NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, November 30, 2010

SAKATA LA SAFARI ZA NJE: OBAMA NAYE AWEKA REKODI YA KUSAFIRI SANA KWA MARAIS WOTE WA MAREKANI. ALALAMIKIWA!

  • Rais wetu alishawahi kulalamikiwa sana kwa safari zake za nje za mara kwa mara. Wapo waliohoji manufaa ya safari hizo kwa taifa hasa ukizingatia kwamba zinatafuna pesa nyingi za walipa kodi. Wachambuzi wengine makini waliona kwamba safari hizo zilikuwa na tija kwa taifa letu. Kutokana na utata huu, Rais mwenyewe aliamua kupunguza idadi ya "wapambe" katika misafara mbalimbali ya viongozi. 
  • Rais Obama naye ameweka rekodi ya kuwa rais anayesafiri sana kwa kipindi alichokaa madarakani. Yeye amevunja rekodi ya kusafiri ya maraisi wote wa nchi hiyo kwa kutumia siku 55 akiwa safarini katika kipindi cha miaka yake miwili aliyokaa madarakani. Rekodi ya mwanzo ilikuwa inashikiliwa na rais George W. Bush (II) aliyetumia siku 54 akiwa safarini nje ya nchi katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ya utawala wake. 
  • Baadhi ya mambo yaliyoibuliwa katika safari hizi za Obama ni pamoja na ukweli kwamba dege lake la Air Force One linatafuna karibu dola 181,000 kwa saa moja!. Hizi ni pesa ambazo zinamtosha Mmarekani wa kawaida kuweza kununua nyumba nzuri ya vyumba vitatu!
  • Inasemekana pia kwamba safari yake ya hivi karibuni aliyoifanya katika nchi za Asia ilikuwa inatafuna karibia dola milioni 200 kwa siku moja. Hiki ni kiasi kikubwa cha pesa hasa katika wakati huu ambapo hali ya uchumi inalegalega kiasi kwamba nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi wote wa serikali imependekezwa kupigwa marufuku.
    • Sitaki kuibua upya mjadala huu lakini nadhani "common sense" inabidi itumike na kutanguliza matakwa ya taifa mbele kwa kuepuka safari ambazo si za lazima. Agizo la rais la kupunguza wapambe katika safari hizi pia ni hatua nzuri sana ya kupunguza gharama. 
    • Malalamiko kuhusu safari za Obama yanapatikana hapa; na kama kawaida malalamiko haya yanatoka kwa wahafidhina wa Fox News.

          Monday, November 29, 2010

          ATI, KWA NINI SHULE IFUNGULIWE KABLA HAIJAKAMILIKA? NI KUWAKOMOA WANAFUNZI, WAZAZI AU JAMII???

           
          Mashujaa wa Kidato cha Sita - HGK Sengerema High School.
          Hapa kuna maprofesa, maofisa wa jeshi na polisi, watawala, waalimu, wakaguzi wa fedha, wanasheria, wahasibu, watangazaji, wabunge n.k
          ***************
          • Ni nani anayeruhusu shule ya Sekondari ifunguliwe huku akijua kuwa bado haijakamilika? Utatoaje ruhusa shule ifunguliwe wakati unajua kabisa kwamba haina waalimu (wa kutosha), haina vitabu, haina maabara, haina vifaa vya michezo, haina vyoo, haina mesi, haina nyumba wala ofisi za waalimu na mambo mengine ya msingi?
          • Ni kweli mtoa ruhusa huyu angetoa ruhusa hii kama angejua kwamba watoto wake au ndugu zake wa karibu wangeenda kusoma katika shule ya aina hii? Au anafanya hivi kwa kutojali kwa sababu anajua kwamba watoto watakaosoma katika shule hii ni watoto wa wakulima na hawana la kufanya, na hivyo ni bora elimu badala ya elimu bora?
          • Hivi ndivyo ilivyotokea kwetu tulipopelekwa na kubwagwa Sengerema High School kusomea "combination" mpya ya HGK iliyokuwa imeanzishwa pale. Pamoja nasi walikuweko wenzetu wa PCB na PCM. Hawa wenzetu walichachamaa mpaka mtoa ruhusa akaamua kuwahamishia Shule za Sekondari za Shinyanga (Shy Bush) na Tosamaganga. Hata sisi watu wa HGK, wengi waliokuwa na uwezo na uamuzi wa kuhamia shule nzuri kama vile Mzumbe, Musoma Alliance na Tabora Boys walifanya hivyo. Tuliobakia pale ni "vichwa ngumu" na kusema kweli tulisoma kwa kutegemea"madesa" kutoka shule zingine. Na mtihani wa kidato cha sita ulipofika hivyo hivyo tulijikongoja na wachache wetu tuliweza hata kupata hiyo inayoitwa "divisheni wani"
          • Inashangaza sana kuona jinsi uzembe na kutojali kwa hawa wamiliki wa mfumo unavyoweza kuathiri na kudunisha maisha ya watu. Ati, ingekuwaje kama nasi tungepelekwa katika shule yenye walimu na vitabu vya kutosha nasi tukasoma na kufundishwa kama wenzetu wa Mzumbe, Musoma Alliance na Tabora Boys? Ni wangapi kati yetu ambao tulishindwa mitihani ya kidato cha sita kutokana na ukosefu wa waalimu na vitabu? Kuna hata anayejali? Kuna hata ambaye nafsi yake inamsuta kwamba pengine aliharibu maisha ya watu kwa kuwapeleka katika shule ambayo ilikuwa haijakamilika?
          • Inashangaza na kusikitisha sana kuona watu wanavyocheza na maisha ya watu namna hii. Na mchezo huu ndiyo sasa umeshika kasi katika haya "majengo ya kata" (a.k.a. shule za kata) yaliyotapakaa nchi nzima. Mengi yana upungufu mkubwa wa waalimu, hakuna vitabu wala maabara, hakuna nyumba wala ofisi za walimu, hakuna vyoo, hakuna mesi, hakuna...na bado majengo haya yanarundikiwa wanafunzi mamia kwa mamia kila mwaka. Kwa mtindo huu jamani, tunaanda taifa la aina gani? Unakuta shule ina wanafunzi 300 lakini walimu watatu au wanne. Kweli kuna elimu inayoendelea hapo? Halafu watoto hawa wakipata divisheni ziro tunawalaumu kwamba ni mbumbumbu na kwamba hawajui umuhimu wa elimu. Halafu nasi, kama vile wenye chongo mbele ya vipofu, tunasimama majukwaani na kujipiga kifua kwamba tumeboresha sekta ya elimu kwa kuongeza idadi ya mashule ya sekondari na idadi ya wanafunzi. Na vipofu wetu, pengine kwa kuona maluweluwe hafifu wanatushangilia. Kweli?
          • Ukweli unabakia pale pale kwamba bila elimu bora na kombozi hatutakaa tuendelee kwani Historia ndivyo inavyotuambia. Sijui ni kitu gani kinachotufanya sisi tufikirie kwamba tunaweza kuwa kighairi (exception) katika kanuni hii ya jumla. Inashangaza sana!

          Sunday, November 28, 2010

          USAHAULIFU MWINGINE NI HATARI TUPU: SAFINA NDIYO HIYOOOO INAONDOKA (UCHESHI).

          UTAFITI: ETI MBWA WANA AKILI KULIKO PAKA !!!

          • Utafiti uliofanywa na wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza unaonyesha kwamba mbwa wana akili zaidi kuliko paka. Katika utafiti huu, wanasayansi walikuwa wanachunguza uhusiano kati ya saizi ya ubongo na ukubwa wa miili ya wanyama mbalimbali; na waligundua kwamba ubongo wa nyani ndiyo ulikua kwa kasi zaidi ukifuatiwa na ule wa farasi, pomboo, ngamia na hatimaye mbwa.
          • Wanasayansi hawa pia waligundua kwamba ubongo wa wanyama wanaoishi katika makundi na wenye maingiliano ya kifamilia na kijamii ulikua kwa haraka zaidi kuliko ule wa wanyama wanaoishi peke yao kama paka na vifaru. Kwa ujumla "wanyama wanaoishi katika makundi hufikiri zaidi kuliko wale wanaoishi peke yao". Kwa matinki hii, wanahitimisha wanasayansi hawa, mbwa wana akili kuliko paka.
          • Ikisiri (abstract) ya utafiti huu inapatikana hapa; na unaweza kusoma habari zaidi hapa.

          Saturday, November 27, 2010

          MMEZAJI KUWA MMEZWA??? - 2015 ITAWEZEKANA???

          Ni yale yale ya mwinda kuwa mwindwa? Na hilo jina la mmezaji limenifurahisha. Hii ni kazi ya Said Michael.

          MIJIBABA LAIVU IKILANA DENDA HADHARANI. KAZI NI KUWAELEWESHA WATOTO !!!

          • Sina tatizo na tabia na mapendeleo ya kingono ya mtu ye yote na ninaamini kwamba kila mtu anao uhuru wa kuserebuka kivyake kama anavyoona inafaa. Pamoja na ukweli huu ni lazima nikiri kwamba huwa napatwa na ukakasi fulani hivi ninapoona mijibaba ikikukurushana kimahaba mchana kweupe. Pengine hii inatokana na ukweli kwamba hii si tabia yetu Waafrika ambako mambo ya kimahaba (hata kati ya mwanamke na mwanaume) yalitendeka kwa siri sana kiasi kwamba katika makabila mengi (mf. Wasukuma) hata wapenzi kushikana mikono tu hadharani ilitosha kuwashangaza watu.
          • Alhamisi ya wiki hii nikawa nimepeleka watoto Mc Donald. Ile tunatoka tu na kukata kona kuingia barabara kuu chini ya mti mkubwa karibu na supamaketi moja hivi, kukawa na mijibaba miwili yenye miili iliyokakawana kwa ushupavu ikiwa inatembea huku imeshikana mikono. Nilijaribu kuongeza mwendo kidogo ili watoto wasione lakini nikawa nimechelewa. Binti wa kati (miaka 7) ndiye alikuwa wa kwanza kupiga makelele "Dad, look, look. Those men are kissing". Nilipogeuza kichwa kweli jibaba moja lilikuwa limegeuka na kusimama tisti mbele ya jenzake na nyuso zao zilikuwa zimeshonana. Baadaye nilisikia magari yaliyokuwa nyuma yakipiga honi fulani hivi pengine kuunga mkono (au kupinga) kitendo cha mijibaba ile.
          • Pengine hiki si kisa cha kushangaza kwani kwa wenzetu hawa mambo haya ni ya kawaida. Tatizo ni ugumu na kigugumizi nilichokipata kujibu mvua ya maswali kutoka kwa mabinti hawa wachanga wasioelewa cho chote bado. Nilijaribu kuwaambia kwamba nitayajibu maswali yao yote tukifika nyumbani nikiamini kwamba tutakapofika nyumbani watakuwa wamesahau. Tena niliwaahidi kwamba tukifika nyumbani basi wanaweza kucheza michezo yao ya video waipendayo. 
          • Pamoja na juhudi zote hizi, tulipofika nyumbani tu kitu cha kwanza walichokifanya ni kumsimulia mama yao kisa kile na hapo tena mvua ya maswali ikaanza kunyesha upya. Tulijaribu kuyajibu maswali yao "kistaarabu" kwa kadri tulivyoweza. Tuliwaambia kwamba ile mijibaba ilikuwa hai"mushi mushi" kama walivyodhani lakini pengine ilikuwa inacheza mchezo fulani hivi wa kivita, mchezo ambao unawataka washiriki wake kusogeleana kabisa huku wakiwa ana kwa ana. Yule mdogo (miaka mitano) alionekana kuridhika lakini yule mkubwa (miaka 7) alikuwa na mashaka na maelezo haya ingawa naye mwishoni alikubali - japo kwa shingo upande.
          • Ati, ungekuwa ni wewe ungewapa maelezo gani watoto wa miaka saba na mitano kuhusu jambo hili. Ungewaambia ukweli au "ungewadanganya" kama tulivyofanya? Watu wa Saikolojia na utambuzi mnasemaje? 
            • Ni wazi kwamba mambo ya malezi hayana fomyula ati! Siku moja wataugundua ukweli na kama watakuwa hawajasau kuhusu kisa hiki si ajabu watatunyeshea tena mvua ya maswali kwa nini tuliwadanganya.

            NONDOZ - JAPO NI KWA MTINDO WA "HONORIS CAUSA" !!!


            Hongera kwa mtunukiwa!. Kwa habari zaidi kuhusu shahada za uzamivu za aina hii, soma sehemu inayosema "controversy" hapa.

            Thursday, November 25, 2010

            TAMADUNI ZINAPOGONGANA: SUALA LA KUCHOKONOA PUA BARABARANI NA KWENYE DALADALA

            Tangazo hili liko hapa
            • Juzi juzi hapa nilikuwa naongea na mwanafunzi wa kike Mmarekani ambaye alikuwa anafanya utafiti wa shahada yake ya uzamivu jijini Dar es salaam na kisiwani Zanzibar. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kwenda Tanzania.
            • Nilipomuuliza kama aliipenda Tanzania alisema bila kusita kwamba ni nchi nzuri sana, yenye amani na kwa muda wa miezi yote mitatu aliyokaa huko hana jambo baya la kulalamika. Aliniambia kuwa mambo yaliyomvutia ni pamoja na ustaarabu wa watu, upole, wema, mazingira mazuri, maliasili kibao na kuambiwa "Mzungu, I love you" mara kwa mara barabarani na kwenye daladala.
            • Nilipomuomba anitajie jambo angalau moja ambalo hakulipenda jijini Dar es salaam mara moja alitaja tabia iliyomkera ya watu kuchokonoa pua zao kwa kutumia vidole vyao tena kweupe mabarabarani na hata kwenye daladala. Alisema kwamba ni kawaida jijini Dar kuona mtu amevalia vizuri akikatiza barabara na huku yuko bize akichokonoa pua yake bila wasiwasi wo wote. Hakuna cha kitambaa, maji wala nini
            • Sikujua kama hili ni tatizo kwani kusema kweli sisi hatujali sana kuhusu jambo hili. Nilijaribu kujitetea kwamba pengine ni kwa sababu ya vumbi, hali ya hewa vuguvugu na joto kali ndivyo hufanya pengine pua zitekenyeke na hivyo kuwalazimu watu kujisafisha. Basi alicheka tu na mjadala wetu ukaishia pale. Katika utamaduni wa kizungu, kuchokonoa pua hadharani kwa kutumia vidole ni jambo ambalo halikubaliki.
            • Ati, wewe una maoni gani kuhusu watu kusafisha pua zao kwa kutumia vidole na kisha haooo wakaendelea na hamsini zao kufukuzia maisha bila wasiwasi. Ulishawahi kufikiria kwamba ni jambo linalotia kinyaa na kwamba watu inabidi wajirekebishe kwa kununua vitambaa au kufanya hivyo kwa siri?

            Huyu mchezaji aliwasha moto hapa Marekani baada ya kunaswa laivu na kamera akichokonoa pua yake

            Wednesday, November 24, 2010

            BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI: MASWALI MAWILI YA KIZUSHI + ANGALIZO

            Mh. J.K. akitangaza Baraza la Mawaziri leo

            Swali la Kwanza

            Vijana wako wapi? Akina Ndungulile, Kigwangalla, Nkamia, January na wengineo?  Mbiu ilikuwa ikipigwa kwamba baraza hili litakuwa la aina yake kwa kuhusisha sura mpya nyingi na hasa vijana. Kumetokea nini?

            Swali la Pili

            CCM wana mtindo wa kuandaa wenyeviti na maraisi wao mapema. Kwa kuangalia hili baraza la sasa, ni nani ambaye anaweza kujivika u-Shekhe Yahaya hapa akatutabiria ni yupi anayendaliwa kubeba mikoba ya CCM hapo 2015 baada ya Mh. J.K. kumaliza ngwe yake?

            Angalizo

            Baada ya kutembelea blogu mbalimbali na vyanzo vingine vya habari, watu wengi wanaonekana kufurahishwa sana na uteuzi wa Mh. John Pombe Maghufuli kurudi tena katika Wizara ya Ujenzi. Inasemekana kwamba Mheshimiwa huyu pengine ndiye waziri mchapakazi kuliko wote. 

            Uteuzi mwingine unaoonekana kuwakuna watu ni ule wa Mh. Dr. Harrison Mwakyembe, Mh. Profesa Anna Tibaijuka na Mh. Samweli Sitta. Nadhani sababu za waheshimiwa hawa kufagiliwa zinajulikana. Na wengine waliokuwa wakipigiwa tetesi sana kama huyu naona wametupwa nje. Mungu Aibariki nchi yetu!

            UTAFITI: HABARI NJEMA KUHUSU MAPAMBANO DHIDI YA MAAMBUKIZI YA UKIMWI


            Picha hii inapatikana hapa
            • Watafiti, madaktari, wanaharakati na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI "wanashangilia" baada ya utafiti mkubwa mpya uliochapishwa katika jarida maarufu la tiba la New England Journal of Medicine kuonyesha kwamba watu wanaokunywa dawa iitwayo Truvada ambayo ni mojawapo ya madawa ya kuongoza nguvu kwa watu walioathirika na UKIMWI inaweza kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa asilimia 44 kwa wanaume mashoga wanaofanya ngono bila kutumia kondomu.
            • Na kama dawa hii ikitumiwa kwa uangalifu kila siku (yaani bila kukosa hata siku moja) basi inaweza kupunguza uwekezano wa kuambukizwa UKIMWI kwa asilimia 90! Washiriki katika utafiti huu walikuwa ni wanaume mashoga kutoka katika nchi sita - Brazil, Ecuador, Peru, Afrika Kusini, Thailand na Marekani. 
            • Cha kufurahisha zaidi ni kwamba Truvada ambayo ni mchanganyiko wa madawa mawili yanayozuia virusi vya UKIMWI kuzaliana yaani Tenofovir na Emtricitabine tayari inapatikana katika nchi nyingi duniani. Hapa Marekani dawa hii hutengenezwa na kampuni la madawa la Gilead Sciences na inaweza kugharibu kati ya dola 12,000 na 14,000 kwa mwaka. Katika nchi masikini ambako ndiko kuna maambukizi mengi ya UKIMWI dawa hii inaweza kupatika kwa bei ya senti 40 (dola za Kimarekani) kwa kila kidonge. 
            Vidonge vya Truvada
              • Truvada bado ni ghali sana hasa katika nchi masikini kama zile za Afrika na swali kubwa linaloulizwa ni kuhusu gharama kubwa za dawa hii hasa ukizingatia kwamba kati ya wagonjwa wa UKIMWI wanaokadiriwa kuwa milioni 33 duniani kote ni milioni 5 tu ndiyo wanatumia madawa ya kuongeza nguvu.
              • Mbali na matokeo haya ya kutia moyo, watafiti hawa wanaonya kwamba huu si wakati wa kuacha kutumia kondomu na kuzingatia mbinu zingine za kujikinga na maambukizi ya UKIMWI. 
              • Makala kuhusu utafiti huu yanapatikana hapa, na ikisiri (abstract) ya utafiti huu kama ilivyochapishwa katika jarida la New England Journal of Medicine inapatikana hapa.

              Saturday, November 20, 2010

              UTAFITI: JOTO LA LAPTOP LINAUNGUZA KORODANI NA HIVYO KUHARIBU RUTUBA YA MBEGU ZA KIUME.

              • Je, wewe ni mwanaume? Unayo tabia ya kutumia laptop yako ikiwa mapajani mwako? Pengine itabidi uache tabia hiyo mara moja kwani unaweza ukawa unaangamiza kizazi kijacho. 
              • Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la Fertility and Sterility unaonyesha kwamba joto la laptop ni hatari kwa sababu linaunguza korodani na hatimaye kuharibu na hata kuangamiza kabisa mbegu za kiume. Joto hilo limetajwa kuwa sababu mojawapo inayosababisha kuongezeka kwa utasa katika nchi zilizoendelea. 
              • Mbegu za kiume zilizoathiriwa na joto la laptop hazina vichwa, hazina mikia na zingine zina mikia mifupi; na kwa hivyo haziwezi kuogoelea na kulifikia yai la mwanamke ili kuweza kulirutubisha. Kwa ujumla, joto la laptop linaweza kusababisha utasa wa kudumu kwa wanaume. 
              Ni mwogeleaji mmoja tu hodari ndiye atashinda hapa...
                • Ushauri wa watalaamu: Kama ni lazima uweke laptop yako mapajani, basi panua miguu yako. Hii inasaidia korodani zisiunguzwe na joto la laptop kwa haraka. Njia ya uhakika zaidi ni kutumia dawati au meza kila unapotumia laptop. Utafiti huu unapatikana hapa na hapa.

                Friday, November 19, 2010

                LEO NI SIKU YA WANAUME DUNIANI. CHAMA CHA WANAUME WANAOPIGWA NDANI YA NDOA TANZANIA KUUNDWA RASMI !!!

                • Japo leo ni siku ya wanaume duniani, kuko kimyaaaaa na sijasikia cho chote kwenye redio na vyombo vingine vya habari kuhusu siku hii muhimu. Naamini ingekuwa siku ya wanawake basi tungesikia "makelele" ya kila aina kutoka kila kona. 
                • Mbona siku yetu akina baba inadharauliwa namna hii? Au kwa vile ni sikukuu iliyoanza hivi karibuni tu (2009)? Au ni kwa vile hatuna mchango muhimu katika jamii mbali na kuanzisha migogoro na vita, kuendeleza mifumo dume yenye kunyanyasa akina mama na masaibu mengineyo? 

                • Hongereni wanaume popote mlipo hapa duniani; na hasa akina baba mnaoshiriki kikamilifu katika malezi ya watoto kama huyo juu katika kibonzo.

                FIKRA YA IJUMAA: TUITAFAKARI TABIA YA HUYU MDUDU

                "Kuna methali ya Kipare inasema, yule mdudu caterpillar aliyetulia kuliko wote ndio mla mbegu za mahindi yaliyopandwa. Kwa hiyo ukiona kimya ujue ndio hivyo tena................mbegu zinaliwa!!!!

                Albert Ngusaru (Kutoka Facebook)

                ******

                Angalizo

                Kwa hivyo ukiona mipango yako mingi haiendi vizuri, chunguza pengine kuna kiwavi (caterpillar) anayemung'unya mbegu za mipango yako kimya kimya. Na usishangae ukigundua kwamba wakati mwingine kiwavi huyo anaweza kuwa ni wewe mwenyewe!  

                Wikiendi njema.

                Thursday, November 18, 2010

                WANAHISABATI MPO? TUSAIDIANE KUKOKOTOA UPYA HAYA "MAFUMBO" YA KIDATO CHA PILI ENZI ZILE

                • Ni kule shule ya Sekondari ya Kahororo mjini Bukoba. Tulikuwa kidato cha pili; ndiyo tu tumekaramka na kuanza kuwakaramsha "form one" wetu. 
                • Tulizoea kupeana mafumbo haya kama utani tu bila kujua kwamba kwa kufanya hivyo tulikuwa tukijifunza (tena kwa lugha tunayoielewa vizuri na katika mazingira yetu wenyewe) baadhi ya misingi muhimu ya hisabati - somo linaloogopwa na kuchukiwa sana kutokana na udhahnia wake na jinsi lifundishwavyo
                • Tatizo ni kwamba, sina uhakika kama nakumbuka tulikuwa tunapataje majibu. Kwa wanamahesabu wakokotoaji, hebu tukumbushane tena.
                ***************

                Fumbo la kwanza
                • Jumamosi iliyopita, Speciosa alinunua ndoo ya maembe na akala theluthi moja (1/3) ya maembe yote. Siku ya Jumapili alikula nusu ya maembe yaliyobakia. Siku ya Jumatatu na Jumanne alikula embe moja moja kila siku. Siku ya Jumatano alikula nusu ya maembe aliyokuwa amebakiza. Siku ya Alhamisi alipoangalia katika ndoo aligundua kwamba alikuwa amebakiza embe moja tu. Je, Speciosa alinunua maembe mangapi siku ya Jumamosi?
                Fumbo la pili.
                • Babu alikuwa anapita msituni siku moja alipoona kundi kubwa la ndege mtini. "Shikamooni ndege mia" Babu aliwasalimia wale ndege "Sisi siyo ndege mia" Ndege wale walijibu halafu wakaendelea. "Sisi sote ukiongeza na wenzetu kama sisi, ongeza na nusu yetu, halafu uongeze robo yetu pamoja na wewe mwenyewe ndipo tutafikia ndege mia" Je, babu aliona ndege wangapi?

                Wednesday, November 17, 2010

                MWALIMU NYERERE ALIWAHI KUULIZA MASWALI MAZITO KUHUSU OFISI HII

                Ofisi rasmi ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

                ************** 


                TAFAKURI YA LEO: WEWE KWELI MZANZIBARI?

                "...Hivi karibuni Mzanzibari mmoja mhitimu wa chuo kikuu alisafiri ndege moja na mtu ambaye muda wote wa safari yao alikuwa akisoma kitabu.  Huyo mhitimu wa chuo kikuu baadaye aliniambia kwamba alishangaa alipogundua kuwa msafiri mwenzake alikuwa Mzanzibari kama yeye.  Nikamwuliza: ‘Kwa nini?’  Akanijibu kwa sababu alikuwa akisoma kitabu. Sikudhania kwamba alikuwa Mzanzibari kwa sababu sisi hatuna kawaida ya kusoma."

                Ahmed Rajab, Rai, Novemba 10, 2010

                **************

                Tuesday, November 16, 2010

                KWENU WANAWAKE: TUKIWALETEA ZAWADI, MANENO. TUSIPOWALETEA NAPO MANENO....

                ...Mnataka tufanye nini? By the way, kipi ni bora? Maua waridi au mchicha?

                **********









                Kikwenu mnahesabuje? Picha imetoka kwa dada Florah Lauwo

                Monday, November 15, 2010

                KAMA KWELI MTEJA NI MFALME, KWA NINI HUDUMA ZETU NI MBOVU NAMNA HII?

                • Mwezi wa sita nilikwenda pale Benki ya Posta (Mpya) ili kumfungulia kijana wangu mmoja akaunti. Binti niliyemkuta pale alikuwa amenuna kama mbogo. Alitupa jibu moja tu kwamba tulikuwa tunahitaji barua ya mwenyekiti wa kitongoji kutoka kijijini, huyoo akafunga mdomo kama vile tulikuwa tumemkosea. Mpaka watu wakawa wananong'ona na kulalamika juu ya kiburi kile cha kutisha. Kwa vile tulikuwa hatuhitaji mkopo basi tuliondoka na kwenda Stanbick ambako tulipokelewa kwa uchangamfu wa kutosha.
                • Halafu nikaenda pale Air Tanzania kutaka kununua tiketi ya kwenda Mwanza. Pamoja na kwamba hawa jamaa shirika limewafia na wana kandege kamoja tu, "customer service" yao pia ni ziro. Nilikaa kwenye benchi la kusubiria huduma kwa karibu robo saa na hakuna aliyenisemesha. Mabinti wawili hivi walikuwa wakisogoa kwenye simu. Niliondoka pale bila kusemeshwa.
                • Nikatoka hapo na kwenda kule Precision. Huko nako mambo ni yale yale. Wafanyakazi ni wachungu wamenuna utafikiri wamelazimishwa kuja kazini. Kuna ugumu gani kusema "karibu" na angalau kutabasamu tu; na kumshughulikia mteja moja kwa moja? Kwa nini mahusiano ya watoa huduma hawa na wateja wao yawe ya kihasama namna hii? Hawafundishwi hata kozi za msingi kuhusu "customer service"? Ukiritimba huu wa kipumbavu unamsaidia nani? 
                  • Halafu ikija kampuni ya kigeni na watu wakaipenda kwa huduma zake tunaanza kulalamika eti hatuna moyo wa kizalendo na tunakimbilia vitu vya nje
                   *****************
                  Hebu sasa sikiliza kisa hiki kuhusu "customer 
                  service" ya hawa wenzetu wanaojua maana 
                  ya biashara na umuhimu wa mteja.
                  • Juzi juzi hapa tulikwenda kula katika hoteli moja iitwayo BJ's. Kwa bahati mbaya tulipata mhudumu ambaye alikuwa anajifunza na pia kulikuwa na watu wengi sana. Huduma tuliyopata siku ile ilikuwa mbaya na hatukuridhika nayo kabisa. Katika risti ya malipo nilitoa dukuduku langu kwa kusema "Not satisfied with today's service". Basi baada ya siku tatu hivi tukapata simu kutoka kwa meneja akituomba msamaha. Alituambia kwamba siku tuliyoenda ilikuwa ni siku ambayo wahudumu wapya walikuwa wanajifunza na wateja kadhaa walikuwa wamelalamika. Meneja alituomba turudi tena na alikuwa anatutumia kuponi ya dola 25.00 kama kiashiria cha kuomba msamaha (tazama barua hapo chini). Alituambia kwamba majina yetu yapo kwenye mfumo wao wa kompyuta na siku tutakayoenda yeye mwenyewe atatukaribisha na kutuhudumia.
                  • Jana Jumapili kweli tulienda BJ's tena na tulipotaja majina yetu tu basi meneja mwenyewe alikuja, tukapewa meza maalumu na huduma safi sana ya kushangaza. Meneja mwenyewe ndiye alikuwa anatuhudumia na mpaka tunaondoka alikuwepo kutuaga. Maneno yake ya mwisho wakati tunatoka nje ya mlango wa hoteli yalikuwa "Kila mteja kwetu ni muhimu, na natumaini kwamba mtaendelea kuja katika hoteli yetu tena na tena".
                  • Hivi ndivyo mahusiano ya mtoa huduma na mteja yanavyopaswa kuwa. Na kwa hili watoa huduma wetu bado wana mengi ya kujifunza.

                  ZOFA AIBUKA KIDEDEA KATIKA UANDISHI WA INSHA JUU YA SIKU YA MASHUJAA

                  • Walimu wake wamevutiwa sana na insha hii ya binti yenu Zofa (Darasa la kwanza) na wamesema itachapishwa na kuwekwa katika kitabu chao cha kumbukumbu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza darasa la mwaka 2010. Watoto hawa hawakupewa maandalizi yo yote. Waliambiwa tu wakasikilize vizuri kilichokuwa kinaendelea katika maonyesho ya kusherehekea siku ya mashujaa yaliyokuwa yameandaliwa na wenzao wa darasa la nne halafu waje waandike insha juu ya kile walichojifunza. Hongera Zofa!!!
                  • Kama unavyoweza kuona, japo kuna makosa ya kisarufi na uandishi, walimu hawakuyagusa. Ni makosa ambayo yanaruhusiwa kwa sasa na watoto hawa wa darasa la kwanza hawapaswi kukosolewa kwa kila kitu. Katika hili (nami nikiwa mwalimu), nimejifunza kitu!

                  Saturday, November 13, 2010

                  KLABU YA WAPINGA RUSHWA KUTOKA TABORA BOYS.....

                  • Ni wazi kwamba upepo wa mabadiliko umeshaanza kuvuma na watu sasa wameanza kuamka kutoka usingizini. Inafurahisha kuona vijana (a.k.a. Taifa la kesho) wakiwa na vilabu vya kupambana na matatizo sugu ya kijamii kama hawa vijana wa Tabora Boys - shule ambayo inasifika kwa kutoa viongozi wengi wa kiserikali pengine kuliko shule nyingine yo yote. 
                  • Sijui klabu hii inajishughulisha na nini lakini natumaini kwamba vijana hawa wanatambua kwamba ili kutibu ndwele sumbufu kama hii inabidi kukitafuta kiini chake na kisha kukitafutia tiba. Ninapenda wajiulize, ni kwa nini rushwa imetanda kila kona mbali na juhudi za serikali kuitokomeza? Ni kundi gani la watu linaloongoza katika kutoa na kupokea rushwa katika jamii? Kwa nini? Wakiweza kuyajibu maswali haya, pengine watakuwa na uwezekano wa kutafuta njia mwafaka zaidi za kuweza kupambana nayo. 
                  • Mimi naamini kwamba rushwa haitatatuliwa kwa kuweka sheria kali (ambazo mara nyingi hazitekelezwi - hasa kwa "wakubwa") au ubabaishaji wa TAKURURU. Yote kwa yote, hongereni vijana wa Tabora Boys kwa juhudi zenu hizi. Ni mwanzo mzuri na ingefurahisha kama vilabu vya aina hii vingeenea katika mashule mengine.

                    Friday, November 12, 2010

                    FIKRA YA IJUMAA: IF YOU KNOW THE SOLUTION, YOU ARE PART OF THE PROBLEM !!!

                    ******************
                    1. Ati, unalijua suluhisho la tatizo linalokusumbua? 
                    2. Kama jibu ni ndiyo; una uhakika kwamba kweli una tatizo au pengine wewe ndiyo (sehemu ya) tatizo? 
                    3. Na kama wewe ndiyo (sehemu ya) tatizo, utawezaje kujisuluhisha? Bado una uhakika kwamba una tatizo?
                    4. Kama jibu ni ndiyo, una uhakika gani kwamba suluhisho ulilonalo kwa tatizo linalokusumbua (mf. ufisadi au huyu ambaye familia yake "imetekwa na maninja") ndilo bora kuliko masuluhisho mengine yote? 
                    Angalizo: Sina uhakika kama kanuni za 
                    mantiki zimezingatiwa. 
                    Wikiendi njema!

                    ******************

                    SWALI GUMU: MTOTO WA MIAKA MITANO ANAPOTAKA KUJUA JINSI ALIVYOZALIWA (UCHESHI)


                    "Daddy, how was I born?" asked a curious son.
                    "Ah, very well," said the father. 
                    "You need to find out anyway! Mom and Dad got together in a chat room on MSN. Dad set up a date via e-mail with your Mom, and we met at a cyber cafe. We snuck into a secluded room, and then your mother downloaded from your dad's memory stick. As soon as dad was ready for an upload, it was discovered that neither one of us had used a firewall. Since it was too late to hit the delete button, nine months later the blessed virus appeared. And that's is the story, son."

                    Thursday, November 11, 2010

                    LEO NI SIKUKUU YA MASHUJAA HAPA MAREKANI: ATI, SISI TUNAWAENZIJE MASHUJAA NA WAASISI WETU?

                    • Leo ni siku ya mashujaa hapa Marekani na ni siku ya mapumziko. Jana kuanzia saa mbili asubuhi wazazi tulikusanyika shuleni ili kushuhudia michezo, nyimbo na maigizo ya watoto wa darasa la nne katika kuwakumbuka mashujaa wao. 
                    • Tukio hili lilinivutia sana kwani wenzetu hawa wanajibidisha kwelikweli kuhakikisha kwamba watoto wao wanakumbuka historia ya mashujaa na waasisi wao. Nyimbo za kizalendo ziliimbwa, hotuba za maraisi mashuhuri wa Marekani zilisikilizwa, vita vilivyopiganwa vilionyeshwa, nukuu muhimu za watu mbalimbali zilirejelewa, matukio muhimu katika historia yao (mf. kutua mwezini, Space shuttle na bomu la kwanza la nyuklia)  yalizungumziwa na hata Historia ya Utumwa pia iligusiwa. Kulikuwa pia na mashindano ya kutaja majina ya maraisi wote 44 pamoja na majimbo yote 50 kwa mpangilio.
                    • Mwishoni kabisa wimbo mmoja wenye maneno yasemayo "I love the USA" ulipokuwa ukiimbwa, niliweza kuwaona wazazi wengi wakidondokwa na machozi. Halafu wazazi wote waliowahi kwenda vitani waliombwa kusimama; na walishangiliwa kwa kelele na vifijo vya kila aina. Lilikuwa tukio la kusisimua sana!
                    • Binti yangu ya kwanza yeye aliigiza kama Harriet Tubman, mwanamke shujaa mweusi ambaye alishiriki kikamilifu katika jitihaza za kutokomeza biashara ya utumwa hapa Marekani.
                    Kutoka kushoto: Susan B. Anthony, Martin Luther King Jr, John F. Kennedy (mbele ya mikrofoni), Eleanor Roosevelt (nyuma ya J.F. Kennedy) na Harriet Tubman.
                    • Wakati nikitazama maonyesho haya, wazo moja lilikuwa likipitapita kichwani mwangu. Hivi sisi tunasherehekeaje sikukuu ya mashujaa wetu - akina Kinjeketile, Mkwawa, Mirambo, Nyerere na wengineo? Nilisikitika kidogo baada ya kukumbuka kwamba hata kutazama video za waasisi wetu na kusoma maandishi yao bado ni hati hati.  Inavyoonekana, hata kuwaenzi tu mashujaa na watangulizi wetu napo hatuwezi. Kwa mfano, kwa nini maandishi na hotuba za mashujaa na waasisi wetu ziwe adimu mpaka tunafikia hata hatua ya kuziwekea hati miliki kinyemela na kuwakoromea wale wanaojaribu kuziweka peupe? 
                    • Nilitembelea pia ubao wa matangazo wa watoto wa darasa la kwanza. Hawa walikuwa wameambiwa kuandika juu ya umuhimu wa uhuru katika maisha yao kama Wamarekani. Hapa chini ni baadhi ya majibu yao:
                    imagebam.comimagebam.com imagebam.com imagebam.com imagebam.com

                    Mwisho, msikilize mtoto huyu akitaja majina yote ya marais 44 wa Marekani kwa mpangilio....

                    KAMA HAZIJAFIKA, HAZIJAFIKA TU. MTOTO WA MIEZI 18 AANGUKA KUTOKA GHOROFA YA NANE. ANUSURIKA BILA MAJERAHA YO YOTE !!!

                    • Polisi kutoka nchini Ufaransa wanasema kwamba mtoto wa kiume mwenye miezi 18 alidondoka kutoka dirisha la ghorofa ya nane, akaangukia juu ya turubai la hoteli moja chini ya jengo hilo, akadunda na hatimaye kuishia mikononi mwa mpita njia mmoja. Madaktari walipomfanyia uchunguzi walibaini kwamba mtoto huyo hakuwa na majeraha yo yote. Kisa hicho kilitokea tarehe 3 mwezi huu na polisi walikuwa wanawashikilia wazazi wa mtoto huyo kwa tuhuma za kutojali kiasi cha kuhatarisha maisha yake.
                    • Japo katika televisheni walikuwa wanajaribu kutoa maelezo ya kisayansi kuhusu sababu zilizomfanya mtoto huyu akapona, Kwangu mimi huu ni mwujiza. Wewe unasemaje? Kisa hiki kinapatikana hapa.

                    Wednesday, November 10, 2010

                    NI ARI ZAIDI, NGUVU ZAIDI NA KASI ZAIDI: AHADI ZILIZOTOLEWA ZAANZA KUTEKELEZWA!

                    • SENIOR Personal Assistant to the President,Mr Lumbila Fyataga (left), hands over auto rickshaw (bajaji) documents to the Lindi Regional Administrative Secretary, Mr Thomas Sowani (right), at the State House in Dar es Salaam on Tuesday. The auto rickshaw was donated by President Jakaya Kikwete to Ms Maria Imakulata Simon Mbonde of Nandete village, Kilwa Kipatimu, who has a physical disability. The president had promised to buy her the vehicle during his campaign tour. Photo by John Lukuwi
                    • Mambo yakienda chapu chapu namna hii na ahadi zote (hasa zile za muhimu kwa wananchi) zikatekelezwa basi pengine "maendeleo ya haraka" yatapatikana. Picha na maelezo ni kutoka kwa blogu ya H@ki Ngowi.

                    HONGERENI WANABLOGU KWA KAZI NZURI MLIYOIFANYA WAKATI WA UCHAGUZI !!!

                    • Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa tofauti sana na chaguzi zilizotangulia. Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia umma wa Watanzania ukiamka kutoka katika usingizi wa pono wa miaka mingi na kuanza kuhoji mambo. Mbali na mambo mengine, umma huu sasa unahoji ni kwa nini ungali ukiishi katika lindi la umasikini wa kutisha wakati nchi imejaliwa raslimali za kutosha? Raslimali hizi zinamnufaisha nani? Umma huu nao sasa unataka kuionja keki ya taifa!
                    • Kutokana na msisimko huu tumeshuhudia majina makubwa (na kongwe) katika medani ya siasa na uongozi yakitupwa nje katika kura za maoni na hata katika uchaguzi wenyewe. Na hili ni jambo jema katika deokrasia yetu changa kwani, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, nchi yetu ilishaachana na mambo ya usultani na watu wachache kuhodhi madaraka miaka nenda miaka rudi si kitu cha kujivunia!
                    Ni nini kilicholeta mabadiliko haya?
                    • Mbali na mambo mengine, naamini kwamba vyombo vya habari vimechangia sana katika kuwaamsha wananchi. Mambo ambayo zamani yalikuwa yakiogopwa kusailiwa sasa yanajadiliwa waziwazi. Na blogu zenu hizi zimekuwa mstari wa mbele katika harakati hizi kwa kuwahabarisha wapiga kura na kutetea ukweli bila kujali kama ukweli huo unawaudhi au unawafurahisha baadhi ya watu. Wakiwa wamejificha katika kunguku la u-anonymous, wadau wengi wa blogu hizi wamekuwa wakitoa mawazo yao ya ndani kabisa bila woga wo wote.
                    • Hata wakati wa kupiga kura na wakati wa kusubiri matokeo, blogu nyingi zilikuwa mstari wa mbele kuripoti kilichokuwa kinaendelea ikiwemo kurusha matokeo kutoka vituoni laivu. Naamini kwamba hili limesaidia katika kupunguza visa visivyothibitishwa vya "uchakachuaji" wa kura.
                    • Bila kutaja majina, napenda kuchukua nafasi hii kuwahongeresha wanablogu wote - hata wale "waliotuhumiwa" kuegemea upande mmoja na kupuuza upande wa pili. Nyote mmetoa mchango mkubwa sana katika kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Na uzuri ni kwamba kila kitu kimefanyika kwa amani na utulivu ukiachilia mbali visa vya fujo za hapa na pale.
                    • Natumaini kwamba uchaguzi wa mwaka 2015 utakapofika Inshallah blogu zenu zitakuwa zimejiimarisha zaidi na zitatoa mchango wa uhakika zaidi. Hebu basi msichoke na kuliacha pigano. Kazi yenu wanablogu si bure katika kujenga "Civil Society" imara nchini Tanzania. Hongereni sana!

                    Tuesday, November 9, 2010

                    WANASEMA ETI KADANGANYA: TAZAMA HALAFU UAMUE MWENYEWE (SEKUNDE 31 TU)

                    • Binadamu ndivyo tulivyo. Hata ufanye jambo zuri namna gani, lazima tu kuna ambao watakerwa na kulalamika. Hata Yesu alilalamikiwa kuhusu miujiza yake na bado kuna watu ambao wanadai na kuamini kwamba pengine alikuwa ni mwanamazingaombwe aliyebobea tu!   
                    • Huyu mama kafumbua fumbo baada ya herufi moja tu na tayari sauti zinapazwa eti uchunguzi ufanyike. Inawezekana amedanganya na hakupaswa kushinda na kujipatia kitita cha pesa alichoambulia. Binadamu!

                      Monday, November 8, 2010

                      HABARI NDIYO HIYO: TAKURURU YAMSAFISHA RASMI MBUNGE WANGU. NJIA YA USPIKA SASA NYEUPE?

                      • Siasa za Tanzania kuna wakati zinashangaza, zinatatanisha na hata kuchanganya. Mbunge wangu (Mzee wa Vijisenti) sasa kasafishwa rasmi na TAKURURU kwamba hakuhusika na kashfa ya rada. Je, hii ina maana kwamba ndiyo ameshasafishiwa njia ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kuna nini ambacho kinawafanya CCM wamkumbatie sana mbunge wangu huyu mwenye kashfa na kesi ya mauaji mahakamani? Ni kweli hakuna wanachama wengine wenye uwezo na wasio na madoa wakagombea nafasi hii muhimu? Baada ya misukosuko waliyoipata katika uchaguzi huu mtu ungedhani kwamba CCM wangejitathmini na kurekebisha baadhi ya mambo muhimu yaliyowafanya wasukwesukwe, mojawapo likiwa hili la kufungamanishwa na ufisadi. Inashangaza sana!
                       ************

                      YAH: UCHUNGUZI KUHUSU TUHUMA ZA RADA

                      Tunapenda kuujulisha umma kuwa uchunguzi na ushahidi uliokusanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Shirika la Upelelezi - SFO la Uingereza kuhusu tuhuma za Rushwa katika ununuzi wa Rada, umeshindwa kumhusisha Bw. Andrew Chenge katika tuhuma hizo.

                      TAKUKURU inawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa chombo hiki kwa kutoa taarifa za kuwafichua wale wote wanaojihusisha na Rushwa kwani jukumu hili ni la kila mmoja wetu.

                      Imetolewa na

                      Doreen J. Kapwani,
                      Afisa Uhusiano-TAKUKURU
                      Novemba 08 , 2010
                      S. L.P. 4865,
                      Dares Salaam. Simu: 2150043-6/2150360 Nukushi: (022) 2150047 Baruapepe:dgeneral@pccb.go.tz
                      Mtandao www.pccb.go.tz
                      ************

                      Taarifa hii ni kutoka Lukwangule Entertainment.



                      Kwingineko: Mh. Chenge mwenyewe anagombea USPIKA kwa sababu

                      "...nagombea kiti cha uspika nikiamini kwamba ninao uwezo wa kutibu majeraha makubwa yaliyoumiza Bunge na Taifa, wananchi na chama changu (CCM) kwa sababu tu ya kuwa kiongozi aliye tayari kujitafutia na kujitwalia umaarufu au ushujaa wake binafsi kwa njia ya kuwahujumu, kuwaumiza na kuwachafua wengine kwa kutengeneza tuhuma na kashifa za kila namna. Tiba ya uongozi wa aina hii ni kuchagua kiongozi bora wa bunge...."

                      Nukuu hii ni kutoka Wavuti.

                      Kwa habari zaidi kuhusu sakata hili soma hapa

                      MDAU ANAULIZA: JAMII FORUMS NI MALI YA CHADEMA? INATUMIWA KUFANYA UCHOCHEZI? NI ZE UTAMU MPYA?


                      Jamani eeh! Mjumbe hauwawigwi. Nauweka ujumbe huu kama ulivyo...

                      ****************

                      JAMII FORUMS NI MALI YA CHADEMA? INATUMIWA KUFANYA UCHOCHEZI? NI ZE UTAMU MPYA?

                      Dr. Matondo. Kila siku huwa natembelea blogu yako kwa sababu kuu mbili. (1) Iko balanced. Huegemei CCM wala CHADEMA na unakosoa na kusifia pande zote bila upendeleo kila inapobidi na kustahili. Napenda pia staili yako ya uandishi wa ki-summary, wenye kufikirisha sana na uliopangiliwa vizuri. (2) Collection nzuri ya blogu zote muhimu tena ziko arranged kufuata topics. Huwa napita kuangalia headings za blogu mbalimbali kabla sijaamua kuchagua mada au blogu ya kusoma. Hata kama blogu yako haina wasomaji wengi, usikate tamaa. You are making a difference kwa watu wachache wanaopenda mambo ya maana na mawazo ambayo yako mature.

                      Leo hata hivyo nataka kuleta hoja hapa kuhusu hawa jamaa wa Jamii Forums a.k.a "Home of Great Thinkers" Binafsi nilikuwa memba wa Jamii Forums kwa muda mrefu sana mpaka hivi karibuni nilipoamua kujitoa na kukimbilia Wanabidii baada ya forum kupoteza mwelekeo na kugeuka kuwa another Ze Utamu. Ni wazi kwamba Jamii Forum sasa inatumiwa kama ukumbi wa CHADEMA na inafanya kazi ya uchochezi. Kwa nini nimefikia conclusion hii?

                      (1) Huko Jamii Forums hoja na mawazo mbadala sasa haviruhusiwi. Ukijaribu kuleta mawazo na hoja mbadala na ukajaribu kuikosoa CHADEMA au kumsema vibaya kiongozi wao (Dr. Slaa) basi utatukanwa na kushambuliwa sana hata kama unatoa hoja nzuri na kwa njia za kistaarabu. Kwenye Jamii Forums CHADEMA na Dr. Slaa ni miungu wanaoabudiwa. Slaa anaitwa rais mteule, masihi wa Tanzania, mkombozi wa wanyonge n.k. Ukisaili tu uhalali wa madai haya basi wewe ni msaliti, msenge uliyeleweshwa kasumba za CCM na ni mtu wa kuonewa huruma. Na matusi utakayotukanwa basi hutakaa uyasahau. Wakati huo huo ni sawa kuwatukana viongozi wa CCM na taifa letu bila wasiwasi wo wote. Huko rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatukanwa, anabezwa na kuitwa majina mbalimbali. Yote hii ni sawa lakini kamwe huwezi kumgusa masihi wao Dr. Slaa. Kwa nini? Ni kwa sababu hii, naamini kwamba Jamii Forums ni mali ya CHADEMA. Kama hii ni kweli basi waendeshaji wake inabidi waseme hivyo ili kila mtu anayekwenda huko ajue. Na hii inaonyesha hasa CHADEMA inaundwa na watu wa aina gani. "Great Thinkers" huwa hawatumii matusi kama silaha bali hutumia hoja. Hata wewe utakapoweka hoja hii si ajabu ukaishia kutukanwa na kutishwa.

                      (2) Katika kipindi cha uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa, Jamii Forums imeibukia kuwa chombo cha propaganda za CHADEMA na chombo cha uchochezi. Ni chombo cha watu wenye jazba, hasira na mihemko mikali kiasi kwamba wengine wanasema eti wako tayari hata kufa ili kutetea na kuipigania nchi yao na kura zilizoibwa (wanaita kuchakachuliwa). Kila mbunge wa CCM aliyeshinda uchaguzi basi ni lazima amechakachua kura na hatua ni lazima zichukuliwe ili kuhakikisha ushindi kwa CHADEMA unapatikana. Jazba na hasira zilizoonyeshwa huko mpaka zinatisha. Sote tunajua nafasi ya vyombo vya habari katika kupalilia na kuchochea misukosuko kule Rwanda, Burundi na sehemu zingine zenye machafuko. Jamii Forums inaingia moja kwa moja katika vyombo vya aina hii na inashangaza kuona kwamba mpaka hivi leo serikali imekaa kimya tu inaangalia. Mpaka lini?????

                      Jamii Forums ni mtandao ambao ulianza vizuri sana na una nafasi kubwa mno katika kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii yetu. Hata hivyo kwa sasa mtandao huu umegeuka na kuwa genge la wahuni wenye jazba na hasira kali, wahuni ambao wako tayari hata kuleta machafuko nchini ili kufikia lengo lao la kisiasa kupitia CHADEMA na Padri wao mteule.

                      Natumaini kwamba serikali inau-monitor mtandao huu ili usije ukaiingiza nchi yetu katika matatizo makubwa. Natumaini pia kwamba serikali haitachelewa kuchukua hatua kama walivyofanya kwenye Ze Utamu. Amani tuliyonayo si mali ya CHADEMA wala ya Dr. Slaa na haipaswi kuchezewa na mtu ye yote yule. Waendeshaji wa Jamii Forums inabidi watambue kwamba mikono yao italowana damu kama jazba na uchochezi wanaoufanya utavuvumka na hatimaye kuwasha moto katika nchi yetu iliyozoea utulivu na amani.

                      Asante na natumaini kwamba hutaogopa kubandika ujumbe huu. Mungu Ibariki Afrika. Mungu Ibariki Tanzania!

                      Ni mimi Mtanzania Halisi (aka Kalumekenge)

                      Mbeya (Tz)

                      Saturday, November 6, 2010

                      TUDUMISHE UTAMADUNI WETU: MH. J.K ALIPOONJA UHONDO WA NGOMA ZA KISUKUMA

                      • Wamasai na Watindiga ni mojawapo ya makabila yanayovuma sana kwa kuendelea kudumisha utamaduni wao - japo nayo yananyemelewanyemelewa na utandawazi. Wasukuma nao bado wanajikongoja na mojawapo ya mambo wanayoendelea kuyadumisha ni utamaduni wao wa kucheza ngoma zao za kienyeji.
                      • Kule wilayani Bariadi, kwa mfano, kila tarehe 30 mwezi wa tano makundi makuu mawili kinzani ya Bagika na Bagalu hukutana na kushindana usiku mzima na mshindi huamuliwa nyakati za mchana majira ya saa 11 siku inayofuatia. Mashindano haya huvutia watu wengi sana na yamekuwa kama sehemu ya sikukuu kwa Wanyantuzu. Katika mashindano haya mamanju huonyesha ubingwa wao wa madawa na uchawi; na anayeelemewa ndiye hushindwa.
                      • Kama mkereketwa wa maswala ya utamaduni, nimefurahi kumwona Mh. J.K. akifurahia ngoma hizi za Kisukuma siku alipotembelea makumbusho ya Wasukuma yaliyoko Bujora jijini Mwanza.  
                      • Utamaduni ndiyo utambulisho wetu hapa duniani na mtu asiye na utamaduni wake mwenyewe ni mtu aliyepotea na asiyejielewa. Japo utamaduni wetu umo katika pigano na unatishwa kuangamizwa na utandawazi, inafurahisha sana kuona kwamba baadhi ya vipengele vyake kama hiki cha michezo ya jadi vinazidi kudumishwa. Tusonge mbele.
                      J.K. akiangalia majina ya Watemi. Picha zote kutoka Blogu ya Ikulu.

                      *****...******

                      Msikilize Ng'wanakanundo hapa chini, manju mashuhuri wa Kisukuma kutoka Mwanza.



                      Friday, November 5, 2010

                      FIKRA YA IJUMAA: WHAT IS IN A NAME? JINA LA BLOGU "LINAPOKINAISHA"

                      • Kabla ya kuanzisha blogu hii rasmi hapo tarehe 8/1/2009, nilitafakari sana kuhusu jina, lengo pamoja na mwelekeo wake. Baada ya kutafakari kwa kina niliiamua kutumia methali maarufu ya Kinaijeria isemayo " Chakuka Kitamu na Kichungu vyote Vinaweza Kumfanya Mlaji Akakunja Uso".
                      • Nilichagua jina hili ili kuakisi hasa ukweli wenyewe kwamba blogu hii haipo hapa ili kumfurahisha mtu ye yote wala kikundi cha watu; na kama vile msumeno itakereza kote kote. Na kwa vile hakuna upande mmoja tu wa ukweli/ubaya, nilijua tangu mwanzo kwamba mambo nitakayokuwa nikiyaandika hapa yatakuwa matamu kwa wengine na yatakuwa machungu kwa wengine. Kwa wale watakaoyaona ni matamu si ajabu wakakunja uso kwa kufurahia, na watakaoyaona ni machungu kama shubiri basi nao watakunja uso kwa uchungu na kukinaika. Kwangu yote ni sawa!
                      • Sasa nimeshangaa kugundua kwamba kuna wadau ambao wamekuwa wakikerwa na jina la blogu hii na hata kuikimbia kwa sababu eti jina lenyewe linaonekana limekaa "kingonongono." Wadau hawa wanasema kwamba japo wanaipenda blogu hii, huwa hawawezi kuitembelea wakiwa maofisini na hata majumbani (wakiwa karibu na watoto) kwa sababu ya kuogopa kushukiwa kwamba wanaangalia mambo machafu.
                      • Ni kweli unapoisikia methali ya "chakula kitamu na kichungu vyote vinaweza kumfanya mlaji akakunja uso" picha inayokujia akilini mwako ni ya mambo ya ngono? Kabla hata sijaanzisha blogu hii rasmi, nililipendekeza jina hili kwa Da Mija (ambaye ndiye alinitia moyo hasa wa kuanzisha blogu). Da Mija hakukereka nalo na nakumbuka tu alisema kwamba inawezekanaje vyakula viwe tofauti lakini "reaction" iwe ni ile ile? Da Mija unakumbuka? Ulinitosa nini (utani tu!)?
                      • Jambo hili hata hivyo linaakisi ukweli halisi katika maisha yetu hapa duniani: Hata siku moja usitende jambo lolote (hata liwe zuri namna gani) bila kutegemea kuwaudhi watu wengine. Hii inatokana na ukweli kwamba hatujui ukweli/wema hasa ni nini, na ukijumlisha na miingiliano ya kitamaduni, mazingira, malezi, hulka yetu kama wanyama na wakati mwingine kutoelewa mambo tu, mitafaruku ni ya lazima.
                      • Nimalizie na swali la kizushi: Ni kwa nini tunaogopa (au pengine niseme tunaipenda) ngono namna hii hata kufikia hatua ya kuinusa kila mahali hata ambapo haikukusudiwa?
                      • Wikiendi njema wadau. Kwa wale mliokuwa mkikerwa na methali hiyo ya Kinaijeria, samahanini sana. Haikukusudiwa iwe hivyo!

                      JIANDIKISHE HAPA

                      Enter your email address:

                      Delivered by FeedBurner

                      BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO