NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, December 11, 2010

JK AWATAKA WASOMI KUANDIKA VITABU (VYA MAISHA YA VIONGOZI WA KITAIFA)

JK awataka wasomi kuandika vitabu

Na Yassin Kayombo

(9/12/2010)

RAIS Jakaya Kikwete, ametoa mwito kwa wasomi kuandika vitabu vya historia ya maisha ya viongozi wa kitaifa ili kuhifadhi historia ya nchi. Alitoa mwito huo jana, Ikulu, Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachoelezea maisha yake kilichoandikwa na Profesa Julius Nyang'oro. Kitabu hicho chenye wasifu wa Rais ni cha pili kuandikwa nchini, cha kwanza kiliandikwa mwaka 1971 kuhusu maisha ya Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere. Kwa mujibu wa Profesa Nyang'oro, msambazaji pekee wa kitabu hicho atakuwa duka la vitabu la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika kitabu hicho, mwandishi Profesa Nyang'oro ameelezea maisha ya Rais Kikwete akiwa mtoto mdogo, elimu, mwanajeshi, mwanasiasa, waziri na hatimaye rais. Rais alisema wasomi wanapaswa kulisaidia taifa kwa kuandika vitabu vinavyozungumzia maisha ya viongozi wa kitaifa kwa ajili ya historia ya kizazi kilichopo na kijacho. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, maprofesa na waandishi wa habari, Rais aliwahimiza wananchi kujenga mazoea ya kusoma vitabu vikiwemo vya maisha ya viongozi. Rais alisema viongozi wengi wakiwemo marais wastaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa hawajaandikiwa vitabu kuhusu maisha yao. Kutoandikwa vitabu vinavyozungumzia maisha ya viongozi wetu wa kitaifa ni kuua historia ya viongozi hao na ya taifa kwa jumla, hivyo wenye uwezo wa kuandika andikeni, alisisitiza Rais.

Chanzo: Uhuru
 
*****************

Angalizo Langu

Huu ni wito mzuri na ni kweli kuandika vitabu vya viongozi wetu wa kitaifa ni jambo la muhimu katika kuwaenzi pamoja na kuhifadhi historia ya taifa letu. Lakini vipi kuhusu viongozi hawa kuanza kwa kuandika vitabu hivi wao wenyewe ili tuwasikie wakijieleza hasa kuhusu mafanikio yao na pale ambapo wanakiri kushindwa. Tumezoea hapa Marekani kuona kwamba kitu cha kwanza anachofanya rais baada ya kumaliza muda wake ni kuandika kitabu kuhusu utawala wake - mafanikio, matatizo na pale aliposhindwa. 

Rais Bush (II), kwa mfano, imemchukua miaka miwili tu tangu atoke madarakani na tayari ameshaandika na kutoa kitabu chake cha Decision Points ambacho kimesifiwa sana kwamba ameweza kujieleza vizuri kuhusu maamuzi yake tata mbalimbali kama vile uamuzi wa kuivamia Iraq, kushindwa kwake kuwasaidia wakazi wa New Orleans wakati wa kimbunga cha Katrina, kilichotokea siku ya mashambulizi ya Septemba 11, mambo anayoyajutia na mambo mengine ya muhimu katika utawala wake. Na kutokana na kitabu hiki na jinsi alivyojieleza, tayari umaarufu wake umeanza kupanda. Kwa nini kiongozi makini na msomi kama Mkapa asiandike kitabu juu ya maisha yake na utawala wake? Ni vizuri viongozi wetu wakianza kuandika wenyewe ili tuwasikie kwa sauti yao wakitueleza walikotoka, misukosuko waliyopitia na hasa walichowatendea Watanzania wakati wa utawala wao.

Akiwa msomi na mwanafalsafa makini, Baba wa Taifa alikuwa na tabia ya kuandika vitabu ili kueleza mawazo yake na falsafa zake mbalimbali. Tatizo ni kwamba baadhi ya maandiko yake ni shida sana kuyapata. Hata hotuba zake mbalimbali zinakumbwa na ukiritimba na ni vigumu kuzipata pia. Kwa nini inakuwa hivi? Kuna uhakika gani kwamba vitabu vya viongozi wengine wa kitaifa vitaweza kupatikana kwa urahisi na kusomwa na Watanzania? Vipi kuhusu wazo la kuwa na maktaba maalumu kwa ajili ya kumbukumbu zote za viongozi wetu wa kitaifa?

Binafsi rais Mkapa ni kiongozi anayenivutia sana na ningependa kuandika historia yake siku moja!

6 comments:

 1. Jamani maendeleo ni mazuri. Tumetoka mbali. Asante Mungu kwa maendeleo haya ya nchi yetu na watu wetu.

  ReplyDelete
 2. Nasi tuwatake watawala wa kiafrika kuandika vitabu ili watawaliwa wajue wanachofikiri na kutenda. Hata hivyo, napingana kidogo na rais Kikwete. Tunahitaji vitabu vya kiada na mambo mengine muhimu kuliko vya miungu watu waitwao watawala.

  Je kwa sasa nchi yetu inahitaji vitabu vya hadithi za wafalme wetu au mapambano dhidi ya kadhia zinazolikumba taifa kama vile ufisadi, uvivu, ujinga, wizi, siasa za majaribio na mengine? Je hawa maprofesa wanaopata muda wa kuandika hadithi za watu binafsi wenye utukufu wametimiza wajibu wao ikizingatiwa kuwa hawaonyeshi kufanya hivyo kwa mahitaji ya jamii pana. Nieleweke. Simaanishi maprofesa wote wako hivi kama huyu aliyejikunja kuandika kitabu juu ya mtu badala ya watu. Je yawezekana juhudi hii ikawa kipaumbele kilichokosewa au kutaka kuwa karibu na mtungi wa neema?

  ReplyDelete
 3. Wazo zuri sana Mwalimu. Pindi utakapoanza projekti ya kuandika wasifu wa Mkapa, nitakuomba pamoja na mengine mengi umwombe atumegee juu ya (1) uamuzi wake wa kuuza (kama sio kugawa) nyumba za serikali (na yeye akiwa ni mmojawapo ya walionufaika na mpango huo), (2) ukwapuaji na urejeshaji wa mgodi wa Kiwira, na (3)alivyoratibu ukwapuaji wa EPA.

  ReplyDelete
 4. Wasifu wa viongozi upo hata kwenye wikipedia, hivyo hatuhitaji kuwa na vitabu vinavyoongelea viongozi wa kawaida. Tunahitaji biography ya mtu muhimu kama Nyerere aliyefanyia mengi Tanzania na Africa kwa jumla. Binafsi sihitaji biography za marais wengine zaidi ya Nyerere.

  ReplyDelete
 5. Tutahitaji vitabu vitakavyongelea mafanikio na mapungufu ya uongozi na utawala wao na si vinginevyo. VIONGOZI WAACHE TABIA YA KUPENDA SIFA NA KUTUKUZWA HATA BILA STAHILI

  ReplyDelete
 6. Anony wa December 12, 2010 6:44 PM:

  Nijuavyo mimi, kama unaandika wasifu wa kiongozi aliye hai, kiongozi mwenyewe anaweza akaamua ni maswala yapi anataka yazungumziwe katika kitabu chake. Kama atataka kuyazungumzia hayo mambo uliyoyataja na kuweka mambo sawa sawa ni sawa pia. Lakini pia unaweza kuandika hizi zinazoitwa "unauthorized biography" na ukazungumzia hata mambo ambayo mlengwa hataki yazungumziwe.

  Nilikuwa nakisoma hiki kitabu kipya cha Bush ambacho amekiandika yeye mwenyewe na amejibu karibu maswali yote tete ambayo yalikuwa yakiulizwa: kwa nini aliamua kuanzisha vita vya Irak, Uzembe wake katika kuwasaidia watu wa New Orleans wakati wa kimbunga cha Katrina; na mengineyo. Unaweza kuona ni kama vile anajitetea mbele ya Historia. Niko siriazi na mradi huu na hivi karibuni nitaanza kutafuta jinsi ninavyoweza kuwasiliana na Mh. Mkapa.

  @Matiya na Mhango: Siyo kosa kuandika vitabu vya viongozi hawa kwani kama vitaandikwa vizuri na kuelezea ukweli huku vikikwepa ushabiki (wa kisiasa) vinayo nafasi nzuri ya kutuhabarisha jinsi walivyoongoza, mitazamo na falsafa zao na michango yao katika jamii yetu.

  Kuandika vitabu vya kiada ni jambo la muhimu lakini kama visipokubaliwa kutumiwa mashuleni nani atavisoma? Una mtu wewe wa "kukupigia debe" mpaka kitabu chako kikubalike na kuingizwa katika mitaala na hatimaye kutumiwa mashuleni? Haina maana mtu unajikunja na unaandika kitabu kizuri halafu hakuna anayejali. Hili ni tatizo ambalo inabidi liangaliwe na vitabu vizuri vinavyopaswa kusomwa na wanafunzi vichaguliwe bila upendeleo.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU