NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, December 8, 2010

UTAFITI: ASPIRINI INASAIDIA KUPUNGUZA VIFO VINAVYOTOKANA NA KANSA

 • Utafiti mpya uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza na kuchapishwa katika jarida la Lancet unaonyesha kwamba Aspirin - kile kidonge cha bei rahisi kabisa kinachotumika kupunguza maumivu na uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo - kinapunguza vifo vinavyotokana na kansa mbalimbali za matumbo na mapafu
 • Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba matumizi ya Aspirin kwa muda mrefu (miaka 20) yanapunguza vifo vya kansa mbalimbali za matumbo kwa asilimia 35 - 60 na ile ya mapafu kwa asilimia 30.
 • Aspirin pia inasaidia kuua seli changa za kansa kabla hazijawa sugu na kuanza kuenea katika sehemu zingine za mwili.
 • Kama utafiti huu utathibitishwa na tafiti zingine basi kuna uwezekano kwamba Aspirin itaweza kuwa mojawapo ya silaha dhidi ya kansa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 45, muda ambao kansa nyingi huanza kujitokeza.
 • Hata hivyo wataalamu hawa wanaonya kuhusu kutumia Aspirin hovyo hovyo kwani inaweza kusababisha kuvuja kwa damu tumboni na hata katika ubongo. Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa. Kwa habari zaidi kuhusu Aspirin, soma hapa.

3 comments:

 1. Habari nzuri hii, lakini ukiwa na peptic ulcers inakuwa sio nzuri...hata hivyo natumai wataalamu wanaweza kuboresha utafiti huo wakachanganya na nyingine ikatokea tiba ya kansa...manake sasa hivi kansa ni tishio! Tuombe mungu ajalie igundulike dawa ya gonjwa hili hatari

  ReplyDelete
 2. Siyo kila mtu itamsadia kama mie nilishakatazwa na doctor kutumia asprin kwa kuwa nina chembe ya moyo. Jingine pia usisahau katika nchi ya Marekani vitu vinavyotangazwa sana ni pamoja na dawa, lobbyst kibao, ni watu wanaotushauri kutumia madawa zaidi kuliko vyakula vyenye kujenga na kulinda mwili. Nchi kama za Japani na China ambapo watu wengi wanaishi miaka mingi hawatumii haya madawa ili kuongeza kinga mwilini bali vyakula na lifestyle yao.

  ReplyDelete
 3. Emu-three: Kansa sasa imeibukia kuwa tishio hata kwa nchi zetu za Kiafrika na wataalamu bado wanajiuliza ni kwa nini. Pengine ni ile tabia yetu ya kugeuzwa dampo la bidhaa mbovu (vikiwemo vyakula) kutoka nchi za Kimagharibi; pamoja na kuiga mfumo wa maisha ya Kimagharibi. Ni hatari sana.

  Anony; maoni yako ni sahihi kabisa. Marekani ni nchi inayoongozwa na makampuni na karibu kila kitu kinachofanyika hapa (kuanzia vita, sera za kiuchumi n.k) utakuta zimeathiriwa na makampuni husika. Hata tafiti mbalimbali hao ma-lobbists uliowataja hawalali. Tafiti nyingi za dawa, kwa mfano, hufadhiliwa na makampuni makubwa ya madawa na si ajabu kukuta kwamba watafiti wenyewe wanaegemea upande mmoja tu na kusifia dawa inayotafitiwa kwa kuwa wamepewa pesa na kampuni husika. Ndiyo maana kumekuwa na madawa mbalimbali ambayo yalipigiwa upatu sana lakini baadaye yakaja kugundulika kuwa ni hatari mno.

  Utafiti huu wa Aspirin umefanyika Oxford nchini Uingereza na wasiwasi wangu ni kwamba pengine makampuni makubwa ya madawa ya Kimarekani yataukorofisha tu kwani hayatakubali eti Aspirin - dawa rahisi na inayoweza kutengenezwa karibu na kila mfamasia ndiyo iwe na uwezo wa kutibu na kuzuia maambukizi ya kansa. Makampuni haya daima yangependa madawa yake ghali ndiyo yachukue jukumu hili na sitashangaa kama tafiti zitakazofuatia zitakuwa kinyume kabisa na huu.

  Bila shaka kuzuia ni bora kuliko kuponya; na kutokana na ukweli kwamba madawa yote yana sumu, njia za kiasili za kujikinga na magonjwa kama vile kula vyakula vya kiasili vyenye kulinda na kujenga mwili, pamoja na kubadili mfumo wa maisha ndiyo njia bora kabisa ya kujikinga na magonjwa. Njia hizi mbadala hazina faida kwa makampuni haya na ndiyo maana hazitajwi wala kusisitizwa sana.

  Kama nilivyogusia hapo juu kwa emu-three, kinachosikitisha ni kwamba nasi tunaiga mitindo ya maisha na kula vyakula tunavyoletewa tukidhani kwamba haya ndiyo maendeleo na usasa kumbe kwa kufanya hivyo tunajiingiza mkenge. Kwa mfano,nyanya za Sokoni Kariakoo zilizotoka Morogoro sasa tunazidharau na badala yake tunataka nyanya za kopo kutoka Afrika Kusini zinazouzwa katika supamaketi.

  Asante kwa maoni yako mazuri!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU