NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, January 29, 2010

FIKRA YA IJUMAA - MFULULIZO MPYA (KWA WAPENDAO KUFIKIRI)

  • Kuanzia sasa kila Ijumaa nitakuwa nabandika hapa "fikra" au wazo la kufikirisha. Safu hii mpya itakuwa inaitwa "Fikra ya Ijumaa". Fikra hii inaweza kuwa katika umbo la swali au nathari na inaweza kuhusu falsafa, dini au maisha tu kwa ujumla. Karibuni tunoe ubongo!

  • Leo napenda tuanze na Epicurus na maoni yake kuhusu kifo. Yeye alikuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi kati ya mwaka 341 na 270 K.K. na ambaye alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi kutokana na mafundisho yake ya kutoamini vitu hovyo hovyo hata kabla ya kuvipima na kuvichunguza sawasawa.
  • Kulingana na Epicurus, lengo kuu la falsafa lilikuwa kuleta furaha na maisha ya utangamano – maisha yasiyo na maumivu wala hofu ambayo aliyaita maisha yenye aponia.
  • Kuhusu kifo alifundisha kwamba kifo kilikuwa ndiyo mwisho wa mwili na roho na kwa hivyo hakipaswi kuogopwa. Hebu fuatilia hoja kuu za Epicurus kuhusu kutoogopa kifo hapa chini.
  1. Unapokuwapo kifo chako hakipo; na kisichokuwepo hakiwezi kukudhuru
  2. Kifo chako kinapokuwepo wewe haupo; na kisichokuwepo hakiwezi kudhuriwa
  3. Ni upumbavu kuogopa ambacho hakiwezi kukudhuru
  4. Ni upumbavu pia kuogopa ambacho hakiwezi kudhuriwa
  5. Katika wakati wo wote ule ama wewe unakuwepo au kifo chako kinakuwepo
  6. Kwa hivyo katika wakati wo wote ama kifo hakiwezi kukudhuru, au huwezi kudhuriwa na kifo.
  • KWA HIVYO (anahitimisha Epicurus): Ni upumbavu katika wakati wo wote ule kuogopa kifo!
  • Baada ya kufuatilia kwa makini hoja hizi za Epicurus, unakubaliana naye? Unakiogopa kifo? Hii ndiyo fikra ya kwanza ya Ijumaa hii!!! Muwe na wikiendi njema!

PARKING INAPOKOSEKANA WAKATI UNAPOIHITAJI SANA

  • Siku za Ijumaa saa tatu mpaka saa nne asubuhi huwa najitolea kufundisha hesabu watoto wa darasa la tatu. Baada ya darasa hilo Ijumaa wiki jana nilipita kwingine na nikafika chuoni karibia saa tano na nusu asubuhi.
  • Ngoma sasa ikawa ni kupata parking kwani kila mahali kulikuwa kumejaa na wakati huo huo darasa langu la Linguistics (tena la wanafunzi wa PhD) lilikuwa linaanza saa sita na dakika ishirini mchana. Hawa jamaa wa Idara ya Usafiri hapa chuoni huuza vibali vya kupaki vingi kwa kadri inavyowezekana bila kujali idadi ya parking walizonazo. Ukijidamka asubuhi unapata, ukichelewa ndiyo hivyo tena...usimlaumu mtu!
  • Hapa ni ghorofa ya nne (na ya mwisho) katika parking mojawapo. Nako kulikuwa kumejaa pomoni na hapa nimejibanza najaribu kusubirisha mtu atoke...

  • Hapa ni parking ile ile lakini kwa upande mwingine. Hapa kuna jamaa alikuwa anatoka kwa upande wa kulia. Alipotoka tu nilipaki na kutimka kwenda darasani. Nilifika nikiwa nimechelewa dakika tano huku nikihema kwelikweli. Kwa watu wanaojali sana muda, hili si jambo jema! Bahati nzuri nilikuwa na mfuko wangu wenye makabrasha na darasa lilikwenda vizuri. Kazi kwelikweli!

JINSI YA KUMWAMSHA GIRLFRIEND - MOTO UKIKUWAKIA USINILAUMU

video
  1. Hapa kuna hatari ya kuulizwa maswali makali sana. Mf. Ulitaka kujua nita-react vipi nikiamka na kukuta mwanaume mwingine kitandani? Unanifikiriaje?

  2. Ni lazima uwe na majibu tayari tayari kwani utani wako hapa unaweza usionekane. Unajua tena wanawake!

  3. Moto ukikuwakia usinilaumu!

Tuesday, January 26, 2010

WATOTO HAWA WATAKUWA WATU WA AINA GANI WAKIKUA?

(Picha: Google)
  • Wanasaikolojia wengi wamekuwa wakijiuliza athari za propaganda hizi za chuki katika maisha ya baadaye ya watoto hawa. Ni sawa kweli kushirikisha watoto wadogo namna hii katika kampeni za chuki? Wanaelewa kweli hata kinachoendelea hawa?

UTAFITI: KUMBE UMBO LA KIBANTU (A.K.A UMBO NAMBA NANE) LINA FAIDA ZA KIAFYA!!!

  • Wanasayansi wa chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza wanasema kwamba umbo la Kibantu (a.k.a umbo namba nane) lina faida nyingi za kiafya. Wamethibitisha kwamba kunenepa mapajani, makalioni na katika mahips husaidia mtu asipate matatizo ya kiafya kama magonjwa ya moyo.
  • Wakati huo huo kuwa na mafuta katika mzunguko wa tumbo (mf. kitambi), kunaongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo na sukari. Kwa maelezo mazuri zaidi katika Kiswahili kuhusu utafiti huu soma hapa. Ripoti ya utafiti huu inapatikana hapa.

  • Masuluhisho: (1) Hakuna haja ya kuogopa kuwa na umbo la Kibantu. Hili ndilo umbo hasa la mwanamke wa kiafrika! (2) Tupunguze vitambi na mafuta ya tumbo.

Monday, January 25, 2010

SHUTTLE ZINAUZWA - WAJASIRIAMALI MPO?

  • Inasemekana kuwa shuttle hizi ndizo mashine tata na za kiwango cha juu zaidi zilizowahi kuundwa na binadamu na ni kielelezo bayana cha kilele cha mafanikio ya kisayansi yaliyofikiwa na Wamarekani katika milenia iliyopita.
  • Ziliundwa sita tu - Enterprise, Columbia, Discovery, Challenger, Atlantis na Endeavour. Challenger iliripuka mwaka 1986 wakati ikijaribu kuruka na Columbia iliteketea mwaka 2003 katika angala la Texas wakati ikielekea kutua kule Kennedy Space Center jimboni Florida. Mpaka sasa ni tatu ndizo bado zinaendelea kupiga mzigo wa kwenda na kurudi katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za juu (Discoverry, Atlantis na Endeavour)
  • Shuttle hizi zimepangiwa kustaafishwa mwaka huu (2010) na tayari NASA inazipiga bei. Bei ya awali ilikuwa dola milioni 42 kwa kila shuttle na sasa bei imepunguzwa na kuwa dola milioni 28.8. Inaaminika kwamba shuttle hizi zitakuwa kivutio kikubwa cha utalii huko mbeleni.
  • Hakuna kweli liTanzania angalau limoja lenye pesa (hata kama ni lifisadi sawa tu) likanunua shuttle mojawapo na kututoa kimasomaso kwa kusaidia kuimarisha sekta yetu ya utalii huko mbele? Tukiongezea shuttle mojawapo na mabaki ya ile rada yetu ya bei mbaya, (+ K'njaro, Serengeti, Ngorongoro na Z'bar yetu) bila shaka tutawika sana katika sekta ya utalii huko mbele.
  • Itazame Atlantis hapa ikitua. Nimepanga kwenda kushuhudia kutua kwa shuttle hizi zitakapofanya safari zake za mwisho mwisho!


Friday, January 22, 2010

NI KWELI AU NI KAULI MBIU YENYE OMBWE?

  • Kama asemavyo mhusika mmojawapo katika tamthiliya mashuhuri ya Tartuffe (Mnafiki) iliyoandikwa na Moliere, sote tunajua kwamba njia kati ya azimio na kitendo ni ndefu. Hayo maneno kwenye picha (ambayo naamini ni kibwagizo cha chama kimojawapo cha siasa) ni dhamira ya kweli watakayoitekeleza au ni kauli mbiu tu yenye ombwe watakayoitelekeza? Kuna lolote ambalo wamelifanya kutuaminisha kwamba wataitekeleza kauli mbiu yao hii kwa vitendo wakiingia madarakani au ni yale yale ya "Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa?"

MHESHIMIWA PINDA ALIPOTEMBELEA "ALMA MATER" YAKE - PUGU SECONDARY SCHOOL

  • Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika Bweni la Mapinduzi One, alilolala wakati akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Pugu kwenye miaka ya 60. Mheshimiwa Pinda alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita ya shule hiyo, Januari 21, 2010. (Picha na maelezo ni kutoka kwa Father Kidevu)
**********************************
  • Picha hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imenifikirisha. Sina uhakika kama hii ndiyo "Pugu Secondary" aliyoiacha. Sina uhakika kama hili ndilo Bweni la Mapinduzi One alimolala wakati akisoma hapa. Sijui hapa Mheshimiwa anawaza nini baada ya kuona bweni lake alipendalo likiwa katika hali hii. Uso wake unaonyesha huzuni!

Thursday, January 21, 2010

"HAKUKUWA NA UZAZI WA MPANGO BARANI AFRIKA KABLA YA KUJA KWA WAKOLONI" NI KWELI?

  • Jamani, naomba mnisaidie. Jana nilihudhuria semina ya mwanafunzi mmoja wa "Medical Anthropology" anayefanya utafiti wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mojawapo ya dai kuu katika mhadhara wake ni kwamba eti hakukuwa na uzazi wa mpango barani Afrika kabla ya kuja kwa watawala kutoka Ulaya.
  • Kwa vile sifahamu cho chote kuhusu mambo haya, sikuweza kuuliza swali mbele ya halaiki lakini baadaye wakati wa mapumziko na vinywaji nilikwenda kuongea naye. Nilimuuliza kama hitimisho lake lilikuwa la ukweli. Nilimwambia kuhusu familia kule kijijini ambako watoto katika familia nyingi wamepishana miaka mitatu mitatu. Hiyo inawezekanaje kama akina mama wa kijijini hawajui cho chote kuhusu uzazi wa mpango? Nilimwambia pia kuhusu elimu ya jadi katika makabila mengi ambako mabinti waliwekwa ndani na kufundwa kuhusu mambo mbalimbali likiwemo hili la mimba na uzazi.
  • Aliniambia kwamba kitu pekee kilichokuwa kinawasaidia (na kinaendelea kuwasaidia) akina mama wa Kiafrika wasipate mimba za dabo dabo ni kunyonyesha. Aliniambia kwamba kunyonyesha kunapunguza uwezekano wa kupata mimba kwa asilimia 80 hasa katika miaka miwili ya mwanzo. Ndiyo maana katika familia nyingi alizozichunguza kule Kongo watoto wengi wamepishana miaka miwili miwili ambacho ndicho kipindi cha wastani cha akina mama kunyonyesha.

  • Aliendelea kuniambia kwamba uzazi wa mpango ni tata mno kiasi kwamba hata yeye (msomi) wakati mwingine huwa hana uhakika na "vipindi vyake vya hatari" - sembuse akina mama wa Kiafrika vijijini tena wasio na "elimu"? Sikupenda kumbishia bila hoja nzito na nilimwacha japo kwa shingo upande huku nikijiahidi kwenda kujisomea kuhusu suala hili na kisha nije nimtafute tena “tubishane”. Lakini pia nikafikiria kwamba pengine vitabu nitakavyovisoma vitakuwa vimeandikwa na watafiti kutoka nje ambao mtazamo wao ni tofauti na ule wa Kiafrika.
  • Ni kweli hakukuwa na uzazi wa mpango wa aina yo yote barani Afrika kabla ya kuja kwa wakoloni?

MIUJIZA KUTOKA HAITI: MTOTO WA MIAKA MITANO AKUTWA AKIWA HAI BAADA YA SIKU NANE

  • Kama nilivyowahi kugusia hapa, kweli kama siku zako hazijafika hazijafika tu. Mtoto wa miaka mitano amepatikana leo kule Haiti akiwa hai SIKU NANE tangu nchi hiyo ikumbwe na tetemeko kubwa la ardhi. Mama yake alifariki katika tetemeko hilo na baba yake hajulikani aliko. Haijajulikana kama mtoto huyo alikuwa na njia ya kujipatia chakula na maji katika kipindi alichokuwa chini ya kifusi. Madaktari wamesema hana mifupa iliyovunjika ingawa alikuwa ana upungufu mkubwa wa maji mwilini. Miujiza kama hii huwa inatia moyo na kuleta matumaini katika nyakati za giza kama zinazoikumba Haiti kwa sasa. Tazama video hapa na kwa habari kamili zaidi tembelea hapa.
KWINGINEKO
  • Serikali ya Haiti imesema kwamba mpaka sasa maiti 72,000 wameshapatikana. Mashirika mbalimbali yanakadiria kwamba pengine watu wapatao 200,000 wameangamia katika tetemeko hilo.
  • Matetemeko mengine matatu katika miaka 100 iliyopita ndiyo yaliangamiza watu wengi zaidi kuliko hili la Haiti:
1920 - China - liliua watu 200,000 au zaidi
1976 - China - liliua watu 225,000
2004 - lilisababisha sunami katika nchi mbalimbali za Asia na kuua watu zaidi ya 300,000.

Tuesday, January 19, 2010

KUNA WAKATI KUTONGOZA ILIKUWA NI FANI.

  • Vijana wa siku hizi huita kushusha mistari. Wengine husema ni kuwa kwenye fani, kusomesha au kumwaga sera. Kwa Kiswahili sanifu ni kutongoza. Mpaka hivi karibuni, kwa kawaida, mvulana ndiye alikuwa anatongoza na msichana alikuwa akitongozwa.
  • Enzi zetu kule Usukumani ulihitajika utaalamu wa hali ya juu sana wa kushusha mistari kama kweli mtu ulitaka kuwa mkali kwenye “gemu” (msishangae, leo natumia lugha ya vijana tu!). Kwa upande wao, mabinti wa Kisukuma enzi zile nao hawakuwa “goigoi”; na kutongoza ilikuwa ni shughuli iliyohitaji ustadi na umakinifu wa hali ya juu. Mtu ilikuwa lazima ujiandae kabla hujamparamia binti na kuanza kumwaga sera zako. Na ilihitajika lugha maalum kwa lengo hili.
  • Lugha hii ilikuwa tamu na iliyojaa taswira, tashbiha, tashtiti na mbinu zingine zikiwemo misemo, methali, nahau na tamathali zinginezo. Ilikuwa ni lugha tajiri sana iliyoweza kuchora mawanda na mandhari ya kuliwaza; na kuweza kumhakikishia binti kwamba wewe ulikuwa ndiye! Ilikuwa ni lugha iliyoweza kumwingiza binti katika ulimwengu wa jazanda mpaka akalainika….
  • Kwa vile mimi nilichepuka mapema na kwenda shule ya sekondari mbali na nyumbani, sikupata bahati ya kuifahamu lugha hii sawasawa. Nakumbuka kila niliporudi kijijini wakati wa likizo rafiki yangu mmoja aitwaye Nkuba Guyambila Milyango alikuwa akijitolea kunifundisha lugha hii. Kwa upande wa barua, pale kijijini kulikuwa na bingwa mmoja wa erotographomania (uraibu wa kuandika barua za mapenzi) aitwaye Yohana Masingija Nkilonhiga Balila (R.I.P). Huyu alikuwa mtaalamu sana wa kutumia lugha hii maalum katika maandishi na vijana walikuwa wakimmiminikia ili awashushie mistari katika karatasi. Gazeti la SANI pia lilikuwa maarufu sana na vijana tulikuwa tunakariri karibu kila kitu kilichokuwa kinatokea katika Harakati za Pimbi.
  • Kwa sasa nadhani lugha hii imeshakufa au inakufa. Sasa uchumi umetawala na mtu haijalishi tena kama unajua kupanga mistari ama la. Kama una pesa, gari na unapiga pamba sawasawa basi hakuna neno. Mambo yamebadilika sana.
  • Kama mkereketwa wa masuala ya lugha na utamaduni, nimekuwa nikiwaza uwezekano wa kuihifadhi lugha hii katika maandishi kabla haijapotea kabisa. Ni lugha iliyobeba utamaduni mwingi na naamini kwamba litakuwa ni jambo jema kama itahifadhiwa. Naangalia uwezekano wa kufanya hivyo.
  • Nimeikumbuka lugha hii baada ya kuona “vibwagizo” kadhaa katika gazeti la wanafunzi. Baadhi yake vinasema hivi:
************************
  1. You should come with road signs. All those curves. And me with no brakes!

  2. You are really hot. You must be the reasons for global warming.

  3. If I had a rose for every time I thought about you, I would be walking through a garden for ever.

  4. You are so hot. You’d make the devil sweat!

  5. If being sexy was a crime, you would be sentenced to life in prison

Monday, January 18, 2010

BARAFU IMEUA MICHIKICHI YANGU!

  • Nilipolalamika kuhusu jimbo lenye hali ya hewa ya kitropiki la Florida kukumbwa na barafu (ambayo ni nadra sana), Mzee wa Changamoto alicheka na kusema kwamba hakuona barafu katika picha nilizoweka. Alidhani kwamba nilikuwa nimekosea na kuweka picha zisizohusiana na mada husika.
  • Ukweli ni kwamba barafu hiyo imeleta kizaazaa kikubwa hapa Florida hasa kwa wakulima wa mboga mboga. Kwa kiasi kikubwa, Marekani hupata kiasi kikubwa cha mboga na matunda kutoka jimbo la Florida hasa katika kipindi hiki cha baridi. Kutokana na barafu hii kuharibu kiasi kikubwa cha mboga na matunda, inategemewa kwamba bei za mboga na matunda zitapanda nchi nzima kwa miezi michache ijayo.
  • Kwangu mimi barafu hii imeua kabisa miti yangu sita ya michikichi ambayo nilikuwa nimepanda. Hii ni pamoja na kila kitu katika bustani yangu. Sasa inabidi kuanza upya na safari hii kila mti na ua la kudumu nitakalolipanda ni lazima nihakikishe kwamba linaweza kuvumilia baridi kali.
  • My wife wangu anatoka sehemu zenye migomba na hapa nilijitahidi nikampandia vimigomba-andunje vinne. Vilitakiwa kutoa vindizi mwaka huu lakini kama unavyoweza kuona navyo vimepigwa dafrau na barafu. Inabidi nianze upya!

LUGHA ZA MITAANI, KISHENG NA "MUHADHARA"

  • Nilipousikia wimbo huu kwa mara ya kwanza nilishangazwa na jinsi neno muhadhara lilivyotumika. Baadaye nikaambiwa kwamba hili ni neno la Kisheng na kule Kenya linatumika kumaanisha shida kubwa, janga au maafa.
  • Kisheng kimevutia watafiti wengi wa Isimu Jamii kutokana na ubunifu unaojitokeza katika uundaji na mpangilio wake wa maneno. Mpaka sasa imeshindikana kujua hasa Kisheng ni nini kwani si rahisi kukipambanua na kukipa sifa za moja kwa moja. Mpaka sasa bado haijajulikana kama ni lahaja ya Kiswahili, lugha ya mseto, lugha ya mitaani, pijini au Creole.

Sunday, January 17, 2010

PHOBIA ZINGINE KIBOKO!!!

Hippopotomonstrosesquipedaliophobia - hii ni phobia ya maneno marefu. Unayo?

Friday, January 15, 2010

EUPHRASE KEZILAHABI, KAPTULA LA MARX NA SAFARI YETU YA KUELEKEA NCHI YA USAWA

  • Kaptula la Marx ni tamthiliya makini dhati iliyoandikwa na Euphrase Kezilahabi (aka Shaaban Robert wa pili) zamani. Inasemekana kwamba tamthiliya hii ilimletea matatizo na ilipigwa marufuku kuchapishwa nchini Tanzania.
  • Baada ya miaka mingi ya ukiritimba wa chama kimoja na udumishaji wa fikra “sahihi” za mwenyekiti wa chama hatimaye tamthiliya hii ilichapishwa mwaka 1999 na Dar es salaam University Press (DUP). Nilifurahi nilipoiona katika maktaba hapa chuoni, nikaiazima na ndiyo tu nimemaliza kuisoma. Sasa najua ni kwa nini tamthiliya hii ilikaa katika makabrasha ya wachapishaji kwa muda mrefu.
  • Katika Kaptula la Marx kuna safari ndefu ya kwenda katika nchi ya ahadi – nchi ya usawa. Safari hii inaongozwa na Rais Kapera akiungwa mkono na mawaziri wake wote. Njia ya kwenda katika nchi ya usawa, hata hivyo, ni nyembamba sana na mawaziri wake ni wanene futufutu kiasi kwamba wanapata shida kutembea katika njia hiyo.
  • Raisi Kapera ameamua kuvaa kaptula kubwa la Marx ambalo kusema kweli halimwenei sawasawa na anaonekana kama kichekesho. Isitoshe, rais huyu pamoja na mawaziri wake hawajui kabisa njia ya kuelekea katika nchi hii ya usawa na hawana ramani. Kwa hivyo wamepotea.
  • Hatimaye linatokea jitu refu pandikizi linalojiita mtu jitu au beberu. Jina kamili la jitu hili ni KORCHNOI BROWN. Rais na mawaziri wake wanaliuliza kama linafahamu njia itakayowafikisha katika nchi ya ahadi – nchi ya usawa. Jitu hili linamhakikishia rais na mawaziri wake kwamba linaifahamu njia hiyo na linawapa maelekezo yafuatayo:
“Mtakwenda! Halafu mtapinda, mtapinda tena, halafu tena mtapinda, mwishowe mtapindapinda hadi mtakapofika mabonde yenye matope. Mtapita katikati ya matope. Halafu milima, halafu misitu yenye miiba hadi mtakapofika jangwani. Kutoka jangwani mtaingia tena bondeni chini kwa chini hadi baharini. Hakuna mitumbwi wala ngalawa. Mtaogelea, ingawa kuna papa wengi. Mkishavuka mtafika nchi iitwayo Svoboda. Kabla ya kuondoka katika nchi hii itawabidi kupambana na majitu yanayofanana na mimi. Mkitoka hapo mtafika kwenye njia nyembamba. (Akiwaonyesha mawaziri) Hawa hawatapita hawa! Njia hiyo itawafikisha katika nchi iitwayo Fraternite. Kutoka Fraternite mtafika Usawa. Ulizeni tu watu watawaonyesha! Mkifika Usawa mtawakuta Waswahili wenzenu wameketi nje ya ikulu ndogo ya Ravensto” Kaptula la Marx (uk). 20)
  • Kwa hivyo usishangae ni kwa nini baada ya miongo mitano ya uhuru bado hatujaifikia nchi ya ahadi. Inavyoonekana safari yetu ya kuelekea katika nchi hii ilikuwa ndiyo-siyo hata kabla haijaanza. Usishangae kama Ujamaa na Kujitegemea bado ndiyo falsafa na dira yetu elekezi ya kutufikisha katika nchi ya ahadi. Usishangae kama ahadi za wanachama wa chama cha Rais Kapera bado ni zile zile. Usishangae kama kinachoropokwa na wenye mikrofoni leo hakifanani na matendo yao. Usishangae kama "fraternite” ya watu wachache wanaofaidi maziwa na asali ya nchi ya usawa “kwa niaba” ya walio wengi inazidi kuimarika na kujitandaza. Usishangae kama (kama anavyosema George Orwell katika riwaya yake ya Shamba la Wanyama), wanyama wote ni sawa lakini wanyama wengine ni sawa kuliko wanyama wengine. Usishangae………..!
*******************************
  • Msikilize Euphrase Kezilahabi hapa chini akisoma mojawapo ya shairi lake; na huyu mwanafunzi akisoma shairi la Chai ya Jioni ambalo limo katika diwani ya Kezilahabi ya Karibu Ndani.




HATA FLORIDA KUMBE KUNA BARAFU!!!

  • Kwa mara ya kwanza tangu nihamie hapa Florida, sijawahi kupambana na baridi ya aina hii. Mpaka tumeweza kurashiwarashiwa na barafu na rekodi za baridi za miaka na miaka zimevunjwa. Mimi sijawahi kuishi sehemu ya baridi na hii ndiyo mara ya kwanza kupambana na baridi ya kweli kweli. Najua Mzee wa Changamoto pengine atacheka tu, lakini mimi hata sikujua la kufanya baada ya kukuta gari limefunikwa na unga wa barafu!
  • Unaweza kuona "yard" yote imeota mvi. Maua na miti yote pia nyang'anyang'a! Kuna hatari ya kulazimika kupanda majani na maua mapya mwaka huu.

  • Mabinti walikuwa na wakati mgumu asubuhi wakati wa kwenda shule. Hapa ilikuwa ni baada ya zaidi ya dakika ishirini nzima za kupasha gari moto na kujaribu ku-defrost hiyo barafu. Hapa nilikuwa ninakaribia kuishiwa mbinu wakati mabinti wakizidi kuchelewa kwenda shule. Kazi kwelikweli!

Thursday, January 14, 2010

NIMEANZA KUWAZA NA KUWAZUA - INAWEZEKANA AIKA M. ALIKUWA NA POINTI!

Siku ya Ijumaa tarehe 14, 2009 nilitundika katika blogu hii mada iliyosema UTAFITI: WATU WEUSI NDIYO WANAONGOZA KWA UNENE. Mada hiyo ilichemka sana na iliishia kuwa na maoni mengi. Kati ya watoa maoni waliochemka sana na kung'ang'ania msimamo wao pamoja na kushambuliwa kulia na kushoto ni mdau mmoja aliyejiita Aika M. Yeye alianza maoni yake hivi:

"Watu weusi wamelaaniwa. Popote pale utakakowapeleka iwe ni Afrika, Ulaya, US, Jamaika, Haiti all ni the same. Incompetence, laziness, dirty and poverty. Halafu tukiambiwa kwamba we are a cursed race tunalalamika. I wish I were not black becauese it is a shame. Nikipata mzungu wa kunioa au siku nikienda nje, I will never come back to Africa again"

Aika M. aliendelea

"Don't blame everything on the white man - allover the world. Mzungu ndiye anatulazimisha tuwe mafisadi? Mzungu ndiye anatulazimisha tuwe lazy? Kwa nini hatuwezi kuwa na transparent society? Kwa nini hatuwezi kuwa na viongozi wanaojali watu wao? Kwa nini tusiwe na responsible leaders? Ni kwa sababu ya mzungu? I don't think so. Ndiyo maana mimi naamini kwamba something is inherently wrong with blacks!...mtu mweusi ni masikini, mchafu, mvivu, maneno mengi, mpenda kufanyiwa vitu na ombaomba POPOTE DUNIANI.."

Nimekuwa nikiangalia taswira za kutoka Haiti tangu nchi hiyo ikumbwe na tetemeko kubwa la ardhi - taswira zinazoonyesha umasikini wa kutisha. Na kama kawaida, watu wanaohusika ni weusi. Inaonekana kama vile umasikini na mtu mweusi ni vitu vinavyokwenda pamoja duniani kote. Ndipo nilipoyakumbuka maoni haya ya Aika M - maoni ambayo sikukubaliana nayo na bado sikubaliani nayo. Japo ni hivi, nimeanza kufikiria, inawezekana Aika M alikuwa na pointi!

**********************************************
Data muhimu za Haiti

Idadi ya watu: 9, 035, 536
Makabila
: Mulatto na wazungu: 5%, Weusi 95%
Dini
: Waprotestanti 16%, Wakatoliki 80%, nyinginezo 4%
Zaidi ya nusu ya wakazi wanaamini pia katika "vudu"
Wanaojua kusoma na kuandika
: 52.9%
Wanaoishi katika umasikini
: 80%
GDP per capital
: $1,300
Ajira
: zaidi ya robo tatu hawana ajira za kuaminika.

Tuesday, January 12, 2010

NAHITAJI MSAADA - NATAFUTA PICHA ZA MAREHEMU DR. RUGATIRI MEKACHA


NATAFUTA PICHA ZA MAREHEMU DR. RUGATIRI MEKACHA

Wadau, nahitaji msaada. Natafuta picha za aina yo yote za Marehemu Dr. Rugatiri Mekacha ambaye alifariki tarehe 29/9/2001 nchini Japan ambako alikuwa amekwenda kikazi katika Chuo Kikuu cha Masomo ya Kigeni cha Osaka. Dr. Mekacha ndiye alinipa misingi ya isimu wakati ule nikiwa bado mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Nilipopata nafasi ya kwenda kusomea shahada za uzamili (Masters) na Uzamifu (Ph.D) katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA), Dr. Mekacha alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na alihakikisha kwamba ninapata kila kitu nilichohitaji kwa ajili ya safari hiyo. Hata baada ya kufika UCLA, aliendelea kunishauri katika masomo yangu na mambo mengine ya kimaisha. Kwangu Dr. Mekacha hakuwa mwalimu tu bali rafiki na mshauri.

Ni kwa sababu hizi ndiyo maana nimeamua kuhariri kitabu ili kumkumbuka na kumuenzi. Kitabu hiki (ambacho maelezo yake mafupi yapo hapa chini) kiko tayari kwenda kwa mchapishaji. Kitu pekee kinachonikwamisha ni picha. Mchapishaji amesisitiza sana kwamba itapendeza kama kutakuwa na picha ya Dr. Mekacha ambayo itawekwa mwanzoni mwa kitabu hicho. Juhudi zangu za kupata picha zake hata hivyo zimekwama kabisa. Kama ningeweza kwenda Tanzania ningeenda nyumbani kwao Nata Serengeti kuzitafuta.


Kutokana na tabia yake ya ucheshi na uanaharakati pamoja na kutambulika kwake, nashawishika kuamini kwamba lazima kuna wadau ambao wana picha zake. Kama mpo basi naomba sana mnitumie picha zake zo zote zile kupitia barua pepe ifuatayo: profesamatondo@gmail.com. Pia kama kuna mdau ambaye yuko Musoma/Serengeti na angependa kunisaidia kwenda kijijini Nata Serengeti kufuatilia picha basi naomba tuwasiliane. (Ng'wanambiti upo?). Nitalipia kila kitu.
Natanguliza shukrani zangu za dhati.

Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

Chuo Kikuu cha Florida

*********************************************************
KUHUSU KITABU CHA KUMBUKUMBU YA DR. MEKACHA

Kitabu kinaitwa: “Bantu Languages and Linguistics: Papers in Memory of Dr. Rugatiri Mekacha”. Ni mkusanyiko wa makala (16) nzuri za masuala ya lugha na isimu katika lugha za Kibantu. Makala hizi zimeandikwa na wanaisimu wenye umashuhuri duniani kote na tunatumaini kwamba kitabu hiki kitatoa mchango mkubwa katika kuzieleza na kuzifafanua lugha za Kibantu ambazo kusema kweli bado zinahitaji kufanyiwa uchambuzi wa kina wa kiisimu kulingana na nadharia za kisasa. Lugha zilizochambuliwa katika kitabu hiki ni Kiswahili (makala mbili - moja imeandikwa kwa Kiswahili), Kisukuma (makala mbili), Kisetswana (makala mbili - Botswana na Afrika Kusini), Kikurya, Kichewa (Msumbiji na Malawi), Kilungu (Zambia), Kikhayo (Kenya), Kibemba (Zambia) na Kihaya. Pia kuna karatasi nne zinazojadili masuala mbalimbali ya lugha nchini Tanzania; ikiwemo sera mpya ya lugha ambayo inapendekeza kukifanya Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi.

Monday, January 11, 2010

BINADAMU NA TAMAA YAKE YA KUJIFURAHISHA - ATI, KWA NINI UNAPENDA MCHEZO UUPENDAO?


  • Katika ung'amu fiche (subconscious) wake, nadhani binadamu anafahamu kwamba ana muda mfupi sana hapa duniani. Kutokana pia na ukweli kwamba anakoenda baada ya kukamilisha safari yake hapa duniani hakueleweki, inamlazimu ajifurahishe kwa kadri inavyowezekana wakati akiwa hai hapa duniani.
  • Pengine hii ndiyo sababu mojawapo iliyomfanya agundue michezo mbalimbali. Michezo mingi ya binadamu ukiichunguza vizuri hata unashindwa kupata maana yake hasa ni nini. Chukulia kwa mfano soka - mchezo nambari wani duniani. Watu ishirini na wawili wanashindania kitu cha mviringo na yule anayefanikiwa kumzidi mwenzake na kukiingiza kitu hicho cha mviringo kwenye nguzo mbili zilizosimikwa ardhini, basi anakuwa amefunga goli. Hapo tena binadamu hushangilia na kurukaruka kwa furaha isiyopimika na wengine huwa hawali wala kulala, na wale sugu wapo tayari hata kupoteza maisha yao ili kutetea timu zao wazipendazo.
  • Hebu ichunguze vizuri michezo mingine mfano "golf", mpira wa kikapu, mpira wa magongo, 'baseball', rugby na mingineyo. Kwenye ''golf", mtu anagonga kampira kadogo keupe kwa kutumia gongo maalum na kukaingiza kwenye kashimo kadogo. Wallah! Makofi na vigelegele...Binadamu anatumia mamilioni ya dola katika kujifurahisha na wachezaji ndiyo watu wanaoongoza kwa kulipwa vizuri!
  • Michezo niipendayo mimi ni ile ambayo kwa kiasi fulani inamwonyesha binadamu kama mnyama. Hii kidogo inamwondolea binadamu lile kunguku lake la U-homo Sapiens na "utakatifu" wake; na kuuanika unyama wake hadharani. Nadhani ndondi/masumbwi unaangukia katika kundi hili. Hali kadhalika "Bull Riding". Waweza kunishangaa lakini ukweli ni kwamba binadamu bado ni mnyama na matendo yake mengi yanathibitisha dai hili. Niambie - kwa mfano - inawezekanaje "binadamu" fisadi aibe "vijisenti" vyote vya umma, yeye na familia yake wawe matajiri wa kutupwa na kuwaacha binadamu wenzake waliompa madaraka wakiwa masikini hohehahe kabisa wasiojua hata watakula nini? Unataka kuniambia kwamba mtu huyu kweli ni "Homo Sapiens?". Huwa anahisi na kufikiri nini anapowaona watu aliowaibia wakihangaika katika umasikini na ukosefu wa huduma za msingi? Tazama vizuri halafu uniambie - ubinadamu na U-homo Sapiens wa binadamu uko wapi?
  • Waroma wa kale wao walijenga Colosseum - mtangulizi wa viwanja vya kisasa vya michezo - ambamo inasadikiwa kwamba wapiganaji mashujaa (gladiators) na binadamu wengine wapatao laki tano (500,000) pamoja na wanyama zaidi ya milioni moja walipoteza maisha yao katika michezo ya kutisha iliyokuwa inachezwa humo.
  • Hivi karibuni kumezuka mchezo mpya ambao unaupiku ule wa masumbwi kwa ukatili na unyama wake (tazama video ya kwanza hapa chini). Katika mchezo huu, hata ukimwangusha mpinzani wako, unaruhusiwa kuendelea kumporomoshea mangumi na mateke haidhuru hata kama ameshafleti!
  • Kutokana na ukweli kwamba mchezo huu umeinukia kuwa maarufu sana kwa muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake, ni wazi kwamba binadamu wenye shauku ya kuona unyama wa binadamu ukianikwa kama mimi ni wengi. Ati, wewe unapenda mchezo gani? Unajua ni kwa nini unaupenda mchezo huo?
***************************************

Rampage Jackson - Yeye huwabeba wapinzani wake na kuwabamiza chini!



Hapa "Homo Sapiens" anahangaika na madume ya ng'ombe

Friday, January 8, 2010

ZUMA YUKO SAHIHI!!!

  • Rais Zuma wa Afrika Kusini alipooa mke wa tano hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari pamoja na watu binafsi nje na ndani ya Afrika walimwandama sana. Katika kujitetea kwake alisema hivi (nanukuu):

    “There are plenty of politicians who have mistresses and children that they hide so as to pretend they are monogamous. I prefer to be open. I love my wives and I am proud of my children.”
  • Kuna anayebisha kuhusu hili suala la nyumba ndogo ambalo Bwana Zuma analizungumzia?

Thursday, January 7, 2010

UDSM YATOA MILIONI NANE KUSAIDIA SHULE ILIYOHARIBIWA NA MABOMU MBAGALA

  • Katika makala yangu ya jana, niliyalalamikia makampuni kujikita katika sekta ya urembo na kuacha kusaidia sekta za msingi za kijamii kama elimu na miundo mbinu (hasa vijijini). Nimefurahi leo nilipotembelea blogu ya jamii, na kukutana na habari hii nzuri ambapo Chuo Kikuu cha Dar es salaam kimetoa msaada wa milioni nane kusaidia shule moja ya sekondari kule Mbagala ambayo iliharibiwa na miripuko ya mabomu. Huu ni mfano wa kuigwa kwa makampuni mengine, taasisi mbalimbali na hata watu binafsi. Picha na maelezo yote hapa chini ni kutoka blogu ya jamii.
*******************************************************************************

Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala (Mwenye suti) akikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi Milioni nane kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Mbagala Dar es Salaam Mwl. Marcelina Kimario ikiwa ni michango ya wafanyakazi na wanafunzi wa UDSM kwa shule hiyo ili zisaidie kukarabati sehemu ya madarasa iliyoharibika kufuatia ajali ya milipuko ya mabomu iliyotokea mwezi Februari mwaka jana.

Makabidhiano hayo yamefanyika shuleni hapo mbele ya viongozi akiwamo diwani Mh. Charles wa kata ya Mbagala Kuu, waalimu na wanafunzi wa shule hiyo. Wengine waliofuatana na Prof. Mukandala ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Jamii Prof. Amandina Lihamba (wa Kwanza kushoto), Mkuu wa Shule ya Elimu Prof. E. Bhalalusesa(wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na utawala Bw. Edward Jambo (hayuko pichani).

HILI NI TUNDA GANI?

  • Tunda hili linapatikana sana katika mikoa ya kanda ya Ziwa (hasa Usukumani na Unyamwezini), mikoa ya kati na sehemu zingine kame kame.
  • Tulizoea kulila wakati ule tukiwa wadogo wakati tunachunga ng'ombe. Mpaka leo nikienda nyumbani huwa naenda porini kulitafuta kama ni wakati wa majira yake. Picha ya huyu bwana mdogo imenikumbusha maisha mazuri ya utoto kijijini miaka ileee! Nimekumbuka!
(...Sikumbuki picha hii niliipata wapi!). Mwenye picha ameshajitokeza. Ni Meshack Maganga wa http://magangam.blogspot.com. Samahani mkuu!!!

Wednesday, January 6, 2010

MAKAMPUNI YETU NA "JINAMIZI" LA MASHINDANO YA UREMBO


Profesa Mbele amekuwa akisema mara kwa mara kwamba Watanzania tunapenda sana kuponda raha. Tunachangishana mamilioni ya shilingi ili kufanya harusi za kifahari lakini hatuwezi kuchangishana ili kujenga shule au kununua madawati kwa ajili ya watoto wetu wanaosomea chini; au kuchimba visima vya maji vijijini tulikotoka. Tunasema hii ni kazi ya serikali.

Kwangu mimi swali ambalo nimekuwa nikijiuliza ni hili: ni kwa nini makampuni mengi yanamwaga mamilioni ya shilingi kila kukicha ili kufadhili mashindano ya urembo ambayo yametanda kila kona (Miss Tanzania, Miss mkoa, Miss Wilaya, Miss Tarafa, Miss Kata, Miss Kitongoji, Miss Kijiji, Miss familia?, Miss Totoz, Miss chuo kikuu, Miss vyuo vya Ualimu, Miss Shule za Msingi, Miss Chekechea, Miss Serengeti Breweries, Miss Vodacom, Miss Tigo, Miss…)?

Inavyoonekana hakuna kabisa shida ya ufadhili katika mashindano kama haya na starehe nyinginezo. Vipi kama tungeelekeza nguvu hizi katika uimarishaji wa sekta zinazotoa huduma za kijamii hasa kule vijijini? Tungeweza kuchimba visima vya maji vingapi? Tungeweza kununua madawati mangapi? Tungeweza kujenga mashule mangapi?

Mwanzoni niliyalaumu makampuni haya kwa hoja kwamba mengi ni ya kigeni na kwa hivyo hayana moyo wa kizalendo wa kujihusisha na miradi ambayo kweli inaweza kuleta mabadiliko ya kudumu katika jamii. Baada ya kufikiri sana, nimegundua kwamba sina haki ya kuyalaumu makampuni haya. Yenyewe yapo kwa ajili ya lengo moja tu – kufanya biashara na kujipatia faida - tena kubwa kwa kadri inavyowezekana! Ili kufikia lengo hili, inabidi yatangaze bidhaa na huduma zake kwa umma. Mashindano ya urembo ni njia mojawapo nzuri sana ya kufikia wateja wengi kwa kadri inavyowezekana tena kwa wakati mmoja.

Mashindano haya ya urembo yanatangazwa sana na vyombo vya habari (televisheni, redio na magazeti) tangu washindani wakiwa katika maandalizi, wanapoingia kambini kujifua na mpaka siku yenyewe ya mchuano. Na mara nyingi wageni waalikwa katika mashindano haya ni viongozi wakubwa wakubwa wa serikali (aka vigogo). Wakati mwingine washiriki wake (eti “warembo!”) wanafikia hadi kualikwa ikulu ambako wanaandaliwa mlo maalum (dinner) na kupata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa nchi. Wanafanyiwa yote haya kwa sababu tu ya kuwa washiriki wa mashindano ya urembo!. Mambo yote haya yanatangazwa na vituo mbalimbali vya televisheni na ni wazi kwamba hii ni nafasi nzuri sana kwa makampuni haya kutoa milioni chache na kupata muda mzuri mrefu wa kujitangaza. Hivi karibuni, kwa mfano, Miss Vodacom Tanzania wa (2009) alipokelewa jijini Mwanza kama “ngole” (malkia) na jiji zima lilizizima.. Kampuni la Vodacom lililokuwa limedhamini mashindano hayo lilikuwepo pale ili kutunisha misuli yake ya kibiashara.

Washiriki wa Miss East Africa (2009) katika "dinner" Ikulu

Ukijitolea kujenga shule, kuchimba visima vya maji au kununua madawati kule kijijini, ni chombo gani cha habari kitakachotangaza habari hizi hasa ukizingatia kwamba vyombo vyote vya habari vimejikita mijini na kamwe haviripoti habari za vijijini (isipokuwa matukio ya kutisha kama mauaji ya vikongwe na albino). Ni waziri gani atakayeacha raha zake za mjini aje kuhudhuria ufunguzi wa visima vya maji au shule kule kijijini? Unafikiri utaalikwa kwenda kula “dinner” Ikulu eti kwa kuwa umenunua madawati kusaidia wanafunzi waliokuwa wanasomea chini?

Kwa hivyo, hili si tatizo la makampuni haya kukosa uzalendo. Ni tatizo letu sisi kama jamii. Mwamko na mkazo wetu haupo katika mambo ya msingi na hasa yale yanayowakera na kuwatesa Watanzania wenzetu wanaokaa vijijini (ambao ndio wengi). Huduma zote muhimu zimerundikana mijini (ingawa nako si wote wanaozipata) na hata vyombo vya habari ambavyo vina jukumu kubwa katika kuelimisha na kuiamsha jamii navyo pia vimebakia kuwa mijini. Hata vyama vya siasa vya upinzani vimeingia katika mkumbo huu (halafu eti vinategemea kuishinda CCM yenye mabalozi wa nyumba kumi kumi katika kila kijiji!). Tunahitaji mabadiliko ya kifikra kama kweli tunataka kuleta mabadiliko ya msingi na ya kudumu katika jamii yetu. Na vijijini ndipo mahali hasa pa kuanzia!

Tuesday, January 5, 2010

MNAKARIBISHWA KANISANI, LAKINI MCHUNGE NDIMI ZENU KWANI.....

NIMEGUSWA SANA NA PICHA HIZI ZA MAREHEMU SIMBA WA VITA

  • Hapa ni wakati akiwa amelazwa Muhimbili. Hii ni nadra kwani tumezoea kuona wakubwa hawa wakikimbizwa "bondeni" au kwa malkia wanapougua utafikiri kwamba kwa kufanya hivyo kifo hakitawabamba. Nimeiangalia picha hii mara nyingi sana!

  • Hata jeneza na kaburi lake Mtanzania huyu halisi ni la Kitanzania - si yale majeneza yaliyoagizwa kutoka nchi za nje, majeneza ghali yaliyonakshiwa na kupambwa kistadi kwa vito na manemane.
  • Hii ndiyo nyumba ya kudumu ya Komredi Simba wa Vita. Hebu Mola na ampe pumziko jema mwana huyu halisi wa Tanzania aliyeipenda nchi yake na kuitumikia kwa moyo wake wote!
Hapa chini ni sehemu ya makala nzuri ya mhariri wa gazeti la Kulikoni yaliyochapishwa jana katika ukurasa wa saba wa gazeti hilo.

********************************************************************************

Yeye na Mwalimu Julius Nyerere mbali na kutotaka masihara kazini walionyesha maisha ya kutojilimbikizia mali. Mzee Kawawa alipotoka madarakani wanaomfahamu wanasema hakuwa na kitu na kama si sheria za pensheni kwa wastaafu, angeweza kuwa mmoja wa watanzania wa kusaidiwa kwa michango ya ndugu ili apate kutibu afya yake iliyokuwa ikidorora licha ya kupata kuwa kiongozi mkuu kitaifa.


Ndio maana aliweza kwenda kuishi eneo kama Madale, nje ya Dar es Salaam na si Oysterbay au Masaki - Kawawa hakuwa na uwezo wa kujenga sehemu hizo ambako mawaziri wakuu wa miongo hii wamejenga, tena kabla hawajafika alipofika, walishakuwa wamejenga mahekalu.

Ndio maana kwa kutambua mchango wake kwa Taifa ama kwa kupigania utawala bora na haki za watu moja kwa moja au kwa yeye kujinyima na kuwa mfano bora, Januari mwaka 2007, Kawawa alitunukiwa tuzo ya Dk. Martin Luther King.

Moja ya maneno yanayoweza kubaki kuwa wosia kwetu ni yale aliyoyasema wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo ambapo kwa kuwa nilikuwepo wakati akikabidhiwa pale kwenye ubalozi wa Marekani niliiona ari aliyokuwa nayo kutamani kuendelea kutoa mchango wake kwa Taifa ingawa nguvu hakuwa nazo tena kutokana na umri.

“Heshima iliyotukuka mliyonipa si tu imeniletea faraja, bali pia ni kichocheo cha kuendelea kuwatumikia Watanzania pale ambapo nitaweza kuwatumikia bila kujali itikadi zao za kidini au za kisiasa, kwa manufaa ya taifa kwa ujumla,” alisema Kawawa na kuongeza: “Sasa nafuga nyuki na nipo tayari kumfundisha mwenzangu yeyote ufugaji wa nyuki wa kisasa,” alisema akieleza maisha yake baada ya siasa kuwa ni ya ukulima.

Pia katika hotuba yake hiyo aliasa viongozi na wanasiasa akisema: “Naomba mtupie macho makundi madogo madogo ambayo sauti zake hazijasikika, yapatiwe misaada ili yapate uwezo wa kujikwamua kiuchumi, yapate fursa sawa katika jamii ili uwezo walionao utumike kuleta maendeleo.”

Mimi sikuwa na mabilioni ya fedha, hivi ningeyapata wapi? Mwalimu Nyerere hakuwa mtu mwenye tamaa, hata hakujilimbikizia mali, hii iwe ni changamoto kwa wana CCM.

Monday, January 4, 2010

"MAUAJI YA HALAIKI" YA WATOTO TANZANIA KUPITIA LUGHA YA KUFUNDISHIA...

  • Nimevutiwa na jina la kitabu hiki. Kuna aliyekisoma? Kinapatikana madukani? Nakitafuta sana!

  • Mwandishi wake ni mmojawapo wa watu muhimu sana katika fasihi ya Kiswahili.

NANI ALISEMA ETI WAAFRIKA SI WADADISI?

  • Unaiona hii pool table? Si ajabu ukakuta hata wana sheria zao wenyewe zinazoendana na mazingira yao...

  • Nilikuwa mbali na kompyuta kwa siku kadhaa na sasa nimerudi. Libeneke kama kawaida...Natumaini nyote mlikuwa na sikukuu njema. Hebu basi mwaka mpya (2010) na ukawe na mafanikio kwenu nyote!

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO