NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, December 4, 2010

FIKRA YA IJUMAA: KAMA TUNGEMSIKILIZA NA KUMWELEWA PROFESA MBELE !!!

Watoto wetu watasomea chini mpaka lini?
 • Wasifu wa Profesa Mbele utakapokuja kuandikwa bila shaka hautakosa kutaja mambo makuu matatu. Kwamba yeye ni: (1) Msomi aliyebobea ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuleta maelewano na utangamano wa tamaduni mbalimbali hapa duniani. (2) Mpiga mbiu aliyejaribu sana kuiamsha jamii ya Watanzania kutoka katika usingizi wake wa pono na kuanza kujisomea (3) Mwanaharakati makini ambaye alijaribu sana kuikumbusha jamii kuhusu kuacha tabia ya "vijiwe" na kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo badala ya kutegemea kila kitu kufanyiwa na serikali. Yeye anakerwa na jamii yenye matatizo sugu lakini haiwezi kujihamasisha ikajichimbia visima vya maji ya kunywa ikidai kwamba ni masikini sana na kwamba hiyo ni kazi ya serikali; na wakati huo huo inaweza kuchangishana na kukusanya mamilioni ya shilingi ili kufanya harusi za kifahari kupindukia au kuchangia kampeni za kisiasa. Yeye anakerwa na jamii inayogida bia kila siku na kutanua mijini katika starehe mzo mzo lakini haiwezi kujitutumua na kununua madawati ya watoto wake au kujijengea madarasa hasa huko vijijini ikisingizia umasikini na kwamba ni kazi ya serikali.
Mwenyewe Profesa Mbele
  • Leo nataka nigusie kidogo tu hili jambo la tatu ambalo naamini kuwa ni jambo la muhimu sana katika jamii yo yote ile ambayo kweli imedhamiria kujitatulia matatizo yake yenyewe.
  • Pengine baada ya kuishi Marekani kwa muda Profesa Mbele ameshauona moyo wa kujitolea na utayarifu wa kujisaidia katika kujitatulia matatizo walionao Wamarekani. Pamoja na utajiri wa nchi yao, Wamarekani wengi hawaitegemei serikali iwafanyie kila kitu. Wanajua kwamba serikali inaongozwa na wanasiasa na popote palipo na wanasiasa basi kuna ukiritimba na upotezaji mkubwa wa muda. Nitatoa mfano.
  • Kila mwanzo wa mwaka wa masomo shule nyingi za umma hapa Marekani huwataka wazazi kupeleka vitu muhimu ambavyo vitatumiwa na wanafunzi katika madarasa yao. Orodha hii inajumuisha vitu vya kawaida tu kama vile mabunda ya karatasi, gundi, kalamu za kuchorea, penseli, kalamu, mikasi, na vitu vingine vidogo vidogo. Unaweza kuitazama orodha hii hapa na hapa kwa mabinti zangu wa darasa la kwanza na darasa la nne. Japo siyo lazima kupeleka vitu hivi, wazazi wanajua umuhimu wake na wanaweza kujinyima raha zingine ili wahakikishe kwamba vifaa hivi vinapatikana na watoto wao wanasoma kwa raha. Wako tayari kujinyima kunywa bia ili kusaidia shule zao. Hata wazazi ambao ni masikini na hawana kazi hujitahidi sana kuhakikisha kwamba wanapeleka angalau vitu vichache katika orodha hii kwa ajili ya watoto wao. Na wazazi wenye uwezo zaidi wanaweza kujitolea na kuwasaidia wazazi wa watoto ambao hawana uwezo ili kununua vifaa hivi. Kwa hivyo siku ya kwanza ya masomo utawaona watoto wameambatana na wazazi wao wakiwa wamebeba vifurushi vya vifaa hivi, na watoto huona fahari kuona kwamba wazazi wao wanashiriki na kusaidia katika elimu yao. Na moyo huu wa kujisaidia na kutokaa tu kudeka na kusubiri serikali iwanunulie mpaka gundi hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ni utamaduni wao. Wao wanajua kwamba serikali, hata kama ingekuwa tajiri namna gani kamwe haiwezi kununua kila kitu na kutosheleza mahitaji ya wote. Ni kama vile walimsikiliza na kumwelewa rais wao mmoja mashuhuri aliyewaasa kwamba "usiulize nchi yako itakufanyia nini, bali jiulize nchi yako utaifanyia nini!"
   • Wiki jana kwa mfano mwalimu wa darasa la kwanza alituandikia barua wazazi akisema kwamba anahitaji ubao wa ziada darasani maalumu kwa ajili ya mazoezi ya kuchora. Ubao huu ni ghali na unagharimu dola 800 hivi. Ilichukua muda mfupi tu siku hiyo hiyo kwa wazazi wachache kuweza kuchangishana na kesho yake ubao ulienda kutafutwa, ukanunuliwa na kuwekwa darasani. Hawakukaa na kusubiri bajeti ya serikali ambako pengine wangeambiwa waandike barua ya kuomba pesa na kueleza ni kwa nini ubao mwingine unahitajika. Bila shaka hii ingechukua muda mrefu na hakuna uhakika kwamba ubao huo ungenunuliwa (kwa wakati). Na wazazi ambao hatukuwahi kuchanga ilitubidi kuwashukuru hawa wazazi waliojitolea kwa kuwanunulia zawadi ndogo ndogo tu na kuwatia moyo kwa kujitolea kwao. Ndivyo hivi wenzetu wanavyoendesha mambo yao. Wanaisubiri serikali katika mambo makubwa makubwa na yanayogharimu pesa nyingi.
   • Ni kweli sisi tu masikini sana, lakini, kama alivyouliza Profesa Mbele, kwa nini tunazo pesa za kufanyia harusi za kifahari ambazo hata wazungu wanazishangaa na kutumbua raha zingine lakini hatuna pesa za kuchimbia angalau kisima kimoja cha maji kijijini tutokako? Ni matatizo mangapi ambayo tungeweza kuyatatua bila kutegemea msaada wa serikali. Ni lazima kweli watoto wetu wakae chini huku tukikaa na kusubiri serikali na ufisadi wake? Unafikiri mafisadi wanawajali watoto wetu wanaosomea chini ya miti?
   Ni kweli hatuwezi kujichimbia visima vya maji?
    • Wapo watakaodai kwamba kujitolea hakuleti maana yo yote wakati pesa zinazotafunwa na mafisadi zingetosha kutatulia matatizo yetu mengi. Japo hii ni kweli lakini ukweli ni kwamba mafisadi hawa hawajali kama watoto wetu wanasomea chini ya miti ama la; na inavyoonekana hatujapata dawa sahihi ya kupambana na mafisadi na ufisadi wao. Tukikaa tu na kuendelea kulalamika na kutumbua starehe wakati watoto wetu wakisomea chini ya miti, mafisadi hawa wanaendelea kufurahi kwani wanajua kwamba kizazi kingine kinaangamia katika elimu duni na hivyo kudumu katika utwana. Wakati tukiendelea kutafuta dawa muafaka ya kupambana na ufisadi na kubadili mfumo unaozalisha mafisadi, mfumo ambao pengine hautachanwachanwa leo jioni au kesho asubuhi, tunaweza kuanzisha mapambano kwa kuhakikisha kwamba tunajitatulia matatizo yetu wenyewe na hasa hili suala la elimu ya watoto wetu. Tukiisubiri serikali kwa hili tutaliwa!
    Ati mfumo wa kifisadi tutautokomeza lini?
      • Japo Watanzania wengi hatutaki kulisikia hili lakini Profesa Mbele alikuwa mtu wa kwanza kulivalia njuga tena kwa hoja nzuri na japo alishambuliwa sana, huko mbele ya safari naamini kwamba watu wengi walio makini wataweza kukiri kwamba yeye aliona mbele zaidi yetu na pengine ni wakati mzuri sasa tukamsikiliza na kumwelewa. Hizi harusi za kifahari na starehe hizi zisizo na mwisho hazitatuletea ukombozi wa kijamii na kukaa tukilalamikia serikali (inayohangaika na ufisadi wake) na kusubiri ije itufanyie kila kitu haiwezekani. Ufisadi utaisha lini ndipo watoto wetu wawe na madawati? Tutasubiri mpaka lini ili vijiji vyetu viwe na visima vya maji ya kunywa? Tutasubiri serikali mpaka lini?
      • Wakati sasa umefika wa kumsikiliza na kumwelewa Profesa Mbele, na hasa katika suala la elimu ya watoto wetu, watoto wa wakulima na wafanyakazi!
      *********
       Angalizo: Nilikosea masaa "nilipoutegesha" ujumbe huu. Ulipaswa kutoka leo Ijumaa saa tatu asubuhi. Kumbe nikawa nimechanganya PM na AM. Nimeshangaa nilipoangalia blogu na kukuta haujajichapisha. Ndipo nikagundua kosa langu. Ni saa tatu PM sasa hapa Marekani na nauchapisha ukiwa umechelewa kidogo tu. Tuwemo!
      **********

       6 comments:

       1. Naafiki ulilosema Mkuu! Nguli Mbele ni Kichwa!

        ReplyDelete
       2. Well said.
        Labda nawe UTAKUMBUKWA KWA KUKUMBUKA KUTUKUMBUSHA JUU YA KUMBUKUMU ZA WASIOKUMBUKWA.
        Duh!!!!!
        Najivunia uwepo wenu nyote ma-Profesa. Mnaojishusha kutuelewesha kina sisi na kujumuika nasi
        BARAKA KWENU

        ReplyDelete
       3. Hakika leo umesema ule ukweli kabisa. Na hii ningependa wengi wajue maana ni ukweli halisi kabisa. Wote waTanzania tungekuwa tumefunguka na kuiga mifano kama hii HAKIKA tungekuwa mbali sana lakini tunakaa tu na kusubiri.

        ReplyDelete
       4. Mtakatifu - nakubaliana nawe kwa asilimia 100!

        Mzee wa Changamoto - pengine mimi nitakuwa mmoja ya wale wasiokumbukwa isipokuwa tu kwa wanablogu wenzangu makini kama wewe! Wakati nilipokuwa nikiyasoma maoni yako, nilikuwa nasoma kijigazeti chetu hapa kijijini na sehemu ya matangazo ya vifo kimetanguliza kwanza "notable deaths" na baadaye sasa vifo vya kapuku ambao hawakuwa "notable". Unaambiwa ni matabaka mpaka kwenye kifo, na watu wanahangaika kufanya kila wawezalo ili nao siku yao ikifika basi angalau wakumbukwe na majina yao yaweze kuchapishwa ule upande wa "notable deaths"

        Kuhusu kujumuika nanyi - kwani sisi ni akina nani mkuu? Ni "notable" ama? Wengine wetu ukikutana nasi tukichunga ng'ombe vijijini Usukumani huku tukipiga zeze na kuimba nyimbo za kilugha hata waweza kututemea mate. Tuko pamoja!

        Dada Yasinta: Profesa amekuwa akilisema hili kwa muda mrefu sasa na ingawa anabezwa tu, naamibi hata hao watu wanaojaribu kumbeza huku wakisingizia umasikini na ufisadi, ndani kabisa mioyoni wanajua kwamba hili ni jambo la msingi sana katika jamii yoyote inayojibidisha ili kujiletea maendeleo.

        ReplyDelete
       5. Shukrani kwa Mwalimu Matondo kwa kunikumbusha yote hayo. Amini usiamini, wakati mwingi nasahau niliandika nini na wapi katika hizi blogu.

        Nikiwaongelea hao akina "Anonymous" wanaonibeza kwenye hizi blogu, naona wanajisumbua. Kadiri siku zinavyoenda, watajionea wenyewe. Mimi natekeleza wajibu niliouelezea, ambao sikupewa na wanadamu.

        ReplyDelete
       6. Wapendwa;

        Asanteni mno. Kabisa tunaweza kujitatulia matatizo yetu ya msingi kama tukiamua; na huu ni mchango mkubwa sana wa Prof. Mbele.

        Mzee wa Changamoto. Pengine kila mmoja wetu atakumbukwa kwa namna moja ama nyingine ingawa sina uhakika kama kuna faida yo yote isipokuwa kwa wale waliojivika majukumu ya kuwa "akina Musa" wetu.

        Wapo watu ambao wako tayari kufanya lolote - jema au baya ili tu waweze kuandika historia na waweze kukumbukwa. Na sikujua kama wakumbushaji nao watakumbukwa.

        ReplyDelete

       JIANDIKISHE HAPA

       Enter your email address:

       Delivered by FeedBurner

       VITAMBULISHO VYETU