NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, December 23, 2010

HII HISTORIA YA NOTI ZETU INAELIMISHA

Historia ya Noti Tanzania Kuanzia 1905 Mpaka sasa

Na Fredy Azzah
Wednesday, 22 December 2010

JK akikabidhiwa noti mpya na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Ndulu. Picha kutoka kwa Kamanda wa Matukio.
**********

TANGU mwaka 1884 fedha zilizotumika Tanganyika zilikuwa ni sarafu, noti zilianza kutumika mwaka 1905 wakati wa utawala wa Mjerumani. Noti hizo zilitolewa katika thamani ya Rupie tano, 10, 50, 100 na 500. Zanzibar mwaka huohuo wa 1905, noti za Rupie za Zanzibar zilitolewa katika thamani za Rupie tano, 10, 20, 50, 100 na 500.

Mbali na rupia iliyodumu kwa muda mrefu katika matumizi ya noti nchini, tangu kupatikana uhuru, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikibadilisha noti zake kutokana na sababu mbalimbali.

Ikiwemo sheria inayoiruhusu kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitano mpaka saba. Kutokana na mamlaka hayo BoT, kuanzia mwaka 1966 imefanya mabadiliko kadhaa ya sura za noti zake pamoja na alama za kiusalama.

Pia kutokana na kupanda na kushuka kwa thamani ya shilingi, BoT imekuwa ikitoa noti zenye thamani tofauti tofauti (denomination),  kuanzia ile ya Sh10 mpaka sasa ambapo noti yenye thamani ndogo ni Sh500 huku kubwa ikiwa ya Sh10,000.

Katika historia ya mabadiliko ya noti, mwanzo kabisa ilikuwa ni mwaka 1966 ambayo yalihusu noti ya Sh20 iliyokuwa na sura ya Rais wa Kwanza wa Tanzania na Sh100 'Mmasai' pamoja na nyingine iliyokuwa na simba. Ilipofika mwaka 1978, benki hiyo ilitoa tena noti za Sh10 na Sh20.

Mabadiliko mengine katika sura ya noti yalifanyika miaka ya 1985, 1987, 1989, 1990 kwa kuwa na noti ya Sh50 ambayo ilikuwa na sura ya Rais wa Pili Ali Hasani Mwinyi, pundamilia na picha nyingine zilizokuwa zikiashiria mavuno.

Noti ya Sh1,000 yenye sura ya Rais Mwinyi na tembo iliingia mwaka 1993 na mwaka 1995 ilingia noti ya Sh10,000 yenye sura ya Rais Mwinyi na simba.

Mwaka 2000 kuliingizwa noti ya Sh1,000 ikiwa na sura ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, tembo na mgodi wa makaa ya mawe, wakati mwaka 2003 ilikuja noti ya Sh 500 ikiwa na picha ya nyati, jengo la Nkurumah lililopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na nyoka.

Mwaka huo huo iliingia noti ya Sh5,000 ikiwa na faru na mgodi na noti ya Sh10,000 ikiwa na jengo la benki na tembo.
Kimsingi mpaka sasa BoT imefanya mabadiliko makubwa ya sura za fedha za Tanzania mara saba, mabadiliko yaliyohusisha rangi, alama (picha) na alama za usalama wa fedha hizo.

Mbali na mabadiliko hayo, Desemba 17 mwaka huu BoT ilizindua noti mpya ambazo zitaanza kutumika rasmi kwenye mzunguko wa fedha wiki ya kwanza ya Januari mwaka 2011.

Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu anasema noti hizo mpya zitakuwa na mabadiliko mbalimbali ikiwemo rangi na alama za utambulisho ambazo sasa zitakuwa na sura za waasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

“Katika noti za sasa, kutakuwa na saini Gavana aliyepo pamoja na Waziri wa Fedha aliyepo madarakani,” anasema Profesa. Mabadiliko ya safari hii yamezihusha noti zote na Profesa Ndulu anasema tofauti na za awali, noti za sasa zina alama mpya tatu, zitakazolinda usalama wake dhidi ya watu wanaoghushi ambao anasema uwezo wao unakuwa kila siku kutokana na kukua kwa teknolojia.

Rais akizikagua noti hizo mpya.

Anasema alama zilizowekwa ni pamoja na ile iliyojificha ya picha ya Mwalimu Nyerere inayochukua nafasi ya twiga katika noti za viwango vyote. Alama nyingine mpya kabisa katika teknolojia ya utengenezaji fedha ni ile ambayo inaonekana kama inatembeatembea wakati noti inapokuwa ikigeuzwa na nyingine ambayo inabadilika au kugeuka rangi.

 

Kadhalika, anasema mbali na kupunguzwa ukubwa, noti hizo zitatambuliwa kirahisi na walemavu wa macho kutokana na alama maalumu zilizowekwa kwa ajili yao katika kila kiwango. 

Alama hizo ni pamoja na mistari iliyovimba, pamoja na ile ya V ambazo zimewekwa kwa idadi maalumu inayoelezea kila kiwango cha noti husika.Mabadiliko mengine yamefanywa katika picha za wanyama simba, nyati pamoja na tembo ambao awali, picha zao zilikuwa zikionyesha miili yao yote, katika noti mpya ni picha za vichwa vyao tu zitakazoonekana.

Kitu kingine kinachozitofautisha noti hizo mpya na zile za zamani ni karatasi zilizotumika kuzitengenezea. Anasema noti hizo mpya zimetengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100 tofauti na noti zilizopo kwenye mzunguko ambazo karatasi zake zinatokana na mbao.

“Kampuni inayochapisha noti zetu, ndiyo pia inayochapisha baadhi ya denomination (noti) ya Marekani, kwa hiyo karatasi zinazotumika kutengeneza dola ya Marekani ndizo hizo hizo zitakazotengeneza fedha zetu,” anasema Profesa Ndulu.

Kwa mujubu wa Profesa Ndulu, mchakato wa kubadilisha noti ulianza Aprili mwaka 2009 na mchakato wa zabuni uliendeshwa na hatimaye makampuni kumi na moja kujitokeza ingawa tisa ndiyo yaliyoingia katika ushindani.

Kampuni ya Crane AB ya Sweden ilishinda kutengeneza noti za Sh500, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 huku kampuni ya Adae La Rue ya Uingereza ikishinda zabuni ya kutengeneza noti za Sh1,000.

Gavana Ndulu anasema gharama ya uchapishaji vipande 1,000 imeshuka ikilinganishwa na wakati ambao Tanzania ilikuwa ikichapa noti zake katika kampuni ya Giesecke & Devrint ya Ujerumani... “Kama mwanzo tulikuwa tukichapisha vipande 1,000 kwa Sh10, sasa tunachapisha kwa Sh saba,” anasema Profesa Ndulu. Anasema kupungua kwa gharama hizo kunatokana na ushindani katika kupambanisha wazabuni.

Anasema kwa kawaida wastani wa noti yoyote kuishi katika mzunguko ni miezi saba na kuwa kutokana na ubora wa noti mpya,  zitaweza kuishi kwa muda huo ili kuipunguzia benki gharama ya kuchapisha fedha mara kwa mara kutokana na uchakavu.

Licha ya madai ya kushuka kwa uchumi hivyo kupungua kwa thamani ya shilingi, Profesa Ndulu anasema BoT haina mpango wa kuchapisha noti yenye thamani zaidi ya Sh10,000 inayotumika sasa.
“Labda mpaka shilingi yetu ifikie pabaya sana, lakini kwa sasa tutaendelea kutumia hizi hizi zilizopo,” anasema Profesa Ndulu.

Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Crane AB Peter Brown, anasema alama za usalama ambazo zimetumika katika utengenezaji wa noti hizo ni teknolojia mpya kabisa ambayo haijawahi kutumiwa na nchi yoyote ya Afrika. Anasema alama hizo ni hatimiliki ya kampuni hiyo ambayo ilitumia miaka mitatu kuzitengeneza.

“Kutokana na teknolojia iliyotumika kutengeneza alama za usalama za noti hizo, si rahisi mtu yeyote kuzigushi,” anasema Brown.

Pia anasema kutokana na kukua kwa tekinolojia, ni vyema nchi zikawa na utaratibu wa kubadilisha noti zake kila baada ya muda unaoshauriwa kisheria ili kupambana na wimbi la watu waogushi.

Anasema kampuni yake inachapisha dola 100 ya Marekani na kuwa  teknolojia inayotumika kutengeneza fedha hiyo yenye soko kubwa duniani ndiyo inayotumika pia kutengeneza noti za Tanzania ambazo zinatatengenezwa na kampuni hiyo

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU