- Nianze na angalizo: Lengo langu hapa siyo kujigamba wala kujionyesha bali ni kuonyesha (kama vile ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara) jinsi matendo madogo madogo ya kibinadamu yanavyoweza kuwa na athari katika maisha ya binadamu wenzetu hususan wale wenye shida.
*********************************
- Tarehe 9/6/2010 nilipanda daladala kutoka Masaki Mwisho kwenda Posta Mpya. Tulipofika mwisho wa safari nilishuka na kuanza kuelekea jingo la Posta Mpya. Kwa mbele yangu alikuweko mzee mmoja ambaye tulikuwa wote kwenye daladala. Mzee huyu alikuwa amevaa kandambili na nguo zilizozeeka.
- Kwa vile kulikuwa na tope kidogo, mzee yule aliteleza kidogo na kandambili yake ya mguu wa kulia ikakatika. Nilimwangalia akiwa ameghafilika huku akiwa hajui la kufanya na wakati huo huo watu wakianza kumrushia maneno ya kuacha kuzubaazubaa na “kulivaa” tope.
- Kwa bahati nzuri kando ya barabara kulikuwa na vijana waliokuwa wanauza fulana, magazeti, viatu (vya bei mbaya), mikanda pamoja na kandambili.
- Nilitoa noti ya shilingi 5,000 na kumpa yule mzee na kumwambia anunue kandambili mpya. Kwa mikono miwili aliipokea ile noti na kunishukuru tena mno “Mungu Akubariki na kukuzidishia mwanangu”. Alisema huku machozi yakimlengalenga. Na kweli alikwenda na kujinunulia kandambili nyekundu mpya. Nilimtakia siku njema na nikaendelea na mishughuliko yangu.
- Kwangu mimi ni matendo madogo madogo kama haya ndiyo hasa yanasaidia kuupambanua ubinadamu wetu. Si ajabu mzee huyu asikisahau kitendo hiki kidogo maishani mwake kama mimi nilivyoshindwa kukisahau kitendo nilichofanyiwa na mzee mwenye kibaraghashia cheupe, kanzu nyeupe na kandambili za bluu zaidi ya miaka 17 iliyopita pale Muhimbili.
- Hebu na tukawasaidie na kuwatendea wema binadamu wenzetu. Hakuna tendo lenye kuliwaza na kuleta furaha na ridhiko la kweli hapa duniani kama kumsaidia binadamu mwenzako hasa mwenye shida!








