NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, December 16, 2010

WAMAREKANI WANAHAHA KUBORESHA ELIMU YAO INAYOZIDI KUDORORA. TUNAWEZA KUJIFUNZA LOLOTE???

 • Matokeo ya mtihani wa kimataifa yaliyotolewa hivi karibuni kwa wanafunzi wenye miaka 15 yamezua kizaazaa hapa Marekani. Katika matokeo hayo Marekani imeshika nafasi ya 17 katika kusoma, nafasi ya 31 katika hesabu na nafasi ya 23 katika sayansi. Alama ya jumla ya Marekani ikilinganishwa na nchi nyingi zilizoendelea ni "wastani" na kwa ujumla imefanya vibaya. Wanafunzi kutoka Korea ya Kusini, Finland, China, Singapore, Canada ndiyo wamefanya vizuri zaidi wakifuatiwa na nchi zinginezo. Wanafunzi kutoka mji wa Shanghai nchini China ndiyo wanaongoza kwa kupata alama za juu zaidi.
 • Kwa Wamarekani jambo hili halikubaliki kwani wanajua kwamba bila kuwa nambari wani katika elimu, haiwezekani kwao kuendelea kuwa nambari wani kiuchumi na kitekinolojia ulimwenguni; na tayari wameshajiwekea malengo ya kurudi kileleni tena katika masomo yote ifikapo mwaka 2020. Wakiweza kufanya hivi, mahesabu yao yanaonyesha kwamba uchumi wao utaweza kujiongezea dola zipatazo trilioni 41 katika miaka 20 ijayo!
 • Watawezaje kurudi kileleni? Hatua ya kwanza waliyoipendekeza ni kuimarisha taaluma ya ualimu na kuifanya iheshimiwe zaidi ili kuweza kuvutia wanafunzi wenye vipaji. Hii ni pamoja na kuwalipa walimu mishahara mizuri pamoja na marupurupu ya kutosha, kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi na nafasi zinginezo za kujiendeleza. Ripoti hiyo inaonyesha kwamba katika nchi zinazofanya vizuri katika elimu, ualimu si kazi ya kiholela tu. Katika nchi kama Singapore, Finland na Korea ya Kusini, kwa mfano, ni wanafunzi bora pekee ndiyo huruhusiwa kujiunga na ualimu (bofya hapa). Hata katika nchi za Kiarabu mkakati kama huu tayari umeanza kupendekezwa.
 • Nilishangaa kuona kwamba sisi tunafanya kinyume. Kimsingi wale wanaofeli ndiyo tunawabebesha jukumu la kuelimisha taifa huku tukiwalipa mishahara kidogo na kuwafanyisha kazi katika mazingira magumu sana hasa kule vijijini. Na hapa hatujawataja hawa wa"Voda Fasta!". Taaluma ya ualimu haiheshimiwi hata kidogo japo kusema kweli ndiyo mama wa kila taaluma na msingi wa kila taifa lililoelimika. Ndiyo maana kuna kipindi fulani walimu walitishia kugoma na waziri wa elimu wa wakati ule inasemekana alitoa tamko kwamba hata walimu wakigoma hakuna neno kwani anaweza kuokota watu mabarabarani na sokoni wakaingia madarasani kufundisha! Tutawezaje kuwa na elimu bora kama tunadharau taaluma ya ualimu namna hii? Ati, ni kwa nini hawa vijana wenye vipaji wanaopata divisheni wani tusiwape kila kitu ili wavutike na kwenda kusomea ualimu? Au tutakimbilia umasikini wetu na kusema kwamba hatuna pesa na kwamba programu ya aina hiyo haiwezekani?
 • Jambo jingine lilinivutia katika ripoti hii ni hili. Karibu nchi zote zilizofanya vizuri sana zinatumia lugha yake zenyewe kufundishia madarasani. Wachina wana Kichina chao, Wakorea na Kikorea chao, Wafin wana Kifini chao n.k. Na sisi je? Tumeng'ang'ania sera ya lugha ambayo ni kichekesho, sera ambayo kimsingi haiwasaidii watoto wetu kumudu lugha yo yote kitaalamu kati ya zile tunazotumia. Kutokana na kizingiti hiki cha lugha, elimu yetu imebutuka na kuwa zoezi la kukariri tu hata kama hatuelewi hicho tunachokikariri kina maana gani. Hii kweli ni elimu?
 • Kuna mengi ya kujifunza katika ripoti hii. Jambo la msingi ambalo inabidi tulitambue ni kwamba hatutaweza kuendelea bila kuwa na elimu bora inayowakaramsha vijana wetu na kuwafanya wawe tayari kwenda kupambana na dunia pale wanapomaliza masomo yao. Na kuboresha taaluma ya ualimu pamoja na kuwa na sera imara ya lugha ya kufundishia vinaweza kuwa mwanzo mzuri katika kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wetu wa ualimu.

4 comments:

 1. ni mkakati mzuri na siye tunayo hapa ila kwa kuwa twachekacheka tu hatuwezi kufikia huko!

  Kama kila $10 inayotengwa kwa kila mwanafunzi shule za msingi inafika chini ya $2 unategemea hayo mengine makubwa yatawezekana?

  Ndimi Ihayabuyaga!

  ReplyDelete
 2. Sema wewe mwalimu labda watakusikia...siunajua hapa kwetu, mabo yote yanaendweshwa kisiasa!

  ReplyDelete
 3. Matondo, ukigusia suala la elimu kwa kweli unatia uchungu. Mimi nilishapata kuwa mwali katika shule mbali mbali za serikali na hata chache za binafsi kama vile Agha Kan Mzizima. Leo nimesoma kwenye gazeti eti waziri wa elimu anaongelea suala la ufundishaji kwa lugha ya kiingereza kuanzia darasa la tatu. Sasa hawa mawaziri wetu kweli wanachekesha, waswahili walisema samaki mkenje angali mbichi. Kwanini lugha hii isingeanza kutumika kuanzia chekechea badala ya darasa la tatu? jibu sina.

  Tatizo kubwa ni la mitaala iliyopitwa na wakati, mitaala ambayo imerithiwa toka enzi za mkoloni. Elimu pia imukuwa ikeshezwa kama mpira wa miguu na wanasiasa badala ya kuwaachia wataalumu waliobobea katika fani hii.

  Nilishandika articles kama mbili kwenye gazeti la mwananchi kuhusu elimu yetu ya Tanzania. Waweza kurejea hapa:

  http://www.mwananchi.co.tz/magazines/33-maarifa/4890-tukiamua-tunaweza-kuzimaliza-changamoto-za-elimu-shuleni.html

  http://www.mwananchi.co.tz/magazines/33-maarifa/5697-walimu-waishinikize-serikali-kurejesha-posho-ya-kufundisha.html

  ReplyDelete
 4. Kwetu kukua kwa elimu ni kuongezeka kwa majengo mabovu, idadi ya mashimo ya vyoo na wingi wa wanafunzi wanao-hudhuria hizo wanazoziita shule.

  Na Viranja wetu hawasiti kujitamba kwa mbembwe kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka katika elimu ya sekondari na ya juu bila kujali ubora wa elimu wanayopata.

  Miaka ya nyuma kidogo walijitahidi, ndio maana kwenye shule za serikali uliweza kukuta hata watoto wa mawaziri.

  Sasa hivi hata mtoto wa mkuu wa shule anayofundisha mtoto wake kampeleka shule binafsi.

  SASA NASUBIRIA HAO WATAALAMU TOKA SHULE ZA VODA FASTA WAJE KUWA WALIMU. wafundishe chemistry wakati wao mpaka wanamaliza kidato cha nne hawajawahi kumuona mwalimu wa somo hilo.

  NCHI INAENDESHWA KISANII KUANZIA NGAZI YA JUU KABISA. NA SASA NAONA WASOMI WETU NAO WAMEINGIA KATIKA MITEGO YA WANASIASA. Sijui ni tamaa au ubinafsi au ni kwa kushinikizwa. SIJUI

  Kazi tunayo na itatuchukua zaidi ya karne kurekebisha usanii uliofanyika/unaofanyika ndani ya muongo mmoja

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU