NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, April 30, 2010

FIKRA YA IJUMAA: TUTAFAKARI KAULI HII YA SOCRATES

Shairi ni kutoka hapa.
  • Socrates - mmojawapo wa vingunge wa falsafa ya Kigriki aliyelichachafya tabaka tawala la Athens ya kale kwa maswali yake yaliyojaa lojiki na mantiki kinzani chokonozi mpaka likaamua kumuua kwa kumnywesha sumu aliwahi kutoa kauli ifuatayo:
"Kitu pekee ninachokijua ni kwamba sijui kitu"
  •  Na ukifikiria vizuri unaweza kuhitimisha kwamba pengine Socrates alikuwa sahihi. Ati ni kitu gani ambacho unaweza kusimama na kusema kwa uhakika kabisa kwamba unakijua? Ati, unaweza kusimama na kusema kwa uhakika kwamba unajua kula? Kulala? Kuendesha gari? Kupumua? Kungonoka? Kufa? Unajua nini???
  • Ati, una uhakika kwamba unakijua hicho "unachojua" kwamba unakijua? 
  • Poleni kwa maswali mengi; na wikiendi njema!!!
********************
  • Ni mwisho wa muhula na ni wakati wa kusahihisha makaratasi ya wanafunzi. Nina wanafunzi wanane wa Ph.D ya isimu na hawa makala zao inabidi zisahihishwe kwa umakinifu wa kiwango cha juu. Ndiyo maana nilipotea kwa siku mbili tatu hivi. Sasa mambo yameanza kupoa kidogo na libeneke litaendelea kama kawaida. Tuwemo!!!

Monday, April 26, 2010

WATU WANAPOPANGA FOLENI USIKU KUCHA WAKISUBIRI KUNUNUA VITABU

  • Profesa Mbele amekuwa akiandika mara nyingi kuhusu tatizo tulilonalo Watanzania la kutopenda kusoma vitabu (tazama hapa na hapa). Markus Mpangala (aka Mzee wa Lundu) naye ameshawahi kuandika makala kadhaa zamifu kuhusu suala hili (tazama hapa na hapa). Baadhi ya sababu zilizotajwa kuchangia tatizo hili ni pamoja na umasikini wa Watanzania, ughali wa vitabu vyenyewe, mfumo mbaya wa elimu (vitabu mashuleni hakuna na tunasoma kwa kutegemea madesa); na kutokuwa na utamaduni wa kujisomea. Pamoja na sababu hizi, swali bado linaweza kuulizwa, kama tuna pesa ya kunywea bia na kitimoto kila siku, mbona tusiwe na pesa ya kujinunulia vitabu?
  • Kila mwaka hapa “kijijini ” Gainesville huwa kunafanyika mauzo ya vitabu vingi vya kila aina kwa muda wa siku tano mfululizo. Mauzo haya yanayojulikana kama Friends of the Library ni makubwa na huwa yanavutia watu kutoka jimbo zima la Florida na majimbo mengine ya jirani.
  • Mwaka huu mauzo haya ya vitabu yalianza juzi Jumamosi (24/4/2010). Watu waliotoka sehemu za mbali ili kuwahi mauzo ya mwanzo mwanzo ambapo vitabu huuzwa kwa bei ya chini sana, walianza kupanga foleni siku ya Ijumaa na walikesha na kulala katika foleni hiyo wakisubiri kesho yake milango ifunguliwe ili waweze kujinunulia vitabu kwa bei nafuu sana.
  • Katika miaka ya nyuma, wapenda vitabu hawa waliruhusiwa kuweka kiti, jiwe au boksi katika foleni kama kishika nafasi. Mwaka huu hata hivyo masharti yamebadilishwa na mtu inabidi uweko mwenyewe katika foleni ili kulinda nafasi yako. Ukiondoka na lako halipo!
  • Katika foleni ile ya Ijumaa jioni kulikuwa na watu wa kila aina - wazee kabisa wenye umri zaidi ya miaka 70, watu wa makamo, vijana, wanawake wakiwa na watoto wao, wazungu, weusi…
  • Kwa Mtanzania, tukiwemo sisi tunaojidai kuwa eti tumesoma, kukesha usiku kwenye foleni ya kununua vitabu pengine haiingii akilini kabisa. Lakini huu ndio utamaduni wa hawa wenzetu, na kwa hili kusema kweli wametuzidi. 
  • Kama nilivyowahi kusema hapa "Taifa lisilojisomea ni taifa la wanakondoo wanaoweza kupelekwa ndiko-siko kwa urahisi sana. Ni taifa lisilojua wala kuhoji matumizi ya raslimali zake. Ni taifa la watu walio tayari kuuza kura zao kwa kuwa tu eti wamepewa jozi ya kanga! Ni taifa lisilo na mwelekeo. Ati, ingekuwaje kama Waafrika (angalau kwa wale tunaokaa mijini na wenye uwezo wa kujinunulia vitabu)  tungekuwa na mwamko wa kujisomea vitabu na kufuatilia mambo kwa kina?" Tutafakari!!!
  • Unaweza kusoma zaidi kuhusu mauzo haya ya Friends of the Library hapa na hapa.

Saturday, April 24, 2010

MLEVI ANAPOKWENDA KANISANI KUTUBU - DHIHAKA

  • Nimeiona hii katika gazeti la wanafunzi la hapa chuoni. Naiacha kama ilivyo.
 *************************
After a heavy night of drinking at the local bar, a drunk stumbles into a Catholic church and slowly makes his way into the confessional booth. There, the priest patiently awaits the man to begin his confession. After a few minutes of silence, the priest politely taps on the window...nothing. The priest taps again and this time clears his throat a bit...still nothing. At this point, the priest begins to lose his patience and bangs on the window.

Finally the drunk yells out;

"Ain't no use knocking, there ain't no toilet paper over here either!"

 *************************

Friday, April 23, 2010

FIKRA YA IJUMAA: LEO TUTAFAKARI UBINADAMU WA BINADAMU (A.K.A "HOMO SAPIENS")

  • Ati, kama binadamu (a.k.a Homo Sapiens) ana ubinadamu, anajisikiaje anapowaibia binadamu wenzake waliomkabidhi madaraka na kujirundikia mamilioni ya dola huku akiwasikinisha na kuwaacha wakiishi katika hali kama hii? Je, hulka ya kibinadamu inamsuta anapowaona watoto wa wakulima wakiwa hivi wakati wa kwake wanabwia unga majuu?
  • Ubinadamu wa binadamu uko wapi anapowaibia watu wa taifa lake na kujijengea majumba ya kifahari kama hili la dola 35,000,000 la Teodoro Nguema Obiang kule pwani ya Malibu, California wakati wananchi wenzake wanaishi katika vibanda vya nyasi?
  • Mifano ya aina hii iko mingi lakini nadhani lengo kuu la Fikra ya Ijumaa hii limeeleweka. Ati, inawezekana ubinadamu wa binadamu umegota na sasa ameanza kusonga mbele kwa kurudi nyuma kama hii picha hapa chini inavyotuonyesha? Kwa ubinafsi huu wa kinyama, binadamu anaelekea wapi? 

  • Wikiendi njema!!!

UKITAKA KUWA NAMBARI WANI, NI LAZIMA UWE NAMBARI WANI.

Wednesday, April 21, 2010

AFRIKA - MAMA TAJIRI MJAMZITO LAKINI MASIKINI KWELI KWELI !!!

     
    Picha hii ni kutoka vijanafm.blog.

    Na watoto wake hawajali na wanakulana  wao kwa wao!

    MBEGU WALETE WAO, KULIMA NILIME MIYE, TENA KWA SULULU!!!

    • Wanafunzi wa darasa la tatu eti tayari wanafundishwa uotaji wa mbegu (germination) – tena kwa vitendo. Basi Alhamisi iliyopita binti akaleta mbegu walizootesha shuleni huku akisisitiza kwamba wameambiwa mbegu hizo ni lazima zipandwe bustanini na waendelee kuzitunza mpaka zikue na kutoa matunda. Walileta mbegu za matikiti maji, bamia, matango na nyanya. 
      • Na kama nilivyotegemea, kazi ya kulima hiyo bustani iliniangukia miye. Basi niliwakumbusha kwamba miye nimekulia kijijini na mara moja niliingia mzigoni. Tatizo pekee ni kwamba huku hakuna majembe ya mkono kama niliyozoea nyumbani na juhudi zangu za kuyatafuta zilishagonga mwamba tangu zamani nilipofika hapa. Hata hivyo sululu ilifanya kazi vizuri tena bila matatizo.
      • Yaani waleta mbegu (kama wanavyoonekana hapa chini) hata hawawezi kutia mguu kwenye nyasi. 
      • Mboga hizi zikishakomaa, nitawakaribisheni tule pamoja! 

        Tuesday, April 20, 2010

        VIINIMACHO VYA UCHAGUZI MKUU VIMESHAANZA RASMI: “WAPIGANAJI WA KWELI” WATOA TAMKO!!!

        Lisome kwanza tamko la "wapiganaji wa kweli" 
        linalozunguka sana mtandaoni HAPA (pdf).
        • Mtu unaweza kujiuliza, hawa “wapiganaji wa kweli” walikuwa wapi? Ni lazima wasubiri mpaka uchaguzi ufike ndipo upiganaji wao uchemke namna hii? Tutajuaje kama siyo watu ambao wana wasiwasi wa kupoteza ulaji wao katika uchaguzi wa mwaka huu na sasa wanatapatapa? Kama wana ujasiri wa kutaja majina ya “maadui” ndani ya ile nyumba kongwe, mbona wasiwe na ujasiri wa kujitaja majina yao? Bila kutaja majina yao (ukijumlisha na e-mail ya yahoo), watu makini wanaweza kutilia shaka lengo hasa la tamko lao hili, pamoja na uzito wake.
        • Pamoja na maswali haya chokozi, mambo wanayoyaibua hawa “wapiganaji wa kweli” ni mazito na yanastahili kutazamwa, kujadiliwa na kutathiminiwa kwa jicho pevu. Naamini kwamba "wamiliki" wa nyumba (kongwe) wanajua kwamba nyumba idumuyo ni ile irekebishwayo na kufanyiwa matengenezo kila inapolazimu kufanya hivyo. Swali la msingi linaloweza kuulizwa hapa ni hili: ni nani atakayeyatekeleza madai haya gonga-kichwa ya hawa wapiganaji? Nauliza hivi kwa sababu mambo wanayoyazungumzia siyo mapya na chama kimojawapo cha upinzani kimekuwa kikipiga kelele hizi hizi kwa muda mrefu sasa. Je, ni kweli tutaona mabadiliko?
        • Uchaguzi ndio huo umeshaanza na bila shaka tutaona mengi. Na muda si mrefu mvua ya kanga, vitenge, chumvi, sukari, baisikeli, mabati, pikipiki na mabulungutu ya pesa itaanza kuwanyeshea wapiga kura. Neema iliyoje!
        • Mungu Aendelee kuibariki Tanzania ili, kama kawaida yetu, tuvuke uchaguzi huu kwa amani na salama. 

          WAMAREKANI NA UMAKINIFU WA KUTUNZA KUMBUKUMBU: RAIS GEORGE WASHINGTON BADO ANADAIWA VITABU NA MAKTABA KUU YA NEW YORK!!!

          • Wamarekani ni watu wanaotunza kumbukumbu sana na karibu kila kitu unachofanya kinaweza kutafutwa na kufukuliwa kutoka katika makabrasha ya kumbukumbu zao. Ndiyo maana watu wenye azima ya kugombea kazi za kuchaguliwa (ukiwemo uraisi) huanza kujiandaa asubuhi na mapema wakijaribu kukwepa kila jambo ambalo litakuja kuwaumbua huko mbele ya safari na kuzizima ndoto zao. 
          • Mkutubi wa maktaba kuu ya jijini New York ametangaza kwamba raisi wa kwanza wa nchi hiyo (George Washington) bado anadaiwa vitabu viwili ambavyo aliazima katika maktaba hiyo zaidi ya miaka 220 iliyopita. Vitabu hivyo - Law of Nations na Debates of the Britain's House of Commons vilitakiwa kurudishwa tarehe 2/11/1789. 
          • Mkutubi mkuu wa maktaba hiyo amesema kwamba japo hawamdai raisi huyo malimbikizo ya faini zinazotokana na kutorudishwa kwa vitabu hivi (dola 300,000) ingekuwa vizuri sana kama vitabu hivyo vingetafutwa na kurudishwa katika maktaba hiyo.
          • Tayari kelele zimeanza kupigwa kwamba pengine kiongozi huyo anayeheshimika sana hakuwa mmakinifu kama inavyosadikiwa; vinginevyo asingesahau kuvirudisha vitabu hivi. 
          • Sisi tunatunza kumbukumbu za viongozi na mashujaa wetu? Kumbukumbu hizi ziko wazi kwa kila Mtanzania? Unaweza kuisoma taarifa hii hapa.

          Saturday, April 17, 2010

          "STUDIO ROOMS" ZINAPOPANGISHWA KWA DOLA 1,200 KWA MWEZI

          • Chuo Kikuu cha California cha jijini Los Angeles (UCLA) kimezungukwa na Hollywood, Beverly Hills, Bel-Air na Westwood, na bei ya vyumba vya kupanga ni ghali kweli kweli. Nilipokuwa nasoma huko, bei ya chumba kimoja cha studio kingeweza kukugharimu dola zaidi ya 1,200. Ndiyo maana wanafunzi wengi tulikuwa tunakimbilia mbali kidogo  na UCLA kama vile Santa Monica na kwingineko.
          • Kumbe hali ni ile ile hata Dar es salaam. Ni Watanzania wa aina gani wanaomudu kupangisha hivi vyumba?  Kwa nini vyumba hivi ni ghali namna hii? Ni mahali vilipo, ni ughali wa viwanja au? Wachumi mnajua?
          *******************

          Bathrooms : 1
          Bedrooms : 1
          Location:
          Regent Estate, Dar-es-Salaam
          Living Area (Sqm):
          Plot Size (Sqm):
          Asking Price: USD 1,200

          Tangazo hili ni kutoka Dally Estate.

            Friday, April 16, 2010

            FIKRA YA IJUMAA: TUEPUKE CATAGELOPHOBIA

               
            • Kwangu mimi blogu imegeuka kuwa ni shule elimishi ajabu na elimu niliyoipata katika mwaka mmoja niliodumu katika kublogu haifundishwi katika chuo cho chote hapa duniani.  
            • Mbali na mambo mengine, nimejifunza kuwa na uvumilivu, subira na nidhamu kila mara ninaporushiwa madongo. Hili si jambo rahisi kwetu kama binadamu. Nimegundua kwamba katika kila dongo, tukiangalia na kufikiria vizuri kuna jambo jema ambalo tunaweza kujifunza. Kwa hivyo tuache kulalamika na kukurupuka kila mara tunapoambiwa kwamba tumefulia, tumeishiwa na madongo mengineyo. Haya ni mambo ya kawaida tu na tuyatazame kama chachu na uthibitisho kwamba angalau kuna watu ambao wanajali kiasi cha kupoteza muda waokiturushia madongo. Bila shaka katika kila u-hasi mna chembechmbe za u-chanya pia. Ni lazima tujitahidi kuziona pande zote mbili.
                • Pia ni lazima tuheshimu mawazo na hoja kinzani. Tunapopingwa kwa hoja tusikarisike na kuanza kulalamika. Hakuna faida yo yote na kusema kweli hatupaswi kutegemea maoni sambamba na yetu. Tujibidishe kuzijibu hoja (hata zile za ma-anony) kila inapowezekana ingawa najua kwamba mara nyingi huwa hakuna muda wa kutosha. 
                • Asanteni sana wanablogu wenzangu kwa hoja zenu nzito nzito pamoja na ma-anony wote mliowahi kunirushia madongo ya kila aina (Fundi Mangungo upo?). Yenu ni elimu ya kweli ambayo imeinukia kuwa ya muhimu sana katika maisha yangu. Tusongeni mbele. 

                • ANGALIZO: Catagelophobia ni hofu ya kurushiwa madongo.

                Thursday, April 15, 2010

                MABINTI: MKILIIGA NA HILI BASI TUMEKWISHA....

                • Mabinti, igeni kujikondesha. Tumieni dawa za Mchina kurekebisha maumbo. Tumieni mkorogo na kuzibabua ngozi zenu nzuri. Igeni kila kitu mnachoweza kutoka nje lakini hili kamwe msiliguse: MSIACHE KUNYONYESHA VICHANGA VYENU!!!
                • Utafiti uliofanywa hivi karibuni na kuchapishwa katika jarida la kitaaluma la afya ya watoto la Pediatrics, unaonyesha madhara makubwa kwa nchi za Kimagharibi na hasa Marekani kutokana na tabia ya kutopenda kunyonyesha watoto wanapozaliwa.
                • Kwa kifupi, utafiti huo unaonyesha kwamba kama akina mama wangezingatia mapendekezo ya serikali yanayowataka kutowapa watoto wachanga chakula kingine zaidi ya maziwa ya mama kwa miezi yote sita ya mwanzo, basi Marekani ingeweza kuokoa DOLA BILLIONI 13 kila mwaka na vifo vya watoto wachanga vinavyokaribia 1,000.
                • Wanasayansi wanakubaliana kwamba mbali na maziwa ya mama kuwa ndicho chakula bora kabisa kwa mtoto, pia ni kinga kwa magonjwa mbalimbali kama vile maambukizi ya masikio na tumbo, kuhara, magonjwa ya kupumua ikiwemo Athma, kisukari cha watoto, leukemia ya watoto na magonjwa mengine mengi. Kunyonyesha pia kunasaidia kupunguza uwezekano wa akina mama kupata kansa ya matiti, kisukari, kansa ya mfuko wa uzazi, msongo wa mawazo baada ya kujifungua na inasemekana pia ndiyo kinga bora ya kuzuia mimba.  
                • Mimi naamini kwamba kunyonya maziwa ya mama ndicho hasa kinachookoa maisha ya watoto wengi wa Kiafrika. Mimi, kwa mfano, kama kitinda mimba nilinyonya kwa miaka zaidi ya mitano na watu wengi walikuwa wakinitania kwamba pengine ndiyo sababu niligeuka kuwa "kipanga" (huu ni utani!). 
                • Kwa wenzetu wazungu, matiti "yanaheshimika" sana na ni nadra mno kumwona mwanamke wa kizungu akinyonyesha mtoto hadharani. Akifanya hivyo basi ni lazima afanye kwa siri. Kwetu ni tofauti na si jambo la ajabu kumwona mtoto akiwa anapata lishe yake mbele ya watu bila wasiwasi.
                • Sasa tunashuhudia mfumuko wa magonjwa mapya kama aina mbalimbali za saratani na kisukari, magonjwa ambayo pengine yameanza kutuandama sana kutokana na  kubadilisha mfumo wetu wa maisha pamoja na kuanza kula vyakula vya Kimagharibi. Sijui itakuwaje tukiiga na hili la kuacha kunyonyesha vichanga vyetu. 
                • Kama kuna jambo ambalo hatupaswi kuliiga basi ni hili la kuacha kunyonyesha vichanga vyetu.  Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

                HIZI NDIZO ZAWADI NILIZOLETEWA.......

                • Wikiendi iliyopita binti yangu (darasa la tatu) alikwenda Kennedy Space Center kwa ziara ya kimasomo. Baada ya hapo alijiunga na mamake huko na akapitiliza kwenda Disneyland Orlando kujiburudisha pamoja na wenzake. Basi aliporejea nilimuuliza kama kulikuwa na zawadi aliyokuwa ameniletea. 
                • Nilishangaa sana alipotoa kimfuko na kunikabidhi. Nilipofungua nilikuta hizo zawadi tatu - Space Shuttle, Boeing 747 na Hummer. Nilipomuuliza ni kwa nini aliamua kuniletea zawadi hizi na si vikombe au kitabu alisema kwamba ameshanisikia mara nyingi nikiongelea juu ya Space Shuttle, madege makubwa makubwa pamoja na Hummer. 
                • Nilikuwa najua kwamba watoto husikiliza sana maongezi ya wakubwa kwa lengo la kujifunza na kuimarisha uwezo wao wa lugha. Kumbe wanajibidisha hata kujua "hobbie" za wazazi wao na mambo yanayowavutia. Wazazi, tuweni waangalifu kwani tunasikilizwa sana na maneno yetu na aina ya lugha tunayotumia vinayo athari kwa hawa malaika wa Mungu tuliowaleta hapa duniani na kujivika jukumu la kuwalea mpaka watakapoweza kujikimu wenyewe.
                • Basi tuliongea mambo mengi na tumepanga kwamba tutakwenda Kennedy Space Center kushuhudia safari ya mwisho ya Space Shuttle itakaporushwa kwenda katika Kituo cha Anga cha Kimataifa baadaye mwaka huu. Rais Obama ameunga mkono kustaafishwa kwa Space Shuttle mwishoni mwa mwaka huu na amesema kwamba serikali ya Marekani haitatoa pesa kufadhili mradi mpya wa NASA unaojulikana kama Constellation.

                Wednesday, April 14, 2010

                TUSISAHAU KIJIJINI TULIKOTOKA, TUSIWASAHAU WALIOTUPIGA TAFU HADI TUKAFIKA HAPA TULIPO!

                Picha ni kutoka kwa Mjengwa
                • Jana nilikuwa naongea na kijana wangu mmoja kutoka kule Unyantuzu Bariadi. Alinisimulia kisa cha jamaa mmoja katika kijiji cha jirani aliyekuwa ameletwa nyumbani kijijini kwao kuzikwa (Mungu Amlaze mahali pema peponi!). 
                • Aliniambia kwamba ilikuwa aibu tupu na watu waliomleta nyumbani kwao katika safari yake ya mwisho kutoka Mbeya hawakuamini kama kweli hapo ndipo palikuwa nyumbani kwao kwa baba na mama yake. 
                • Walishangaa kuona kwamba mamake mzazi alikuwa anaishi katika kibanda kidogo cha nyasi na kwamba umasikini ulikuwa umetamalaki pale nyumbani wakati jamaa huyu alikuwa anaishi maisha ya kifahari sana kule Mbeya. Kumbe akawa amepasahau nyumbani kwao kijijini alipozaliwa na kukulia, nyumbani kwa mama yake mzazi!
                • Ati, mbona tusahau vijijini tulikotoka? Mbona tuwasahau watu waliotulea na kutusaidia mpaka tukafika hapa tulipo? Wengine hata kijijini tulikozaliwa hatuendi tena, mpaka turudishwe tukiwa katika masanduku. Kwa nini?
                • Kama kuna kitu kikubwa ambacho nimejifunza kutoka kwa Mzee wa Changamoto ni kutoa shukrani kwa watu waliotupiga tafu kwa namna yo yote ile mpaka tukafika hapa tulipo. Naamini kwamba hili ni jambo la muhimu sana katika maisha yetu hapa duniani. Unaweza pia kumsoma Mzee wa Uungwana kuhusu mada hii.
                • Hebu tumsikilize Jimmy Gait hapa akitusihi kurudi kijijini na kuwakumbuka ndugu zetu tuliowatelekeza huko!

                Friday, April 9, 2010

                SOTE TUNAHITAJI "KUPIGWA TAFU" ILI KUFIKA KILELENI LAKINI....

                WAMAREKANI WANAVYOHANGAIKA NA OBAMA WAO...SIASA KWELI NI MCHEZO MCHAFU

                • Kwa picha zaidi kumhusu Obama Msoshalisti, tazama hapa.

                FIKRA YA IJUMAA: BINADAMU NA MAPOCHOPOCHO YAKE

                Picha kutoka: iheartguts.wordpress.com
                ****************

                Ilani 
                Fikra ya Ijumaa hii kidogo imepinda. Natanguliza samahani 
                kwa ye yote atakayekereka!
                • Maonyesho haya yanaonyesha kile kinachoendelea ndani ya mwili wa binadamu kuanzia puani, masikioni, tumboni, katika utumbo mwembamba na mkubwa na sehemu mbalimbali zinazotoa uchafu mwilini. Kama jina lake linavyoonyesha kweli ilikuwa ni "gross"
                • Niliondoka hapo nikiwa na maajabu mapya kuhusu mnyama huyu machachari aitwaye binadamu.
                • Swali (pengine la kipuuzi) ambalo mtoa maelezo mkuu katika maonyesho yale aliligusia, na ambalo lilinifanya nifikirie bila kupata jibu ni hili: Binadamu ndiye kiumbe pekee anayepika vyakula vyake na kuviunga mpaka vikapopochoka kwelikweli. Cha ajabu ni kwamba, pamoja na uwezo huu wenye faida na hasara zake nyingi, bado binadamu ni mmoja kati ya wanyama wenye vinyesi vinavyonuka sana.  
                • Cha kushangaza zaidi ni kwamba inavyoonekana kunuka sana kwa kinyesi cha binadamu hakuna faida yo yote kama ilivyo kwa wanyama wengine kama fungo ambao inasemekana harufu hiyo huwa ni kama "GPS" yao inayowasaidia wasipotee katika safari zao.

                • Binadamu (a.k.a) Homo Sapiens hamalizi vituko ati! Na kwa jinsi unavyozidi kumtazama ndivyo anavyozidi "kukushangaza"

                  Thursday, April 8, 2010

                  UTAFITI: KUJITOLEA KUSAIDIA WENGINE KUNA FAIDA NYINGI ZA KIAFYA

                  • Katika Fikra ya Ijumaa iliyopita niliuliza swali lisemalo "Ipi ni raha kuu maishani?" Baadhi ya maoni yaliyotolewa ni haya kutoka kwa mwanaharakati na mchambuzi Dada Koero Mkundi. Yeye alisema hivi:
                  **************** 
                  Koero Mkundi said...
                  "Pesa, anasa na takataka nyingine haziwezi kumpa mwanaadamu furaha kamwe... Hebu jaribu kuwasaidia wale wenye shida na ndipo utakapoipata furaha ya milele..." 
                  ****************
                  • Dada Koero yuko sahihi. Watafiti sasa wamethibitisha kwamba kujitolea kusaidia wengine kuna faida nyingi za kiafya. Watu wanaoshughulika na mambo ya utambuzi (akina Kamala) wanasema kwamba pengine hili ndilo lengo na kusudi kuu la maisha yetu hapa duniani. 

                  • Watu wanaojitolea pia huishi maisha marefu zaidi kuliko wenzao wasiojitolea.
                  • Katika utafiti huu washiriki walijitolea kufanya shughuli za kawaida tu  kwa watu wasiowafahamu mf. kusafirisha wagonjwa, kuwasaidia wazee na wasiojiweza kazi za nyumbani, kulea watoto na shughuli nyinginezo. 
                  Mzee Matonya akiwa kazini
                  • Japo kusaidiana ulikuwa ni utamaduni wetu wa tangu zama na zama, mikondo ya maisha ya kisasa tayari imeanza kutujengea misingi ya kibinafsi na sasa ni wazi  kwamba mambo si kama zamani. Pengine huu ni wakati mzuri wa kuuendeleza utamaduni wetu mzuri wa kusaidiana. 

                  • Tendo moja lililofanywa kwa upendo wa kweli linaweza kuwa na nguvu kubwa ya kubadilisha mtazamo na maisha ya mtu hasa ambaye hatumfahamu. Mbali na kuwafaidisha wale tunaojaribu kuwasaidia kwa kujitolea kwetu, inafurahisha kama nini kuona kwamba kwa kufanya hivyo nasi tunafaidika kiafya ya kimwili, kijamii na kisaikolojia.
                  Kijana Msamaria Mwema kule India
                  • Habari zaidi kuhusu utafiti huu zinapatikana hapa. Unaweza pia kutazama mikakati ya Wamarekani katika suala la kujitolea hapa.

                    MADAKTARI WACHEMSHA: WAMFANYIA OPERESHENI YA UZAZI MAMA "MJAMZITO" AMBAYE HAKUWA NA MIMBA

                    • Sisemi mengi. Kisikilize kisa hiki hapa.

                    VYOO VYA KULIPIA KWENYE NDEGE VINAKUJA............

                    • Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, mashirika mengi ya ndege yamekuwa yakifanya kila njia ili kujipatia pesa za ziada. Hii ikiwa ni pamoja na kuuza vyakula na vinywaji, kutoza ushuru wa mizigo; na matumizi ya mito na blanketi.
                    • Jana shirika moja la ndege la hapa Marekani liitwalo Spirit Airlines limetangaza kwamba litaanza kutoza dola 20 - 45 kwa kila mzigo ambao msafiri ataingia nao kwenye ndege - iwe ni laptop au mikoba ya mikononi (kwa akina dada). Bila shaka mashirika mengine yatafuata muda si mrefu ujao.
                    • Sasa shirika la ndege la Ryanair limetangaza kwamba litaanza kutoza paundi moja au Euro moja kwa ajili ya matumizi ya vyoo katika ndege zake kwa safari fupi fupi.  
                    • Baada ya mlolongo huu, nini kitafuata? Mambo yakiendelea hivi kuna hatari ya baadhi yetu kupiga mguu, au kusafiri pamoja na makontena....

                    Wednesday, April 7, 2010

                    WANASAYANSI: NGONO INA FAIDA NYINGI ZA KIAFYA

                    • Kwa wanyama wengi, lengo kuu la ngono inaonekana ni kuendeleza uwepo wa wanyama hao kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kuhakikisha kwamba hawatoweki. Ni kwa sababu hii wanyama wengi wana vipindi maalumu (wakati mwingine ni mara moja tu kwa mwaka) vya kufanya ngono, vipindi ambapo mnyama jike ana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata mimba.
                    • Binadamu yeye, kama ilivyo kawaida yake ya kupindisha mambo; na pengine kutokana na maumbile yake kama mnyama dhaifu sana, ngono kwake hailengi tu katika kuhakikisha mwendelezo wa vizazi. Kwa mnyama huyu machachari, ngono imegeuka kuwa starehe na biashara inayomwingizia mabilioni ya dola kila mwaka. Mpaka kuna mkondo wa mawazo unaodai kwamba pengine raha za kingono ndiyo lengo hasa la maisha. Mkondo huu wa mawazo unajulikana kama Eunoterpsia
                     Binadamu amejitungia hadi vitabu....

                    Wanasayansi sasa wanasema kwamba ngono (salama) ina faida nyingi za kiafya. Faida hizi ni pamoja na 
                    1. Kupunguza msongo wa mawazo
                    2. Kuongeza uwezo wa kinga asili ya mwili
                    3. Kupunguza uzito
                    4. Kuboresha afya ya moyo
                    5. Kuongeza kujiamini
                    6. Kupunguza maumivu
                    7. Kupunguza uwezekano wa kupata kansa ya "prostate"
                    8. Kuimarisha misuli ya "sakafu" ya nyonga
                    9. Kukufanya ulale "fofofo"
                    10. Kuimarisha upendo na "mshikamano" wa kimapenzi kati ya wenzi.
                    11. Kuongeza uwezo wa kunusa.
                    12. Kupunguza uwezekano wa kupata homa za mara kwa mara
                     Ngono pia imemletea binadamu matatizo...

                    Unaweza kusoma hapa na hapa kuhusu faida hizi. Zitazame pia hekaheka za binadamu wa kiume hapa kuhusu ngono.

                    UTAMADUNI WA KUSOMA VITABU NI MSAMIATI MZITO TANZANIA


                    Nimekutana na makala haya katika blogu ya Markus Mpangala (aka Mzee wa Lundu) na nikavutiwa nayo. Ni uchambuzi wa kina kuhusu suala gumu juu ya uzembe wa kujisomea tulio nao Watanzania. Makala hii imekuja katika wakati mwafaka sana kwani Jumapili ya wiki hii nilishuhudia kufunguliwa kwa maktaba ya umma iliyokuwa imefungwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati karibu na hapa ninapoishi. Nilipita pale na nilikuta mstari mrefu sana wa watu wakisubiri kuingia maktabani....

                    Taifa lisilojisomea ni taifa la wanakondoo wanaoweza kupelekwa ndiko-siko kwa urahisi sana. Ni taifa lisilojua wala kuhoji matumizi ya raslimali zake. Ni taifa la watu walio tayari kuuza kura zao kwa kuwa tu eti wamepewa jozi ya kanga! Ni taifa lisilo na mwelekeo. Ati, ingekuwaje kama Watanzania (angalau kwa wale tunaokaa mijini na wenye uwezo wa kujisomea)  tungekuwa na mwamko wa kujisomea vitabu na kufuatilia mambo kwa kina? Mfuatilie Mzee wa Lundu katika makala hii changamshi hapa chini. 

                    *****************************


                    Mara nyingi napendelea kutembelea mgahawa wa vitabu wa Soma(Soma Café) uliopo mtaa wa Regent, Mikocheni. Na kila mwezi nafanya ukaguzi kujua kuna gani vitabu vipya ama vya zamani ambavyo sikuwahi kuvisoma.

                    Katika kuhudhuria Soma Café iliwahi kujadiliwa ni kwanini Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu au tutajengaje utamaduni wa kusoma vitabu nchini mwetu. Ingawaje hoja zilikuwa zinalenga kuwalaumu Watanzania kwa desturi hiyo, lakini mama Dimere Kitunga alikuwa na hoja tofauti kwayo.

                    Yeye alidai endapo Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu mbona Biblia au Korani zimefika hadi vijijini na vinasomwa sana? Swali hili lilikuwa changamoto kubwa, na ingawa mjadala huo ulifanyika kitambo lakini siyo vibaya kwa Watanzania kuendelea kujiuliza udhaifu huu.

                    Pamoja na hoja kadhaa za wachangiaji, lakini inaelekea mama Dimere Kitunga alitushika pabaya siku hiyo. Na kwakuwa kusudio lake lilikuwa kuona tunajibu vipi hoja hii basi ilinipa changamoto na kujiuliza maswali mengi sana kuhusu desturi hii ya kutosoma vitabu.

                    Ni rahisi sisi Watanzania kwenda kushinda baa na kunywa bia kisha kuota vitambi halafu wengine siku inayofuata wanajigamba kuwa wamechoka kwakuwa walikuwa baa, lakini suala la kutafuta vitabu na kujisomea kama utamaduni halisi imekuwa taabu kwetu. Hali hii imejenga taswira ya watu kupenda habari za udaku kwamba msanii fulani huko Ughaibuni ana mimba au amejianika hadharani hadi nguo za ndani kuonekana.

                    Ama ni rahisi watu kujisomea habari kwamba kondomu yapasuka mwanamke aangusha kilio, ni rahisi sana kusomwa na kuvutiwa tu na maudhui ya mahusiano ya jambo hilo na mazingira yetu. Si vibaya kusoma habari makini, na siyo vibaya kusoma habari nyepesi endapo tu wepesi wake unaleta matokeo chanya kwa jamii na uelewa.

                    Hata hivyo asilimia 99 ya habari za udaku ni upuuzi mtupu, na imekuwa rahisi kwa baadhi ya watanzania kuchukua nafasi ya kusoma habari hizo. Utamaduni wa kusoma vitabu umetoweka, na upo kwa wachache sana.

                    Ni rahisi kwetu kwenda mitaani au kukaa vijiweni huku tukipeana michapo motomoto, lakini asilimia nyingi ya michapo hiyo ni upuuzi. Na tabia ya kuendekeza upuuzi ni kuwa mtumwa kisha kujenga jamii ya kitumwa iliyokosa ufahamu na kuendekeza ujinga na kujenga taifa la watu wasiojua lolote.

                    Tukumbuke kwamba kiwango cha ujinga kimeongezeka ndani ya taifa letu. Hili lilisemwa wazi katika kikao cha bunge kilichopita na waziri anayehusika na dhamana ya elimu nchini Profesa Jumanne Maghembe kwamba ujinga kwa sasa umeongezeka kwa 30% sasa, tofauti na enzi za Mwalimu Nyerere na sera za ujamaa.

                    Ni dhahiri kiwango cha ujinga hiki hakiwahusu wasiosoma pekee bali kuanzia kwa wanazuoni yaani wasomi wa ngazi za juu na wasiokuwa wasomi. Jambo hili ni mkusanyiko wa jamii ambayo inapimwa kwa kiwango cha uelewa wa mambo. Sasa kwa asilimia hizi, tutajengaje utamaduni wa kusoma vitabu?

                    Utamaduni wa kujitafutia vitabu au kujiwekea utaratibu wa kujua ni vitabu gani vimeingia madukani na vinahusu nini haupo miongoni mwetu. Ndiyo maana nasema swali la mama Dimere Kitunga lina changamoto nyingi. Na kama tunaweza kukiri tumekuwa wazembe katika suala zima la usomaji vitabu, basi ni muhimu kujiuliza pia ufahamu wetu wa mambo.

                    Kama kawaida, ninapoingia katika maduka ya vitabu, jambo la kwanza ni kuangalia aina ya vitabu vilivyopo ambavyo vipya au vile ambavyo sikuwahi kuvisoma huko nyuma. Wakati Fulani niliamua na naendelea kukusanya riwaya zote za Joran Kiango zilizotungwa na hayati Ben Mtobwa.

                    Dhumuni langu ni kutaka kuhifadhi kazi zote za Ben Mtobwa, na nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini wakati nikifanya hivyo kunajitokeza hali ya mshangao kwa baadhi ya watu kuona suala hilo, lakini wapo tayari kwenda baa na kunywa pombe na kula nyama choma. Na wengine wanaweza kutumia muda mrefu wakitumia huduma za Facebook au Twitter, lakini siyo rahisi kuamua kujisomea vitabu pia.

                    Na kwa sasa zipo njia nyingi za kujisomea vitabu kwani baadhi ya watunzi wameweka vitabu vyao kwenye mtandao jambo ambalo linarahisisha usomaji pia kupata habari juu ya vitabu vipya. Kwasasa maduka yapo hadi mtandaoni, kwa mfano teknolojia ya uchapaji vitabu ya LULU, ambapo baadhi ya watunzi huchapa hapo vitabu vyao na kuviuza kwa wasomaji.

                    Huduma hiyo inarahisisha kujua ni vitabu gani na mwandishi gani ametoa kazi mpya. Au huduma za Amazon ambapo utaweza kuona vitabu(endapo unatafuta) ambavyo huuzwa. Haya ni mapinduzi makubwa sana katika masuala ya vitabu.

                    Lakini suala hili limekuwa likifanywa na wachache kwani wengi wetu tunasingizia vipato vidogo lakini ndani ya vipato hivyo tunaweza kushinda baa na marafiki tukinywa pombe na kula nyama choma kuliko kujua kulikoni katika maduka ya vitabu.

                    Na kwa wengine hata kujisomea magazeti imekuwa taabu kubwa sana. Katika mgahawa wa Soma Café mijadala ni mingi,michezo ya watoto na vitabu hupatikana hapo vya kila aina, lakini ni wachache wanaotumia muda wao kwenda kujionea kuna nini.

                    Nakumbuka mwezi mei mwaka 2009 wakati wa ziara ya mtanzania Fred Macha, wapo waliojaribu kuuliza alifanya nini katika warsha zake, lakini kutumia muda kwenda British Council, nyumba ya Sanaa, na Soma Café kumsikiliza anatujuza nini kutokana na kuishi kwake ughaibuni na suala zima la uandishi wa raia au usomaji wa vitabu, hawataki kulitenda.

                    Kwa hili tunatakiwa kujiuliza ni namna gani tunaweza kujenga dhana ya ‘networking’ au kutumia warsha na makongamano ya vitabu ili kujenga utamaduni wa kuongeza ufahamu. Suala hili limekuwa gumu kueleweka na naona watanzania halichukulia kama ajenda muhimu maishani mwao.

                    Na wimbi la kutojisomea vitabu limeshamiri katika jamii yetu huku tukitegema matokeo chanya kwa kulea uzembe. Ndiyo maana tunaona kiwango cha ufahamu wa mambo ni duni sana katika jamii yetu, kila mtu anawazia hela ya kula, ,lakini hatutambui hela ya kula ni pamoja na kula vitabu yaani kujisomea.

                    Wimbi hili la kulea jamii isiyopenda vitabu imetmalaki sana, na hata wanazuoni wetu hawataki kujijuza ziadi ya kile walichonacho katika taaluma zao. Na hili niliwahi kujadili na rafiki yangu Ambroce Nkwera, ambaye anaeleza kwamba hadi vyuo vyetu vikuu vimejaza wazembe wengi ambao hutumia muda kusoma vitabu kwa manufaa ya kushinda mitihani pekee.

                    Mbali na umri mdogo wa wanavyuo hao ambao huamabatana na ufahamu duni, ni dhahiri suala hili limekuwa likizidi kujenga jamii isiyopenda kusoma vitabu. Siyo siri ukitaka kuboresha lugha,ufahamu wa masuala mbalimbali ni muhimu kujisomea vitabu.

                    Vitabu vinao utajiri mwingi sana, na nakumbuka katikia moja ya mijadala pale Soma Café, mwandishi mahiri afrika Shafi Adam Shafi alilaumu sana jamii yetu kwa kulea utamduni mbovu wa kutojisomea vitabu. Pamoja na malalamiko ya ukosefu vya vitabu vya Kiswahili, lakini kwa hakika tunavyo vitabu vingi tu lakini watanzania tumelala usingizi mnono wenye madhara kwa taifa letu.

                    Ukipita kwa wauzaji wa vitabu mitaani utapambana na vijitabu vya kipuuzi ambavyo waandishi wake hujigamba kwa kusimulia mambo ya kipumbavu kabisa. Vipo vijitabu ambavyo nachelea kusema ni ujinga hata kuviingiza sokoni na ujinga kuruhusu kuviingiza sokoni kwababu havina msaada wowote kwa jamii.

                    Orodha ya vijitabu hivyo kwa namna nilivyochunguza vimejazana kwa majina ya mapenzi yaani jamii yetu imechukulia suala la ngono na mahusiano ya kimapenzi kama ajenda muhimu hivyo kujisomea vijitabu vyenye kila dalili za kutoongeza ufahamu wowote. Nakumbuka Shafi Adam Shafi aliwahi kusema, unaweza kuona vitabu vipya lakini havina lolote la maana.

                    Anasema vitabu vingine ukivisoma ni kama umesimama katikati ya shimo la takataka kwani havishtui wala havina lolote ambalo jamii inaweza kujivunia kwa maana ya kujielimisha kwalo. Na mbaya zaidi mambo mengi ya kipuuzi yameshika kasi nchini mwetu.

                    Tunalea watoto wetu kwa misingi ya kuwafanya watumie muda mwingi kutazama runinga, kuwnunulia simu, na kuwshirikisha kwenye mambo ambayo hayana msaada wowote kwao. Na wimbi la kulea watoto kwa misingi ya tamaduni za kigeni yaani zile ambazo tunadhani bora, lakini suala la kuwasomea vitabu,kuwanunulia vitabu ni ajenda ngumu huku tukisingizia umasikini.

                    Ninajisikia vibaya kukumbuka hali ilivyo nchini mwetu Tanzania huku tukitumia kigezo cha umasikini kuhalalisha ujinga wetu. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake kwenye duka la vitabu?

                    Ni mara ngapi mtoto amehimizwa umuhimu wa kujisomea vitabu?Sasa, kama watoto wanalelewa hivyo, je, tunaweza kutegemea kuwa Taifa letu litaweza kushindana na wenzetu wa ughaibuni katika ulimwengu huu wa leo na wa kesho ambao unategemea elimu na maarifa? Ni lini na vipi watanzania tutajenga utamaduni wa kusoma vitabu?

                    Na la maana zaidi ni kwanini tufikie hatua ya kuona suala la usomaji vitabu linaambatana na utajiri? Je ni kweli kwamba kwa mwaka mzima hatuwezi kujinunulia hata kitabu kimoja? Nini hatima ya nchi yetu katika usomaji vitabu? Na nini hatima ya Taifa letu la Tanzania katika maendeleo?

                    Friday, April 2, 2010

                    FIKRA YA IJUMAA: IPI NI RAHA KUU MAISHANI???

                    • Tunasaka pesa usiku na mchana mpaka tunadai eti muda hautoshi!
                    • Tunajirundikia "vijisenti" kwa kadri inavyowezekana, potelea mbali hata kama ni kwa njia za haramu!
                    • Tuna........
                    • Halafu siku ya siku inapofika, tunaacha vitu vyote tulivyohangaikia katika maisha yetu, tunavishwa "masulupwete" yetu na kutupwa gizani...
                    • Upo mkondo wa mawazo unaodai kwamba pengine lengo letu kuu mojawapo hapa duniani ni kusaka raha..
                    • Kama hivi ndivyo, ati ni raha gani ikupayo raha sana hapa duniani hadi ukaridhika na kusema kwamba sasa hata ukiondoka utakuwa umefaidi?
                    Ijumaa na Pasaka njema kwa waaminio. 

                    HUYU BABU "UZALENDO" UNATAKA KUMSHINDA NINI...


                    Binadamu sie.....

                    NI ULIMI HAUNA MFUPA AMA?


                    Rais Bush (II)  aliwahi kusema maneno yafuatayo kuhusu Afrika.

                    "We spent a lot of time talking about Africa, as we should. Africa is a nation that suffers from incredible disease."

                    Kumbe jamaa walimjibu kwa njia ya tisheti!

                     
                    Angalizo: Ni ulimi uliteleza au ni kweli raisi huyu alikuwa anaamini kwamba "Africa is a nation that suffers from incredible disease?"

                    Thursday, April 1, 2010

                    MAREKANI YAFIKIRIA KUTUMA NDEGE ZA KIVITA KUISAIDIA SERIKALI YA SOMALIA

                    • Marekani inafikiria kutuma ndege zake za kipelelezi zijulikanazo kama "drones" pamoja na vifaa vingine vya kivita nchini Somalia ili kuisaidia serikali ya nchi hiyo katika vita vyake na wapiganaji wa Al-Shabaab wanaosadikiwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda. 
                    • Ndege hizi za drones huongozwa na marubani ambao hubakia ardhini; na pamoja na mafanikio yake makubwa katika vita vya Iraq, Afghanistan na Pakistan, mara nyingi pia zimekosea shabaha na kusababisha maafa makubwa kwa raia.
                    • Inavyoonekana Wamarekani hawataki kupeleka wanajeshi wao katika uwanja wa mapambano huko Mogadishu. Pengine bado wanakumbuka kisa cha mwaka 1993 ambapo wanajeshi wake 18 waliuawa na hatimaye kuwafanya wafungashe virago kwa haraka haraka na kuondoka.
                    •  Naamini kwamba tatizo la Somalia ni letu Waafrika na kama kweli tungekuwa na  nia ya dhati la kulitatua tungeweza. Historia hata hivyo inaonyesha vingine. Kwa habari zaidi soma hapa.

                    YULE MWANAFUNZI MLEMAVU KUTOKA GHANA ALIYEPIGWA RISASI NA POLISI WA CHUO APATA NAFUU, AZUNGUMZA


                    Photo by Rob C. Witzel / Staff photographer
                    • Yule mwanafunzi mlemavu kutoka Ghana aliyepigwa risasi na polisi wa chuo hatimaye amepata nafuu na kuzungumza juu ya kisa kilichosababisha mzozo wake na polisi na hatimaye kuishia kutandikwa risasi ya usoni.
                    • Tangu kupigwa risasi kwake, alikuwa analindwa na polisi kwa masaa ishirini na nne na pamoja na kwamba ni mlemavu wa miguu na anatembea kwa kutumia magongo, bado polisi walimfunga minyororo miguuni wakati alipohitaji kwenda chooni baada ya kupata nafuu.
                    • Leo alikuwa anatarajiwa kutolewa hospitalini na kupelekwa moja kwa moja katika zahanati ya gereza lakini familia yake imeweza kulipa dola 10,000 na kufanikiwa kumwekea dhamana.
                    • Matibabu yake tangu apigwe risasi yanakadiriwa kugharimu dola 290,000 na Idara ya polisi inabidi ilipe kwa sababu kwa muda wote aliokuwa amelazwa alikuwa chini ya uangalizi wake. Ni kwa sababu ya kuogopa gharama ndiyo maana leo alitaka kuhamishiwa katika zahanati ya gereza.
                    • Anadai kwamba siku aliyopigwa risasi hakuwa na matatizo yo yote na aliwaomba polisi waondoke. Hata walipovunja mlango wa chumba chake, hawakumwambia kunyosha mikono juu au kama alikuwa chini ya ulinzi kama ilivyo kawaida.
                    • Habari kamili inapatikana hapa.

                    JIANDIKISHE HAPA

                    Enter your email address:

                    Delivered by FeedBurner

                    BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO