NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, May 31, 2010

TANZANIA TANZANIA, NINAKUPENDA KWA MOYO WOTE: UZALENDO, USASA NA UTANDAWAZI

 • Mwalimu Nyerere alikuwa "jiniazi". Mbali na kufanikiwa kuutokomeza ukabila, propaganda zake za "zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM" na porojo zingine zilizokuwa zimefumwa mumo kwa mumo katika masomo ya siasa mashuleni, elimu ya watu wazima, nyimbo za mchakamchaka na hata JKT, zilifanikiwa kutufanya vijana (wa enzi zileeeee) tuipende sana Tanzania. 
 • Ni kwa sababu hii kamwe huwa sioni aibu "kujimwambafai" kwamba mimi ni Mtanzania  halisi ninayetoka kwenye nchi yenye amani, upendo (sijui kama bado upo), isiyo na ukabila (ingawa hii inaua lugha zetu za kiasili), Tanzania yenye Mlima Kilimanjaro (ingawa inasemekana na kuaminika kwamba uko Kenya), Tanzania iliyo mzalishaji pekee wa Tanzanite (ingawa pengine Kenya ndiye muuzaji mkuu), Tanzania yenye Serengeti, Zanzibar na kila aina ya utajiri (ambao sijui kama Mtanzania wa kawaida anaufaidi). Ndiyo maana  sijawahi kufikiria hata siku moja kwamba nitaweza kuukana uraia wa nchi hii na kuchukua uraia wa nchi nyingine. 
 • Kuna kitu fulani cha thamani na cha fahari sana kuwa Mtanzania, na kwa hili Mwalimu Nyerere anastahili pongezi.  
Ndiyo maana ukiingia katika ofisi hii...


Utakutana na Tanzania na Utanzania papo kwa papo

(1) Utakaribishwa Tanzania...

(2) Na si ajabu ukaondoka na kofia ya Tanzania

(3) Au kunywea chai kwenye kikombe cha "I Love Tanzania"
 
 • Japo ni hivi, bado huwa nasikitika na kupatwa na kigugumizi ninapoulizwa kama kweli niyasemayo ni ya kweli. Kama ni kweli kwamba nchi hii niipendayo sana ina amani, maliasili za kutosha na ilibahatika kuwa na mmojawapo wa viongozi bora kabisa barani Afrika (Mwalimu), mbona bado ingali masikini hivi? Hali huwa mbaya zaidi ninapobanwa kuhusu suala la ufisadi - ile tabia kengeufu tena angamizi ambapo "mashing'weng'we" wachache tu waliofanikiwa kuipakata keki ya taifa wanaiguguna wao kwa wao bila kujali wenzao wanaokufa na njaa. Kwa hili huwa sipendi kuitetea Tanzania na huwa naiacha iparurwe.
 • Kizazi cha dot.com - hiki kinachokulia katika utandawazi na usasa kinajivunia Utanzania? Kina sababu ya kufanya hivyo? Inabidi tuwe na wasiwasi?
Angalizo: Nimeandika kwa "kuparaza" tu kwani mtandao ninaotumia una vituko kwelikweli. Kama kuna makosa ya hapa na pale katika mantiki au vinginevyo, natangulia kuomba msamaha!

Saturday, May 29, 2010

TAARIFA FUPI: JAMANI NIKO SAFARINI NA NILIKO HAKUNA MTANDAO (WA KUAMINIKA)

 
Wadau na wanablogu wenzangu;
 • Niko safarini na niliko hakuna mtandao (wa kuaminika). Nitarudi uwanjani wiki kesho japo kwa kwikwi kidogo. Japo nimepotea kidogo bado sijaliacha (na sitaliacha) pigano. Libeneke litaendelea kama kawaida. Tuko pamoja daima!!!

Friday, May 21, 2010

FIKRA YA IJUMAA: TUNASONGA MBELE AU TUNARUDI NYUMA? USHIRIKINA, VIBAKA NA HUKUMU YA PAPO KWA PAPO

 • Huyu kijana ambaye anasemekana ni kutokea Mwanza (haijulikani kama ni Msukuma msije mkaanza kunirushia vijembe/madongo) amepigwa na kuuawa na wananchi wenye hasira baada ya kudaiwa kuwa ameanguka wakati akiruka na ungo akiwa katika safari zake za kishirikina kule Mbezi Luis jijini Dar es salaam siku ya Jumanne (18/5/2010).
 • Nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari miaka ile nilikuwa nafikiri kwamba imani hizi za kishirikina zitaanza kupungua baada ya watu wengi kujipatia elimu na "kuelimika". Leo hii tuna mashule ya sekondari mpaka vijijini, vyuo vikuu vinazaliwa kila siku, academy ndiyo usiseme lakini bado imani za kishirikina ndiyo zinazidi kujiimarisha katika jamii. Kuna nini? Kwa wataalamu wa Elimu Jamii (Sosholojia), tatizo hasa ni nini?
 • Inasemekana polisi nao iliwachukua zaidi ya masaa mawili kufika katika tukio hili na kumkuta huyu kijana tayari ameshauawa na wananchi wenye hasira.  

 • Tabia hii ya kuua mtu kwa tuhuma kama hizi au eti kwa vile tu amekwapua simu au saa nayo inatatanisha. Ni kweli maisha ya mtu yanalinganishwa na simu au saa? Wapo wanaounga mkono tabia hii ya kuua vibaka kwa vile eti vibaka wamezidi, lakini sidhani kama hili ndilo suluhisho sahihi na la kudumu. Inabidi tujaribu kutafuta hasa kiini cha tatizo ni nini. Vibaka hawa wanatoka wapi? Kwa nini vijana  wengi wanaamua kuwa vibaka au majambazi? Pengine ni kwa sababu ya mfumuko wa matabaka na ufa mkubwa unaozidi kupanuka kati ya wachache wanaokula na kusaza hadi kutupa makombo majalalani kwa upande mmoja na wale wengi wanaoshindia chips dume au kulala na njaa kwa upande mwingine. Tukijaribu kuchunguza na kutafuta hasa kiini cha tatizo, na kujibidisha kutafuta masuluhisho yenye mashiko, tutakuwa tunajiepusha na misukosuko zaidi huko mbele ya safari. Na wamiliki wa mfumo wasikae na kukenua meno wakidhani kwamba hukumu hizi za papo kwa papo kamwe hazitawagusa eti kwa vile tu wanamiliki vyombo vya dola. Historia ina mifano mingi inayoonyesha kwamba mambo kama haya yakiachiwa yanaweza kuleta mtafaruku mkubwa katika jamii. Wikiendi njema!
  • Kwa habari zaidi juu ya kisa hiki, tembelea blogu ya Amani Masue

  Thursday, May 20, 2010

  "TATIZO" LA NGUO ZA MITUMBA; NA TULIKOTOKA

  • Kama nguo kama hii inavaliwa katika jamii ambayo haifahamu lugha iliyotumiwa, basi hakuna neno. Sidhani kama huyu mama na wanajamii wenzake wanafahamu ujumbe ulio katika fulana hii. Inawezekana pia kwamba pengine fulana hii imevaliwa kwa makusudi ili kuwasilisha ujumbe fulani. Nimeshawahi kuona mabinti hapa Marekani wakiwa wamevaa kaptula fupi zenye maandishi yasemayo "Self Service" makalioni. Hii pia yaweza kuwa ni, kama wasemavyo wenyewe, "fashion statement!" kama huyu mdot.com hapa chini.

  • Mheshimiwa Salim Ahmed Salim "alituokoa" alipochukua uwaziri mkuu baada ya Morani kuanguka enzi zile na kuruhusu nguo za mitumba. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba katika sehemu nyingine za nchi watu walikuwa wameanza kuvaa nguo za magunia. Tumetoka mbali ati!

  Wednesday, May 19, 2010

  MGEMA AKISIFIWA...TUJIFUNZE KUTOKANA NA MISUKOSUKO YA KAMPUNI LA TOYOTA

  • Kampuni la Toyota lilikuwa limejijengea heshima kubwa duniani kote kwa kutengeneza magari yanayoaminika na yenye kudumu kwa muda mrefu. Ndiyo maana utayaona mashangingi (Toyota Land Cruisers) yakikata mbuga kwenye matope na kwenye barabara za kila aina miaka na miaka. Hali kadhalika Toyota Corolla, Camry, RAV4 na aina nyinginezo. Ndiyo maana watu wengi walishangaa waliposikia kwamba Toyota ilikuwa imeanza kutengeneza magari yenye matatizo ya kiusalama.  
   • Mimi pia nimeathiriwa na tatizo la Toyota kupuuzia sifa zake za msingi zilizoifanya Toyota iwe Toyota. Mwaka 2008 nami nilijitutumua nikanunua Toyota FJ Cruiser mpya tena yenye kila kitu ndani. Hili ni gari la ukubwa wa kati ambalo lilielezwa kuwa ni kama Land Cruiser ndogo na muundo wake ukawa unafananafanana na Hummer ndogo. 
    • Kwa nje ni gari zuri linalovutia sana
    • Milango yake inafunguka kwa pamoja, na kiu yake ya petroli ni ya kawaida tu.
     • Tatizo hata hivyo ni kwamba ukiliendesha kwa muda mfupi tu utagundua kwamba karibu kila kitu kilichomo ndani ni plastiki na unaweza kuona kabisa kwamba limetengenezwa kwa kufinyangwafinyangwa tu bila umakinifu wa kutosha. Baadhi ya vitu vya ndani vinadondoka au kuchanika vyenyewe hata miaka mitatu halijamaliza. Kwa hakika hii si tabia ya magari ya Toyota tuliyokuwa tumezoea. Ndiyo maana imebidi nilitelekeze na kurudia mkweche wangu wa zamani.
     • Wachambuzi wengi wanaamini kwamba katika juhudi zake za haraka haraka kulipiku kampuni kinzani la General Motors, Toyota ilijikuta inakata njia za mkato na kusahau sifa zake za msingi zilizoifanya ijizolee sifa duniani kote kwa kutengeneza magari ya kuaminika na yanayodumu sana. Pengine ni yale yale ya mgema akisifiwa......
     • Hata sisi, ni mara ngapi tumeipuuzia misingi na kanuni zetu ongozi tulizojiwekea maishani, kanuni pweke anuai zinazoupambanua usisi wetu kwa lengo tu la kuwafurahisha, kuwaridhisha au kushindana na binadamu wengine au kujinufaisha? 
     •  Tunayo mengi ya kujifunza kutokana na misukosuko inayolikumba kampuni la Toyota.

       MALIZIA SENTENSI IFUATAYO: KAMA HUMPENDI YESU, KAMWE HUTAINGIA....

       • Tazama jibu kwenye fulana ya huyu "mlokole!"

       Monday, May 17, 2010

       ATI, ARISTOTLE ALIKUWA SAHIHI "ALIPOWAPIGA VIJEMBE" AKINA MAMA NAMNA HII?


       Aristotle alisema hivi:
       • "Mothers are fonder than fathers of their children because they are certain they are their own."
       • Tazama hapa na hapa kuona kama Aristotle alikuwa sahihi. 

        Friday, May 14, 2010

        BAJETI YA MFANYAKAZI INAPOJUMUISHA NYUMBA NDOGO NA MICHANGO YA ARUSI, SEND OFF NA KOMUNIO...

        • Japo bado kuna usafiri, huduma za matibabu, chakula na mahitaji mengineyo, mahitaji mengine pia si ya lazima (mf. nyumba ndogo, michango ya harusi, michango ya send-off, michango ya komonio...)
        • Japo katuni hii imefumbata ucheshi na dhihaka, inaashiria ugumu wa maisha unaomkabili mfanyakazi wa kawaida wa Tanzania kwa ufasaha. Halafu tunategemea kweli huyu apewe rushwa akatae?

        Wednesday, May 12, 2010

        TAHAJUDI (MEDITATION) - TAALUMA INAYOENDELEA KUKUA KWA KASI

        • Taaluma na falsafa ya tahajudi-meditation sasa imekubalika hata katika nchi za Kimagharibi. Hata madaktari wameanza kuwashauri wagonjwa wao kufanya meditation kama sehemu ya tiba, mazoezi ya kimwili pamoja na kuleta utulivu wa kifikra na kisaikolojia. Katika viwanja vya ndege vingi, kwa mfano, sasa kuna vyumba maalum ambamo wasafiri waliochoka wanaweza kuingia na ku-meditate kabla ya safari zao.
        • Hapa ni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O'Hare kule jijini Chicago nchini Marekani. Nilipoiona picha hii nilimkumbuka Kamala

        Tuesday, May 11, 2010

        UNAOGOPA KUSAFIRI KWA NDEGE? SOMA HAPA UONE KAMA UNAWEZA KUISHINDA AEROPHOBIA!!!

        Jana wakati natoka Toronto Canada jambo la ajabu lilitokea. Japo kulikuwa na misukosuko na ndege ilikuwa inatikisika sana, sikuwa na hofu wala mshtuko. Mwenyewe nilijishangaa kwani kwa kawaida katika hali kama hii ningekuwa ninatoka jasho na nimeshikilia kiti kwa nguvu zangu zote. Inawezekana nimeishinda  Aerophobia - hofu ya kusafiri kwa ndege!

        Sina uhakika lakini pengine inawezekana. Mbali na mambo mengine, nimesoma na kujielimisha sana juu ya ajali za ndege.  Baadhi ya mambo niliyojifunza ni haya:
        1. Usafiri wa ndege ndiyo salama zaidi kuliko usafiri mwingine wo wote.
        2. Uwiano wa uwezekano wa kufa kwenye ajali ya ndege kwa mashirika ya ndege yenye ndege mbovu ni mara moja tu kwa safari 724,000. Kwa mashirika ya ndege yenye kuzingatia usalama, uwiano ni chini ya mara 1 kwa 10,000,000. Na kama unasafiri kila siku kwenye ndege kwa miaka 30 mfululizo, uwiano wa uwezekano wa kufa kwenye ajali ni mara moja kwa 787.
        3. Uwezekano wa kupigwa na radi ni mara moja kwa 750,000 na kama utaishi mpaka kufikisha miaka 80 basi uwezekano wako wa kupigwa na radi ni mara 1 kwa 6250.
        4. Uwiano wa uwezekano wa kufa katika ajali ya gari ni 1 kwa 67. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kufa katika ajali ya gari kuliko kufa katika ajali ya ndege.
        5. Isitoshe, kuna vitu vingi vinavyoweza kuhitimisha maisha ya binadamu ikiwemo kurogwa (washirikina mpo?). Hapo ulipo kuna mifumo tata lukuki katika mwili wa binadamu ambayo kila mmoja ni lazima ufanye kazi barabara vinginevyo binadamu aweza kuanguka na kukata roho na kuwaacha watu wakisema eti ametupiwa jini kumbe ni kiharusi, kisukari, mshtuko wa moyo na mengineyo.
        6. Isitoshe, kama alivyosema Marcus Aurelius (a.k.a Mwenye hekima) - mtawala wa himaya ya Roma ya kale kutoka mwaka 161 mpaka kifo chake mwaka 180 B.K, kuna tofauti gani kati ya yule anayeishi siku tatu na yule anayeishi vizazi vitatu? Ati, kuna tofauti yo yote ukifa leo na ukifa baada ya miaka 50 kuanzia sasa? Kama ipo ni ipi?
        • Baada ya kusomasoma huku na huko na kutafakari sana, nimefikia hitimisho kwamba pengine ni upuuzi tu kuogopa kusafiri kwa ndege kwani uwezekano wa kufa humo ni mdogo mno.Inabidi tuogope zaidi kufa katika ajali za barabarani kuliko kufa katika ajali za ndege.........Lakini siku moja wakigundua ndege ambayo haitikisiki sitalalamika! Kwa maoni zaidi kuhusu kifo gonga hapa na halafu usikose kumtazama huyu rubani mbabaishaji hapa chini.        Monday, May 10, 2010

        DUNIA INGEKUWAJE BILA MWANAMKE? HAPPY MOTHER'S DAY KWA MAMA NA AKINA MAMA POPOTE MLIPO

        Ni mama na mimi nilipokuwa mwaka wa pili Mlimani. 
        Hapa ni kijijini Bariadi. NAKUMBUKA!!! 
        ******
        • Mzee Matondo aliuacha mwili mapema sana na kuniacha nikiwa na miezi mitatu tu. Ni mwanamke machachari shujaa aitwaye Eunice Long'hwe Mugema Dindai ndiye alijifunga kibwebwe na kuhakikisha kwamba ninakua, kusoma na kunifanya niwe kama nilivyo leo.
        • Kutokana na mahusiano haya ya pekee na mama, pengine ndiyo sababu ninayo heshima na upendo wa ajabu kwa akina mama. Kwangu mimi mwanamke ni shujaa na nguzo kuu ya familia na jamii kwa ujumla. Bila mwanamke sijui kama familia nyingi na jamii vingeweza kusimama tisti. Sijui bila mwanamke ulimwengu huu ungekuwaje.
        • Japo Mother's day ilinikuta nikiwa safarini jana, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mama na akina mama wote. Asanteni kwa kujidamka asubuhi na mapema kwenda kutafuta maji. Asanteni kwa kusafiri maili nyingi kwenda kutafuta kuni. Asanteni kwa kulea watoto wenu katika mazingira magumu. Asanteni kwa kila kitu.
        • Hebu tuungane na Emmy Kosgei, mwimbaji mahiri wa Injili kutoka Kenya anayeimba katika lugha ya Kikalenjin   katika kuwabariki na kuwasherehekea mama zetu wapendwa kwa yote waliyotutendea na wanayoendelea kututendea. Tuwakumbuke, tuwaenzi, tuwaheshimu na kuwatunza hasa wakati huu wa uzee wao wanapotuhitaji sana. Tusikakawane mijini tukiponda raha kumbe mama zetu wazazi waliotuleta hapa duniani wanateseka vijijiniAti, ni nani kama mama?

        Huyu hapa Emmy Kosgei akiuliza Nani Kama Mama?
        • Unaweza pia kusoma hapa na kuwasikiliza Boys II Men katika wimbo wao wa A Song to Mama.

        Friday, May 7, 2010

        TOFAUTI KATI YA WAKURYA NA WAJITA


        Nilianza kiuchokozichokozi na kimzahamzaha tu hivi.....

        NB: Tofauti ya Wakurya na Wajita ni ipi? Wajita ni wapole lakini Wakurya ni wakali sana. Wajita ni wavuvi (si wavivu?) lakini Wakurya ni wafugaji. Nyingine???

        ********************
        Nikajibiwa hivi......
        1. Wajita ni karibu na Wakerewe na Wakara...Wazinza, Wahaya, Wahangaza. kusema kweli majina mengine ya mahali huko sehemu za Burundi, Rwanda, na Uganda Kusini na Kusini Magharibi ni sawa na sehemu nyingine za Majita: Bulinga, Buinja!
        2. Wakurya wanachonga meno na kutoboa masikio; wako karibu na Wazanaki, Waikizu, Wanata, Waikoma, Wangurwimi (Wangoreme), na Wasimbiti.
        3. Wakurya ni karibu na makabila ya Bonde la Ufa: Wakisii, Wakalenjini, Wamaasai, Waturkana wa huko Kenya na makabila mengi ya Tanzania ya Bonde la Ufa, kwa mfano, Watatoga, Wambulu na kadhalika. Niseme ni  mchanganyiko wa Wabantu na Wanailotiki.
        4. Ninaamini Wajita ni Wabantu zaidi ukilinganisha na Wakurya!
        5. Wajita wako Musoma na Wakurya wako huko Tarime.
        6. Ni mwiko kwa Wajita kutahiri wasichana wao.
        7. Wajita wengine hawatahiri wavulana wao, pia.
        8. Wajita si wachunga ng'ombe sana (wakulima na wavuvi) kama Wakurya.
        9. Wajita hawatoboi masikio.
        10. Wajita hawachongi meno.
        11. Wajita hawadai mahari ya ng'ombe wengi kama Wakurya, kiasi cha vijana wao kujihusisha na wizi wa ng'ombe.
        12. Wajita walikumbatia elimu ya kisasa zaidi kuliko Wakurya.
        13. Wajita walipeleka vijana wao mashuleni kuliko Wakurya waliopenda wavulana wao kuchunga ng'ombe na wasichana wao kuthaminiwa kwa mahari kuliko elimu ya mashuleni.
        14. Wajita ni akina yego (wanaume) na yebhe (wanawake); Wakurya ni akina mura wanaume na mukari (wanawake).
        Kibwagizo: Nahene!
        Hili ni jibu la mdau makini wa blogu hii anayejiita Esteemed Reader. Kuna cha kuongeza hapa? Mzee wa Mataranyirato upo?

        Thursday, May 6, 2010

        NIKO TORONTO KANADA TANGU JANA JIONI KUHUDHURIA MKUTANO WA ISIMU YA KIAFRIKA

         
        • Mwaka huu wanaisimu na wakereketwa wote wa lugha za Kiafrika tumekutana katika chuo kikuu cha Toronto ili kuhudhuria mkutano wa 41 wa Isimu ya Lugha za Kiafrika. Ni safari ya masaa kama manne hivi kwa ndege kutoka Florida (kupitia Chicago).
        • Nitatoa mada yangu leo saa tano asubuhi. Mada itakuwa juu ya Ruwaza za Toni (au mkazo-sauti) katika Maneno ya Mkopo katika Kisukuma (Tonal Patterns in Kisukuma Loanwords) na kufanya uchambuzi kwa kutumia nadharia ya Fonolojia inayotamba kwa sasa ya Optimality.
         • Ninakerwa sana na ukweli kwamba Kisukuma - pengine lugha nzuri kuliko zote duniani, na tata sana kiisimu bado haina kitabu cha sarufi hata kimoja pamoja na kwamba ndiyo lugha kubwa kuliko zote Tanzania ukiachilia mbali Kiswahili. Yaani kuna vitabu vingi juu ya Kimasai kuliko Kisukuma. Hii haikubaliki!
          • Ni kwa sababu hii ndiyo maana nimeamua kujifunga kibwebwe na kuandika sarufi makini inayojitosheleza ya Kisukuma kwa ajili ya matumizi ya wanaisimu na wapenda lugha za Kiafrika popote duniani. Natumaini kwamba kazi hii itanichukua miaka miwili (najua Mungu Ataniweka hai tu).
           • Ukitaka kuona kama lugha yako itachambuliwa katika mkutano huu basi tazama muhtasari wa mkutano mzima kwa kubofya hapa na halafu bofya kwenye ACAL 41 PROGRAM.
            • Libeneke litaendelea kwa kadri muda unavyopatikana. 

             Monday, May 3, 2010

             NIMEUPENDA HUU UJUMBE

             RAIS KIKWETE ANAFANYA VIZURI ANAPOFANYA HIVI

             • Picha hizi za Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete zinahuzunisha, zinafariji na pia zinatia matumaini. Zinahuzunisha kwa sababu zilipigwa wakati Rais alipokwenda kuifariji familia ya Marehemu Evaristi Semeni - mtoto mwenye umri wa miaka kumi na moja aliyefariki katika ajali ya kugongwa na gari tarehe 26/4/2010 jioni katika kijiji cha Msoga ambapo yeye pamoja na watoto wengine wawili walifariki dunia.
             • Unaweza kuiona huzuni katika uso wa raisi pamoja na baba mzazi wa Marehemu Evaristi Semeni. Tulikuwa tumezoea kuwaona viongozi wa ngazi za juu wakihudhuria mazishi ya familia zenye majina. Picha hii inagusa hisia sana na inamwonyesha raisi katika ubidanamu na utu wake kabisa. Naamini kwamba mzazi huyu, pamoja na huzuni yake yote ya kuondokewa na mtoto wake, alifarijika kwa pole na faraja iliyoletwa na ujio wa kiongozi mkuu wa nchi.
             • Hapa Rais yupo na waombolezaji ndani ya nyumba. Na ukitazama vizuri utaona. Haya ndiyo maisha halisi ya Watanzania wa vijijini ambao kwa bahati mbaya ndiyo wengi. Sijui Rais anawaza nini...
             • Hapa Rais anatoka nje kwenda kuungana na waombolezaji wengine. Nimefikiri mambo mengi sana baada ya kuzitazama picha hizi. Pengine safari kama hizi za viongozi wa kitaifa kwenda kuyaona maisha halisi ya Mtanzania wa kawaida kule kijijini zinaweza kuwa kichocheo kinachoweza kuiamsha upya ari mpya na kuhakikisha kwamba kweli maisha bora kwa kila Mtanzania yanapatikana tena kwa kasi mpya na nguvu mpya!
             • Mungu Awalaze marehemu mahali pema peponi; na tunamuunga mkono rais kwa kwenda kuungana na wananchi hawa wa kijijini katika huzuni yao; na kama alivyosema Mjengwa, kuwapelekea mwanga katika giza lao na matumaini katika hali yao ya kukata tamaa.

             Saturday, May 1, 2010

             NI KALE KAMNYAMA "KAJANJA" KALIKOJIPACHIKA U-HOMO SAPIENS!!!

             • Huyu jamaa anaitwa Rampage Jackson na yeye ana nguvu za ajabu kwani ana tabia ya kuwabeba wapinzani wake na kuwafletisha kwa kuwabamiza chini.
             • Halafu sikiliza wadau wanavyofurahia hapa chini. Homo Sapiens eeh!!!. Pata habari zaidi hapa.

             MJADALA JUU YA MUNGU, DINI, WOKOVU NA MOTO WA MILELE: MAONI BINAFSI YA MTU ASIYEAMINI KWAMBA KUNA MUNGU

             • Leo niliuona ujumbe huu umebandikwa nyuma ya gari kubwa (SUV) karibu na maktaba nilikokuwa nimekwenda kurudisha vitabu. Katika upande wa dereva alikuwa amekaa mwanamke wa makamo huku akisikiliza muziki kwa chini chini.
             • Japo mimi si mwongeaji sana kiasi kwamba watu wengi husema nina aibu na kwamba eti niko "anti-social", niliamua kuongea kidogo na mwanamke yule na kutaka kujua hasa kisa cha ujumbe ule kwenye gari lake.
             • Kiufupi alisema kwamba yeye haamini kwamba kuna Mungu na hataki  sala na maombi kuendeshwa mashuleni au sehemu yo yote isiyohusika mbali na makanisani na sehemu zingine za ibada. Alijitambulisha kwa makeke kwamba yeye ni "proud atheist" na anaamini kwamba dini ni mbinu tu za kumtawala na kumnyonya binadamu na kumzuia asikue na kufikia malengo yake. Aliendelea kusisitiza kwamba dini ni kwa watu "wasiofikiri" (Bofya hapa).
             • Ningekuwa mlokole pengine ningemwashia moto wa sala, mapambio na kusema  katika roho, lakini nilizungumza naye kidogo juu ya sababu zangu za kuamini kwamba kuna Mungu. Nilimuuliza kama anaamini kwamba eti vitu vyote tunavyoviona na tusivyoviona vilitokea kwa bahati tu kama wanasayansi wanavyotuambia. Jibu lake kidogo lilinishangaza. Alisema kwamba anaamini kuna nguvu fulani ambayo pengine iliendesha na inaendelea kuendesha mambo yote, lakini nguvu hiyo si Mungu na wala haina athari zo zote katika maisha yetu. Tunatakiwa kuishi tukiwa huru bila kutishwa wala kukumbushwa kila siku kwamba tutakufa na kwamba eti tutakwenda katika moto wa milele wakati hao wanaotuambia hivyo nao hawajui na wala hawawezi kuthibitisha kile wakisemacho. Dini, aliendelea kusisitiza, ni njia mojawapo tu ya binadamu ili kuwatawala binadamu wenzake na kuwanyonya kupitia zaka, sadaka na njia nyinginezo. Alitoa mfano wa mambo mengi yaliyowahi kutendwa na kanisa Katoliki. Alitaja pia wasiwasi wake juu ya dini ya Kiisilamu na mambo yanayofanyika sasa kupitia makundi kama Al Qaeda na mengineyo.
             • Mwishowe alinipa kadi yake na kuniambia kwamba kama nilikuwa nataka kuendelea na mjadala ule basi nimtafute. Nilimwomba ruhusa ya kupiga picha huu ujumbe nyuma ya gari lake na kisha nikaagana naye. Kuna mwenye maoni yo yote kuhusu mjadala huu juu ya Mungu, dini, wokovu na moto wa milele?

             JIANDIKISHE HAPA

             Enter your email address:

             Delivered by FeedBurner

             VITAMBULISHO VYETU