NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 30, 2010

KIKWENU MNAHESABUJE? KIKWETU KUNA NAMBA ZA KIKE (BAKIMA) NA ZA KIUME (BAGOSHA)


FIKRA YA IJUMAA: MDAHALO WA KUKATA NA SHOKA KATI YA “BABA MTAKATIFU” NA MZEE WA KIYAHUDI. TUTAFAKARI !!!

  • Hiki ni kisaasili cha Papa (AKA “Baba Mtakatifu”) na mzee mmoja wa Kiyahudi asiyejua kusoma wala kuandika aitwaye Moishe. Tafadhali kisome kwani kuna jambo kubwa la kujifunza kuhusu maisha na maarifa yetu; na jinsi tunavyoyatazama mambo. Nimekifupisha!
*****************

 
  • Karne moja hivi iliyopita, Papa aliamua kwamba Wayahudi wote ilikuwa lazima wauhame mji wa Roma. Baada ya uamuzi huo kupingwa na Wayahudi wengi, na kutaka aonekane kwamba ni mtu anayependa maelewano, Papa alikuja na pendekezo moja zuri ambalo alidhani kwamba lingewafurahisha Wayahudi na wakati huo huo kuweza kuwaondoa kutoka mji wa Roma bila mtafaruku mkubwa. Aliamua kwamba angefanya mdahalo na mtu ye yote atakayeteuliwa na Wayahudi kuwawakilisha. Kama mwakilishi yule angeshinda mdahalo ule basi Wayahudi wangebakia katika mji wa Roma. Lakini kama Papa angeshinda mdahalo basi Wayahudi wangelazimika kuuhama mji wa Roma mara moja!
  • Wayahudi walianza kutafuta wasomi, wanaakademia, wanafalsafa na watu wengine wenye maarifa ili kuchagua mmoja aliyebobea ambaye angeweza kupambana na Papa katika mdahalo ule. Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, hakuna msomi hata mmoja wa Kiyahudi ambaye alikubali kukabiliana na Papa. Wakiwa katika hatua ya kukata tamaa hatimaye mzee mmoja mfanya usafi (janitor) aitwaye Moishe alijitokeza. Mfanya usafi huyu asiyejua kusoma wala kuandika alikubali kukabiliana na Papa katika mdahalo ule wa kukata na shoka.
 
  • Kwa vile hakuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza na kupangilia hoja kwa mantiki na mpangilio, Moishe alipendekeza kwamba mdahalo ule ufanyike katika ukimya kabisa, yaani bila kuzungumza. Papa alikubali.
  • Siku ya mdahalo ule wa kukata na shoka ilipofika, Moishe na Papa walikaa katika viti vilivyotazamana. Kwa dakika nzima ya kwanza, walikaa wakitazamana tu huku wakiwa kimya kabisa. Hakuna aliyesema neno lolote kwa mwenzake.
  • Dakika ya pili ilipoanza, Papa alinyosha mkono wake wa kulia na kunyosha vidole vitatu. Moishe alimwangalia naye bila kusita alinyosha mkono wake wa kulia na kunyosha kidole kimoja. Papa alipoona hivyo alinyosha kidole kimoja na kukizungusha juu ya kichwa chake. Moishe alijibu kwa kunyosha kidole chake kuelekea chini kwa msisitizo.
  • Kuona hivyo Papa alitoa ule mkate unaoliwa kanisani na waumini kila Jumapili na glasi moja ya mvinyo na kuviweka katika meza iliyokuwa mbele yake. Moishe alijibu kwa kutoa tofaa (apple) kutoka katika mfuko wake na kuliweka katika meza mbele yake. Kuona hivyo Papa alinyanyuka na kusema kwa sauti kubwa, “Nimeshindwa! Myahudi huyu ni mweledi mno. Ameshinda na Wayahudi wanaweza kubakia Roma!.”
  • Baada ya mdahalo huu mkali makadinali wote walikaa wakimzunguka Papa na kumuuliza kilichotokea katika mdahalo ule. Papa aliwajibu, “Kwanza niliinua vidole vyangu vitatu kuonyesha utatu wa Mungu. Myahudi yule aliinua kidole kimoja kunikumbusha kwamba bado kuna Mungu mmoja tu – kitu ambacho ni kweli katika dini zetu mbili. Baada ya hapo nilizungusha kidole changu juu ya kichwa changu kuonyesha kwamba Mungu Alikuwa Ametuzunguka. Myahudi alijibu kwa kunyosha kidole chake chini kuashiria kwamba Mungu Alikuwepo pale pale tulipokuwa tumekaa. Nilitoa mkate na mvinyo ili kuonyesha kwamba Mungu alitufia na kutufutia dhambi zetu, Myahudi alitoa tofaa kunikumbusha juu ya dhambi zetu wanadamu. Alikuwa na jibu kwa kila swali nililouliza. Sikuwa na kingine cha kufanya
  • Wayahudi nao kwa upande wao walikuwa wamekusanyika kushangilia ushindi wa Moishe. Walitaka sana kufahamu jinsi mfanya usafi yule mzee asiyejua kusoma na kuandika alivyoweza kumshinda Papa katika mdahalo ule. “Sawa nitawaambia” Alianza Moishe huku wasomi na wanafalsafa wa Kiyahudi wakisikiliza kwa makini.
  • Kwanza alinyosha vidole vyake vitatu kunionyesha kwamba Wayahudi walikuwa na siku tatu tu kuuhama mji wa Roma. Mimi nilinyosha kidole kimoja kumwambia kwamba hakuna hata Myahudi mmoja ambaye alikuwa tayari kuondoka. Alinyosha kidole chake na kukizungusha juu ya kichwa chake ili kuniambia kwamba hakuna hata Myahudi mmoja ambaye angebakia katika mji huu. Mimi nilinyosha kidole changu chini ili kumwonyesha kwamba Wayahudi wote tulikuwa tunabakia hapa hapa.”
 “Halafu kukatokea nini?” Aliuliza mwanamke mmoja kwa shauku kubwa
“Sijui” Moishe alisema. “Alitoa mlo wake wa mchana nami nikatoa wa kwangu.”
  • Na kisaasili chetu kinaishia hapa…Umejifunza nini?
******************

Thursday, July 29, 2010

HUYU "MGONJWA" ATAAGA DUNIA LINI TUPUMUE???

HIZI NDIZO FAIDA ZA KUPANDA DALADALA (SEHEMU YA KWANZA)

  • Ninapokuwa Tanzania na hasa Dar mimi hupenda kusafiri kwa daladala (na mara chache sana kwa teksi). Pamoja na ukweli kwamba sina gari, kuendesha Dar ni changamoto kwelikweli. Kuna wakati mmoja niliendesha kutoka Masaki kwenda Posta Mpya na mambo niliyopambana nayo siku ile niliona kwamba pengine ni bora tu kupanda daladala. Mbali na kutukanwa na madereva wengine (hasa wa daladala) na kupigiwa honi mfululizo, shida kubwa ilikuwa ni maegesho mwisho wa safari yangu. Nilizunguka mjini kwa muda mrefu bila kupata sehemu ya kuegesha mpaka jamaa mmoja akajitolea kuniegeshea gari langu (na kulilinda) kwa malipo. Mjini shule ati!
  • Tabia yangu hii ya kupanda daladala hata hivyo kumbe ni kero kwa baadhi ya watu ambao hawaelewi ni kwa nini mtu anayebeba maboksi Marekani kama mimi ashindwe kununua hata ka-Corolla na aishie kupanda daladala. Nimewahi kuambiwa eti nina roho ya kimasikini, mshamba, nimezubaa na majina mengine ya kushangaza. Ambacho hawaelewi waita majina hawa ni kwamba si kila mbeba maboksi wa Marekani anaweza kumudu kununua gari. Marekani dola hazimwagwi barabarani ati! Basi mimi huishia kucheka tu na kujikalia kimya. Maisha!
  • Mbali na kwamba ni usafiri rahisi na unaopunguza msongamano wa magari barabarani (ukiachilia mbali kubanana, mwendo wa kasi na kunukishiana vikwapa) kuna faida nyingi zinazonifanya nipande daladala.
  • Kwanza: Kama mwanaisimu, lugha inayozungumzwa kwenye daladala pengine ndiyo inaakisi kwa ufasaha zaidi mabadiliko yanayotokea katika jamii. Baada ya kukaa nje kwa muda, daladala kwangu ni maabara ya kujifunzia misemo, nahau, misamiati, vijembe na mitindo mipya ya lugha. Kiswahili kinachozungumzwa na makondakta, wapiga debe na abiria kina utajiri wa tamathali za semi na vikolombwezo vingine vinavyoakisi kwa uangavu wa kutosha mabadiliko yanayotokea katika lugha. Na kwa vile lugha haikakawani katika ombwe, mara nyingi mabadiliko katika lugha huakisi pia mabadiliko katika jamii husika kwa usahihi wa kutosha.
  • Pili: Daladala ndiyo sehemu bora kabisa ya kusikilizia hali halisi na matatizo ya wananchi wa kawaida. Ukitaka kujua dukuduku la watu wa tabala la chini (ambao ndiyo wengi), matatizo na hata matumaini yao, basi panda daladala. Katika daladala utavisikia visa vya akina mama wajawazito waliopoteza maisha yao kwa vile tu hawakuwa na pesa za kulipia operesheni za uzazi ambazo pengine zingeokoa maisha yao. Katika daladala utawasikia wananchi wakilalamikia uzembe wa viongozi, rushwa na upendeleo katika ugawaji wa vyandarua vya kuzuia mbu na huduma zingine za jamii. Katika daladala utasikia uchungu, kilio na matumaini ya jamii. Katika daladala utasikia kuzaliwa na kufa kwa penzi changa. Katika daladala……. Badala ya kuitisha mikutano pengine ingekuwa bora kama viongozi wangepanda daladala japo mara mbili kwa mwezi, wakakaa kimya humo na kuwasikiliza waongozwaji wao. Naamini kwamba wangejifunza mengi zaidi kuliko yale wanayojifunza katika mikutano yao ya hadhara iliyojaa wapambe na shamrashamra za kila aina!
  • Tatu:   Katika daladala ndimo pia unaweza kuvipata visa vya kweli vya kusisimua kama hiki nilichokishuhudia laivu katika daladala ya kutoka “uzunguni” Mbagala kwenda Posta Mpya. Tulipofika pale Mtoni Mtongani jamaa mmoja ambaye alikuwa ametinga pamba za kwelikweli alikuwa anashuka. Aliposhuka, konda aliamru mchuma uondoke. Yule jamaa mtanashati aliruka juu na kumwamru konda atulize ngoma. Jamaa alirudi ndani ya daladala na kutangaza kwa sauti kubwa kwamba alikuwa amedondosha HIRIZI yake ya hatari sana na kwamba kama hirizi hiyo isingepatikana basi safari ya daladala ile ingekuwa na mikosi. Basi wasafiri wote kwa juhudi walianza kuhangaika kuangalia huku na huko. Na baada ya muda, mama mmoja aliokota kidude cheusi na kukinyosha juu.

“Ni hii?”
“Ndiyo yenyewe”
  • Alijibu yule jamaa mtanashati kisha akachukua hirizi yake na kwenda zake. Tukio lile lilitawala mazungumzo katika daladala ile mpaka tulipofika mwisho wa safari yetu. Mazungumzo yale, mbali na mambo mengine, yalionyesha jamii ambayo bado imejikita sana katika imani za kishirikina, jamii yenye hofu ya “nguvu za giza" katika karne hii ya sayansi na teke linalokujia!
  • Nitaendelea kuelezea faida zingine katika toleo lijalo. Nawatakia safari njema wapanda daladala wenzangu! 

Wednesday, July 28, 2010

NI KWELI KUNA DAWA ZA KUNENEPESHA MAKALIO YA WANAWAKE (AKA MCHINA) AU NI POROJO TU ZA KIBONGO?

  • Profesa mmoja wa "Medical Anthropology" ambaye hufanya utafiti wake nchini Tanzania aliniomba nimletee sampuli ndogo ya dawa za kunenepesha makalio ya wanawake ambazo alikuwa ametajiwa tu na mwanafunzi mmoja kutoka Tanzania. Aliniambia kwamba anataka kwanza kuzifanyia uchambuzi wa kisayansi ili kufahamu kemikali zilizomo katika dawa hizo (kama kweli zipo!).
  • Mbali na kuandika makala mengi ya kiutafiti kuhusu tiba za jadi katika makabila ya Kusini mwa Tanzania, utafiti wa sasa wa Profesa huyu unajaribu kuangalia athari za utandawazi katika tiba hizi za jadi ambazo zimedumu kwa miaka mingi miongoni mwa Waafrika.
  • Nilipokuwa Tanzania mwezi wa sita mwaka huu nilijaribu sana kuzitafuta dawa hizi lakini sikufanikiwa. Nilikwenda katika maduka ya madawa karibu matano lakini kote niliambiwa kwamba hata wao walikuwa wanazisikia tu. Hata baada ya kujitambulisha na kueleza lengo langu la kuzitafuta dawa hizo, majibu yalikuwa ni yale yale. 
  • Ni kweli dawa hizi za kunenepesha makalio ya wanawake zipo au ni porojo tu za Kibongo? Kama kweli zipo, kuna anayejua kama kuna uchanganuzi wo wote wa kisayansi ambao umekwishafanywa kuhusu kemikali zilizomo katika dawa hizi na madhara yake kwa binadamu? Nitawezaje kupata japo sampuli kidogo tu? Matone au mabonge machache tu yanatosha.
******************************
Angalizo: Hata hapa Marekani, nasikia vuguvugu la mabinti "kujijaziajazia" lipo lakini inasemekana wenyewe wanafanya operesheni kabisa. Binti katika picha hiyo juu ni modo mashuhuri kule jijini New York na inasemekana kuwa amefanyiwa operesheni. Kazi kweli kweli!

RIWAYA MPYA YA MWALIMU NKWAZI MHANGO WA MPAYUKAJI.BLOGSPOT.COM SASA IKO TAYARI

  • Kwa maelekezo zaidi jinsi ya kuipata riwaya hii mpya pamoja na ile ya SAA YA UKOMBOZI wasiliana na Mwalimu Nkwazi Mhango kwa kubofya hapa; au tembelea blogu yake ya mpayukaji.blogspot.com

Tuesday, July 27, 2010

MAJI SAFI NA SALAMA VIJIJINI YATAPATIKANA LINI?


  • Picha hizi nilizipiga mwenyewe nilipokuwa nyumbani Usukumani mwezi wa sita mwaka huu. Hapa ni kijiji cha jirani na wanakijiji hawa huwa wanapata maji yao kutoka katika kisima hiki ambacho pia nadhani hutumiwa na mifugo pia.
  • Ni kweli tumeshindwa kuchimba visima na kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata maji safi na salama? Tutaulaumu umasikini wetu hata katika jambo la msingi kama hili mpaka lini? Nilishawahi kutoa dukuduku langu kuhusu suala hili hapa.

Monday, July 26, 2010

SUALA LA CHETI CHA KUZALIWA KWA OBAMA BADO LINAZIDI KUCHOKONOLEWA NA MAGAZETI YA UDAKU

  • Hili ni gazeti la Globe ambalo lipo mitaani kwa sasa. Sasa linadai kwamba eti lina ushahidi usiopingika kuonyesha kwamba Obama alizaliwa Kenya na kwa hivyo urais wake si halali. Pia unaweza kutazama hapa na hapa kuhusu suala hili. Ni suala hili hili ambalo lilichangia kumfukuzisha kazi Lou Dobbs kutoka CNN. 
  • Nimeandika makala ndefu ya kiuchambuzi juu ya mchango wa magazeti haya ya udaku katika ujenzi wa jamii na hasa kule nyumbani ambako, kama vile kwingineko duniani, ndiyo yanasomwa sana hasa na vijana. Makala hayo nitayatundika hapa Jumatano ijayo pamoja na kuyatuma katika magazeti ya udaku ya nyumbani Tanzania.

TOM & JENNY IN TANZANIA: KITABU CHA VIBONZO VYA KUCHEKESHA

  • Kitabu hiki kimelengwa hasa  kwa watu ambao waliwahi kutembelea Tanzania au wanaotegemea kutembeleaTanzania (Watalii).
KITABU KIPO

Novel Idea Slipway, Seacliff, Shoppers Plaza, Steers, Arusha na Iringa katika maduka ya Green Bookshop, Southen Sun bookshop, Lapette Gelende, Eplodor Mbalamwezi, Scholastic Bookshop, Irish Pub,Trinit Bar & Restaurant.
Simu +255 713 4713 71,

*******************************************

Wednesday, July 21, 2010

KWA MNAOTANGAZA NIA. MMESHALISIKIA HILI?

  • Inasemekana kwamba mbali na kuwa na mamilioni ya kuwahonga wapiga kura, inakubidi sasa uwe na "mtaalamu" bingwa wa kukulinda. Vinginevyo kampeni yako haitafika popote! Na mwenyewe ukizubaa eti unaondoka. Kauli hizi nilizisikia sana kutoka kwa wapiga kura kule Usukumani hivi karibuni. Sijui hali katika sehemu zingine za nchi ikoje!

  • Kuzidi kuimarika kwa imani hizi za kishirikina katika jamii yetu kidogo kunashangaza. Mbona hali inazidi kuwa hivi wakati ambapo tuna shule za msingi kila kijiji, shule za sekondari kila kata, akademi kila "mtaa" na vyuo vikuu lukuki? Lengo la elimu yetu ni nini hasa kama siyo kutukomboa kutoka katika umasikini, ujinga, maladhi na dhuluma kama Baba wa Taifa alivyotuahidi enzi zile? Mbona utandawazi unaonekana kushindwa kuziangamiza imani hizi za kishirikina wakati unaonekana kufanikiwa kuvipiga dafrau vipengele vingine vya utamaduni wetu kama vile lugha zetu za mama, ngoma za kiasili, mavazi na mfumo wetu wa maisha kwa ujumla? Kwa nini ushirikina unazidi kujiimarisha? Tufanye nini?

JENGO KONGWE NA MAARUFU KULIKO YOTE JIJINI MWANZA. WALIJUA?

Monday, July 19, 2010

NI LILE SAMAKI LA MWANZA LINALOTEMA MAJI USIKU NA MCHANA NG'WANAWANE

  • Nami nilifika na kuliona lile samaki la Mwanza. Mlinzi wa pale siku ile alikuwa mbogo na hakuturuhusu kulisogelea. Alituambia kama tulitaka kulisogelea basi ilibidi twende makao makuu ya Manispaa kuomba kibali. Bagosha!

HII NI MOJAWAPO YA AJALI MBAYA KABISA "KAZINI" (SEKUNDE 15)

  • Angalizo: Ni ajali mbaya. Jihadhari !!! 
Au hapa....

video
....na hapa.

Saturday, July 17, 2010

ILI KUONDOA MIKANGANYIKO, WAKATI MWINGINE NI BORA "KUJITAMBULISHA"

  • Juzi nikiwa katika duka la Walgreens, nilikutana na jamaa ambaye naamini kabisa alikuwa ni mwanaume japo alikuwa amevaa gauni safi na kujipodoa sawasawa. 
  • Nikiwa naangalia mashine ya kunyolea ndevu, huyu "jamaa" alinisogelea na kuanza kuniambia kwamba alikuwa amevutiwa na shati langu (kikoi cheupe chenye ramani ya Afrika ikiwa imepambwa na wanyama mbalimbali). Alitaka kujua ni wapi angeweza kupata shati kama hili. 
  • Japo sina tatizo na watu kujibadilisha jinsia zao, unapokutana na mtu aliyefanya hivyo kwa njia ya operesheni na/au matumizi ya homoni kidogo unaweza kushangaa. Pamoja na kwamba huyu jamaa alikuwa "mwanamke mzuri" kwa umbo, bado unaweza kuiona asili yake ya kiume katika sauti, sura na hata mwonekano wa miguu na mikono yake. Ndiyo maana namfagilia sana huyu jamaa hapo juu kwa kuweka mambo bayana namna hii. Dunia hii we acha tu!
    *******************
    • Kwa habari zaidi kuhusu masuala haya bofya hapa.

    Friday, July 16, 2010

    SWALI: ETI NI KWA NINI BWANA HARUSI HUVAA SUTI NYEUSI SIKU YA HARUSI?


    A little boy at a wedding looks at his mom and says
    "Mommy, why does the bride wear white?"
    His mom replies,
    "The bride is in white because she is happy
    and this is the happiest day of her life."
    The boy thinks about this then says,
    "Well, then why is the groom wearing black?"

    UTAFITI: FACEBOOK INACHOCHEA TALAKA

    • Ni kule Uingereza.
    • Kwa kila talaka tano, moja kati ya hizo imesababishwa na facebook.
    • Wanandoa wanatumia "facebook" kujua kama wapenzi wao wanaikandamiza amri ya saba; na pia kutafuta wapenzi wapya ili kuziba mapengo ya kile kinachokosekana katika ndoa zao.
    • Karibu asilimia 20 ya madai ya talaka yaliyorekodiwa katika tovuti ya Divorce-Online yanataja "facebook"
    • Wewe una maoni gani kuhusu "facebook"? Unaiona kama huduma ya hatari au tovuti ya muhimu kwa vile imekufanya ukutane na marafiki zako wa zamani, na wapya? Utandawazi!
    **************
      • Kwa habari zaidi kuhusu mada hii soma hapa.

      Thursday, July 15, 2010

      "VITUKO" VYA MTAA WA MAKOROBOI JIJINI MWANZA (NA KWINGINEKO). KULIKONI ???

      • Niliipiga hii picha tarehe 7/6/2010 pale mtaa wa Makoroboi jijini Mwanza. Kuna maduka mazuri sana ya nguo na vifaa mbalimbali lakini katikati kabisa ya maduka haya ndipo kuna "kituko" hiki. Naona manispaa wameweka tu hili "karandinga" la kukusanyia uchafu halafu wakalitelekeza na kuingia mitini.
      • Tabia hii ya kuanzisha miradi (tena mingine mizuri sana) na halafu kuitelekeza tunayo sana. Utakuta mkandarasi kapewa barabara kisha anajenga kakipenda kadogo tu halafu huyo anatokomea. Na hapo mabilioni ya shilingi za walipa kodi yanakuwa yameshatafunwa. Mifano ya jambo hili ni mengi sana na ni mojawapo ya tabia za kizembe ambazo inabidi tuzipige vita kama kweli tunayo nia ya dhati ya kusonga mbele. Ni kweli manispaa ya jiji la Mwanza haina uwezo wa kuja kuzoa uchafu huu na kuupeleka kunakotakiwa kwa muda uliopangwa kabla haujarundikana namna hii? Au ni uzembe tu na kutojali? Halafu kipindupindu kikifumuka eti tunaanza kulaumiana!
      • Kwingineko nilivutiwa sana na juhudi za usafi zinazofanywa katika jiji la Arusha na hasa katika mji wa Moshi. Huko sasa mtu mpaka unaona aibu kutupa ganda la chungwa hovyohovyo. Tatizo hata hivyo ni kwamba bado kuna upungufu wa mapipa ya kutupia takataka. Pale Arusha inabidi utembee na ganda lako la chungwa kwa muda mrefu kabla hujaona sehemu ambayo unaweza kulihifadhi. Hata hivyo hatua nzuri zimepigwa na kwa mara ya kwanza kuna dalili za kweli kuonyesha kwamba watu wenyewe wameanza kubadilika kiasi kwamba mtu unaona aibu kutupa ganda la chungwa hovyo hovyo. Haya ni mabadiliko chanya na hili ni jambo jema!



        Tovuti ya Manispaa ya Arusha inapatikana hapa.

      Wednesday, July 14, 2010

      WANABLOGU MLIOKO TANZANIA - SASA NAWAHESHIMU ZAIDI!!!

      Umeme ulipotukatikia ghafla. Ni "Internet Cafe" ya Benki ya Posta Mpya jijini Dar.
      • Nimemuona Dada Koero akilalamika kuhusu mtandao kuwa kimeo. Kwa sisi tunaobeba maboksi kwenye hizi nchi za wenyewe, tumezoea na pengine kuchukulia upatikanaji wa mtandao kasi kama jambo la kawaida tu.
      • Nilipokuwa Mwanza, Arusha na Dar es salaam hivi karibuni ndipo niliiona tofauti na jitihada ambazo inabidi tuzipige ili kuifanya huduma hii muhimu ya mtandao iwe ya kuridhisha. Juhudi zangu za kwenda katika migahawa ya mtandao zilikwama baada ya kugundua kwamba nilikuwa napoteza muda mwingi kusubiri kurasa zihuike badala ya kufanya kile kilichokuwa kimenipeleka huko. Mambo yalikuwa mabaya zaidi jijini Arusha.
      • Baadaye niliamua kununua "modemu" ya Sasatel ambayo watengenezaji wake walidai kwamba ilikuwa na uwezo wa kuniunganisha na mtandao kwa kutumia mikonga ya Voda, Zain, Zantel na Tigo. Kwa bahati mbaya sana laptop yangu iligoma kuipokea na kufanya kazi na modemu hii. Ndiyo maana niliamua tu kukaa kimya na kukiacha chakula kitamu na kichungu kidode!
      • Bado pia kuna tatizo la umeme. Picha hiyo juu ni mgahawa wa intaneti pale Posta Mpya jijini Dar es salaam. Na hapa ndiyo tu nilikuwa nimemaliza kulipia shilingi 2,000 kwa saa moja na ghafla umeme ukakatika. Tulijaribu kusubiri weeee lakini wapi; na ilipofika robo saa mimi nikaamua kuondoka. Dada anayefanya kazi pale ni mchungu na jeuri kweli kweli. Niliondoka pale na kumwacha angali akifoka na kulalama kwamba kukatika kwa umeme halikuwa kosa lake na alikuwa hana mpango wa kurudisha pesa za wateja. Kiendacho kwa mganga hakirudi ati!
         
      • Ni wazi kwamba baadhi ya wanablogu wenzetu walioko nyumbani wanablogu katika mazingira magumu na wanafanya jitihada za ziada kuhakikisha kwamba blogu zao zinasonga mbele. Kama Mwalimu, mimi huwa sipendi kusoma makala au ingizo katika blogu ambalo limeripuliwa tu huku limejaa makosa ya kiuandishi huku likiungwa mkono na mantiki na mtiririko ulioparaganyika. Kuanzia sasa sitakasirika tena kwani ni wazi kwamba inawezekana wanablogu hawa huwa wanaandika makala yao wakiwa katika mazingira haya ya mtandao wa kubahatisha. Baada ya kuona mtandao ule wenye kasi ya kobe kiasi kwamba "kupandisha" picha moja tu ya kawaida kunaweza kuchukua zaidi ya robo saa - wanablogu wenzetu mnastahili pongezi kwa uvumilivu na kujitolea kwenu kublogu.Msikate tamaa na tunatumaini kwamba baada ya huo mkonga wa Taifa kukamilika sawasawa pengine hali ya mtandao nchini itabadilika
        *********************
        Kuhusu Changamoto na Tija za Mikahawa ya Mtandao jijini Dar es salaam, jaribu kusoma hii Tasnifu ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Eindhoven nchini Uholanzi.

      Tuesday, July 13, 2010

      NI KWELI HATA KWA JIHAD???

      • Ni katika maandamano ya kudai mahakama ya kadhi hivi karibuni. Binafsi nina wasiwasi sana na haya maneno ya mwisho katika hili bango!

      MBINGU NA JEHANAMU - TAFSIRI MPYA (UCHESHI)

      Monday, July 12, 2010

      NIMERUDI: SAFARI YANGU YA NYUMBANI, HARAKATI ZA UCHAGUZI, MSIBA, NG’WANAMBITI NA MENGINEYO

      • Kwa muda wa karibu mwezi mzima sasa blogu hii imekuwa katika mwendo wa kusuasua. Sababu kubwa ni kwamba kuanzia tarehe 25/5/2010 – 27/6/2010 nilikuwa nyumbani Tanzania kwa likizo (ya kikazi).
      • Nilikwenda kijijini ili kumwona mama. Kama ambavyo nimeshawahi kusema hapa, mwanamke huyu shujaa ndiye alinilea na kunisomesha tena kwa jembe la mkono na nikiwa kama mtoto wa mwisho, uhusiano wangu naye ni wa kipekee sana.
      • Nilikuwa na miaka zaidi ya mitatu hivi bila kuonana naye na nilikuwa na wasiwasi kwamba pengine nitamkuta akiwa amezeeka sana. Nilishangaa kumkuta akiwa bado ngangari na akiendelea kuchapa kazi zake za kawaida bila wasiwasi. Kizazi hiki tangulizi kwa hakika kilikuwa na nguvu na afya ya ajabu na sina uhakika kama sisi (na hiki kizazi cha dot.com) kama tutaweza kufikisha miaka zaidi ya 80 huku bado tukiwa na nguvu za kutafuta kuni, kuchota maji na kuvuna mpunga!
      • Nilifika nyumbani salama na kazi ya kula kuku (na mbuzi) wa kienyeji ikaanza. Niliweza pia kuchunga ng’ombe na kuchimbua karanga. Familia nzima ilikuwa na furaha sana na nilikuwa na wakati mzuri wa kukaa faragha na mama na kuongea naye vizuri.
      • Bariadi huwa inachanganya sana wakati wa uchaguzi na tayari harakati za uchaguzi zilikuwa zimeshaanza. Niliweza kuongea na wazee kijijini juu ya maoni yao kuhusu uchaguzi huo na hasa tathmini yao juu ya utendakazi na uchapakazi wa wabunge wao wawili – Waheshimiwa John Momose Cheyo wa chama cha UDP na John Andrew Chenge wa CCM. Kuna makala mbili ambazo nimeziandika juu ya suala hili na nitazibandika hapa (na kuzichapisha magazetini) katika kipindi cha wiki mbili hivi zijazo. Watanzania inabidi tuuendeleze na kujivunia utamaduni huu mzuri wa kuchagua viongozi kwa amani kila baada ya miaka mitano.
      • Nilikwenda Dar es salaam ambako nilikaa kwa siku tatu hivi na halafu nikaelekea Arusha mjini ambako nilifanya kazi (na kupumzika) katika kahoteli haka kapya kabisa. Baadaye nilihamia Usa River kwenye chuo cha MS-TCDC ili kuangalia jinsi wanafunzi wa Kimarekani wanavyojifunza Kiswahili wakiwa katika mazingira na utamaduni wa Waswahili wenyewe.
      MSIBA
      • Mpwa wangu ambaye alikuwa ndiye mkuu na mwangalizi wa masuala yote pale nyumbani aliugua ghafla wakati nikiwa Usa River. Alipelekwa hospitalini ambako madaktari walijaribu sana kujua kilichokuwa kinamsumbua bila mafanikio. Vipimo vyote – kuanzia Malaria mpaka kichaa cha mbwa – vilirudi vikiwa hasi. Mambo yalipowazidia, na kutokana na uzoefu wao, madaktari walishauri mgonjwa apelekwe kwa madaktari wa kienyeji kwani walikuwa wanaamini kwamba ugonjwa wake haukuwa wa kawaida.
      • Kijana alirudishwa nyumbani siku iliyofuata na alipata nafuu ya ghafla, akala chakula vizuri na kuongea mpaka tukapata matumaini kwamba atapona. Usiku huo hata hivyo alizidiwa sana na kesho yake asubuhi roho yake ikauacha mwili.
      • Kifo hiki kilinishtua na kunisikitisha sana kwani kijana huyu, mbali na kuwa binamu yangu, pia alikuwa rafiki yangu sana! Kuanzia hapo ratiba yangu ilivurugika kabisa. Hata juhudi nilizokuwa nazifanya ili kukutana na binti wa Mkundi (a.k.a Mchungaji) zilikwama. Sijaguswa wala kuhuzunishwa na kifo kama nilivyoguswa na kuhuzunishwa na kifo tatanishi na cha ghafla cha huyu mpwa wangu mpendwa!
      Picha hizi nilizipiga mwenyewe. Hapa Marehemu akiwa na mabinti 
      zake. Sikujua kama picha hizi ndizo zingekuwa za mwisho!
       
      NG’WANAMBITI
      • Jioni ya siku hiyo hiyo ya msiba, wakati nikipanga vitu vyangu tayari kwa safari kesho yake, mlango wa nyumba niliyokuwa nikikaa uligongwa. Nilipouliza mgeni wangu alikuwa nani, nilipigwa na butwaa nilipoisikia sauti kakamavu ya Kikurya ikijibu “Ng’wanambiti”.
      • Mwanaharakati huyu alikuwa amesafiri zaidi ya nusu saa kutoka Arusha mjini tena usiku kuja Usa River kunitafuta baada ya siku nzima mkutanoni. Lilikuwa farijiko la ajabu lililofika kwa wakati hasa uliotakiwa.
      • Tulikwenda mesini tukapata chakula cha jioni na kuongea mambo mengi ya muhimu juu ya mambo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu. Nilipata pia bahati ya kuongea na Mama Ng’wanambiti na nilifurahi kugundua kwamba kumbe Ng’wanambiti mwenyewe ni shemeji yangu!
      • Niliongea pia na Mwanautambuzi makini Shabani Kaluse na mbali na kunipa pole ya msiba, tulipanga tukutane Dar es salaam pamoja na Mwanamalenga Fadhy Mtanga ambaye aliniandikia ujumbe mrefu wa kunipa pole. Dada Yasinta naye pia aliniandikia ujumbe mzuri wa kiroho ili kunipoza na kifo hicho. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuruni nyote – Ng’wanambiti, Kaluse, Yasinta na Fadhy.  Ninyi ni ndugu na wema wenu katika kipindi kile kigumu sitausahau. Asanteni sana!
      • Nilipofika Dar es salaam ilinilazimu nipande ndege kukimbia Mwanza kwani mambo yalikuwa hayajatulia na nilikuwa na wasiwasi sana na hali ya mama kwani sikujua jinsi ambavyo angeweza kuukabili msiba wa kuondokewa na mjukuu wake aliyempenda sana! Kutokana na misukosuko hii, nilipoteza ile nafasi ya kuweza kuonana na Kaluse na Mtanga. 
      • Pamoja na misukosuko hii, maisha ni lazima yaendelee na kuanzia sasa blogu hii itarudi katika hali yake ya kawaida. Pia nitaanza rasmi sasa kutembelea vijiwe mbalimbali na kushiriki katika mijadala mbalimbali.
      Asanteni sana na Mungu Aendelee kutubariki !!!

      ********************* 
      • Nilifurahi sana niliporudi na kuvikuta vibinti vyangu virembo vyema vikinisubiri kwa hamu. Furaha iliyoje!!!




      JIANDIKISHE HAPA

      Enter your email address:

      Delivered by FeedBurner

      BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO