KWENU MLIONYANYULIWA MIKONO (I) - Kwenu mliokubali mikono yenu ikanyanyuliwa na wanyanyua mikono. Ipi ni sababu hasa iliyowafanya mkubali mikono yenu inyanyuliwe? Lengo, wajibu na jukumu lenu hasa ni nini? Je ahadi mlizozitoa ni za kweli? Mtazikumbuka na kuzitekeleza?
*************......*************
KWENU MLIONYANYULIWA MIKONO (II)
- Zipo tetesi kwamba wengi wenu mmezikimbia taaluma zenu na kuhakikisha kwamba mikono yenu inanyanyuliwa kwa sababu ya marupurupu na posho hizi nono kupindukia. Kama lengo lenu la msingi ni hizi posho na marupurupu haya ya kilafi; na madaraka mengine mtakayoyapata, basi historia itawahukumu kwa kuwasaliti watu wenu waliowatuma na kuwabariki katika safari yenu ya kunyanyuliwa mikono na hatimaye kwenda "tafrijani" Chimwaga.
*************......*************
KWENU WANYANYUA MIKONO (III)
- Bila kujali ni mnyanyua mikono yupi ataingia Ikulu, naomba na kutumaini kwamba miaka mitano ijayo itakuwa ya furaha, amani na matumaini kama inavyoonekana kudokezwa na taswira hapa chini. Hebu furaha, amani na matumaini yakawafikie walio wengi na hasa Watanzania wa kawaida.
*************......*************
- Japo mimi sitaweza kupiga kura, nawatakieni Watanzania wenzangu wote uchaguzi wa amani na utulivu. Mungu na Atupatie kiongozi mwenye uoni, kiongozi mwenye uchungu na nchi hii pamoja na maendeleo ya watu wake, kiongozi anayeumia na kukosa usingizi anapoona wananchi wake wakiishi katika umasikini wa kutisha, kiongozi ambaye atatuongoza kuelekea katika "nchi ya ahadi" bila kutetereka wala kumakinikia maslahi ya watu wachache tu katika jamii, kiongozi ambaye ataendelea kulinda na kudumisha mshikamano na amani tuliyonayo. Mungu Ibariki Tanzania!
*************.....*************