NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, March 28, 2010

NENDENI MKASALI KWANZA, POMBE MTANUNUA MKITOKA MAKANISANI!

  • Hapa Florida (na naamini hata katika majimbo mengine) siku za Jumapili vilevi haviuzwi mpaka ifike saa saba mchana. 
  • Nilipoulizia niliambiwa kwamba lengo la sheria hii lilikuwa/ni kuwahimiza watu kwenda makanisani kuabudu nyakati za asubuhi badala ya kuanza kuhangaika na pombe. 
  • Hata hivyo mtu unaweza kujiuliza, kama mtu hataki kwenda kanisani siku za Jumapili na badala yake anataka kuanza kuzitwika asubuhi asubuhi, kuna ugumu gani wa kujinunulia kilevi akipendacho mapema?

Thursday, March 25, 2010

"BLOGGING FOR DUMMIES" NA ELIMU YETU YA JADI

  • Leo katika pitapita yangu katika duka moja la vitabu nilikutana na kitabu hicho juu. Niliamua kukisoma na nilishangaa kugundua kwamba mambo mengi ya msingi yanayozungumziwa humo tayari ninayafahamu. Na kama ilivyo kwa wanablogu wenzangu wengi, hakuna aliyetufundisha kublogu na wala hatukuhitaji kusoma vitabu. Tulianza tu, tukajifunza kwa vitendo na sasa tunaweza - kwa kiwango chetu. Tunapokwama tunakimbilia kwa "mkombozi" wetu Dada Subi. Hivi pia ndivyo wengi wetu tulivyojifunza kutumia kompyuta. Hatukuhitaji kusoma vitabu. 
  •  Kimsingi hii ndiyo ilikuwa elimu yetu ya Kiafrika ambayo ilikuja kuvurugwa na wakoloni. Sisi hatukuhitaji kusoma vitabu bali elimu yetu ilikuwa ni ya vitendo na iliyoendana vyema na mazingira yetu. 
  • Japo bara letu liliitwa kuwa la giza na lenye watu wasio na historia wala ustaarabu (kwa vile historia yetu ilikuwa haikuandikwa), leo hii watu wengi wanasaili uamilifu wa elimu tuliyoletewa, elimu ambayo, pamoja na faida zake nyingi, mara nyingi imeonekana kuwa ni dhahnia sana na  isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na mazingira yetu.  Mara nyingi elimu hii haimwandai aipataye kwenda kupambana na mazingira na ulimwengu halisi.
  • Elimu ya kweli ni lazima izingatie misingi hii ya elimu yetu ya kiasili na naamini kwamba lilikuwa ni kosa kutupilia  mbali kila kitu tulichokuwa nacho katika elimu yetu ya jadi. Kusoma vitabu tu darasani bila kuelewa maarifa hayo ya vitabuni yana faida gani katika ulimwengu halisi na mazingira yetu ni kuelimika nusunusu tu.
  • Watunga sera za elimu inabidi wazingatie ukweli huu kama kweli wanataka kuwa na taifa la wananchi WALIOELIMIKA! 

Wednesday, March 24, 2010

LUGHA TUNAYOTUMIA INAONYESHA UNDANI WETU: TUWE WAANGALIFU

  • Misahafu mbalimbali inaonya kuhusu hatari za ulimi; kwamba ni kiungo kidogo lakini madhara yake ni makubwa. Wanasaikolojia wengi na "watenda miujiza" wanaamini kwamba maneno yana nguvu (unakumbuka mambo ya laana?). Inasemekana kwamba hata dunia iliumbwa kwa maneno tu!
  • Wanaisimu jamii pia hudai kwamba lugha anayotumia mtu inaweza kumwonyesha yeye ni mtu wa tabaka gani katika jamii hiyo. Kwa hivyo, kama wewe ni mtu wa tabaka la juu, jamii inakutegemea uongee kwa mtindo fulani unaolitambulisha tabaka lako. Kama wewe ni kiongozi, jamii pia inakutegemea kutumia lugha fulani inayoakisi wadhifa wako katika jamii. Na kama wewe ni mwanamuziki wa kizazi kipya/Bongo fleva/kufokafoka kuna mitindo fulani ya lugha inayokutambulisha ambayo pengine kiongozi au mtu wa tabaka la juu hategemewi kuizungumza.
  • Suala hili limeibuka hapa Marekani baada ya makamu wa Rais Joe Biden kutumia neno "fuck" wakati akimpongeza bosi wake (Obama) kwa kufanikiwa kupitisha sera mpya tata ya mfumo wa matibabu. Kama Snoop Dogg au 50 Cent angelitumia neno hili, nadhani pengine hakuna ambaye angejali sana lakini halitegemewi kutamkwa na makamu wa rais.
  • Tuwe waangalifu na lugha tunayotumia. Maneno yanaweza kuumiza na kuleta makovu ya kisaikolojia yasiyotibika. Msikilize Joe Biden hapa na watu wengine waliowahi kutumia lugha isiyo mwafaka kulingana na matabaka yao hapa na kuibua mijadala mikali. 

    Tuesday, March 23, 2010

    UTAFITI: UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME UNAWEZA KUWA NI DALILI ZA MAGONJWA YA MOYO

    • Kama unahitaji Mkuyati au Supu ya Pweza kabla ya ligwaride, basi ni vyema ukachunguze afya ya moyo wako. 
    • Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la Circulation: Journal of the American Heart Association la mwezi huu unaonyesha kwamba wanaume wanaousumbuliwa na matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume (uzimbezimbe) wana uwezekano mkubwa zaidi ya mara mbili wa kuugua magonjwa ya moyo kuliko wenzao wasio na tatizo hilo.  
    • Utafiti mwingine uliofanywa na madaktari wa hospitali maarufu ya Mayo Clinic unaonyesha kwamba wanaume wenye matatizo ya nguvu za kiume wana uwezekano wa kuugua magonjwa ya moyo kwa asilimia 80 zaidi kuliko wenzao wasio na tatizo hilo. 
    • Japo tatizo la upungufu wa nguvu za kiume linaweza kusababishwa na sababu za kisaikolojia, wataalamu wanashauri kwamba ni vizuri watu wenye tatizo hili wachunguze afya ya mioyo yao badala tu ya kukata njia za mkato kama kula Viagra, mkuyati au Supu ya Pweza.   
    • Kwa habari zaidi juu ya utafiti huu soma hapa na hapa.

    Monday, March 22, 2010

    SWALI LA KIZUSHI: "KITCHEN PARTY" NI NINI HASA? INA UMUHIMU GANI KATIKA ARUSI NA NDOA KWA UJUMLA?

    Picha ni kutoka Blogu ya Zeze
    • Pengine nianze kwa kusema kwamba pengine mimi ni "mshamba" au "Old school" na inawezekana kidogo "nimefulia". Baada ya kukaa Marekani kwa miaka karibu 10 sasa nimejikuta Kiswahili changu kinaanza kudorora na mambo mengi yamekuwa yanabadilika kwa haraka kiasi kwamba si rahisi kwenda nayo sambamba. Hata neno kufulia lenyewe ilibidi niulize lina maana gani.  
    • Hivi karibuni nimekuwa nikisoma mara kwa mara kuhusu "kitchen party" na kusema kweli nimekuwa sifahamu hasa undani wake ni nini. Kitchen party ambayo imenivutia sana mpaka imebidi niulize swali hili ni hii iliyowasilishwa katika Blogu ya Shamim "Zeze" Mwasha. Ati, kitchen party ni nini hasa? Ina nafasi na umuhimu gani katika mchakato mzima wa harusi na ndoa? Tangu hapo kuuliza si ujinga ati! Asanteni.

    HUYU MWIZI ALIWAZA NINI?

    • Mwizi mmoja ametoa kali ya mwaka baada ya kuwarahisishia polisi kazi ya kumkamata. Alianza kwa kuingia katika duka la samani za ofisini liitwalo Bella Office Furniture usiku.
    • Badala ya kufanya kilichompeleka (kuiba), mwizi huyo mwenye miaka 17 alitumia masaa matano akiwa mtandaoni akitumia laptop aliyoikuta humo dukani. Katika hayo masaa matano aliweza kuangalia ngono na alijaribu kuuza baadhi ya vitu vya wizi mtandaoni. Kosa kubwa alilofanya ni kufungua "akaunti" yake ya MySpace wakati akiwa dukani humo. 
    • Kesho yake polisi hawakuwa na shida ya kumkamata kwani akaunti yake ya MySpace ilikuwa na habari zake zote ikiwemo jina lake, anuani na namba yake ya simu. Ati, mwizi huyu aliwaza nini? Au naye ni walewale wanaume laptop kama wa kule Mataranyirato? Tazama hapa.

    Sunday, March 21, 2010

    ANZIA SEKUNDE YA 35: NI W. KLITSCHKO JANA ALIPOMFLETISHA EDDIE CHAMBERS

    • Pambano hili lilifanyikia Ujerumani ambako akina Klitschko wanapendwa sana. Pambano hilo lilihudhuriwa na watu zaidi ya 50,000! Sababu yangu kubwa ya kupenda masumbwi iko hapa.

    Saturday, March 20, 2010

    LINI ZITAPIGWA BUNGENI CHIMWAGA? STAILI YA KICHINA MPAKA LINI?

    UTURUKI

    TAIWAN

    KOREA YA KUSINI

    URUSI

    MEXICO

    JAPAN

    INDIA

    ITALIA

    *******************
    NA MWISHO - CHINA

    Asante "dad" kwa picha hizi...

    JAPO KILIO NI TIBA, TAFADHALI USILIE MBINGUNI....


    Kama ungeangua kilio mbinguni, kila mtu angeangua 
    kicheko akidhani kwamba ulikuwa unatania tu.

    Friday, March 19, 2010

    FIKRA YA IJUMAA: MASWALI YASIYO NA MAANA YO YOTE

    1. Ati, kama mtu angekuita kwa jina lisilo lako, ungeitika?
    2. Leo unafikiri kwamba unachofikiri ndicho unachofikiri?
    3. Unafikiri kwamba unachokifikiri kwa sasa ndicho unachopaswa kukifikiri?
      Fikiri!!!
      Wikiendi njema.

      Thursday, March 18, 2010

      MWANAFUNZI MLEMAVU KUTOKA GHANA APIGWA RISASI USONI NA POLISI WA CHUO

      • Kama wiki mbili hizi zilizopita, tukio la kushangaza lilitokea hapa chuoni. Mwanafunzi mmoja anayesoma shahada ya Uzamifu (PhD) katika idara ya Jiografia alipigwa risasi usoni na polisi wa chuo. Inasemekana taya lake limefumuliwa kabisa na inabidi lipangwe upya na madaktari mabingwa wa upasuaji rekebishi.
      • Mwanafunzi huyu alikuwa na tatizo la kuwa na wasiwasi na "jazanda"; na alikuwa anadhani kwamba kuna watu waliokuwa wanataka kumuua. Mwalimu na msimamizi wake wa tasnifu aliwapigia simu polisi na kuwaomba wakamwangalie na kuona kama alikuwa anahitaji kumwona daktari wa akili ili kupata msaada.
      • Polisi walikwenda na kuzungumza naye; na walifikia hitimisho kwamba alikuwa mzima na hakukuwa na sababu ya kumpeleka kwa daktari wa akili. Hata hivyo kesho yake hali yake ilibadilika na alijifungia chumbani mwake na kuanza kupiga makelele. 
      • Polisi walipoitwa walimwomba afungue mlango na alipokataa wakavunja mlango na kuingia ndani. Habari zinasema kwamba walipovunja mlango walijaribu kumkamata lakini walishindwa pamoja na kutumia risasi za bandia na kujaribu kumpiga shoti ya umeme. Wanadai kwamba waliposhindwa, walimwona eti akiwajia akiwa na bomba la chuma. Ndipo polisi mmoja akamtandika risasi usoni. 
      • Hata hivyo imekuja kugundulika kwamba mwanafunzi huyu aliugua ugonjwa wa polio alipokuwa mtoto na ni mlemavu wa miguu. Kwa hivyo huwa anatembelea fimbo na hilo walilodhani kwamba lilikuwa ni bomba la chuma kumbe ilikuwa ni fimbo yake inayomsaidia kusimama na kutembea. 
      •  Kibaya zaidi mwanafunzi huyu amefunguliwa mashtaka makubwa zaidi ya matatu na japo bado yu taabani hospitalini, analindwa usiku na mchana na polisi na wanasema siku akipata nafuu basi watampeleka selo kwa makosa mengi tu likiwemo la kuwatishia uhai polisi.
      • Watu wamebaki wanajiuliza: inawezekanaje polisi watano washindwe kumkamata na kumtuliza mtu mmoja ambaye ni mlemavu wa miguu mpaka wampige risasi usoni? Jana wanafunzi walifanya maandamano kwenda kwa mkuu wa chuo na bodi ya usimamizi ambayo ilikuwa inafanya kikao chake hapa. Katika maandamano hayo  wanafunzi na walimu walidai kwamba, mbali na mambo mengine, mashtaka yote dhidi ya mwanafunzi huyu yafutwe na polisi aliyempiga risasi afukuzwe kazi mara moja.
      • Wengine tayari wameanza kuingiza hisia za ubaguzi wa rangi na kudai kwamba hawaamini kama kweli mwanafunzi huyu angepigwa risasi kama asingekuwa mweusi.
      • Kwa habari zaidi kuhusu mkasa huu soma hapa.

      Wednesday, March 17, 2010

      UTAJIRI WETU UNAPOGEUKA LAANA. KUNA NINI NORTH MARA GOLD MINE???

      • Japo nilikuwa nimeshawahi kusoma juu ya athari za kimazingira zilizosababishwa na mgodi wa dhahabu wa North Mara, picha hizi kubwa zimenisikitisha sana (bofya mojamoja utazame vizuri)
      • Ni kweli tu masikini kiasi cha kukubali kufanyiwa hivi, eti tu wawekezaji hawa wasiojali wachimbe dhahabu nasi tufaidike? Pengine sielewi kiini hasa cha sakata hili lakini kwa vyo vyote vile, hali hii inatia huzuni na kusikitisha sana. Halafu ukitazama mapendekezo ya serikali kuhusu suala hili (tazama chini ya post hii), mtu unatikisa kichwa na hata kupata kizunguzungu.


      Edit: Ripoti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyotolewa Juni 4, 2009 inaishia hivi:
      *************************
      Recommendations:

      - Local village residents around the mine should be educated on the environmental impacts caused by vandalism and theft of liners...

      - There should be timely reporting of various incidents by the mine to the licencing authority.

      - It is proposed that liners be covered with compacted thick materials as deterrent to vandalism and theft.

      - Mine management should work on ways to ensure that such environmental incidents do not occur in the future.
      ***************************
      Picha zote ni kutoka hapa; na mapendekezo ya ripoti ya serikali yapo hapa. Unaweza pia kusoma hapa kuhusu suala hili. 

      EMBE LILILOCHUMWA NA LILILOACHWA LIKAIVIA MTINI

      • Embe lililochumwa na lile lililoachwa likaivia mtini mpaka likadondoka lenyewe yanaweza kuwa na ladha tofauti
      (Nilikuwa nafikiria jambo fulani la muhimu ndipo nikamkumbuka 
      mjomba wangu mmoja aliyekuwa na miembe mingi sana...)

      HII IMEKAA VIZURI: POLISI AKATAA RUSHWA YA DOLA 3,000. ATUZWA TSH. 4,000,000!!!

      • Askari namba E. 7235 PC John Anthony Mwesongo wa kituo cha polisi cha Polisi Kiwanja cha ndege cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye ni mtunza vielelezo wa kituo hicho, akionyesha hundi ya T. Sh. 4,000,000 motisha baada ya kukataa rushwa ya dola za kimarekani 3,000 na watu waliokamatwa na madawa ya kulevya waliomtaka abadilishe vielelezo hivyo. 
      • Hundi hiyo alikabidhiwa na Inpekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema Jana  (13/3/2010) katika ukumbi wa maofisa wa polisi Oysterbay Jijini Dar es Salaam. (Picha Na Hassan Mndeme- Jeshi la Polisi) 
      • Hongera PC John Anthony Mwesongo. Wewe ni mfano wa kuigwa! Picha na maelezo ni kutoka kwa Mzee wa Mshitu.

      Tuesday, March 16, 2010

      UTAFITI: VIFO VYA AKINA MAMA WAJAWAZITO VINAONGEZEKA HAPA MAREKANI. WEUSI NDIYO WANAKUFA ZAIDI

      Picha iko hapa.
      • Tukisikia vifo vya akina mama wajawazito kuongezeka mara moja tunafikiria kuwa ni tatizo la nchi za ulimwengu wa tatu. Ndiyo maana ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa hapa Marekani ikionyesha kwamba vifo vya akina mama wajawazito vimeongezeka zaidi ya mara mbili katika miaka 20 iliyopita imewashtua watu wengi.
      • Na kama kawaida, akina mama wanaokumbwa  na masaibu haya kwa wingi ni wale ambao si wazungu; wale ambao ni masikini, wahamiaji na wale ambao hawazungumzi au kufahamu Kiingereza sawasawa. 
      • Idadi ya vifo kwa wanawake wa kizungu ni 9.5 kwa kila mimba 100,000 na kwa Wamarekani weusi ni 32.7 kwa kila mimba 100,000. Unene pamoja na kupenda sana uzazi kwa njia ya operesheni (C-Section) vimetajwa kuwa unachangia katika tatizo hili.
      • Marekani ni nchi ambayo ina mfumo mbaya wa bima ya afya na kama huna bima au ni masikini hapa unaweza kupoteza maisha kwani gharama za matibabu ni kubwa mno. Bado haijulikani kama juhudi za Obama za kuufanyia mabadiliko ya kimsingi mfumo huu zitafanikiwa au zitagonga ukuta kama ilivyotokea kwa maraisi waliomtangulia.
      • Sikiliza na soma habari zaidi juu ya utafiti huu hapa na  hapa.

        POLISI ATUHUMIWA KUTAZAMA VIDEO ZA NGONO KWENYE SIMU YAKE AKIWA KAZINI. AJIUZURU

        • Polisi mmoja katika mji ninaoishi amejiuzuru kazi wakati akiendelea kuchunguzwa kwa kosa la ku-download na kutazama video za ngono katika simu yake aina ya ipod touch (kama hiyo juu) wakati akiwa kazini.
        • Katika kipindi fulani polisi huyo aitwaye Laurence Gilbert alimwomba polisi mwenzake wa kike ajumuike naye katika kutazama video hizo chafu. Badala yake polisi huyo wa kike alikwenda kutoa taarifa kwa bosi wao akidai kuwa alikuwa amenyanyaswa kijinsia.  Habari kamili inapatikana hapa.
        • Sehemu nyingi za kazi zimeshapiga marufuku mambo kama haya na zinafuatilia shughuli zote zinazofanywa na wafanyakazi wao mtandaoni hasa wakati wakiwa kazini. Makampuni mengi pia yanafuatilia mazungumzo ya wafanyakazi wake katika tovuti za kijamii kama facebook na myspace. Mzee wa Changamoto alishawahi kuonya kuhusu jambo hili. Na Mura kutoka kijijini Mataranyirato pia alishawahi kugusia kuhusu wanaume laptop.
        • Tuwe waangalifu!

        JAMII AMBAYO BADO INASHABIKIA MAMBO HAYA INA MUSHKELI!

        • Nina wasiwasi sana na jamii ambayo katika karne hii na wakati huu tulionao bado inafagilia mambo ya kupiga ramli na kusoma alama za vidole kama njia ya mkato ya kufikia malengo yake.
        • Upigaji wa ramli, usomaji wa nyota za watu na alama za vidole vinapochukuliwa kama njia mojawapo muhimu ya kutatulia matatizo ya jamii na kuijengea matumaini ya wakati ujao (mf. bahati, utajiri, mafanikio katika ndoa, kilimo, michezo n.k), jamii hiyo kwa hakika ina lake jambo.
        • Pengine hatupaswi kushangaa ndugu zetu maalbino wanapochinjwa kikatili eti kwa sababu viungo vyao vinafungamanishwa na ngekewa ya utajiri, au watoto wachanga wanapokatwa mikono kwa sababu tu eti viganja vyao vina alama zenye bahati.
        • Ni wazi kwamba jamii ya aina hii ina matatizo na ni wajibu wetu sote kuitafutia dawa. Uongozi bora na elimu makini ndiyo mkakati mama katika kujaribu kuikomboa jamii ya aina hii.

        HII PROGRAMU YA KUREKEBISHIA PICHA IMENIUMBUA

        • Leo nilikuwa najifunza kutumia programu moja ya kurekebishia picha na bila kujua nikajikuta nimefika huku kwenye hizi noti za wenyewe. Hata sijui nilichobonyeza mpaka nikajikuta picha yangu imepotea na badala yake nina hii noti. Na sijui kama nimeshavunja sheria! Nikiswekwa korokoroni kaeni tayari kuja kunikomboa. Kazi kwelikweli!

        Saturday, March 13, 2010

        UTAFITI: ETI WATU AMBAO WANAAMINI KWAMBA HAKUNA MUNGU (ATHEISTS) WANA IQ KUBWA

        • Angalizo: Hii nimeona niisogeze hapa kutokana na mada iliyowekwa kule kwa Kamala.
        Picha ipo hapa.
        • Kama anavyopenda kusema Ng'wanambiti, hili nalo neno. Mtafiti wa Saikolojia ya Kimabadiliko aitwaye Satoshi Kanazawa wa Chuo cha Uchumi na Sayansi ya Siasa cha London amefanya utafiti unaoonyesha kwamba, mbali na mambo mengine, watu wasioamini kwamba kuna Mungu (atheists) wana IQ kubwa kuliko wenzao wenye imani hiyo.
        • Kwa kufuata mawazo mapya yanayopingana na matapo makuu ya kiitikadi na kifalsafa yanayotawala katika kipindi wanachoishi, watu hawa wasioamini katika Mungu au wanaopinga itikadi za kihafidhina wanakuwa na nafasi ya kusonga mbele kwa haraka zaidi kimabadiliko kuliko wenzao wasiofanya hivyo. Na watu wenye akili sana ndiyo wana uwezekano mkubwa wa kufuata mawazo na itikadi hizi mpya kinzani.
        • Utafiti huo umeonyesha kwamba vijana ambao walijitambulisha kama wahafidhina halisi (very conservative) walikuwa na IQ ndogo ya 95 wakati wenzao waliojitambulisha kuwa ni waliberali halisi (very liberal) walikuwa na IQ kubwa ya 106.

        • Utafiti huu ulifanyika Marekani ambako kimsingi wahafidhina, mbali na mambo mengine, wanaamini kwamba kuna Mungu, wanapinga utoaji wa aina yo yote wa mimba, ndoa za jinsia moja na huduma za bure za kijamii. Kwa upande mwingine waliberali si lazima waamini katika Mungu, wanaunga mkono utoaji wa mimba na hawahangaishwi sana na ndoa za jinsia moja.
        • Watu wasiokula nyama (vegetarians) wana uwezekano mkubwa wa kuwa waliberali na kwa ujumla wana IQ kubwa kuliko wenzao wanaokula nyama. Kutokula nyama kwenyewe kunaweza kuchukuliwa kuwa kama njia mojawapo ya kujionyesha kuwa una akili au ni bora zaidi. Kamala upo? Ripoti kamili juu ya utafiti huu inapatikana hapa.
        • Eti jamani, mnauonaje utafiti huu?

          Picha iko hapa.

        Friday, March 12, 2010

        KITABU CHA UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA CHA MWL. NYERERE SASA KINAPATIKANA MTANDAONI!


        • Leo katika pitapita yangu mtandaoni nilikutana na habari nzuri zinazohusu kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere na kuchapishwa na Zimbabwe Publishing House mwaka 1994. Kitabu hicho sasa kinapatikana mtandaoni na unaweza kujipatia nakala yako hapa.
        • Inasemekana kwamba Mwalimu Nyerere mwenyewe alishindwa kukichapishia nchini Tanzania kwani hakuna mchapishaji aliyetaka kukigusa ndiyo maana ikambidi akimbilie Zimbabwe kwa rafiki yake Mugabe.
        • Kitabu hiki pia hakipatikani kwa urahisi nchini Tanzania na kuna tetesi zisizothibitishwa kwamba eti kimepigwa marufuku. Kama tetesi hizi zina ukweli wo wote, basi nitashangaa kwani hakuna neno baya la kushangaza ambalo Mwalimu Nyerere analizungumza katika kitabu hiki. Mimi nilikinunua kwa bahati jijini Dar es salaam mwaka 1994 na nakumbuka muuza duka la vitabu aliyeniuzia aliniuzia kwa siri sana.
        • Ni kitabu ambacho kinafaa kusomwa na kila Mtanzania bila kujali itikadi yake ya kisiasa. Na kama nilivyowahi kugusia hapa, video, kaseti na vitabu vyote vya Mwalimu Nyerere vinapaswa kutazamwa kama hifadhi ya historia ya taifa letu na ni vyema vikakusanywa na kuwekwa mahali pamoja ambapo kila Mtanzania (au mtu yeyote duniani) ataweza kuvisoma. Kidogo inashangaza kusikia eti vitabu vya Mwalimu na hotuba zake hazipatikani; au zimefichwa katika makabrasha ya Redio Tanzania na kwingineko. Jamani, Mwalimu Nyerere ni hifadhi na hazina ya Watanzania wote na msijimilikishe kazi zake na kuzificha kwa manufaa yenu binafsi.
        • Baadhi ya nukuu muhimu kutoka katika kitabu hiki zinapatikana hapa na hapa. Unaweza pia kusikiliza hotuba mbalimbali za Mwalimu hapa. Na sasa unaweza kupata nakala yako ya kitabu kizima cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania hapa. Asanteni "wanaume" wa Jamii Forums kwa kuweka nakala ya kitabu hiki katika mtandao. Mungu Ibariki Tanzania!

        HUYU MZEE ALISHAUA WANGAPI?

        FIKRA YA IJUMAA: ATI, BINADAMU ANGEKUWAJE KAMA ANGEZIBWA MATUNDU YAKE YOTE? (E. KEZILAHABI)

        • Euphrase Kezilahabi (aka Shaaban Robert wa pili) ni mwandishi ambaye ametoa mchango mkubwa katika fasihi ya Kiswahili. Yeye ndiye anatambuliwa kama mwanzilishi wa ushairi huru (free verse) katika Kiswahili alipoandika Kichomi na baadaye Karibu Ndani.
        • Kezilahabi anajulikana kwa ushujaa wake wa kujaribu mitindo mipya katika uandishi wake na ukisoma vitabu vyake kama Rosa Mistika, Dunia Uwanja wa Fujo, Kichwamaji, Gamba la Nyoka na Kaptula la Marx utakutana na chembechembe za upya katika nyanja mbalimbali na hasa matumizi ya falsafa.
        • Kezilahabi pia ndiye mwandishi wa Nagona na Mzingile - viriwaya viwili ambavyo vimeleta kizaazaa katika Fasihi ya Kiswahili kwa wasomaji pamoja na wahakiki kwani si rahisi kuelewa hasa anazungumzia nini. Inabidi kwanza uwe na welewa mpana wa matapo makuu ya falsafa za Kimagharibi (mf. Existentialism, Epistemology, Metaphysics, Psychoanalysis, Aesthetics na Phenomenology) na pia falsafa za Kiafrika kama unataka kuelewa cho chote kinazungumziwa katika vitabu hivi.
        • Kutokana na ugumu wa kueleweka wa vitabu hivi, wahakiki wengi wamemlaumu Kezilahabi kwamba pengine ameuleta mtindo huu wa uandishi katika fasihi ya Kiswahili wakati riwaya ya Kiswahili bado haijakomaa sawasawa. Wahakiki wengine wamefikia hata kumhukumu kwamba pengine ameiua riwaya ya Kiswahili.
        • Katika Mzingile kuna mazungumzo yafuatayo kati ya kijana msafiri aliyekuwa ametumwa kupeleka taarifa ya msiba na mzee kipofu.
        ...Tulitembea kwa muda kitambo bila kusema neno. Alikuwa wa kwanza kuzungumza kwa njia ya swali. "Unajua kwa nini ubikra hupendwa sana?" Sikutegemea swali kama hili kutoka kwake.
        "Hapana," nilijibu.
        "Ni kwa kuwa palipozibwa ndipo penye njia ya kweli."
        "Na pale palipozibuliwa?" nilimuuliza. Alikaa kimya kidogo, halafu akasema, "Muulize swali hilo aliyepazibua."

        Baada ya hatua chache aliendelea: "Unafikiri kama binadamu angezibwa matundu yote angekuwaje?" Nilikaa kimya. Swali kama hili lilikuwa halijapata kunijia akilini. Nilianza kuhesabu idadi ya mashimo aliyonayo binadamu na kazi zake. Halikuwa swali rahisi.
        "Nafikiri asingekuwa kama alivyo, na labda asingeweza kuishi."

        "Mimi nafikiri angeishi, na angeweza kuwa bora zaidi."

        "Wazo hili la ajabu ulilipata wapi?"
        "Zamani zile, wakati maji ya gololi zangu bado kupasuliwa nilipata kusoma kitabu."
        "Kitabu gani?"
        "Sikumbuki, na wala simkumbuki mwandishi. Ila wazo hilo lilikuwa limeandikwa na msomaji fulani pembezoni mwa ukurasa mmoja. Wakati huo sikujua kama macho yangu yangeziba siku moja." (Mzingile, DUP 1991. Uk. 26)
        • Swali hili la kipofu linafikirisha, na kulingana na imani yako kuhusu chanzo cha binadamu, linaweza kukufanya ujiulize kama kweli binadamu alipaswa kuwa kama alivyo (lakini angalia usikufuru!) Lipo kundi la wanasayansi wanaoamini kwamba kama kuna uwezekano wa kumfanya binadamu aishi milele siku moja, pengine itakuwa ni lazima kuangalia udhaifu alionao katika umbo lake la sasa na kuufanyia marekebisho. Na pengine baadhi ya matundu aliyonayo hayahitajiki. Mawazo ya kiwendawazimu ati! Soma ufupisho mfupi wa Novela za Nagona na Mzingile hapa.
        • Msikilize Euphrase Kezilahabi hapa chini akisoma mojawapo ya shairi lake; na huyu mwanafunzi akisoma shairi la Chai ya Jioni ambalo limo katika diwani ya Kezilahabi ya Karibu Ndani. Unaweza pia kusoma makala juu ya Nagona na Mzingile hapa, hapa na hapa (pdf). Wikendi njema!


        Thursday, March 11, 2010

        WAKATI WA VIJANA NDIO HUU - DR. HAMISI KIGWANGALLA ATANGAZA RASMI KUWANIA UBUNGE JIMBO LA NZEGA

        Dr. Hamisi Kigwangalla hasa ni nani?
        • Dk. Hamisi A. Kigwangalla (MD, MPH, MBA) ni kijana msomi mwenye umri wa miaka 35, mwenye digrii tatu na aliyebobea katika taaluma ya afya ya jamii na utawala wa biashara.
        • Ni kijana wa kitanzania anayeamini kwenye fikra mbadala na za kisasa lakini anaamini katika misingi iliyowekwa na wazee waasisi wa TANU na ASP
        • Alihitimu masomo ya digrii ya udaktari wa tiba ya binadamu (yaani Doctor of Medicine, MD) kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 2004. Pia ni muhitimu wa digrii mbili za uzamili; moja ambayo ni Masters in Public Health Sciences (Karolinska Institutet, Stockholm, Sweden) na ya pili ni Masters in Business Administration (Blekinge Institute of Technology, Ronneby, Sweden).
        • Dk. Kigwangalla ni mtu anayefanya kazi zake kwa umakini, spidi na maarifa, na kuzingatia misingi ya maendeleo na uwajibikaji. Ni mwanapinduzi anayeamini mapinduzi ya Uchumi wa Tanzania yako karibu, na kwamba tutaendelea tu kama tutabadilisha fikra zetu (change of mindset).
        • Anaiona Tanzania kama ni nchi yenye fursa nyingi na kwamba ni nchi iliyokaa vizuri na tayari tayari kuyapokea mapinduzi ya kiuchumi (Tanzania ni miongoni mwa emerging economies in Africa).
        • Anaamini kuna haja ya kuwapa nafasi watu ambao wanayaona maisha kwa macho tofauti, badala ya kuangalia matatizo tu wanaangalia fursa ziko wapi ndani ya hayo matatizo. Bila kubadilisha mtazamo wetu hatutoweza kusonga mbele, itakuwa ni sawa na kujaribu kukimbiza jahazi nchi kavu!
        • Kwa wasifu zaidi kuhusu mwanasiasa huyu kijana, tembelea hapa. Wakati wa vijana ndio huu ati! Inavyoonekana ile kesho inayotajwa katika kauli mbiu ya "vijana ndiyo viongozi wa kesho" imeshafika.

        Wednesday, March 10, 2010

        TABIA YA KUKOJOA HOVYO YAMPONZA MWANAMICHEZO HUYU

        • Tabia inayokera ya kukojoakojoa hadharani hovyo (ambayo niliwahi kuigusia hapa), katika nchi nyingi za wenzetu ni marufuku na inaweza kukutia matatani. Hiki ndicho kilichotokea tarehe 24/1/2010 wakati mchezaji wa kutegemewa wa timu ya mpira wa kikapu ya Chuo Kikuu cha Villanova aitwaye Corey Stokes alipopewa tiketi (ya faini) baada ya kufumwa na polisi akikojoa hadharani katika sehemu ya kuegeshea magari nje ya baa moja.
        • Mchezaji huyo alibambwa akilimwaga kojo muda wa saa tisa usiku katikati ya magari mawili huku akiwa amezungukwa na wachezaji wenzake. Tukio hili liliripotiwa katika vyombo vya habari, kuandikwa magazetini na mitandao mbalimbali.
        • Kocha wa timu ya Villanova baadaye aliamua kumsamehe mchezaji huyo baada ya kuomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena kukojoa hadharani. Isome habari juu ya kikojozi huyu hapa na hapa.
        • Tuwe makini na kuziacha tabia korofi kama hizi tunapotembelea hizi nchi za wenzetu kwani jambo "dogo" kama hili linaweza kukugharimu kitita cha dola, kukulaza selo na hata kuwekwa katika rekodi yako ya kudumu.

        Monday, March 8, 2010

        KAMERA ZIPO KILA MAHALI. KUWA MAKINI

        SIKUJUA KAMA KUNA "RADIO IKULU MBINGUNI" MPAKA NILIPOKUTANA NA HII TAARIFA YA HABARI

        • Kama mkereketwa wa masuala ya lugha, nimevutiwa na Kiswahili kilichotumika katika taarifa hii ya habari. Huyu jamaa ni mtangazaji mzuri sana na lugha ya Kiswahili anaimudu vyema!

        NAKUMBUKA SIKU NILIYOGEUZWA "DARASA" KABLA YA OPERESHENI KUBWA PALE MUHIMBILI

        • Mwaka 1993 nilifanyiwa upasuaji mkubwa wa sikio langu la kulia pale Muhimbili. Nakumbuka ilikuwa ni asubuhi majira ya saa mbili nilipopelekwa katika chumba cha upasuaji. Taa zinazong'ara sana zilikuwa zikiwaka na manesi walikuwa wanamaliziamalizia kuandaa vifaa.
        • Mara waliingia madaktari wawili wakanisalimia na kuniulizia kama nilikuwa tayari kwa operesheni ile. Niliwajibu kwamba nilikuwa najisikia vizuri sana na kwamba sikuwa na woga. Niliwaambia kwamba sikio hilo lilikuwa limenisumbua mno kuanzia utoto na nilikuwa tayari kuhakikisha kwamba tatizo hilo linatatuliwa.
        • Nilipimwa joto, shinikizo la damu na vipimo vingine. Daktari anayeshughulika na ganzi pia aliingia. Timu nzima ilikuwa imekamilika - madaktari wawili bingwa, mmoja wa ganzi na wasaidizi watatu - wote katika mavazi meupe yaliyong'ara na kuwafanya waonekane kama malaika. Muda si mrefu ujao, maisha yangu yangekuwa mikononi mwao.
        • Wakati nikisubiri operesheni hiyo kuanza waliingia watu wengine kama wanane hivi - wote wakiwa wamevaa majoho yale yale meupe. Mara moja nilitambua kwamba hawa walikuwa ni wanafunzi wa udaktari. Nilikuwa sahihi kwani mara moja darasa lilianza.
        • Daktari kiongozi alianza kuwaambia tatizo langu lilikuwa ni nini na visababishi vyake. Baada ya hapo aliendelea kuwaelekeza hatua za kufuata katika operesheni ile. Aliwaambia kwamba operesheni inachukua kati ya masaa mawili na nusu hadi matano. Kwamba ilikuwa ni operesheni ya hatari na uwezekano wa mgonjwa kufa, kupofuka au kuwa kiziwi wa kudumu ulikuweko. Aliendelea kuwaambia kwamba tatizo lilikuwa ni "gland" moja iliyokuwa ndani kabisa karibu na sikio la ndani na kazi yao ilikuwa ni kutafuta mzizi wa gland hiyo na kuung'oa kabisa. Gland hiyo korofi ilikuwa inatoa kemikali ambazo mwili ulikuwa hauzitambui na hivyo kusababisha sikio na kichwa kizima kuvimba kila mwaka. Aliendelea kuwaambia wanafunzi wake kwamba sehemu iliyopo gland hiyo ilikuwa imezungukwa na mifumo tata ya neva mbalimbali (zikiwemo za macho, sikio la ndani na za mfumo wa fahamu) pamoja na mirija mingi sana ya damu. Kwa hali hiyo kosa lolote dogo, lingeweza kuleta matatizo makubwa.
        • Baada ya darasa lile, yule daktari wa ganzi aliniuliza kwa mara ya mwisho kama nilikuwa tayari. Nilipotikisa kichwa kuashiria ndiyo, basi aliniwekea kifaa cha kupumulia mdomoni na kuniomba nihesabu mpaka 10. Nadhani hata tano sikufikisha. Nilikuja kupata fahamu majira ya saa saba mchana nikiwa kwenye eleveta nikirudishwa wodini. Operesheni ilikuwa imefanikiwa!
        • Inabidi niseme hapa kwamba maelezo ya darasa lile yalinitisha sana; na kidogo nilijisaili kama ilikuwa sawa kisaikolojia kwa daktari yule kutoa darasa la aina ile mbele ya mgonjwa tena anayekaribia kufanyiwa upasuaji hatari kama ule. Isitoshe, habari karibu zote zilikuwa ngeni kwangu. Nilibaki nikijiuliza, mbona sikuambiwa mambo haya mapema?
        • Nilipofika hapa Marekani na kuwaambia watu mkasa huu hawakuamini na waliniambia kwamba nilikuwa natania. Eti jambo kama hilo haliwezi kutokea. Niliambiwa kwamba hapa mahospitali hununua maiti kwa masomo yo yote yanayohusu mazoezi ya ana kwa ana/vitendo.
        • Baadaye nilikuja kugundua kwamba daktari bingwa profesa aliyenifanyia upasuaji ule na aliyefundisha darasa lile asubuhi ile njema ni mmojawapo wa madaktari bora kabisa kwa matatizo ya masikio na pua nchini Tanzania. Nilipokwenda kufanyiwa uchunguzi baada ya kufika hapa Marekani, madaktari waliniambia kwamba operesheni niliyofanyiwa kule Muhimbili ilikuwa imefanyika vizuri mno na hakukuwa na uwezekano wo wote wa tatizo lililokuwa likinisumbua kujirudia tena.
        • Japo sikulipenda darasa lake, daima huwa namshukuru na kumwombea daktari profesa bingwa aliyenifanyia upasuaji ule uliofanikiwa. Isitoshe, nikiwa kama mwanafunzi wa chuo kikuu, operesheni ile nilifanyiwa bure. Nimeambiwa kwamba hapa Marekani operesheni kama hiyo inaweza kugharimu zaidi ya dola 20,000!
        • Isitoshe, ni kutokana na operesheni hii hatimaye niliweza kukutana na ubinadamu wa kweli pale Muhimbili, tukio ambalo liliniathiri sana na kubadili mtazamo wangu kuhusu maisha na nafasi yetu hapa duniani kama binadamu!

        DEMOKRASIA NI NINI HASA?

        Picha: Inatoka hapa.

        Uchaguzi ndio huo umekaribia na mimi bado najiuliza. Demokrasia hasa ni nini? Ni kuwa na mfumo wa vyama vingi kama tulionao Tanzania? Je, ni ule uwezo wa wananchi kupiga kura kila baada ya miaka mitano? Ati, tuliyonayo Tanzania ni demokrasia?

        Wamarekani huwa wananiacha katika kunguku kila mara wanaposema kwamba eti wako kila mahali duniani wakijaribu kueneza demokrasia.

        Sunday, March 7, 2010

        FIKRA YA IJUMAA: KARIBU KILA MTU ANATAKA KWENDA PEPONI; LAKINI PEPO IPI?

        • Kifo. Ndiyo kifo. Kipo, kilikuwepo na kitakuwepo. Pengine siku moja kitakoma...
        • Kifo, kimemsumbua binadamu tangu enzi na enzi na kimeyakunguwaza na kuyashinda matumaini yake ya kuishi milele.
        • Ati, kipi ni bora? Kufa na kusahaulika (na pengine kukumbukwa - kwa mema au mabaya) au kuishi milele, hata kama ni milele isiyo timilifu?
        • Wapo wanaoamini kwamba dini "ziligunduliwa" ili kuendelea kupalilia matumaini ya binadamu ya kuishi milele. Ndiyo maana kila dini inatoa matumaini fulani ya umilele peponi ama kwingineko.
        • Wikiendi iliyopita nilikuwa namsikiliza mchekeshaji mmoja akijaribu kuhoji hii dhana ya kuishi milele peponi. Kimsingi alikuwa analinganisha pepo zinazoahidiwa na dini mbalimbali.
        • Alisema kwamba pepo pekee inayomsisimua ni ile inayoahidiwa katika Uisilamu. Inasemekana kwamba katika pepo hiyo, ukitekeleza majukumu yako vizuri hapa duniani, kuna uwezekano wa kuishi na mabikra tena wasiomaliza ubikra hata baada ya kuwabikiri milele na milele. Mchekeshaji huyu alisema kwamba hii ndiyo pepo hasa atakayopigana kufa na kupona mpaka aingie!
        • Aliendelea kusema kwamba pepo inayoahidiwa katika Ukristo kidogo inaboa. Inasemekana katika pepo hiyo kuna kuimba, kupiga vinubi na kumsifu Mungu usiku na mchana milele na milele. Alisema kwamba hana uhakika kama anataka kuishi maisha yake ya umilele namna hii.
        • Pepo zingine zote, hazivutii na zingine zinatisha. Aliitaja ile ya "incernation" ambako kuna uwezekano wa kuzaliwa tena na tena katika maumbo mbalimbali - na wakati mwingine ukiwa kama mnyama. Alisema kwamba hataki pepo hii ya kubahatisha.
        • Hitimisho lake: Pepo pekee inayovutia na ambayo inapaswa kupiganiwa ni ile inayoambatana na kufaidi mabikra wasiomaliza ubikra!
        • Ambacho alikisahau mchekeshaji huyu ni kile kinachoahidiwa kwa wale ambao hawatakwenda katika pepo hizi. Katika Ukristo kuna moto wa milele. Kwenye Uisilamu sijui makafiri wanasubiriwa na adhabu gani. Mimi nadhani ni bora kuishi kwa kuimba, kupiga vinanda na kumsifu Mungu usiku na mchana milele na milele kuliko kuitumia milele yote katika Ziwa la moto ambako inasemekana kuna kuungua bila kuteketea. Oh, mateso yaliyoje!
        • Makanisa mengine kama Mashahidi wa Jehova wanaamini kwamba moto wa milele ni mafundisho ya Kipagani yaliyoingizwa kinyemela katika Ukristo na kwamba Mungu mwenye upendo usiopimika kamwe hawezi kuwachoma binadamu aliowaumba mwenyewe milele na milele. Kifo ndiyo Jehanamu yako!
        • Kwa wengine pepo na Jehanamu ziko hapa hapa duniani!!!

        Swali la kizushi: Ati, nawe wategemea kwenda peponi? Ipi?

        *****************************
        Natamani kama ningekuwa na uwezo wa kuiandika fikra hii katika mtindo wa Mtakatifu Kitururu. Hoja ingenoga ajabu lakini wapi. Nimejaribu nimeshindwa. Hata hivyo natumaini kwamba hoja imeeleweka; na kwamba sijamkwaza mtu!
        ******************************

        UTAFITI: CCM KINARA WA RUSHWA WAKATI WA UCHAGUZI. HEBU TUTAFAKARI!!!

        • Mbali na mambo mengine utafiti uliotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURURU) unaonyesha kwamba CCM ndiyo chama kinachoongoza kwa rushwa wakati wa uchaguzi (49.5%) kikifuatiwa na CHADEMA (7.0%) , CUF (2.7%), NCCR Mageuzi (0.5%) na TLP (0.5%).
        • Nijuavyo mimi ni kwamba tumefikia mahali sasa ambapo hata wapiga kura wetu wanategemea baisikeli za bure, kanga, vitenge, chumvi, vyerehani, mabati, saruji, pikipiki, sukari na ahadi tamu zisizotekelezeka. Ni wazi kwamba bila kutoa rushwa ya vitu hivi, kamwe hutapata kura hata kama uwe na sera nzuri na uadilifu wa kupigiwa mfano.
        • Kama hali ndiyo hii, ni nani wa kulaumiwa kwa kosa hili? Ni mgombea ubunge/uraisi anayetoa rushwa na ahadi za uongo huku akijua kuwa bila kufanya hivyo hatapata kura au ni mpiga kura ambaye hatoi haki yake ya kikatiba bila kupewa kitu kidogo?
        • Mimi nadhani siyo sawa kuvibebesha lawama vyama vya siasa au wagombea pekee wakati hili ni tatizo la jamii nzima, tatizo ambalo mimi naamini kiini chake ni umasikini na ukosefu wa elimu makini na itikadi kombozi kwa wanajamii. Wanajamii wakifahamu kwamba hizi pea za kanga wanazopewa si za bure na ndizo zinachochea moto wa ufisadi unaoendeleza kudumaza maendeleo yao, mambo yatabadilika. Bado safari ni ndefu!
        • Taarifa kamili ya UDSM na TAKURURU niliyoirejelea hapo juu inapatikana hapa. Niliwahi pia kuligusia suala hili hapa.

        Saturday, March 6, 2010

        TOTALLY USELESS FACT

        • Women blink nearly twice as much as men.

        JIANDIKISHE HAPA

        Enter your email address:

        Delivered by FeedBurner

        BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO