NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 24, 2010

FIKRA YA IJUMAA: HUENDA MWALIMU NYERERE ALIKUWA SAHIHI. PENGINE URAIS NDIYO KAZI NGUMU KULIKO ZOTE

 • Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Ikulu palikuwa panamliza. Kwamba kulikuwa na siku alikuwa halali hasa baada ya kufanya ziara za vijijini na kuona umasikini wa wananchi na huku yeye akiwa ndiye mwenye jukumu la kuwaongoza na kuwaonyesha njia ya kutokea katika umasikini huo wa kutisha. Alisema kwamba kuna wakati hata alikuwa akidondokwa na machozi. Alichojaribu kufanya, japo kilishindwa, sote tunakijua.
 • Kwingineko tunamsikia akilalamika kuwa Ikulu siyo mahali pa kukimbilia hasa kwa kiongozi mwadilifu na aliwakoromea vikali makomredi wenzake waliokuwa wakijaribu kuingia Ikulu kwa kutumia njia za mkato zikiwemo kukopa mamilioni ya pesa (sijui kama ni kweli!). Mwalimu alitaka kujua biashara ambayo wangeifanya Ikulu ili kuweza kurudisha mamilioni waliyokuwa wameyakopa. Akihutubia katika Sherehe za Mei Mosi Mbeya mwaka 1995 Mwalimu aliunguruma akisema "Mtanzania wa leo hawezi kununua kura bila kwanza yeye kununuliwa"
 • Picha hii ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni kielelezo kizuri cha kauli hiyo ya mwalimu kuhusu "raha" na majukumu mazito ya Ikulu. Akiwa ndani ya nyumba hii pamoja  na waombolezaji hawa, naamini kwamba rais ni lazima alishikwa na uchungu usiopimika kuhusu umasikini wa wananchi hawa ambao kimsingi wanamtegemea yeye awaonyeshe njia ya kuendea katika nchi ya ahadi. Naamini kwamba huu ndiyo umasikini ambao ulikuwa unamliza Mwalimu Nyerere. Sitashangaa kama na yeye machozi yalimdondoka!
 • Hata hii picha anayotoka nje inaweza kuonwa kama taswira ya Musa aliye tayari kuwaongoza watu wake kuelekea katika nchi ya ahadi tena kwa Nguvu Zaidi, Ari Zaidi na Kasi zaidi. Akiwa na mabuti, suti nyeupe na kalamu tatu katika mfuko wa suti yake, rais anaonekana kuwa amejiandaa vizuri na yuko tayari kwa safari. Bado ana miaka mitano zaidi ya kuleta mabadiliko yenye kuonekana na kuhakikisha kwamba Watanzania tunapiga hatua za kweli katika safari yetu. Tumezunguka jangwani kwa miaka 49 na sasa wakati wa angalau kuona dalili za nchi ya ahadi tunayoiendea umefika. Na dalili zinaonyesha kwamba wapagazi na wasafiri wengine wameanza kuchoshwa na mizunguko hii ya jangwani isiyo na mwisho!
Picha hizi za rais sijui nilizipata wapi. 
Kama ni zako nijulishe nikushukuru!

19 comments:

 1. Hata mimi nawashangaa wanaogombea urais hata kufikia kumwaga damu. Jamani majukumu ya uraisi ni magumu, ujue dhamana ya nchi ipo mikononi mwako.
  Watu wa imani wansema kazi ya uraisi ina kufanya usikwepe moto wa jahanamu kwanii utaulizwa hata mbuzi wa jamaa kule ndani ndani aliyepotea na kula vyakua vya shamba la jirani...hebu fikiria wewe utajitetea ningejuaje hilo! Utaambiwa kama unajua hivyoo mbona uliutafuta uraisi hata kwa kuhonga, hiyo honga ya kupata kura ya huyu mtu aliyedhulumiwa shamba lake uliipataje, mbona yeye aliweza kukupa kura yake!
  Watembee waone, utaangusha machozi kama wewe kweli una ubinaadamu!

  ReplyDelete
 2. Jamani ni X-mass kwa baadhi ya watu! Stori hii inaweza kuliza washerehekeao watakao kujidanganya kuwa mambo shwari angalau KIYESUYESU!

  Au?

  ReplyDelete
 3. Hahahahaaaa! Kitururu umenifanya nicheke japo sikua "nina bajeti ya kucheka leo!" Ati "kujidanganya kuwa mambo shwari angalau KIYESUYESU!" Huwa una falsafa ngumu sana Kitururu!!!
  Nilisikitika sana kukosa japo dakika moja ya kukusalimia "kwa kukushika mkono" nilipokuona pale Morogoro, WAMO, mwezi wa nane, kulikua na mahafali ya watu wa Bible Translation, na mie nilifika jioni sana...labda saa moja kasoro hivi, na nikakutana nawewe ukiwa ndio unatoka! Nilikusalimia, lakini nadhani watu walikua wengi, na mie sikua miongoni mwa "waheshimiwa" kwahiyo wala sikua recognised! Lakini nilifurahi sana kukuona...japo nilikosa bahati ya kukushika mkono ambapo naamini "Ningeambukizwa" utakatifu kama sio falsafa zako!!! Hahahaaaaa!!!

  Xmas njema kakangu...hata kama "mambo si shwari sana" ama ni shwari kwa kujidanganya!!!!

  ReplyDelete
 4. @Anony: Xmas Njema sana Mkuu !


  ......ingawa ingekuwa bomba sana ningekujua jina WEYE ni nani MKUU ingekuwa bonge la sindimba!:-(

  Tuko Pamoja sana Mkuu!

  ReplyDelete
 5. Urais ulikuwa mugumu wakati wa akina Nyerere. Kwa sasa hauna tofauti na ujambazi ambapo mtu hutumia kila hadaa na balaa kuupata ili ale na watu wake.
  Urais siku hizi si jukumu la kuwa kwenye mabega ya mtu bali zana ya kulia bila kuguswa na mkono wa sheria kutokana na kinga za kijambazi zilizojazwa kwenye katiba viraka za kiafrika.
  Urais kwa sasa ni urahisi wa kawaida wa kuiba bila kukamatwa. Rejea EPA, Richmond-Dowans na walio nyuma yake.
  Zamani urais ulikuwa utumishi. Kwa sasa urais ni ubwana, utukufu, ulaji wa dezo na mengine kama hayo.
  Hivyo kwa watu wasio na adili, idili na visheni urais ni rahisi kweli kweli.

  ReplyDelete
 6. @Kitururu: Yesu mwenyewe alikuja kuwapigania na kuwaokoa watu masikini na wanyonge kama hawa. Umesahau alivyowafurusha mafisadi uchwara pale hekaluni?

  Musa alikuwa mwonyesha njia (japo had no clue) Yesu yeye alidai ndiye alikuwa njia na huyu baba naamini hana clue kama vile Musa.

  Ikumbukwe kwamba maana hasa ya Krismasi ni kuwasaidia wanyonge na wenye shida na kamwe siyo hizi customs za kipagani zilizoongezewa na Waroma. Kwa hivyo Krismasi siyo kunywa pombe wala kungonoka bali kutafakari na kujisaili (self determination). Ni wakati mzuri wa kutafakari ukombozi wetu kama jamii unavyoendelea.

  Thanks Mr. Matondo kwa kuiweka hii wakati huu tunapomkumbuka Savior namba wani. Huwa napenda ubunifu wako na jinsi unavyoweka na kujadili mambo mazito kirahisi na kwa kutumia mtindo wa bullets. Believe me hii inatusaidia sana wasomaji. Aluta continua!!!

  ReplyDelete
 7. @Kimwana wa KOMBO aka Binti KOMBO: nikinukuu chembechembe za mdokezo wako:``...maana hasa ya Krismasi ni kuwasaidia wanyonge...´´ -mwisho wa nukuu yangu kizembe.:-(

  Sasa kwa hivyo hudhani unapendelea siku fulani ndio ziwe zakukumbuka zaidi WANYONGE wakati kikweli na kihalihalisi wanyonge wako kila siku ya mwaka?

  Na sijui kwanini kunywa pombe na kungonoka wakati wa krismasi sioni kunaathari gani kama ATHARI ZA NGONO na KUNYWA pombe hazitachukuliwa kuwa ziko kila siku ya mwaka kikupata dhambi ya uasherati, KUPATA MDUDU au tu kikumpa mimba binti ya mtu .:-(


  Na moja ya sababu sisherehekei siku hii ni kutokana na kutopenda WATU waegemeavyo siku fulani ndizo ziwe na maana ya kitu fulani,.....

  ...Si kuna waaminio leo sio siku ya WANAWAKE duniani au sio siku ya UKIMWI duniani kisa eti leo ni KRISMASI kitu kifanyacho labda leo kuna wasahauo MAALBINO duniani kisa wanaamini kuna siku yao na sio leo kwakuwa leo Papa wa KIROMA aliitisha mkutano na wakaamua kuchagua leo iwe ni siku ya Yesu wakati hakuna ajuaye kikweli YEsu alizaliwa lini?

  Kwani Yesu ni kweli kama ni mwana wa Mungu anahitaji vinyangalakata kama wanadamu WAWE na siku maalumu kwa ajili yake?


  Nawaza tu kwa sauti!:-(

  ReplyDelete
 8. Inasikitisha nikiangalia picha ya jengo la kiongozi mkuu wan chi na picha ya nyumba ya waombolezaji. Hii inanidhihisha kuwa safari iliyoanzishwa na Mwalimu bado ni ndefu sana kwa wananchi hawa kufika katika nchi ya ahadi. Miaka 49 sasa, siamini kama wananchi hawa wanaamini wataiona hata hiyo dalili ya nchi ya ahadi wanayoiendea. Najalibu kufikilia, kama miaka 49 imepita watu bado wanaishi maisha ya aina hii, sijui miaka mingine 49 ndio watakuwa wamekaribia karibia kuishi maisha yanayofanana na mazingira ya jengo la kiongozi mkuu ambalo mpaka kuna mzunguko(roundabout) kuonyesha ni jinsi gani jengo hilo linapurukushani za hapa na pale!!.
  Kila kukicha safari inazidi kuwa ni ngumu na iliyojaa majaribu ya kila aina. Nakumbuka kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi ilikuwa ni lazima uziseme kwa sauti ahadi za mwanachama wa chama cha mapinduzi kabla ya kupewa kadi ya uanachama. Katika ahadi hizo kipengele cha tatu kinasomeka, ‘’Nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma’’ pia kipengele cha nne kinasomeka ‘’Rushwa ni adui wa haki, sitapokea rushwa wala kutoa rushwa’’ na adhabu ilikuwa siyo chini ya miaka miwili jera na viboko 24. Hii angalau natumaini ilisaidia kuwakumbusha watu umuhimu wake wakiwa safarini jangwani. Awamu tatu na nusu ya viongozi kwa sasa, hivi vyote natumaini vimeishazikwa.
  Ukimwangalia kwa nje kiongozi wa sasa wa nchi na waziri mkuu wake, wanaonekana ni watu wenye utu na ubinadamu wa kwelikweli lakini hizi sifa hazitoshi kuwaongoza watu kwa kipindi hiki jangwani kwa sababu safari ya leo imejaa majaribu yanayohitaji kiongozi awe pia mkali. Matukio ya ufisadi(Richmond/dowans,rada, CIS, DCP,SONGAS, IPTL, EPA, na BOT) ni mfano wa kuwa na kiongozi ambaye siyo mkali na ambaye anawaonea haya viongozi wa chini yake.
  Cha kushangaza waziri mkuu anakataa gari la kifahali(shangingi) wakati huohuo ofisi yake ndiyo inayoshughulika kuyaidhinisha hayo magari. Kwa nini asizuie mradi mzima wa ununuzi kama kweli anaamini niya kifahali kama marehemu sokoine alivyokataa kuwaongezea marupurupu wabunge akiwashangaa na kuwaambia waone aibu kwa kuwa maisha yao ni mazuri zaidi ya wananchi wanaowaongoza. Hakuna maana ya kujigamba kuwa mtoto wa mkulima bila kuwajengea mazingira mazuri ya kilimo wakulima ambao bado wanatumia zana za karne ya mawe katika hii karne ya sayansi na tekinologia.
  Ndiyo maana hata katika biblia kwenye kitabu cha KUTOKA 32:1 watu walianza kukata tamaa hata Musa naye akalifikia hatua ya kukata tamaa katika kitabu cha KUTOKA 32:19 kama hali yenyewe ndiyo hii.

  ReplyDelete
 9. @Binti Kombo: Nikinukuu Mdokezo wako: ‘’.......kamwe siyo hizi customs za kipagani zilizoongezewa na Waroma. Kwa hivyo Krismasi siyo kunywa pombe wala kungonoka bali kutafakari na kujisaili......’’ mwisho wa kunukuu. Hapa nashindwa kuelewa kama nimejifunza kitu furani au ndio nimechanganyikiwa baada ya kusoma dokezo lako, kumbe Mpagani ni yule mny’wa pombe na mng’onokaji, halafu huyu mpagani huwa hasaidii wanyonge na wenye shida wakati tu wa krismasi na pia hatafakari na kujisaili!!.
  Mimi naamini Upagani nao ni dini, ila sijui kama ni dini ya kweli au la, na kwa hilo namuachia Mola. Kwa mtazamo wako Binti Kombo, kama mpagani anaweza kusaidia wanyonge na wenye shida katika siku 364 na siku ya 365 akasherekea kwa kung’onoka na pombe, natumaini kwa akili ya kawaida atapata baraka zaidi ya huyu anayesaidia wanyonge na wenye shida wakati tu wa siku ya krismasi. Binti Kombo unanikumbusha watu wa nchi za magaribi ambao wakati wa krismasi utawaona wanapigana vikumbo wanagawa vyakula na nguo kwa watu wasio na makazi na kazi, baada ya krismasi hawaonekani tena. Kama Simon Kitururu alivyoainisha, Wanyonge wako kila siku ya mwaka, kwa nini wasifanye hivyo kila siku.
  Umenishangaza kwa kuwalaumu Waroma halafu nikiangalia kwa undani zaidi nagundua kuwa matendo unayopenda jamii iyafuate niya hao Waroma.
  Unanipelekea kukubaliana na usemi usemao Nyani huwa haoni kundule.
  Sijui kama nawaza akilini!!

  ReplyDelete
 10. Nimegundua kuwa kumbe rais wetu hana uzalendo! Naona bendera ya rais wala sioni ile ya taifa ingawa kuna mlingoti wake japo u mtupu. Jengo zuri kweli kweli na linafaa kuwa patakatifu pa patakatifu ingawa siku hizi limegeuka kuwa kaburi ambalo hung'ara juu ili ndani limesheheni uoza. Hayo tuyaache.

  ReplyDelete
 11. Mkuu Kitururu nilikua nafurahia sana katika kukuona kwenye kipindi (nimesahau jina lake) kilichokua kinaonyeshwa na Aboud Television, sina hakika kama hicho kipindi bado kipo...biba viji miaka "sijaangalia" Aboud Televison! Nilibahatika kukuona kwenye majadiliano-nadhani ya mambo ya MAZINGIRA na pia mambo ya UTAMADUNI na kwakweli ninafurahia sana unavyojenga hoja na unavyojibu maswali! Ndio mana "sikauki" kwenye kijiwe chako kufaidi "hekma" na falsafa zako!!! Naamini tutakutana tena! Kwasasa "nasaka" maisha ughaibuni!!!!

  Krismas njema mkuu!!!

  ReplyDelete
 12. Typo hapo juu..."kipo....biba viji miaka...ilitakiwa iwe NINA VIJI MIAKA...."

  ReplyDelete
 13. @Anony: Mkuu unajua yule aliyekuwa anajadili Abood TV ni Davie Kitururu kaka yangu na sio . Tumefanana lakini mpaka nahisi akiiba mie naweza kushikwa!:-)

  ReplyDelete
 14. Sentesi Hapo juu haikuisha kumbe:-(

  Nilitaka kusema yule ni Davie Kitururu Kaka yangu na sio mie aliyekuwa anajadili maswala kwenye TV.

  ReplyDelete
 15. Uko sawa mkuu! Umenikumbusha...jina ni Davie Kitururu!!! Ila kwakweli MMEFANANA SANA! Nadhani hata kina "shemeji" wana kazi kubwa ya kujua "who is who!" lol! Kumbe inawezekana hata pale WAMO Morogoro nilimuona Davie??? Hapa nachanganyikiwa kwakweli!!!!

  ReplyDelete
 16. Suala la "watu kufanana" liliwahi kuvunja uchumba wa mabinti mapacha mahali flani! Jamaa alichanganyikiwa...leo anaongea na kumwaga mistari kwa huyu, kesho akikutana na mwingine anadhani ni yule aliyeongea naye jana! Mabinti nao wakawa "wanafanya kamchezo" ka kumchanganya kaka wa watu! Mwisho akaacha wote!!!! Kazi kwelikweli!

  ReplyDelete
 17. Nakumbuka jina la Simon Kitururu enzi zile za Mazengo High School pale Dodoma 1993 - 1995. Nadhani ndo wewe, nakukumbuka especially kwenye masuala ya mijadala mbalimbali (debate)

  ReplyDelete
 18. @Anony wa 7:43PM: Mambo ya kufanana wee acha tu yani! Unaweza kuingia mkenge usioujua kwa kufananishwa tu au kinyume chake pia.

  @Anony wa 8:29: Simon Kitururu wa Mazengo High school wa midahalo na mwenyekiti wa Bweni la MWENGE enzi hizo ndiye mimi umepatia.

  ReplyDelete
 19. HAHAHAHAAAAAAA! SIMON KITURURU!!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU