NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, September 30, 2010

PROFESA AFUKUZWA KAZI KWA KUTOA KAULI YA "KUDHALILISHA" WANAWAKE WA KILATINO

Picha ni kutoka Grinning Planet
  • Profesa mmoja wa Sayansi katika Chuo Kikuu cha Florida amefukuzwa kazi baada ya kutoa kauli darasani kwamba eti wanawake wa Kilatino huvaa nguo zenye kutamanisha zaidi kuliko wanawake wa Kimarekani. 
  • Profesa huyo pia anadaiwa kuwa na tabia ya "kuwakazia macho" wanafunzi wa kike kwa jicho ambalo huwanyima raha na huko nyuma alishawahi kuonywa mara mbili kuhusu mahusiano yake yasiyorishisha na wanafunzi wa kike ikiwemo kugusa nywele zao na kumlazimisha mwanafunzi wa kike kucheza muziki darasani baada ya simu yake ya mkononi kuita/kulia. 
  • Profesa huyu amepinga kufukuzwa kwake na amekata rufaa akidai kwamba maprofesa inabidi wawe na uhuru kamili wa kujadili masuala mbalimbali darasani bila kuogopa kuchukuliwa hatua.
  • Wanafunzi hapa Marekani ni "wafalme" na kashfa ndogo tu - hata iwe ya kusingiziwa inaweza kumletea mwalimu matatizo makubwa. Hapa inabidi kuwa mwangalifu sana na hasa kwa sisi wageni (weusi) kwani tofauti za kitamaduni tu zinatosha kukuletea kasheshe mpaka ukashangaa. Inabidi "kubeba maboksi" kwa uangalifu kweli kweli!!!
  • Habari kuhusu mkasa huu zinapatikana hapa na hapa.

UNDERCOVER BOSS SHOW: NIMEJIFUNZA KITU KUHUSU UBINADAMU, UCHAPAKAZI NA KUYACHUKULIA MAISHA KAMA YALIVYO

  • Undercover Boss ni kipindi cha runinga ambapo mabosi wa makampuni mbalimbali hujifanya kuwa wafanyakazi wa kawaida na kutembelea vitengo mbalimbali vya makapuni yao na kushiriki katika kazi zinazofanywa na wafanyakazi wa kawaida.
  • Katika toleo la kwanza la kipindi hiki hapa Marekani, rais wa Waste Management - kampuni kubwa la kuzoa takataka lenye thamani ya dola bilioni 13 na wafanyakazi wapatao 45,000 alikuwa anatembelea wafanyakazi wa kawaida wa kampuni hilo huku akijifanya kuwa kama mfanyakazi wa kawaida.
  • Kilichonivutia ni pale rais huyu alipomtembelea mfanyakazi mmoja aitwaye Fred ambaye kazi yake kubwa ni kubeba kinyesi kutoka katika vyoo vya muda (vinavyohamishika) katika matamasha mbalimbali.
  • Mbali na ukweli kwamba kazi hii ni ya kutia kinyaa, Fred alikuwa akiifanya kwa uchangamfu na ucheshi wa kutosha na bila malalamiko yo yote. Jambo hili lilimvutia sana rais wa kampuni kiasi kwamba baadaye alipojitambulisha na kuitisha mkutano wa wafanyakazi wote, alimsifia sana Fred kiasi cha kumuomba atoe hotuba kwa viongozi wote wa juu wa kampuni kuhusu motisha, uchapakazi na jinsi anavyoweza kuifurahia kazi yake hiyo yenye kutia kinyaa .
  • Kama wewe umeajiriwa, bosi wako wa ngazi ya juu kabisa ataondoka na picha gani kama siku moja ataamua kwenda "undercover" na kukutembelea katika kituo chako cha kazi? Kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa Fred !!!
  • Tazama hapa kwa habari zaidi, na ufupisho wa onyesho zima katika video hapa chini. 

Wednesday, September 29, 2010

MBUNGE WANGU (MZEE WA VIJISENTI) MAMBO "POA": MAHAKAMA YAFUTA HATI YA KUMKAMATA.


Mahakama yafuta hati ya kumkamata Chenge
29 Sep 2010, 7:08 am
Ummy Muya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Kinondoni imefuta hati yake ya kuruhusu kukamatwa kwa mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge iliyotolewa juzi kutokana na mshtakiwa huyo kushindwa kutokea mahakamani.

Hakimu Sundi Fimbo alitoa hati hiyo juzi wakati Chenge, ambaye anatetea kiti chake cha ubunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki akiwa kwenye mkutano wa kampeni ambako alipigiwa debe na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa yuko mikoa ya Kanda ya Ziwa.
   
Lakini mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, David Mwafwimbo aliiambia Mwananchi jana kuwa mdhamini wa Chenge aliibuka juzi akiwa amechelewa na akamuomba hakimu afute hati hiyo na ombi lake likakubaliwa.

"Mdhamini wake anayeitwa Masanja alimrudisha Hakimu Fimbo mahakamani ili kuomba kufutwa kwa kibali cha kumkamata mshtakiwa... ingawa mdhamini huyo alifika mahakamani hapo akiwa amechelewa, alienda kumuomba hakimu afute  hati hiyo na akakubaliwa" alisema Mwafwimbo.

Mwafwimbo alisema baada ya mdhamini huyo kufika, hakimu aliitisha tena jalada hilo na kuifuta amri hiyo ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Chenge alitakiwa kuanza kujitetea jana katika kesi inayomkabili ya kuendesha gari kizembe na kufanya makosa mawili ya kusababisha vifo vya watu wawili na jingine la kuendesha gari bila bima halali.

Chenge anadaiwa kugonga pikipiki ya maguruduma matatu, maarufu kama Bajaj iliyowabeba wasichana wawili na kusababisha vifo vyao ambavyo kisheria huchukuliwa kama makosa mawili tofauti.

Kutokuwepo kwake kulimfanya Hakimu Fimbo kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5. Lakini Zulfa Mfinanga na Herman Meza wanaripoti kutoka Shinyanga kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo lilikuwa halijapokea hati ya kumkamata.

Afisa upelelezi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Adam Nyakipande alikiri kusikia habari hiyo, lakini akasema walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakupata kibali cha mahakama hiyo.

"Ninachoweza kusema ni kwamba sisi tunasubiri hati ya kumtia nguvuni... kwa ufupi bado hatujapewa kibali cha kumkamata lakini tukipata tutalifanyia kazi," alisema.

Chanzo: Mwananchi (via Dada Subi)

UTAFITI: KATI YA MASHOGA WATANO MMOJA ANA UKIMWI !!!

Picha ni kutoka GLN.
  • Utafiti mpya unaonyesha kwamba kati ya mashoga watano hapa Marekani, mmoja tayari ameshaambukizwa UKIMWI; na wengi wao (asilimia 44)  hawajui kama tayari wameshaambukizwa. 
  • Wamarekani chini ya asilimia moja wana UKIMWI lakini mashoga wanaendelea kuambukizwa kwa kasi kubwa zaidi kuliko watu wengine. Ni kwa sababu hii serikali ya Marekani imeamua kuelekeza nguvu zake za kupambana na UKIMWI hasa kwa mashoga. Maelekezo mapya yanawataka mashoga wote kupima UKIMWI angalau mara moja kwa mwaka. 
  • Mashoga weusi ndiyo wanaongoza kwa kuambikizwa (au tuseme kuambukizana) UKIMWI (asilimia 28), wakifuatiwa na mashoga wa Kilatino (asilimia 18) na mashoga wa kizungu (asilimia 16). 
  • Mashoga weusi pia ndiyo wenye uwezekano mkubwa zaidi wa kutojua kama wameambukizwa  ama la (asilimia 60) ikilinganishwa na asilimia (46) kwa mashoga wa Kilatino na asilimia (26) kwa mashoga wa kizungu.
  • Kama utafiti huu ungefanyika Tanzania, hali ingekuwaje kwa mashoga wetu? Jamani mashoga na wapenda "tigo", kuweni macho! Kwa habari kamili kuhusu utafiti huu bofya hapa.

Tuesday, September 28, 2010

MBUNGE WANGU (MZEE WA VIJISENTI) MATATANI - MAHAKAMA YATOA AMRI AKAMATWE MARA MOJA !

  • Wakati akiwa katika kampeni za ubunge na Mwenyekiti wa chama chake, kesi ya Mheshimiwa Andrew Chenge iliendelea kuunguruma katika Mahakama ya Kinondoni bila ya yeye kuwepo wala wakili wake.
  • Kutokana na utoro huu, hakimu Fimbo aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo aliamru Mh. Chenge akamatwe mara moja 
  • “Haijalishi kuwa mshitakiwa yuko kwenye kampeni au wapi, Mahakama haitambui jambo lolote kuhusu kampeni, hivyo kwa kuwa hajahudhuria mahali hapa, inabidi akamatwe kwa kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama,” alisema Hakimu Fimbo.
  • Ni kweli amri ya mahakama itatekelezwa na mheshimiwa huyu kukamatwa? Ni lazima pia "tujivunie" demokrasia YETU WENYEWE tunayoiendesha kwani katika nchi zingine ni nadra sana kukuta wagombea ambao wana kesi kubwa mahakamani wakiendelea kugombea nafasi kubwa za kisiasa - na wakategemewa kushinda!

CHACHACHA, TAI NA SHATI LISILOCHOMEKEWA WAPI NA WAPI? MAISHA YA KUMBUKONI.

  • Kwa mliokuwepo, mnazikumbuka chachacha? Kweli jamani tumetoka mbali na picha hii inanikumbusha mambo mengi sana. Hapa ni kidato cha nne, Shule ya Sekondari ya Kahororo Bukoba kwa watani zangu wenye matatizo sana na herufi h-. Ukitaka kuona "homework" yangu ya Fizikia ya kidato cha nne gonga hapa.
  • Miaka nayo inakimbia wanguwangu na siamini kama tayari ni zaidi ya miaka 20 tangu picha hii ipigwe. Maisha!
  • Angalizo:  Methali yangu niipendayo sana niliyojifunza huko Bukoba ni hii: Ebigambo bingi bikatanga enkoko okwikukusa!!!  Methali hii imegeuka kuwa falsafa (mojawapo) ya muhimu sana katika maisha yangu.

    Sunday, September 26, 2010

    UTAFITI: KAMA VILE UKIMWI NA EBOLA, KUMBE HATA MALARIA NAYO ILIANZIA AFRIKA !!!

    • Inavyoonekana bara la Afrika ndilo chanzo cha magonjwa mengi hatari ya kuambukiza. Baada ya "kuthibitishwa" na wanasayansi kwamba magonjwa kama vile Ebola na UKIMWI yalianzia Afrika, utafiti mpya uliochapishwa katika toleo la mwezi huu la jarida la Nature unaonyesha kwamba hata ugonjwa wa Malaria ulianzia katika nyani aina ya Western Gorillas wanaopatikana hasa nchini Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na katika misitu ya Kongo. 
    • Unaweza kuusoma utafiti huu kwa kifupi hapa, au ufupisho wake katika jarida la sasa la Nature.  
    • Kwa nini Afrika ndiyo kiwe chanzo cha magonjwa yote haya? Ni bahati mbaya au? Sina nia mbaya bali najiwazia tu!

    Friday, September 24, 2010

    SWALI PEKEE SI KUNYONGA BALI KUNYONGAJE?

    • Jumatano tarehe 15, 2010 Mzee wa Changamoto alitundika tundiko lenye kichwa kisemacho "Swali pekee si NAWEZA, bali pia NAWEZAJE?" Swali hili lilitokana na mjadala mzuri kati yake na Anony. mmoja kuhusu nafasi ya mjasiriamali mmoja mashuhuri kutoka Tanzania. 
    • Katika mantiki hii hii pengine pia swali pekee siyo KUNYONGA bali KUNYONGAJE. Jana Alhamisi usiku kule katika jimbo la Virginia hapa Marekani mwanamke mmoja mwenye matatizo ya akili aitwaye Teresa Lewis alinyongwa kwa njia ya sindano za sumu. 

    • Kwa Wamarekani njia hii ya kunyonga kwa kutumia sumu inaonekana kuwa ya "kistaarabu" zaidi kuliko ile ya kupiga mawe kama ya Wairan. Ndiyo maana Marekani ilikuwa na bado ipo mstari wa mbele sana kupinga mauaji ya mwanamke wa Iran aliyehukumiwa kunyongwa kwa kupigwa mawe kwa kosa la uzinzi na kumuua mume wake. 
    •  Juzi rais wa Iran ambaye alikuwa New York kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliligusia jambo hili na kuhoji iweje hukumu ya mwanamke wa Iran izue zogo dunia nzima wakati Wamarekani wananyonga mwanamke mwenye matatizo ya akili na dunia yote iko kimya? Mtazame Fareed Zakaria hapa akijaribu kuitetea Marekani.
    • Pia inashangaza kidogo kuona kwamba Marekani hiyo hiyo inayopigania "ustaarabu" ilimwachia Saddam Hussein akanyongwa kwa njia ambayo si ya "kistaarabu" kabisa.

      FIKRA YA IJUMAA: NAMFAGILIA MZEE ANTHONY MATONYA !!!

      • Watu wengine hupenda kusifia watu mashuhuri – wanasiasa wenye majina, madikteta wa kutisha, wanafasihi waliobobea, mashujaa wa kupigiwa mfano, wafalme waliotukuka, wanautambuzi makini, vigogo wa ufisadi, wastareheshaji makini, makamanda wa vita wasioshindika, waanzilishi wa fikra mpya, wanaharakati waliokaramka, wanazuoni washika kurunzi, matajiri wa kutupwa, warembo kupindukia na wengineo wa aina hiyo.
      • Mimi leo nataka kumtukuza Mzee Anthony Matonya – ombaomba mashuhuri nchini Tanzania. Mzee huyu kipofu anajulikana kwa staili yake ya kuomba kwa kulala chali kando ya barabara na kuinua kopo lake juu – bila kujali ukali wa jua la Dar es salaam.
      • Serikali imeshajaribu sana kumwondoa mjini pamoja na ombaomba wengine (ikidai kwamba eti wanatia aibu na kuchafua mazingira), lakini baada ya muda mfupi, mzee huyu kipofu huchomoza tena jijini Dar es salaam tena kwa staili yake ile ile.
      • Ati, ni azma gani na kutokata tamaa kupi kunakozidi huku kwa Mzee Matonya? Ni bidii gani ya kazi inayozidi hii ya Mzee Matonya ya kulala chali siku nzima katika jua kali la Dar es salaam huku ukibezwa na kughasiwa? 
       Hapa akiwa Morogoro. Picha ni kutoka Dullonetwork.
      • Kwa hakika tuna mengi ya kujifunza kuhusu uchapakazi, uvumilivu na kutokata tamaa kutoka kwa mzee huyu kipofu ombaomba. Na hii kwa kifupi ndiyo fikra ya Ijumaa ya wiki hii. Wikiendi njema na mbakie salama!

      Thursday, September 23, 2010

      NI KWELI KWAMBA WATU WA VIJIJINI NI WAJINGA WASIOTAKA KUELEWA UKWELI?

       Picha ni kutoka kwa Mpayukaji
      ******************
      Katika mada yangu ya Siasa za Maji Taka, Anony wa September 21, 2010 4:57 AM alitoa maoni yafuatayo:

      ***********************
      Ni kudanganyana kwa kwenda mbele. Tatizo la wananachi hasa walioko wilayani na vijijini ni wajinga wasiotaka kuelewa ukweli. Anakuja mgombea anaahidi MAISHA BORA kwa kasi mpya na nguvu mpya! Baada ya Miaka 5 anarudi na kuwapa ahadi nyingine lukuki tena za anasa kama viwanja vya ndege vya kimataifa na hosipitali za rufaa, mishahara minono kwa wafanyakazi wote. Watu wote lukuki walioenda kumsikiliza (hawazuiwi kwenda) wanasima na kupiga makofi na kusema na kuimba nambari waniiiiiiiiiix2.

      Ukiwatizama kwenye hizo picha unaona wanaishi katika maisha yaliyokata tamaa, mazingira na sura choka mbaya sasa sijui hayo ndio maisha bora walioahidiwa. Kwanini wasihoji tu hapo kuwa maisha bora yamepelekwa wapi? Watoto wachanga na wajawazito wanapoteza maisha kila siku (Takwimu zisizo sahihi ni kama 20 kwa siku!), Maajali ya kila siku yanaongezeka barabarani na lawama zinapelekwa kwa madereva, ndio madereva wanamakosa, sasa wanafanywa nini ili kuwarekebisha? Au ndio kama mwendo wa kuomba kura (kula?) wakati wa uchaguzi. Elimu i nazidi shuka chini, watoto kibao wanafeli kidato cha nne (chukulia asilimia 20, ndio wanafaulu). Kilimo kinazidi kurudi nyuma ihali wachache wanakuwa makabaila(kwa kujilimbikizia mashamba) na kudai eti kilimo kwanza? Ukienda pale Meatu au Mpanda au Lushoto ukamwuliza mkulima maana ya kilimo kwanza hajui! DUH huu ni upumbavu mkubwa sana! Samahani.
        
      **********************
      • SWALI: Japo pengine kuna ukweli fulani katika maoni ya huyu anony, swali ninalotaka kuuliza hapa ni hili: Ni kweli watu wa Wilayani na vijijini ni wajinga wasiotaka kuelewa ukweli? 
      • Pengine inabidi tujiulize: Ni kwa nini walimpokea Mheshimiwa Chenge kwa mapokezi makubwa yasiyowahi kutokea katika wilaya ya Bariadi baada ya ile kashfa yake ya vijisenti? Naamini pia kwamba Mheshimiwa Chenge (ambaye ni mbunge wangu) atashinda tena kwa kishindo katika uchaguzi huu. Atashinda kwa sababu eti wapiga kura wake ambao wengi ni watu wa kijijini ni wajinga wasiotaka kuelewa mambo?
      • Tukiweza kutambua ni kwa nini hasa watu hawa wa kijijini na wilayani bado wanachagua viongozi wao wapendwa ambao katika macho yetu sisi "wenye uelewa" wana madoa ya ufisadi na kashfa zingine tutakuwa tumepiga hatua katika kuelewa aina ya demokrasia tunayoiendesha. 

      Tuesday, September 21, 2010

      Monday, September 20, 2010

      SIASA ZA MAJI TAKA: NI DALILI YA KUKUA KWA DEMOKRASIA NCHINI MWETU?

      Katuni ni kutoka kwa Fede
       ****    *****  ****
      Uchaguzi huu unaonekana kuwa tofauti na chaguzi zilizotangulia.
      • Kwanza: Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia majina makubwa katika medani ya siasa za Tanzania yakianguka katika kura za maoni. Hili ni jambo jema!
      • Pili: Kwa mara ya kwanza kuna mgombea wa uraisi wa upinzani ambaye kidogo ni tofauti na wagombea wote waliotangulia. Huyu wa sasa ni msomi aliyebobea, bingwa wa kujenga hoja, mwenye bashasha; na mwenye rekodi nzuri sana ya kutetea maslahi ya wanyonge bungeni.
      • Tatu: Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia "kashfa" mbalimbali za wagombea na watu wengine wenye majina makubwa zikiibuliwa. Wapo wanaotuhumiwa kuyakimbia maisha ya utawa na kuanza kupora wake za watu. Wapo wanaotuhumiwa kubaka na kutia mimba wanafunzi wakati wakiwa bado walimu. Wapo wanaotuhumiwa kuwa na nyumba ndogo za siri n.k.
      • Siasa hizi za ki- Argumentum Ad Hominem ni jambo la kawaida katika nchi zilizoendelea hususan hapa Marekani. Hapa mtu huwezi kukurupuka tu leo na kusema kwamba unagombea cheo cho chote kwani watu watachimbua maisha yako tangu ulipozaliwa. Kwa mfano, katika kura za maoni za kuchagua mgombea wa useneta wa jimbo la Florida kupitia chama cha Democrat, mgombea mmoja mashuhuri aliangushwa baada ya kudaiwa kwamba boti yake ya bei mbaya iliwahi kwenda Cuba kinyume cha sheria huku ikiwa na wanawake watingishaji (strippers). Ilidaiwa pia kwamba Mike Tyson, mwanamasumbwi tishio wa zamani ambaye hana sifa nzuri hapa Marekani alikuwemo katika msafara ule.
      • Japo mgombea huyu alijitetea sana kwamba boti yake ilibidi iende Cuba baada ya kupata matatizo ya kiufundi; na kwamba yeye mwenyewe hakuwamo katika msafara ule (japo baadaye alikiri kuwamo) na kwamba hakukuwa na wanawake watingishaji wala Mike Tyson, tayari hii ilitosha kuwapa wasiwasi wapiga kura na aliangushwa.
      • Hivi sasa mgombea wa Useneta kule jimbo la Delaware kupitia chama cha Republican ambaye tu ndiyo amechaguliwa naye moto umemwakia baada ya video yake moja ya zamani wakati akiwa shule ya Sekondari kuanza kuzunguka mtandaoni. Katika video hiyo anaonekana akisema kwamba alishawahi kujaribu mambo ya uchawi japo hakupata kubobea sawasawa.
      • Je, kwa vile nasi tumeshaingia katika siasa hizi za maji taka badala ya kumakinikia sera, hii ni dalili kwamba demokrasia yetu inakua? Je, hili ni jambo jema?
      *******************
      Angalizo: Hii iikuwa ni Fikra ya Ijumaa ya wiki jana lakini kwa bahati mbaya nilikosea "nikaitegesha" katika siku na tarehe ndiyo-siyo. Kunradhi!

      Sunday, September 19, 2010

      KIBAKA AKIONA CHA MOTO, ABANIKWA KAMA NDAFU!

      • Hiki ni kichwa cha habari kuelezea tukio lililotokea Septemba 15, 2010 kule Singida ambapo kibaka mmoja aliuawa na wananchi wenye hasira na kisha kuchomwa moto. 
      • Ni kweli kwamba wananchi wameshachoshwa na vibaka lakini (kama nilivyowahi kusema hapa) siungi mkono unyama huu unaotokea katika jamii yetu inayojidai kuwa ya kidemokrasia na yenye amani, usawa, upendo huku ikiwa na vyombo vya dola vinavyopaswa kusimamia usalama wa raia na mali zao. 
      • Polisi na mahakama vina kazi gani basi kama watu wanajichukulia maamuzi wenyewe kiasi cha kutoa maisha ya watuhumiwa kwa ukatili namna hii?
      • Mimi pia siwapendi vibaka kwani walishawahi kunikwapulia laptop yangu mpya kabisa pale Kariakoo lakini kamwe sipendi unyama huu. Hali hii inasikitisha na kama jamii inabidi tufike mahali tutafute suluhisho mwafaka kwa tatizo hili. Vibaka hawa ni zao la mfumo mbovu wa elimu, matabaka na umasikini uliokithiri katika jamii yetu.
      • Kupambana na umasikini na kujitahidi kuboresha maisha ya Watanzania wote, kutokomeza ufisadi na rushwa, kupunguza matabaka na kuboresha mfumo wetu wa elimu ni baadhi ya hatua za msingi tunazobidi kuzichukua kama kweli tunataka kupunguza hii chuki ya ajabu inayotufanya tuwaue vijana wetu kwa makosa ya kukwapua simu, heleni, saa na vitu vingine vidogo vidogo. 
      • Pengine nimalizie kwa kuuliza swali lililowahi kugusiwa na Euphrase Kezilahabi katika diwani yake ya Karibu Ndani: Tukichomana moto sisi kwa sisi, safari ni lazima iendelee???
      • Kwa habari kamili kuhusu tukio hili tembelea blogu ya Full Shangwe.

      Thursday, September 16, 2010

      SIDANGANYIKI !!!

      • Nilipokuwa nyumbani mwezi wa sita 2010, nilivutiwa sana na tangazo hili lililokuwa likionekana mara kwa mara katika runinga. Umasikini, kufuata mkumbo (peer pressure) na tamaa ndivyo vinawaponza matineja wengi.

      • Hongereni sana TAMWA kwa tangazo hili la kuelimisha. Mafataki bila shaka matumbo moto! Kwa nini mhangaike na watoto wadogo wa shule na kuwaharibia maisha yao bure wakati dunia imejaa wanawake wa kila aina?

      Wednesday, September 15, 2010

      MAISHA YA KIJIJINI, AMRI ZISIZOTEKELEZEKA NA "UPOFU" WA WATUNGA SERA

      • Sijali kama eneo hili ni hifadhi inayolindwa. Sijali kama ni shamba la mtu binafsi. Sijali kama....Kama eneo hili lipo maeneo ya kijijini amri hii itavunjwa na watu watalivamia na kuanza kukata kuni.
      • Ati, kama hujawapatia nishati mbadala, na tayari walishakata karibu miti yote (mf. kule Shinyanga) unategemea watapikia nini au unataka wale vyakula vibichi? Watu wa vijijini (ambao ndiyo wengi) ni kama vile wamesahaulika, na halafu wewe mtunga sera na watekelezaji wako mnakurupuka na kwenda kubandika tangazo kama hili bila kujali na kuangalia mahitaji halisi ya watu wanaoishi pale. 
      • Swali: Amri hii ikivunjwa, tumchukulie nani hatua? Ni hao akina mama hapo juu ambao hawana njia nyingine ya kupikia vyakula vyao au huyo mkazi wa mjini ambaye ametoa hii amri?
      • Mtazamo na mantinki hii tenge ndivyo husababisha miradi mingi isiyo shirikishi katika jamii - miradi ambayo inapendekezwa na watunga sera waishio "dunia nyingine" bila hata kwenda kuangalia hasa maisha ya walengwa wa miradi hiyo yakoje na kama wakitakacho watunga sera ndicho kinachotakiwa na walengwa. Matokeo yake miradi hii haifiki popote, halafu tunaanza kupiga makelele na kulalamika kwamba walengwa wengi wa miradi hii hawajasoma, hawasaidiki wala kuendelezeka. Kumbe ukiangalia vizuri tatizo hasa ni sisi "tuliosoma" ingawa kusema kweli bado hatujaelimika!
      Picha ya pili na ya tatu ni kutoka kwa Mjengwa. Ya kwanza sikumbuki niliipata wapi.

      Tuesday, September 14, 2010

      VIJANA - WAKATI WENU NDIYO HUU !!!

      • Vijana - hatimaye wakati wenu wa kuleta mabadiliko ya kweli na ya msingi katika jamii umefika. Bila kujali vyama vyenu, tunawaomba sana mkatangulize maslahi ya taifa na wale mnaowawakilisha mbele.
      • Nendeni mkawapiganie wananchi masikini na hasa wale wa vijijini (ambao ndiyo wengi) na kuhakikisha kwamba angalau nao wanaanza sasa kuonja utamu wa keki ya taifa.
      • Nendeni mkapambane na mfumo! Bila shaka mnazo mbinu mpya makini na kombozi za kuweza kuleta mabadiliko ya kweli ya kimfumo, na nashawishika kuamini kwamba hii ndiyo sababu mama iliyowafanya mgombee. Blogu hii inawatakia kila la heri!!!

      Saturday, September 11, 2010

      ETI KIINGILIO NI SH. LAKI MOJA! KWENDA KUANGALIA WASICHANA VIMBAUMBAU "WAKIREMBUA"?

      Jisomee zaidi hapa
      *****************
      Mpambano wenyewe - Laki moja ndiyo hiyo inakwenda!!!

      Warembo waliofanikiwa kuingia nafasi tano bora ikiwa ni fainali ya kumpata Vodacom Miss Tanzania 2010, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutangazwa washindi…
       

      Warembo waliofanikiwa kuingia nafasi kumi bora wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutangazwa…

      Mrembo akianguka jukwaani wakati akipita na wenzake na vazi la ufukweni Duh aibu we acha tuuu.

      Warembo wakipita jukwaani na vazi la Ufukweni….
       
      Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, wakifurahia jibu la Mrembo Pendo, aliyemfagilia Rais Jakaya Kikwete wakati akijibu swali lake aliloulizwa.

      **************************
       Na Hatimaye Mrembo kuliko wote Tanzania Ndiye Huyu!!!


      Vodacom Miss Tanzania 2010 Geneviv Mpangala (katikati) akiwa na washindi wenzake msindi wa pili, Glory na Consolata, baada ya kutangazwa washindi katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika katika uku bi wa Mlimani City Mwenge Jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo

      Picha zote na maelezo (mengi) ni kutoka hapa




      Friday, September 10, 2010

      UCHOMAJI WA KURANI HAPA GAINESVILLE NINAPOISHI - HALI BADO NI YA WASIWASI

       Tangazo mbele ya kanisa lake
      • Ni wasiwasi mtupu. Masaa machache yaliyopita huyu Mchungaji Mhafidhina (Terry Jones) alitangaza kwamba alikuwa ameahirisha zoezi la kuteketeza Kurani hapo Jumamosi saa 12 jioni baada ya kuhakikishiwa kwamba ule msikiti ulioleta mzozo kule New York ungehamishiwa sehemu nyingine mbali na "Ground Zero"
       Wafuasi wake huvaa hizi fulana
      • Mara moja, shekhe anayesimamia ujenzi wa msikiti huo tata kule New York amekanusha kwamba hajaongea na huyu Mchungaji mchoma Kurani. Huyu Mchoma Kurani sasa amecharuka upya na anasema kwamba kumbe amedanganywa na wajenzi wa Msikiti wa kule New York. Kwa hivyo uchomaji wa Kurani unaweza ukawa pale pale siku ya Jumamosi kama sehemu ya kuadhimisha mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 11 Septemba, 2001. Kwa ujumla hali ni ya wasiwasi kwani hakuna ajuaye nini kitatokea. Mchoma Kurani huyu haaminiki na anabadilikabadilika kama kinyonga.
      Alama hii ipo mbele ya kanisa lake
        • Jumamosi tarehe 11 Septemba pia kuna mechi kali sana ya mpira wa miguu wa Kimarekani hapa katika chuo kikuu cha Florida na inategemewa kwamba mashabiki wapatao elfu tisini (90,000) au zaidi watahudhuria. Kwa hivyo mapolisi, FBI na walinda usalama wa taasisi zinginezo wanahangaika kweli kweli.
        Meya wa hapa ni shoga wa wazi. Jones na kanisa lake walipinga sana kuchaguliwa kwake 
        • Tuombeni hili lipite salama lakini vinginevyo nadhani moto utawaka duniani kote. Kama vibonzo tu vya Mtume vilivyochapwa na gazeti moja la Denmark wakati ule vilileta kasheshe duniani kote, fikiria uchomaji wa kitabu kitakatifu cha Kurani itakuwaje.
          Kitabu alichoandika

          ****************************************
          Wasiwasi

          Picha hii iko hapa.

          Mwishowe: Ujumbe Mzuri

          Wednesday, September 8, 2010

          MJUMBE "HAUWAWIGWI". MSAIDIENI HUYU MDAU ANAYEMTAFUTA MWENYE HUU MGUU KWA HALI NA MALI

          Mr Matondo;

          Niliiona hii picha somewhere in one of the blogs lakini sikumbuki which one. Since you have a nice collection of blogs on your blog, can you or one of your readers let me know ni blog gani? I desperately need to establish a contact with the owner of this leg, no matter what!

          Thanks; 

          James (True Mdau!)


          ********

          Angalizo langu: Binadamu (a.k.a Homo Sapiens) ni kiumbe tata ambaye hunivutia sana. Baadhi ya matendo yake ni ya kufurahisha, mengine ya kipumbavu, mengine ya kinyama, mengine ya kibinadamu ali mradi vurugu tupu. Nilikuwa nimekata shauri kuupuuzia ujumbe huu lakini baada ya kufikiri vizuri nikaona pengine ni vizuri niuweke hapa. Nina sababu zangu kwa kufanya hivyo. Msaidieni Homo Sapiens huyu anayemtafuta mwenye mguu huu kwa hali na mali!!!

          Monday, September 6, 2010

          VIBONZO VYA UCHAGUZI: SAFARI YA IKULU, USINGIZI HAUJI, MIMI NI MWENZENU NA TAALUMA IMEINGIA LUBA.

          Uchaguzi wa mwaka huu naona "umenoga" sana. Kwa hakika tutaona na kusikia mengi - yakiwemo yale ya binafsi. Tunaomba tu yote yafanyike kwa amani. Mungu Ibariki Tanzania!!!

          MAKARATASI YOTE YA TALAKA KWA DOLA 199.99 TU !!!

          • Nililiona hili tangazo jana kando ya barabara karibu kabisa na hapa ninapoishi. Inasemekana sasa kiwango cha talaka hapa Marekani kimefikia karibu asilimia 50 - yaani karibu nusu ya ndoa zote zinazofungwa zinaishia katika talaka.
          • Tuombe "balaa" hili lisije likatukumba kwani talaka zina athari nyingi hasa kwa watoto. Nchi za Skandinavia ambazo ndizo zinaongoza kwa masuala ya usawa wa kijinsia pia ndizo zinaongoza kwa kuwa na viwango vingi vya talaka. Sina uhakika kama kuna uhusiano kati ya usawa wa kijinsia na talaka. Tuwe macho!

          HALAFU "WAKAMCHAKACHUA"

          Saturday, September 4, 2010

          MADAKTARI WAZIPIGA KAVUKAVU HUKU MAMA MJAMZITO AKISUBIRI KUFANYIWA UPASUAJI

          • Madaktari wawili kule Italia wametoa kali ya mwaka baada ya kuamua kuzipiga kavu kavu huku mama mjamzito akisubiri kufanyiwa operesheni ya uzazi. Kutokana na kuchelewa kufanyiwa operesheni hiyo, mfuko wa uzazi wa mwanamke yule ilibidi uondolewe kabisa. Isitoshe mtoto alipata matatizo ya moyo na kuna uwezekano huenda amepata madhara ya kudumu ya ubongo kutokana na ukosefu wa hewa ya Oksijeni. Waziri wa afya wa Italia ilibidi asafiri kwenda kuomba msamaha kwa mwanamke yule ana kwa ana. 
          • Habari hii inapatikana hapa au unaweza kuisoma hapa chini. 
           ****************

          Italy health minister apologizes for botched birth

           MESSINA, Sicily (AP) — Italy’s health minister traveled to Sicily on Monday to apologize to a woman whose delivery of a son was botched when her two doctors got into a fistfight in the operating room.

          Laura Salpietro, 30, had to have her uterus removed and her son, Antonio, suffered heart problems and possible brain damage following his birth Thursday in Messina’s public hospital, Italian news reports said.

          Health officials and Salpietro’s husband, Matteo Molonia, said the two doctors disagreed about whether to perform a cesarean section and fought while Salpietro was in labor. Molonia said that delayed the C-section by over an hour, leading to complications for mother and son.

          fistfight occurred at a state hospital between a doctor who works there and a private physician Mrs. Salpietro paid as her gynecologist.

          Prosecutors have placed five doctors under investigation, and Health Minister Ferruccio Fazio visited Salpietro on Monday in the hospital to apologize.

          “I tried to give her words of hope, and above all I tried to tell her that the government was with her and her family at this time,” Fazio was quoted as saying by the ANSA news agency.
          The incident was the latest evidence of medical mistakes frequently reported in southern Italian hospitals, and it underscored Italians’ increasing use of private doctors if they can afford them. Italy has universal health care, but some Italians use private doctors to avoid long waits for procedures.

          Fazio said the botched delivery raised questions about this increasing intermingling of private doctors working in public hospitals. While many women choose to deliver in private clinics, some who have private doctors give birth in public hospitals equipped with neonatal units and other emergency facilities not always available in private clinics.

          The case also cast a fresh spotlight on the unusually high C-section rates in southern Italy. Some 38 percent of all births in Italy are done by C-section, more than twice the 15 percent recommended by the World Health Organization.

          In Sicily, however, the average is 52 percent. In Campania — the southern mainland region that includes Naples — it reaches 60 percent, Fazio noted.

          Earlier this year, the WHO reported that China had registered the highest C-section rate in the world at 46 percent, a quarter of them medically unnecessary.

          The United States is recording record C-section rates as well, with one-in-three mothers undergoing the procedure, according to the U.S. Centers for Disease Control and Prevention.

          Friday, September 3, 2010

          FIKRA YA IJUMAA: KIZUNGUMKUTI CHA "WASOMI" NA Ph.D ZAO!!!

          UCLA - 2004 (Baada ya kuhenya kwa miaka 6)
          • Kwa walio wengi Shahada ya Uzamivu (Ph.D) huashiria kilele cha mafanikio na ukomo wa safari yao ya kusaka elimu na maarifa darasani. Ni shahada inayoheshimika sana duniani kote kiasi kwamba watu wengi hufikia hatua ya kukata njia za mkato ili kuipata. Watu hawa huona fahari kubwa kuitwa madaktari wa falsafa hata kama udaktari huu ni wa bure na hawakuusomea wala kuufanyia kazi!

          • Shahada hii hata hivyo inatatanisha kutokana hasa na mfumo mzima wa elimu ambao umekaa kipiramidi. Katika shahada ya kwanza mtu unafundishwa mambo mengi kwa ujumla. Lengo hapa ni kupata maarifa ya juu juu tu juu ya mada mbalimbali katika masomo kadhaa unayosomea. Katika shahada ya uzamili (Masters), piramidi inaanza kufanya kazi yake na mtu unaanza sasa kujibana katika kaeneo kadogo tu katika taaluma yako. Halafu inakuja hii shahada ya uzamivu. Hapa mtu unachagua kaeneo kadogo zaidi na kukafanyia utafiti wa kina mpaka utoe mchango fulani mpya katika kaeneo hako. Tena ni lazima usimamiwe na magwiji katika kaeneo hako unakokashughulikia na wakiridhika kwamba kweli utafiti wako umetoa mchango fulani mpya basi Ph.D unaipata Ng'wanawane.
          • Kuna "wasomi" ambao mara wakiipata hii Ph.D basi wanajiona kuwa wamefika na kujifanya kwamba wanajua kila kitu. Ukweli hata hivyo ni kwamba Ph.D inapaswa kuonwa kama mwanzo tu wa safari ndefu ya kusaka maarifa ya kina - safari ambayo kusema kweli haina mwisho. Kwa mantiki hii hata wenye hizo Ph.D bado ni wanafunzi hata katika vile vieneo vyao vidogo walivyovisomea. Na kuwa na Ph.D siyo kuelimika!
          • Mimi ni mmoja wa wale wanaoamini kwamba haiwezekani kuwa na ujuzi timilifu na sisi binadamu ni wanafunzi wa kudumu hapa duniani. Kwa hivyo badala ya kukakawana na hiyo Ph.D na kujifungia katika kaeneo hako kadogo ambako mtu umesomea,bado ni lazima kuendelea kujisomea kwa bidii na kujifunza maarifa ya jumla katika taaluma zingine. Mimi kwa mfano ni mpenzi sana wa vitabu vya falsafa na fasihi ya Kilimwengu na huvutiwa sana na maandishi ya wanafalsafa na waandishi mbalimbali mashuhuri kama George Orwel, Pablo Neruda na wengineo. Maandishi haya ni yenye kufikirisha sana na kusema kweli yanapanua mawazo na hata uwezo wa kujenga hoja.
          • Kwa sasa nimeanza kusoma vitabu juu ya wanasayansi mbalimbali, maisha yao na vitu vilivyowafanya mpaka wakafanya ugunduzi muhimu wa Kisayansi. Nimeshangaa kugundua kwamba mara nyingi ugunduzi muhimu ni mkusanyiko wa mawazo ya watu wengi katika wakati maalumu na wanasayansi wengi walichofanya ni kuyachukua mawazo yale na kuyafanyia majaribio ili kuyathibitisha kisayansi na hatimaye kuyapanga vizuri, kuyaundia fomyula na kisha kuyachapisha. Ugunduzi wa bomu la Nyuklia hapa Marekani, kwa mfano, ulikuwa ni juhudi za wanasayansi wengi ambao walikusanya mawazo yao pamoja mpaka wakafanikiwa. Ni wanasayansi wachache sana (Albert Einstein ni mmoja wao) ambao walianzisha matapo mapya kabisa ya kinadharia bila kutegemea mawazo ya watu wengine kwa kiasi kikubwa.
          • Tuendelee kusaka maarifa kwa kujisomea kwa bidii na tukumbuke kwamba hata hawa wenye Ph.D, hawajui kila kitu na tuwe huru kuhojiana nao bila woga wala kujidogosha. Maarifa hayana mwenyewe wala ukomo na msomi wa kweli ni yule anayeheshimu na kuitambua kanuni hii. Na kusema kweli, HATUHITAJI KUWA NA Ph.D KUWA WASOMI!!! Wikiendi njema.

          JIANDIKISHE HAPA

          Enter your email address:

          Delivered by FeedBurner

          BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO