   3. Mwalimu Matondo,

    Dada Yasinta aliwahi kutafsiri sala ya Baba Yetu kwa ki-Ngonni, ikabidi nisalimu amri, maana alifanya kazi nzuri sana.

    Mimi naongea ki-Matengo, ila nikisikia au kusoma ki-Ngoni nafahamu kiasi kikubwa, na nilipendezwa na tafsiri yake.

    ReplyDelete
   4. Prof. Mbele. Yasinta anakifahamu Kingoni kwa undani na unje wake. Pengine nitamwaga mtama mbele ya kuku wengi hapa lakini binti huyu wa Kingoni ambaye amekataa kuusahau utamaduni wake yuko anaandika kitabu juu ya utamaduni wa Wangoni. Mimi huwa nafurahi sana kuona watu wanaojivunia utamaduni (utambulisho) wao. Na dada Yasinta ni mfano mzuri sana kuhusu jambo hili.

    ReplyDelete
   5. Hapo juu ni cover za madaftari au ni vitabu? Na kwa nini ni juu ya lugha za mkoa wa Mara tu?

    ReplyDelete
   6. Shukran Mkuu, Heri ya Mwaka Mpya na kwako pia uwe mwaka wa mafanikio zaidi

    ReplyDelete
   7. Kaka Matondo ahsante sana kwa yote ngoja niende huko nikafaidi. Utamaduni huu hauwezi kuachwa tu hivi hivi ni lazima uendelezwe. Prof. Mbele nawe nakushukuru kwa huo wasifu hata mimi kimatengo nakielewa na naweza kuongea kidogo. utamaduni oyeeeeee!!

    ReplyDelete

   JIANDIKISHE HAPA

   Enter your email address:

   Delivered by FeedBurner

   VITAMBULISHO VYETU