Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Wednesday, December 1, 2010

KWA NINI NI VIGUMU SANA KUPATA "A" KATIKA VYUO VYETU? TUNAWAHUJUMU WANAFUNZI WETU ???

Matokeo ya Mwaka wa nne Mlimani

1. Kwa shahada ya kwanza pale Mlimani gredi zenyewe zimekaa hivi (kama hazijabadilika)

A: 75-100, B+: 70-74, B: 60-69, C: 50-59, D: 45-49 na E: 0-44

2. Gredi za hapa Marekani (kutoka katika silabasi yangu katika darasa la Language and African Society) zimekaa hivi:

A: 93-100, A-: 90-92, B+: 87-89, B: 83-86, B-: 80-82, C+: 77-79, C: 73-76, C-: 70-72, D+: 67-69, D: 63-66, D-: 60-62, E: 0– 59.

Japo profesa unaweza kujipendekezea gredi zako mwenyewe, mfumo huu wa alama ndio umependekezwa na chuo kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza.

3. Hali ilivyo kule nyumbani (kama bado haijabadilika)
 • Utakuta darasa lina wanafunzi 100, na kati ya wanafunzi hawa pengine wawili, watatu na hata mmoja tu ndiyo atapata "A". Hata madarasa makubwa yenye wanafunzi 300, eti wanafunzi wanne au watano tu ndiyo wanapata "A". Kwa nini? Ni kwa sababu masomo ni magumu sana? Wanafunzi hawajisomei sawasawa (Na kama hawajisomei ni kwa nini?), maprofesa hawafundishi vizuri kiasi kwamba wanafunzi hawawaelewi? Au maprofesa wanatunga mitihani migumu kupindukia? Au pengine wanafunzi wa vyuo vikuu vyetu ni mbumbumbu na hawana uwezo wa kupata A?
 •  Ninacholalamikia hapa siyo kila mwanafunzi kupata A bali ule ugumu uliopo wa kupata alama hizi kwani siamini kama kweli eti katika darasa la wanafunzi 300, ni wanafunzi watatu au wanne tu ndiyo wana uwezo wa kufaulu vizuri. Kama hivi ni kweli basi ni wazi kuna tatizo kubwa katika mfumo wetu wa elimu. 
4. Hali ilivyo hapa Marekani
 • Hapa kupata A ni jambo la kawaida na maprofesa na wanafunzi wanalijua hili. Mahusiano kati ya wanafunzi na maprofesa ni ya wazi na wanafunzi wanaweza kuuliza maswali na kujadili masuala ya gredi watakazozipata na maprofesa wao kwa uwazi. Hali hii inasababisha matatizo fulani na haya nitayaongelea siku nyingine.
 • Kwa wanafunzi wanaotegemea kuendelea na shahada za uzamili na uzamivu ni lazima wahakikishe kwamba wanapata A kwa sababu ushindani wa kupata ufadhili ni mkubwa sana na vyuo vingi vinataka wanafunzi ambao ni bora kabisa. Kwa ujumla alama za B, na hata B+ na pengine A- hazimsaidii sana mwanafunzi kuweza kujiunga na vyuo vikuu vyenye hadhi kama Harvard, Yale, Columbia, UCLA, Stanford, Berkeley na vinginevyo
5. Uzoefu Wangu
 • Nina uzoefu na uteuzi wa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu hapa Marekani na huwa nashangaa sana kugundua kwamba kwa kawaida waombaji kutoka Afrika huwa na alama za chini sana hasa ikilinganishwa na waombaji kutoka sehemu zingine duniani kama China, Korea, Ulaya, Amerika ya Kusini na hata nchi za Uarabuni. Maprofesa hapa huwa wanajiuliza inawezekanaje mwanafunzi mwenye azma na ari ya kujisomea ashindwe kupata A (75) ambayo hapa ni C? Na kama hakuna profesa wa kuwafahamisha wanakamati wenzie wanaofanya uteuzi kuhusu mambo yalivyo, mara nyingi maombi ya wanafunzi kutoka Afrika huwa hafifu sana na huishia kutupiliwa mbali. Ndiyo maana nahoji hapa kwamba pengine tunawahujumu vijana wetu kwa kuwapa alama za chini na kuishia kuwakosesha ufadhili ambao ungewawezesha kusomeshwa bure. Na sijui mfumo huu unamsaidia nani.
6. Ilivyokuwa Kwangu
 • Mwaka 1997 nilipata nafasi ya ufadhili wa kusoma shahada za uzamili na uzamivu katika Idara ya Isimu pale UCLA ambapo pia nilitakiwa kufanya kazi kama mwalimu msaidizi wa Kiswahili. Barua ya mwanzo niliyopata ilikuwa na masharti mawili yaliyonichanganya na kuninyima usingizi. Sharti la kwanza lilisema kwamba ilikuwa ni lazima nipate "first class" katika shahada yangu ya kwanza na la pili ni kufanya mtihani korofi wa GRE.
 • Sharti la kwanza liliwashtua watu wengi sana na niliambiwa kwamba kwa muda mrefu kulikuwa hakujawa na mtu aliyepata hiyo "first class". Niliambiwa kwamba pengine hawa jamaa wa UCLA walikuwa hawataki niende na niliambiwa kuachana nao kwani walichokuwa wananiomba kufanya kilikuwa hakiwezekani. Kilichonishangaza ni kwamba kulingana na matokeo yangu ya miaka mitatu iliyopita, ningeweza kupata hiyo first class kama ningepata angalau A nne tu katika mitihani yangu ya mwisho ya mwaka wa nne. Na kupata A nne katika masomo 10 niliyokuwa nikisoma eti ilikuwa haiwezekani. Sikukubali!
7. Nilichokifanya na Matokeo Yake
 • Sijawahi kusoma kwa nguvu zaidi, ari zaidi na kasi zaidi kama katika kipindi kile katika maisha yangu yote mpaka nikapachikwa majina ya "Librarian", mkazi wa "Special Reserve", "Aliyetumwa na kijiji" na mengineyo. Sikujali!
 • Matokeo ya mwaka wa nne yalipotoka nilikuwa nimepata A tisa, B+ moja na B moja. Nilikuwa nimeipata hiyo "first class!" tena nzuri. Haraka haraka niliyatuma matokeo hayo UCLA na msimamizi wangu (ambaye anafahamu ugumu wa kupata first class) alifurahishwa sana kiasi kwamba aliiomba kamati ya ufadhili kufuta sharti la mimi kufanya mtihani wa GRE. Habari hizi kuhusu GRE hata hivyo zilikuwa zimechelewa kwani tayari nilikuwa nimeshaanza maandalizi na nilikuwa nimeshalipia ada (dola 120). Niliufanya mtihani huu ili kujipima nguvu tu lakini first class tayari ilikuwa imesharekebisha mambo. Na hivi ndivyo nilivyoweza kusomeshwa UCLA kwa miaka sita (mitatu shahada ya uzamili na mitatu shahada ya uzamivu) huku nikilipiwa karibu dola 30,000 kwa mwaka.
Risti ya malipo ya GRE
 • Ati, kwa nini ni vigumu sana kupata A na hatimaye "first class" katika vyuo vikuu vyetu? Tatizo hasa ni nini? Ni mfumo wa elimu tuliorithi kutoka kwa Waingereza? Pengine inabidi tulifikirie jambo hili kwani inawezekana tukawa tunawahujumu wanafunzi wetu kwa kuwapotezea nafasi za ufadhili katika mashirika mbalimbali vikiwemo vyuo vikuu, jambo ambalo si jema hasa katika kipindi hiki ambapo kusema kweli mambo yako wazi sana kuhusu masuala ya ufadhili wa kimataifa.

12 comments:

 1. Nilipoisoma hii mada yako mwalimu nilikumbuka siku ya kwanza nilipojiunga na chuo cha IDM Mzumbe, tulipoingia darasani, aliingia mwalimu wa `COST' na sio yeye tu hata wa MATH, na wamasomo mengine, nafikiri math ilikuwa haiitwi math...mnisamehe kidogo kwa hilo!
  'Duuuh, hewa nzito kabisa humu ndani...' akasema huyo mwalimu
  Sisi wanafunzi tukashangaa, kwani hali ilkuwa safi na ukumbi ulikuwa na upepo wa asili kwani madirisha ni makubwa ya kutosha, ...yeye hakujali kushangaa kwetu akapita hadi mwisho wa ukumbi ule , au tuuite darasa.
  'Hivi mimi nitafundishaje watu wote hawa, mmmh, natumai ikifika mwisho wa semister hii nitakuwaa nimebakiwa na robo ya darasa...na mwisho wa semister nyingine, sana sana nitakuwa na watu kumi tano katika somo langu. Sijawahi kubakia na watu zaidi ya hao...' akashika chaki na kuanza kuandika somo la siku hiyo, na mwisho wa somo akatoa zinga la quiz, akasema
  `Maksi tano.' ikiwa na maana katika mitihani ya mwisho, hiyo quiz inabeba maksi tano...
  Hakuna hata mmoja aliyepata tatu, katika quiz ile...
  Ninachotaka kusema, ni kuwa wakati mwingine wanaochangia kufeli pia ni walimu wenyewe, hawafurahii wakufunzi, au wanafunzi wao kufaulu sijui, na sifa kwao ni kuonekana somo lake ni gumu sana.
  Nakumbuka katika kipindi chetu hicho alikuwepo mwalimu mmoja mwenye asili ya Kihindi, yeye alipoingia alisema `somo langu, wote huwa wanafulu, na nitasikitika sana nikikuona wewe umefeli katika somo langu...kwasababu nitajiona sijui kufundisha..'
  Sasa kwa mtizamo huo utaona nini, kinachochangia kufeli, sio tu `utaratibu mbaya' bali `ufundishaji usio na malengo mema'
  Wengine walifikia kusema, ngozi yetu inachangia...hapa sitasema zaidi, kwani mwalimu Matondo atanisuta...
  lakini ukifeli utatafuta `mchawi' ni nani!
  Ni hayo tu mwalimu

  ReplyDelete
 2. ahsante sana kaka Matondo na M3 kwa kuleta changamoto kubwa sana

  ReplyDelete
 3. Asante kwa mada hii Matondo.Bologna grading system yenye kutumia percentile on grading would have been a solution lakini pia mfumo huo una mapungufu yake ambayo mimi sikuyafurahia during my MSc degree.Russia na baadhi ya nchi za Ulaya wanatumia mfumo huu.

  ReplyDelete
 4. Usemayo ni kweli. Maswali yako yanahitaji majibu ingawa tunaweza kusema kuwa chanzo kikubwa cha kufeli na maanguko ya jumla ya nchi za kiafrika ni mtimanyongo.
  Nakumbuka nikiwa kwenye mtihani wa Criminal Procedure pale Mlimani kuna prof alininyang'anya Statutes kwa hofu kuwa nimefanya annotation. Hili lisingekuwa kosa kama siyo kuniambia: "nasikia ukiitwa profesa sasa tutaona uprof wako."
  Hii ilitokana na wenzangu kupenda kuniita prof kutokana na kuwasaidia waliokuwa wameshikwa wakafanya vizuri na kufuta sup zao.

  Kwenye mitihani ya sheria unaruhusiwa kuingia na vitu kama penal code, constitution na statutes mbali mbali. Hali ni mbaya kwetu. Jiulize ni wataalamu wangapi tunawanyima ajira na kuajiri ma-TX? ajabu wanasiasa nchini wanathaminiwa kuliko wanataaluma. Angalia wabunge wanavyolipwa kuliko walimu, madaktari, mainjinia na wengine ilhali wanawakilisha matumbo yao.
  Tusipoacha ujinga huu tutaendelea kutokuwa huru kwa maana ya kuwa huru. Tumewekeza mno kwenye siasa na uongo badala ya kuuangalia ukweli na hali halisi kama vilivyo.

  ReplyDelete
 5. Binti Mrembo kuliko wote Mlimani...December 1, 2010 at 7:16 PM

  Maprofesa wazee waliopitwa na wakati nao wanachangia. Pia umalaya kwa wanafunzi wa kike, uzembe, wivu na kutotakiana mema. Sababu ni nyingi. Mpaka imefikia hatua sasa msichana mzuri kama mimi ukipata A eti watu wanakuzushia kwamba umevua chupi kwa profesa. Tunahitaji kubadilika jamani, lakini hili ni tatizo kubwa sana na linavunja moyo kweli. Mtu unajisomea weeee halafu unaambulia B - hata kama mtihani ni take home.

  ReplyDelete
 6. Nice blog! I like your writing way. I'm doing practice GRE here: masteryourgre.com . I hope it's useful for GRE test takers.

  ReplyDelete
 7. Duuu msukuma ulikuwa unatisha ndo maana daftari lako la notisi ulikua unaibiwa mara kwa mara na walevi wa Igongwe, Msewe na wapenda disco la Silent Inn

  ReplyDelete
 8. Hii ni kweli, Sports Journalism ulifundishwa na marehemu Mziray naona akakukamata kwa B... Unahitaji kuigwa ingawa watoto wetu usongo wako huwezi kuwarithisha..

  ReplyDelete
 9. Mkuu kama kupasi kungepeleka mtu mbinguni ,....


  ..... nahisi ulikaribia kabisa kusamehewa dhambi ya asili bila ubatizo!:-(

  ReplyDelete
 10. kimsingi matondo amemshika simba masharubu, ni kweli wanafunzi wanamatatizo yao lakini baado haiingii akilini kuona katika wanafunzi mia na nane wanne au hata mmoja anapata "A" peke yake. na hii iliwahi kututokea sisi chuoni kwa mwanafunzi mmoja kati ya 114 akapewa "A" ya 86, tuliobaki tukachezea 50 tu. kiukweli waalimu wengi siku hizi wanajivunia taaluma yao na kwakuwa ni wachache wanamadaraka makubwa mno dhidi ya wanafunzi, kwahiyo wanachofanya ni kuendeleza unyanyasaji na ubabe usio na haki kwa wanafunzi na ni kwasababu wanaroho mbaya.tangu 2000 karibu kila mwanafunzi anaehitimu atakuwa ni mnafiki kama hajawahi ku-expirience tatizo hili la elimu ya hapa bongo.

  ReplyDelete
 11. Udah punya Asuransi belum? Pasti belum, iya kan. Yuk baca artikel berikut Asuransi Kendaraan MSIG, Berkendara Tanpa Cemas kali aja setelah baca artikel berikut langsung kepincut beli asuransi. Asuransi itu penting loh.

  ReplyDelete
 12. Huu ni lazima ushuhudia usomaji na kila mtu, nipo hapa kuruhusu ulimwengu wote kujua kuhusu mtu aliyeokoa uhusiano wangu na mtu huyu mkuu anaitwa Dr IZOYA. Hakika alifanya kazi nzuri kwangu kwa kumrudisha mpenzi wangu wa zamani ambaye aliniacha na kuahidi kamwe kurudi kwangu tena. Kwa hili, nimekuja kutambua kuwa kutoa maelezo ya Dk IZOYA kwa ulimwengu utafanya mengi mazuri kwa wale walio na nyumba zilizovunja au uhusiano kwa ajili yake ili kukusaidia kurekebisha uhusiano huo uliovunjika au ndoa yako. Unaweza kumfikia kupitia barua pepe yake: drizayaomosolution@gmail.com. Kuwasiliana naye na kuona jinsi tatizo lako litatatuliwa ndani ya 24hours. Pia mtaalamu katika mambo yafuatayo ...
  (1) Unataka kurudi nyuma yako.
  (2) Unataka kukuzwa katika ofisi yako.
  (3) Unataka wanaume / wanawake kukufuate.
  (4) Unataka mtoto.
  (5) Wewe ni mjasiriamali na unataka kushinda mikataba
  (6) Unataka mume wako awe wako milele
  (7) Unahitaji msaada wa kiroho.
  (8) Umeshambuliwa na unataka kupona fedha zilizopotea.
  (9) Weka talaka
  (10) Kualika kwa mila ya fedha
  (11) Chagua uchaguzi

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

ASANTE KWA MAONI YAKO

Widget by ReviewOfWeb