NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, December 21, 2010

HOSEA AKANUSHA UVUMI WA WIKILEAKS

Hii Wikileaks kweli italeta "mtafaruku" duniani. Na bado tutasikia mengi. "Uzuri" ni kwamba hakuna anayejali.

************

Hosea Akanusha Uvumi wa Wikileaks

Na Mwandishi Wetu 
(Tarehe: 20th December 2010)


TAARIFA zilizovuja za mtandao wa Wikileaks, ambazo zilitoka kwa Serikali ya Marekani, zimemgusa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, na kwa haraka, amekanusha kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa ni kikwazo cha utendaji wa taasisi hiyo, kama alivyonukuliwa humo.

Dk. Hoseah, anadai katika taarifa za mtandao huo zilizoripotiwa jana na gazeti la The Guardian la Uingereza kueleza kuwa Rais Kikwete alikuwa anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, na pia madai kuwa anahofia maisha yake kama Mkuu wa Takukuru.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Dk. Hoseah anakiri kukutana na ofisa wa Marekani ofisini kwake Julai 2007, lakini katika mazungumzo yake, anakanusha kuwa hakuna mahali popote alipoeleza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.

“Nilichosema ni kwamba Rais hataki kuruhusu uchunguzi wa maofisa waandamizi wa serikali au mtu yeyote yule kufanywa kwa kuegemea katika minong’ono au ushahidi dhaifu, kwa sababu kwa kufanya hivyo, serikali inaweza kuwa katika hatari ya kulipa fidia kubwa kama watuhumiwa watashinda kesi mahakamani,” alidai Dk. Hoseah katika taarifa yake jana.

Kuhusu madai ya ‘hofu ya maisha yake’, alisema anakumbuka kuulizwa na ofisa huyo kama anahofia uhai wake au la, akiwa ni Mkuu wa Takukuru, na kwamba jibu lake lilikuwa rahisi, “ndio, wakati unaposhughulika na vigogo au matajiri, ni lazima uwe mwangalifu na tahadhari na maisha yako.”

“Lakini hakuna mahali popote nilipotamka kuwa nina mpango wa kukimbia nchi kwa sababu maisha yangu yalikuwa hatarini. Ni jambo la kushangaza kwa mara nyingine, Ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani amenikariri kinyume na ukweli na sijui nia yake hasa ilikuwa nini.”

Dk. Hoseah alisema kupokea vitisho ni sehemu ya kazi yake kwa sababu anawachunguza watu matajiri na wenye nguvu, lakini kwa kuwa kila kitu kinafanyika kulingana na sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, “hakuna cha kuhofia sana kwa sababu kila kitu kiko katika sheria.”

Aliihakikishia jamii kwamba ingawa kazi yao ni ngumu, wataendelea na dhamira yao ya kupambana na rushwa katika ngazi zote kwa kushirikiana na wadau wote nchini.

“Tunaamini kwa pamoja tutashinda vita hii, lakini tukigawanyika, itakuwa kazi ngumu kufikia dhamira yetu.”

Chanzo: Habari Leo. Pia gazeti la Uhuru.

4 comments:

  1. Asipokanusha KIBARUA kinaweza kuota majani!:-(

    ReplyDelete
  2. Tindo Mhando was used and abused. Jamaa yaani hawana hata huruma duh! Kile kipindi kimoja tu cha kurusha midahalo ya wagombea kimemponza pamoja na kwamba ni wazi TBC ilikuwa inapendelea CCM. Sasa ni mali ya taifa na sijui wanataka iendeshwaje. Bongo yenye watu wasio na Bongo!!!

    ReplyDelete
  3. Hosea ameishachafuka anapaswa kujiuzulu. Amekanusha ndiyo. Kwanini balozi aseme hayo na si mengine? Angekuwa mtu mwema angajiuzulu kabla hajachafuka zaidi. Hali ilivyo kuna ukweli zaidi ya asilimia 90 kwenye yaliyodaiwa. Hosea asiumizwe na njaa. Kama hali ndiyo hiyo kuendelea kuwa kazini ni kuzidi kujichafua zaidi ingawa aliishachafuka zamani.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU