NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 31, 2010

FIKRA YA IJUMAA: HEBU TUMALIZIE MWAKA HUU (2010) KWA KUISOMA MANIFESTO HII KWA UANGALIFU !!!

***************
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa wanablogu wenzangu na wadau wote wa blogu hii. Tuendelee kupendana na kushirikiana. Nyote nawatakieni mwaka mpya (2011)  mwema na wenye mafanikio tele. Mungu Aendelee kutulinda na kutubariki. Panapo majaliwa, tutaonana tena mwaka kesho (2011)

***************
Manifesto hii inapatikana hapa.

Thursday, December 30, 2010

BIBLIA, SINEMA YA MAISHA YA YESU NA REKODI MBALIMBALI ZA DINI KATIKA LUGHA ZETU ZA KIASILI.

Picha hii inapatikana hapa.
  • Wamishenari wa mwanzo katika miaka ya 1900 walitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha zetu za kiasili. Mbali na kuitafsiri Biblia Takatifu katika lugha zetu, wao pia ndiyo waliandika sarufi na kamusi za mwanzo za lugha hizi, pamoja na kwamba wengi wao hawakuwa wanaisimu wala wataalamu wa mambo ya lugha. Cha kushangaza (au pengine niseme cha kusikitisha) ni kwamba hata baada ya miaka mingi ya uhuru, lugha zetu nyingi bado hazijashughulikiwa ipasavyo kwa kuandikiwa sarufi za kina na machapisho mengine; na badala yake zimeendelea kudharauliwa na nyingi zipo katika hatihati ya kutozungumzwa na pengine hatimaye kuweza kutoweka kabisa.
  • Wamishenari na watu wanaojishughulisha na mambo ya dini bado wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha na hata kuhifadhi lugha zetu kupitia azima yao isiyotetereka ya kueneza neno la Mungu. Ndiyo maana kama Mwanaisimu, nimefurahi sana kugundua kwamba Sinema ya Maisha ya Yesu sasa inapatikana mtandoni katika Lugha mbalimbali za Kitanzania kama Kibena, Kidigo, Kigogo, Kihaya, Kihehe, Kimasai, Kimeru, Kimoshi (Kichaga), Kimakonde, Kimakua, Kinyakyusa, Kinyilamba, Kimasai, Kinyamwezi, Kinyakyusa (cha Ngonde), Kishambala, Kisukuma, Kiswahili na Kiyao. Sinema hii pia inapatikana katika lugha nyingine za Afrika. Ukitaka kuisikiliza na kuitazama, tembelea tovuti ifuatayo na chagua lugha unayotaka.
  • Pia unaweza kusoma Biblia Takatifu, kusikiliza na kutazama filamu ya Yesu pamoja na rekodi mbalimbali za Kikristo katika lugha kadhaa za Tanzania kupitia tovuti ya Joshua Project (chagua Tanzania, halafu languages). Mungu Atubariki tunapouanza mwaka mpya wa 2011.    
  • Swali: Hivi Kurani Tukufu inapatikana katika lugha nyingine yo yote ya Tanzania mbali na Kiswahili? Au hairuhusiwi kuitafsiri hovyo hovyo kama ilivyo kwa Biblia Takatifu? 

      Wednesday, December 29, 2010

      TUMEVUNJA REKODI YA BARIDI ILIYOWEKWA MWAKA 1925!!!

      • Najua kuwa wakazi wa sehemu zenye baridi kali kama vile Minnesota, Maryland, Cambridge, kule Ulaya (Da Mija na Candy1) na nchi za Skandinavia (Mtakatifu, Matiya, Yasinta na Edna) mtacheka mtakaposoma hapa lakini hata sisi huku Florida hali ya hewa imetuchachia kiasi kwamba rekodi ya baridi iliyowekwa mwaka 1925 (nyuzi 24F) imevunjwa usiku wa kuamkia leo joto liliposhuka na kufikia nyuzi 21F
      • Kama picha hiyo juu inavyoonyesha, jimbo la Florida ni mzalishaji mkuu wa matunda hasa machungwa na malimao na barafu kama hii inaweza kuleta hasara ya mamilioni ya dola kwa wakulima. 
      • Tatizo jingine ni kwamba karibu miti yote ya maua tunayopanda hapa huwa haivumilii baridi kali kama hii na unaweza kuona kwamba hata michikichi nayo imeanza kunyauka. Watoto kwa upande wao, walifurahia kuona vibonge hasa vya barafu pengine kwa mara ya kwanza maishani mwao.
      • Kutokana na baridi hii iliyotanda sehemu mbalimbali duniani, wapinzani wa ile dhana ya kuongezeka kwa joto duniani wanaonekana kufurahia huku wakidai kwamba baridi hii inaonyesha kwamba makelele yaliyokuwa yakipigwa kuhusu kuongezeka kwa joto duniani yalikuwa ni ya uwongo.
      • Hapa chini ni picha mbali mbali zikionyesha baridi hii iliyovunja rekodi hapa kijijini ninapoishi.
      ****************
      Kwa picha zaidi nilizopiga mwenyewe kuhusu hii barafu hapa Florida bofya HAPA.

      Tuesday, December 28, 2010

      KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA HII HAPA

      • Vuguvugu la kudai katiba mpya limepamba moto nchini Tanzania. Sijui ni wangapi wanaoshiriki katika vuguvugu hili wameshawahi kuisoma katiba nzima na kutafakari mapungufu yake. Hapa chini ni katiba nzima kama ilivyowekwa katika tovuti ya Wizara ya Mambo ya Katiba. Hebu na tuisome kwa makini kabla hatujaamua ni mabadiliko gani tunayotaka kuyafanya. Mungu Ibariki Tanzania!!!


         ********
        Au unaweza pia kutembelea hapa... (Kutoka udadisi)

         
        TOLEO LA MWAKA 2000 LA KATIBA:

        Monday, December 27, 2010

        ATI, MILA HII NI UNYANYASAJI WA KIJINSIA? WANAWAKE MNASEMAJE?

        • Katika makabila mengi ya Kiafrika wanawake kupiga magoti wanaposalimiana na wanaume na watu wanaowazidi umri ni jambo la kawaida. Upigaji huu wa magoti hutofautiana kutoka kabila moja hadi jingine. Kwa Wanyantuzu (Wasukuma wa kule Bariadi), kwa mfano, mwanamke alitegemewa kupiga magoti mpaka chini kabisa hasa anaposalimiana na wazee; na upigaji huu wa magoti ulikuwa (na bado) ni ishara mojawapo kuonyesha kwamba binti amelelewa vyema na ana sifa za kuoleka!
        • Picha hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Bi. Etta Banda akipiga magoti wakati wa kusalimiana na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete imezua maswali kuhusu mila hii kongwe. Ni heshima au udhalilishaji?
        • Inabidi tukumbuke pia kwamba wanaopigiwa magoti si wanaume pekee bali mwanamke anaweza kumpigia magoti mwanamke mwenzake anayemzidi umri au anayetaka kumwonyesha kwamba anamheshimu. Na katika jamii nyingine, wavulana na hata wanaume ndiyo hupiga magoti. Nakumbuka wakati nikisoma katika shule ya Sekondari ya Kahororo kule Bukoba, vijana wa Kihaya ndiyo walikuwa wakipiga magoti walipokuwa wakiwapa watu wazima vitu na jambo hili lilikuwa likitushangaza sana sisi "Banyamahanga" wa kutoka mikoa ya Shinyanga na Mara.
        • Kuna njia nyingi za kuonyesha heshima kwa watu wazima au watu wenye wadhifa katika jamii mbalimbali duniani. Ndiyo maana Rais Obama aliwasha moto hapa Marekani alipopigwa picha huku akiinamisha kichwa wakati akisalimiana  na Mfalme Hirohito wa Japan. Hii ilionwa kama dalili ya udhaifu na kutojiamini wakati ni jambo la kawaida katika utamaduni wa Kijapani.
        • Mimi nadhani kinachohitajika ni maelewano na utangamano wa kitamaduni. Kwa wakati huu wa dot.com, wakati wa usasa na utandawazi ni rahisi sana kutupilia mbali mila zetu kwa kudai kwamba zimepitwa na wakati. Na wakati mwingine tunaweza kushangaa baadaye tunapokuja kugundua kwamba hata hao "wakubwa zetu" tunaojaribu kuwaiga kumbe nao wana mila zinazofananafanana na zetu tunazojaribu kuzitupilia mbali. Umeshawahi kujiuliza, kwa mfano, ni kwa nini, wafalme wachache waliobakia Afrika wanapigwa vita sana na nchi za Kimagharibi wakati huo huo Ulaya nzima imejaa wafalme na malkia? Au pengine kwa vile Wafalme waliobakia Afrika (mf. Mswati wa Swaziland) ni "madikteta?" na wengi walioko Ulaya wapo "kiishara" tu?
        • Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba ni lazima tuwe waangalifu kwani si kila mila yetu ni mbovu na si kila mila ya Kimagharibi ni nzuri !!! Mila ikionekana ni potofu (mf. ukeketaji, au hata hii ya wanawake kupiga magoti) basi ni lazima tuitupilie mbali na kama ni nzuri, ni lazima tuishikilie. Vinginevyo tutapoteza utambulisho wetu na kuwa watu wasio na chao hapa duniani! Kama kupiga magoti kwa lengo la kuonyesha heshima ni unyanyasaji (na hapa simwongelei J.K. wala picha hii), basi inabidi tutafute njia nyingine ya kuonyesha heshima hiyo. Au pengine hata hakuna haja ya kuonyesha heshima!
        • Na kwa hili la kupiga magoti, ningeomba hasa wanawake watupe maoni yao (ili tusije tukawa kama huyu jamaa). Wanajisikiaje wanapofanya hivyo. Ni kweli wanahisi kuwa wananyanyaswa? Dada Yasinta, Koero, Da Mija na wengineo tuambieni.
        • Soma maoni ya Profesa Mbele - bingwa wa maswala ya kitamaduni na Mwl. Mhango wa Blogu ya Mpayukaji hapa.

        Sunday, December 26, 2010

        KWA WAKWE ZANGU SIKU YA KRISMASI KWEUPEE !!!

         Mzunguko wa Posta: makutano ya Boma road, Double road, na Railway road
        • Mila ya wakwe zangu (Wachaga) ya kwenda kijijini kwao kujumuika na kusherehekea sikukuu ya Krismasi pamoja na ndugu na jamaa ni mila nzuri inayopaswa kuendelezwa. Haipendezi kuona watu wakitumbua raha mijini na kusahau nyumbani walikotoka.
        Barabara ya Tanesco
        • Siku ya Krismasi jana Moshi mjini kulikuwa kweupeeee kabisa kwani watu wengi walikuwa wamerudi milimani kusherehekea sikukuu pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao. 
         Barabara ya Boma

         Hakukuwa na watu Moshi mjini.

        Hata hivyo wapo wanaokerwa na tabia hii ya Wachaga kwenda Moshi hasa kama kunaambatana na kufanya matambiko. Picha zote na baadhi ya maelezo ni kutoka kwa Amani Masue.

        Friday, December 24, 2010

        FIKRA YA IJUMAA: HUENDA MWALIMU NYERERE ALIKUWA SAHIHI. PENGINE URAIS NDIYO KAZI NGUMU KULIKO ZOTE

        • Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Ikulu palikuwa panamliza. Kwamba kulikuwa na siku alikuwa halali hasa baada ya kufanya ziara za vijijini na kuona umasikini wa wananchi na huku yeye akiwa ndiye mwenye jukumu la kuwaongoza na kuwaonyesha njia ya kutokea katika umasikini huo wa kutisha. Alisema kwamba kuna wakati hata alikuwa akidondokwa na machozi. Alichojaribu kufanya, japo kilishindwa, sote tunakijua.
        • Kwingineko tunamsikia akilalamika kuwa Ikulu siyo mahali pa kukimbilia hasa kwa kiongozi mwadilifu na aliwakoromea vikali makomredi wenzake waliokuwa wakijaribu kuingia Ikulu kwa kutumia njia za mkato zikiwemo kukopa mamilioni ya pesa (sijui kama ni kweli!). Mwalimu alitaka kujua biashara ambayo wangeifanya Ikulu ili kuweza kurudisha mamilioni waliyokuwa wameyakopa. Akihutubia katika Sherehe za Mei Mosi Mbeya mwaka 1995 Mwalimu aliunguruma akisema "Mtanzania wa leo hawezi kununua kura bila kwanza yeye kununuliwa"
        • Picha hii ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni kielelezo kizuri cha kauli hiyo ya mwalimu kuhusu "raha" na majukumu mazito ya Ikulu. Akiwa ndani ya nyumba hii pamoja  na waombolezaji hawa, naamini kwamba rais ni lazima alishikwa na uchungu usiopimika kuhusu umasikini wa wananchi hawa ambao kimsingi wanamtegemea yeye awaonyeshe njia ya kuendea katika nchi ya ahadi. Naamini kwamba huu ndiyo umasikini ambao ulikuwa unamliza Mwalimu Nyerere. Sitashangaa kama na yeye machozi yalimdondoka!
        • Hata hii picha anayotoka nje inaweza kuonwa kama taswira ya Musa aliye tayari kuwaongoza watu wake kuelekea katika nchi ya ahadi tena kwa Nguvu Zaidi, Ari Zaidi na Kasi zaidi. Akiwa na mabuti, suti nyeupe na kalamu tatu katika mfuko wa suti yake, rais anaonekana kuwa amejiandaa vizuri na yuko tayari kwa safari. Bado ana miaka mitano zaidi ya kuleta mabadiliko yenye kuonekana na kuhakikisha kwamba Watanzania tunapiga hatua za kweli katika safari yetu. Tumezunguka jangwani kwa miaka 49 na sasa wakati wa angalau kuona dalili za nchi ya ahadi tunayoiendea umefika. Na dalili zinaonyesha kwamba wapagazi na wasafiri wengine wameanza kuchoshwa na mizunguko hii ya jangwani isiyo na mwisho!
        Picha hizi za rais sijui nilizipata wapi. 
        Kama ni zako nijulishe nikushukuru!

        Thursday, December 23, 2010

        HII HISTORIA YA NOTI ZETU INAELIMISHA

        Historia ya Noti Tanzania Kuanzia 1905 Mpaka sasa

        Na Fredy Azzah
        Wednesday, 22 December 2010

        JK akikabidhiwa noti mpya na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Ndulu. Picha kutoka kwa Kamanda wa Matukio.
        **********

        TANGU mwaka 1884 fedha zilizotumika Tanganyika zilikuwa ni sarafu, noti zilianza kutumika mwaka 1905 wakati wa utawala wa Mjerumani. Noti hizo zilitolewa katika thamani ya Rupie tano, 10, 50, 100 na 500. Zanzibar mwaka huohuo wa 1905, noti za Rupie za Zanzibar zilitolewa katika thamani za Rupie tano, 10, 20, 50, 100 na 500.

        Mbali na rupia iliyodumu kwa muda mrefu katika matumizi ya noti nchini, tangu kupatikana uhuru, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikibadilisha noti zake kutokana na sababu mbalimbali.

        Ikiwemo sheria inayoiruhusu kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitano mpaka saba. Kutokana na mamlaka hayo BoT, kuanzia mwaka 1966 imefanya mabadiliko kadhaa ya sura za noti zake pamoja na alama za kiusalama.

        Pia kutokana na kupanda na kushuka kwa thamani ya shilingi, BoT imekuwa ikitoa noti zenye thamani tofauti tofauti (denomination),  kuanzia ile ya Sh10 mpaka sasa ambapo noti yenye thamani ndogo ni Sh500 huku kubwa ikiwa ya Sh10,000.

        Katika historia ya mabadiliko ya noti, mwanzo kabisa ilikuwa ni mwaka 1966 ambayo yalihusu noti ya Sh20 iliyokuwa na sura ya Rais wa Kwanza wa Tanzania na Sh100 'Mmasai' pamoja na nyingine iliyokuwa na simba. Ilipofika mwaka 1978, benki hiyo ilitoa tena noti za Sh10 na Sh20.

        Mabadiliko mengine katika sura ya noti yalifanyika miaka ya 1985, 1987, 1989, 1990 kwa kuwa na noti ya Sh50 ambayo ilikuwa na sura ya Rais wa Pili Ali Hasani Mwinyi, pundamilia na picha nyingine zilizokuwa zikiashiria mavuno.

        Noti ya Sh1,000 yenye sura ya Rais Mwinyi na tembo iliingia mwaka 1993 na mwaka 1995 ilingia noti ya Sh10,000 yenye sura ya Rais Mwinyi na simba.

        Mwaka 2000 kuliingizwa noti ya Sh1,000 ikiwa na sura ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, tembo na mgodi wa makaa ya mawe, wakati mwaka 2003 ilikuja noti ya Sh 500 ikiwa na picha ya nyati, jengo la Nkurumah lililopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na nyoka.

        Mwaka huo huo iliingia noti ya Sh5,000 ikiwa na faru na mgodi na noti ya Sh10,000 ikiwa na jengo la benki na tembo.
        Kimsingi mpaka sasa BoT imefanya mabadiliko makubwa ya sura za fedha za Tanzania mara saba, mabadiliko yaliyohusisha rangi, alama (picha) na alama za usalama wa fedha hizo.

        Mbali na mabadiliko hayo, Desemba 17 mwaka huu BoT ilizindua noti mpya ambazo zitaanza kutumika rasmi kwenye mzunguko wa fedha wiki ya kwanza ya Januari mwaka 2011.

        Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu anasema noti hizo mpya zitakuwa na mabadiliko mbalimbali ikiwemo rangi na alama za utambulisho ambazo sasa zitakuwa na sura za waasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

        “Katika noti za sasa, kutakuwa na saini Gavana aliyepo pamoja na Waziri wa Fedha aliyepo madarakani,” anasema Profesa. Mabadiliko ya safari hii yamezihusha noti zote na Profesa Ndulu anasema tofauti na za awali, noti za sasa zina alama mpya tatu, zitakazolinda usalama wake dhidi ya watu wanaoghushi ambao anasema uwezo wao unakuwa kila siku kutokana na kukua kwa teknolojia.

        Rais akizikagua noti hizo mpya.

        Anasema alama zilizowekwa ni pamoja na ile iliyojificha ya picha ya Mwalimu Nyerere inayochukua nafasi ya twiga katika noti za viwango vyote. Alama nyingine mpya kabisa katika teknolojia ya utengenezaji fedha ni ile ambayo inaonekana kama inatembeatembea wakati noti inapokuwa ikigeuzwa na nyingine ambayo inabadilika au kugeuka rangi.

         

Kadhalika, anasema mbali na kupunguzwa ukubwa, noti hizo zitatambuliwa kirahisi na walemavu wa macho kutokana na alama maalumu zilizowekwa kwa ajili yao katika kila kiwango. 

Alama hizo ni pamoja na mistari iliyovimba, pamoja na ile ya V ambazo zimewekwa kwa idadi maalumu inayoelezea kila kiwango cha noti husika.Mabadiliko mengine yamefanywa katika picha za wanyama simba, nyati pamoja na tembo ambao awali, picha zao zilikuwa zikionyesha miili yao yote, katika noti mpya ni picha za vichwa vyao tu zitakazoonekana.

        Kitu kingine kinachozitofautisha noti hizo mpya na zile za zamani ni karatasi zilizotumika kuzitengenezea. Anasema noti hizo mpya zimetengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100 tofauti na noti zilizopo kwenye mzunguko ambazo karatasi zake zinatokana na mbao.

        “Kampuni inayochapisha noti zetu, ndiyo pia inayochapisha baadhi ya denomination (noti) ya Marekani, kwa hiyo karatasi zinazotumika kutengeneza dola ya Marekani ndizo hizo hizo zitakazotengeneza fedha zetu,” anasema Profesa Ndulu.

        Kwa mujubu wa Profesa Ndulu, mchakato wa kubadilisha noti ulianza Aprili mwaka 2009 na mchakato wa zabuni uliendeshwa na hatimaye makampuni kumi na moja kujitokeza ingawa tisa ndiyo yaliyoingia katika ushindani.

        Kampuni ya Crane AB ya Sweden ilishinda kutengeneza noti za Sh500, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 huku kampuni ya Adae La Rue ya Uingereza ikishinda zabuni ya kutengeneza noti za Sh1,000.

        Gavana Ndulu anasema gharama ya uchapishaji vipande 1,000 imeshuka ikilinganishwa na wakati ambao Tanzania ilikuwa ikichapa noti zake katika kampuni ya Giesecke & Devrint ya Ujerumani... “Kama mwanzo tulikuwa tukichapisha vipande 1,000 kwa Sh10, sasa tunachapisha kwa Sh saba,” anasema Profesa Ndulu. Anasema kupungua kwa gharama hizo kunatokana na ushindani katika kupambanisha wazabuni.

        Anasema kwa kawaida wastani wa noti yoyote kuishi katika mzunguko ni miezi saba na kuwa kutokana na ubora wa noti mpya,  zitaweza kuishi kwa muda huo ili kuipunguzia benki gharama ya kuchapisha fedha mara kwa mara kutokana na uchakavu.

        Licha ya madai ya kushuka kwa uchumi hivyo kupungua kwa thamani ya shilingi, Profesa Ndulu anasema BoT haina mpango wa kuchapisha noti yenye thamani zaidi ya Sh10,000 inayotumika sasa.
        “Labda mpaka shilingi yetu ifikie pabaya sana, lakini kwa sasa tutaendelea kutumia hizi hizi zilizopo,” anasema Profesa Ndulu.

        Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Crane AB Peter Brown, anasema alama za usalama ambazo zimetumika katika utengenezaji wa noti hizo ni teknolojia mpya kabisa ambayo haijawahi kutumiwa na nchi yoyote ya Afrika. Anasema alama hizo ni hatimiliki ya kampuni hiyo ambayo ilitumia miaka mitatu kuzitengeneza.

        “Kutokana na teknolojia iliyotumika kutengeneza alama za usalama za noti hizo, si rahisi mtu yeyote kuzigushi,” anasema Brown.

        Pia anasema kutokana na kukua kwa tekinolojia, ni vyema nchi zikawa na utaratibu wa kubadilisha noti zake kila baada ya muda unaoshauriwa kisheria ili kupambana na wimbi la watu waogushi.

        Anasema kampuni yake inachapisha dola 100 ya Marekani na kuwa  teknolojia inayotumika kutengeneza fedha hiyo yenye soko kubwa duniani ndiyo inayotumika pia kutengeneza noti za Tanzania ambazo zinatatengenezwa na kampuni hiyo

        Chanzo: Mwananchi

        WATONGOZAJI NA WATONGOZWAJI - HEBU SOMENI "UTAFITI" HUU



        • Tafiti nyingi - hata zile zinazohusu mambo muhimu ya kiafya, kisiasa, kiuchumi na kijamii hufanyika nje; na matokeo yake pamoja na majumuisho mengi yanayotolewa huwa hayaakisi hali halisi ya Afrika. Ndiyo maana mimi huwa nazitilia shaka tafiti nyingi za aina hii. Kwa mfano huwa nashawishika kuamini kwamba pengine unene wa Mwafrika anayeishi kijijini, kula chakula kilichokuzwa kiasili na kufanya kazi za mikono kila siku una tofauti na ule unene wa mtu anayeishi New York katika maisha ya deko huku akila vyakula vilivyojazwa makemikali ya kila aina. Wataalamu wa shibe na tiba mnajua.  
        • Katika mkondo huu huu, utafiti mpya wa kidaku uliofanywa na tovuti ya kimapenzi ya Badoo.com (inayodai kuwa na memba wapatao milioni 90) unasema kwamba eti wanawake katika sehemu nyingi duniani hupenda sana kusifiwa kuhusu uzuri wa midomo yao, ingawa wanawake kutoka sehemu zingine hupenda kusifiwa vitu vingine mbali na midomo.
        • Wanawake wa Kimarekani, Kifaransa, Kiitalia na Kibrazil, kwa mfano, wao hupenda kusifiwa jinsi wanavyovaa wakati wanawake wa Kiingereza hupenda kusifiwa kuhusu uzuri wa miguu yao. Wanawake wa Kihispania wao hupenda kusifiwa kuhusu uzuri wa nywele zao huku Wanawake wa Kijerumani na Kikanada wakipenda kufagiliwa kuhusu unyororo wa ngozi zao. Wanawake wa Kidachi na Kireno wao eti hupenda kusifiwa kuhusu uzuri wa masikio yao.
          • Wataalamu wa Saikolojia wanasema kwamba midomo kushika namba wani haishangazi kwani wanawake hutumia muda mwingi sana wakipamba midomo yao kuanzia tu wanapobalehe; na wamekuwa wakifanya hivyo tangu enzi za Wamisri wa kale.

          • Nilipousoma utafiti huu niliwakumbuka hawa jamaa katika picha ambao niliwahi kuwadokeza hapa. Hapa wanaweza kuwa wanasifia nini? Ati, wanawake wa makabila mbalimbali wanapenda kusifiwa kitu gani? Au pengine ni sifa za ndani na za maana zaidi kama uchapakazi, upole, ukarimu na zinginezo za aina hii (Noeclexis). Watongozaji na watongozwaji leteni data tuzione. Ati, huko facebook nako mambo yakoje? 
          • Utafiti huu unapatikana hapa.

          Wednesday, December 22, 2010

          SAKATA LA DOWANS, TANESCO, KUPANDA KWA BEI ZA UMEME NA MLALAHOI !!!

          (1) Mgao Tena

           (2) Anamezeka?

          Kwa habari zaidi soma hapa na hapa

          Katuni zote ni kutoka kwa Said Michael.

          BAADA YA MIAKA 1O YA NDOA, HATIMAYE LEO NIMEPATA MAUA WARIDI KWA MARA YA KWANZA. KULIKONI ???

          (1) Ati, kipi ni bora? Maua waridi (Roses) au mchicha ili tuje tule wote?


          (2) Ati, kulikoni ??? Kwa nini maua baada ya miaka 10 ya ndoa? Na Wanaume twaruhusiwa kuhoji kama huyu mke wa Hagar the Horrible hapa chini?


          (3) Au pengine tusome na kuzingatia 1 Wakorintho 13:4 - 8


          4. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; 5. haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; 6. haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; 7. huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. 8. Upendo haupungui neno wakati wo wote...

          *************
          Asante sana mama watoto wangu mpendwa. Asante kwa kunishangaza namna hii. Asante sana kwa wema wako usio na kikomo. Asante kwa kuwa rafiki yangu wa kweli. Asante kwa kila kitu. Mungu Aendelee kutubariki katika safari yetu hii tunayosafiri pamoja hapa duniani!!!

          *************

          Acheni nifurahie maua yangu mimi...tena na Noeli juu!!!

          Tuesday, December 21, 2010

          HOSEA AKANUSHA UVUMI WA WIKILEAKS

          Hii Wikileaks kweli italeta "mtafaruku" duniani. Na bado tutasikia mengi. "Uzuri" ni kwamba hakuna anayejali.

          ************

          Hosea Akanusha Uvumi wa Wikileaks

          Na Mwandishi Wetu 
          (Tarehe: 20th December 2010)


          TAARIFA zilizovuja za mtandao wa Wikileaks, ambazo zilitoka kwa Serikali ya Marekani, zimemgusa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, na kwa haraka, amekanusha kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa ni kikwazo cha utendaji wa taasisi hiyo, kama alivyonukuliwa humo.

          Dk. Hoseah, anadai katika taarifa za mtandao huo zilizoripotiwa jana na gazeti la The Guardian la Uingereza kueleza kuwa Rais Kikwete alikuwa anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, na pia madai kuwa anahofia maisha yake kama Mkuu wa Takukuru.

          Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Dk. Hoseah anakiri kukutana na ofisa wa Marekani ofisini kwake Julai 2007, lakini katika mazungumzo yake, anakanusha kuwa hakuna mahali popote alipoeleza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.

          “Nilichosema ni kwamba Rais hataki kuruhusu uchunguzi wa maofisa waandamizi wa serikali au mtu yeyote yule kufanywa kwa kuegemea katika minong’ono au ushahidi dhaifu, kwa sababu kwa kufanya hivyo, serikali inaweza kuwa katika hatari ya kulipa fidia kubwa kama watuhumiwa watashinda kesi mahakamani,” alidai Dk. Hoseah katika taarifa yake jana.

          Kuhusu madai ya ‘hofu ya maisha yake’, alisema anakumbuka kuulizwa na ofisa huyo kama anahofia uhai wake au la, akiwa ni Mkuu wa Takukuru, na kwamba jibu lake lilikuwa rahisi, “ndio, wakati unaposhughulika na vigogo au matajiri, ni lazima uwe mwangalifu na tahadhari na maisha yako.”

          “Lakini hakuna mahali popote nilipotamka kuwa nina mpango wa kukimbia nchi kwa sababu maisha yangu yalikuwa hatarini. Ni jambo la kushangaza kwa mara nyingine, Ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani amenikariri kinyume na ukweli na sijui nia yake hasa ilikuwa nini.”

          Dk. Hoseah alisema kupokea vitisho ni sehemu ya kazi yake kwa sababu anawachunguza watu matajiri na wenye nguvu, lakini kwa kuwa kila kitu kinafanyika kulingana na sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, “hakuna cha kuhofia sana kwa sababu kila kitu kiko katika sheria.”

          Aliihakikishia jamii kwamba ingawa kazi yao ni ngumu, wataendelea na dhamira yao ya kupambana na rushwa katika ngazi zote kwa kushirikiana na wadau wote nchini.

          “Tunaamini kwa pamoja tutashinda vita hii, lakini tukigawanyika, itakuwa kazi ngumu kufikia dhamira yetu.”

          Chanzo: Habari Leo. Pia gazeti la Uhuru.

          BEI YA UMEME JUU MWAKANI KWA ASILIMIA 18.5 !!!

          Bei ya umeme juu mwakani
          (Monday, 20 December 2010)
           
          Nora Damian na Pilly Hashimu  

          MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imeruhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari Mosi mwakani.  

          Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa ongezeko hilo la bei ni chini ya mapendekezo ya Tanesco kwa asilimia 16.1.  Kwa mujibu wa Masebu, Tanesco ilipendekeza umeme upande bei kwa asilimia 34.6, lakini, baada ya uchambuzi wa kina, mamlaka imekubali kuruhusu nyongeza ya asilimia 18.5 kwenye nishati hiyo. 

          "Shirika hilo liliomba kupandisha bei ya umeme kwa miaka mitatu mfulululizo na kwa viwango tofauti kuanzia 2011 hadi 2013, lakini, tumeona kuwa kuna hoja za msingi ambazo haziwezi kutufanya tukubali ombi hilo," alisema.

          Masebu alibainisha kuwa Tanesco iliomba kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 34.6 mwaka 2011, asilimia 13.8 mwaka 2012 na asilimia 13.9 ifikapo mwaka 2013. “Najua kwa uamuzi huu tutakuwa tumewaumiza watumiaji umeme na hatutakuwa tumewaridhisha Tanesco, lakini tumefanya hivyo kwa vigezo ili kufanya sekta iwe endelevu,” alisema Masebu.  Mkurugenzi huyo wa Ewura alisema kuwa ili shirika hilo liweze kujiendesha, linahitaji zaidi ya Sh 691bilioni na uchambuzi walioufanya umeonyesha kuwa ongezeko hilo jipya la bei ya umeme, linaweza kukidhi hitaji hilo.  

          Alisema  pia wameondoa mfumo wa shirika hilo uliokuwa unawapa nafuu wafanyakazi wake kulipia garama za umeme na kuanzia sasa wafanyakazi hao watalipa gharama hizo kama watumiaji wengine.  “Si sahihi wao kulipa pungufu, lazima walipe kama  watumiaji wengine na wasipolipa hata kwenye mahesabu itaonekana,”alisema.  Hata hivyo, alisema watumiaji wadogo wa umeme wasiozidisha kilowati 50 kwa mwezi, wataendelea kusaidiwa na watumiaji umeme mkubwa. 

          Kwa mujibu wa Ewura, bei ya zamani kwa watumiaji hao wa umeme, ilikuwa Sh 49, lakini bei mpya itakuwa Sh60.  Kwa upande wa watumiaji umeme mkubwa zaidi bei ya zamani ilikuwa Sh 2,303 na Tanesco waliomba ipandishwe hadi Sh 3,109, lakini bei iliyokubaliwa ni Sh 2,738 kwa kilowati moja.

          "Tumeamua kuruhusu ongezeko hilo na kama Tanesco wanadhani gharama zao za uendeshaji zinapanda kwa sababu ya ongezeko la gharama za mafuta ya kuzalishia umeme, wanaweza kujenga hoja na tukabadilisha bei ya mafuta pia," alisema Masebu.  Alisema ili kuhakikisha kwamba fedha zitakazopatikana hazitatumika vibaya, wameiagiza Tanesco kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya kuboresha huduma ya umeme.

          "Akaunti hizo zitakuwa zikikaguliwa na Ewura kila baada ya miezi mitatu na fedha zitakazokusanywa zitasaidia pia kununulia umeme mkubwa kwa wazalishaji wengine wa umeme," alisema Masebu na kuongeza:  “Tumewaagiza baada ya mwaka mmoja watueleze mabadiliko haya ya bei yameleta mafanikio gani katika kupunguza hasara.”  Masebu alisema pia kuwa wameiagiza Tanesco ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mabadiliko hayo ya bei, kuwapelekea mkataba ili kujiridhisha kama hautakuwa na madhara kwa watumiaji wa nishati hiyo.

          Mkurugenzi wa umeme katika mamlaka hiyo, Pius Mbawala aliitaka Tanesco kuangalia mifumo ya manunuzi ya vifaa ili kupunguza garama za kuunganisha umeme kwani garama kubwa ni kikwazo mojawapo cha watu kuunganisha umeme.  Alisema pia wameliagiza shirika hilo hadi kufikia mwaka 2011 wawe wameunganisha wateja wapya zaidi ya 100,000, kuwa na idadi ya wafanyakazi inayotosheleza na kuhakikisha umeme unarudishwa mapema baada ya kukatika.

          Chanzo: Mwananchi. Unaweza pia kusoma hapa.

          Sunday, December 19, 2010

          Friday, December 17, 2010

          DO YOU WANT ANOTHER RAP? NA YOWERI KAGUTA MUSEVENI (ROCK RECORDS)

          Rais Yoweri Kaguta Museveni
          ***



          Ubeti wa kwanza (Kutoka Mtandaoni)

          Natema Akati kaarara
          Kaarara nikaza Igara
          Igara owa Ntambiko
          Ntambiko yampa akasyo
          Akasyo nakaha abagyesi
          Abagyesi bampa oruro
          Oruro naruha Warukoko
          Warukoko yampa ihuri
          Ihuri nariha abaana
          Abaana bamp'engyeya
          Engyeya naagiha omukama
          Omukama yampa Kasha
          Kasha nagishweza omukazi
          Omukazi yanzaarira omwana
          Namweeta Mugarura
          Yaagarura eby'ow'ishe n'ishenkuru

          Ubeti wa pili

          Mp'enkoni mp'enkoni mp'enkoni
          Mp'enkoni engarama ziizire
          Ziizire niicund'ebinio
          Ebinio bya Rutendegyere
          Rutendegyere enkuba emuteere
          Emuteerere ahaiguru mpariya
          Ahaiguru hariyo orwitiri
          Orwitire oruzaarwa n'enkura
          Enkura eshoroma etegire
          Etegire akaara k'embogo
          Ak'embogo karimu omwonyo
          Omwonyo guruga Nsharira
          Nsharira omunda y'engoma
          Y'engoma, y'engoma, y'engoma

          Tafsiri ya Kiingereza (Kutoka Mtandaoni)

          Ubeti wa Kwanza

          The stick I cut strayed into Igara where Ntambiko reigns. Ntambiko gave me a knife which I gave to millet harvesters, who gave me millet, that I gave to a hen, which gave me an egg, that I gave to children who gave me a monkey that I gave to the king, who gave me a cow that I used to marry my wife. She gave me a child I called Mugarura who raided back what belonged to me and my fathers. 
          Ubeti wa pili

          Give me my stick! Invaders from Ngarama have arrived, shaking their bums like Rutendegyere. May thunder strike Rutendegyere from above where there is abundance that helps the rhinoceros to thrive. The rhinoceros feeds but reamins ready for a buffalo attack. The buffalo, whose meat is salty. The salt that comes from Nsharira deep inside the kingdom.

          ********

          Asante Mzee wa Mataranyirato kwa kuubandika wimbo huu. Nilikuwa nimesoma habari zake mtandaoni lakini nilikuwa sijawahi kuusikia. Umenikumbusha kisa fulani cha Kisukuma kinachofanafanana na hiki. Tangu hapo madaraka matamu ati!

          FIKRA YA IJUMAA - LEO TUKITAFAKARI KIFO

          Picha hii iko hapa.

          Kutokana na kuondokewa kwetu na Dr. Remmy Ongala - Mwanamuziki mashuhuri aliyeimba nyimbo zilizoigusa jamii mpaka ikambatiza jina la Sauti ya Mnyonge, leo napenda tutafakari juu ya kifo kwa kuyarejelea makala haya niliyoyaandika zamani wakati naanza kublogu.
           
          Wikiendi njema jamani wakati tukimtafakari huyu adui (au pengine niseme rafiki) aitwaye kifo!

          Thursday, December 16, 2010

          WAMAREKANI WANAHAHA KUBORESHA ELIMU YAO INAYOZIDI KUDORORA. TUNAWEZA KUJIFUNZA LOLOTE???

          • Matokeo ya mtihani wa kimataifa yaliyotolewa hivi karibuni kwa wanafunzi wenye miaka 15 yamezua kizaazaa hapa Marekani. Katika matokeo hayo Marekani imeshika nafasi ya 17 katika kusoma, nafasi ya 31 katika hesabu na nafasi ya 23 katika sayansi. Alama ya jumla ya Marekani ikilinganishwa na nchi nyingi zilizoendelea ni "wastani" na kwa ujumla imefanya vibaya. Wanafunzi kutoka Korea ya Kusini, Finland, China, Singapore, Canada ndiyo wamefanya vizuri zaidi wakifuatiwa na nchi zinginezo. Wanafunzi kutoka mji wa Shanghai nchini China ndiyo wanaongoza kwa kupata alama za juu zaidi.
          • Kwa Wamarekani jambo hili halikubaliki kwani wanajua kwamba bila kuwa nambari wani katika elimu, haiwezekani kwao kuendelea kuwa nambari wani kiuchumi na kitekinolojia ulimwenguni; na tayari wameshajiwekea malengo ya kurudi kileleni tena katika masomo yote ifikapo mwaka 2020. Wakiweza kufanya hivi, mahesabu yao yanaonyesha kwamba uchumi wao utaweza kujiongezea dola zipatazo trilioni 41 katika miaka 20 ijayo!
          • Watawezaje kurudi kileleni? Hatua ya kwanza waliyoipendekeza ni kuimarisha taaluma ya ualimu na kuifanya iheshimiwe zaidi ili kuweza kuvutia wanafunzi wenye vipaji. Hii ni pamoja na kuwalipa walimu mishahara mizuri pamoja na marupurupu ya kutosha, kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi na nafasi zinginezo za kujiendeleza. Ripoti hiyo inaonyesha kwamba katika nchi zinazofanya vizuri katika elimu, ualimu si kazi ya kiholela tu. Katika nchi kama Singapore, Finland na Korea ya Kusini, kwa mfano, ni wanafunzi bora pekee ndiyo huruhusiwa kujiunga na ualimu (bofya hapa). Hata katika nchi za Kiarabu mkakati kama huu tayari umeanza kupendekezwa.
          • Nilishangaa kuona kwamba sisi tunafanya kinyume. Kimsingi wale wanaofeli ndiyo tunawabebesha jukumu la kuelimisha taifa huku tukiwalipa mishahara kidogo na kuwafanyisha kazi katika mazingira magumu sana hasa kule vijijini. Na hapa hatujawataja hawa wa"Voda Fasta!". Taaluma ya ualimu haiheshimiwi hata kidogo japo kusema kweli ndiyo mama wa kila taaluma na msingi wa kila taifa lililoelimika. Ndiyo maana kuna kipindi fulani walimu walitishia kugoma na waziri wa elimu wa wakati ule inasemekana alitoa tamko kwamba hata walimu wakigoma hakuna neno kwani anaweza kuokota watu mabarabarani na sokoni wakaingia madarasani kufundisha! Tutawezaje kuwa na elimu bora kama tunadharau taaluma ya ualimu namna hii? Ati, ni kwa nini hawa vijana wenye vipaji wanaopata divisheni wani tusiwape kila kitu ili wavutike na kwenda kusomea ualimu? Au tutakimbilia umasikini wetu na kusema kwamba hatuna pesa na kwamba programu ya aina hiyo haiwezekani?
          • Jambo jingine lilinivutia katika ripoti hii ni hili. Karibu nchi zote zilizofanya vizuri sana zinatumia lugha yake zenyewe kufundishia madarasani. Wachina wana Kichina chao, Wakorea na Kikorea chao, Wafin wana Kifini chao n.k. Na sisi je? Tumeng'ang'ania sera ya lugha ambayo ni kichekesho, sera ambayo kimsingi haiwasaidii watoto wetu kumudu lugha yo yote kitaalamu kati ya zile tunazotumia. Kutokana na kizingiti hiki cha lugha, elimu yetu imebutuka na kuwa zoezi la kukariri tu hata kama hatuelewi hicho tunachokikariri kina maana gani. Hii kweli ni elimu?
          • Kuna mengi ya kujifunza katika ripoti hii. Jambo la msingi ambalo inabidi tulitambue ni kwamba hatutaweza kuendelea bila kuwa na elimu bora inayowakaramsha vijana wetu na kuwafanya wawe tayari kwenda kupambana na dunia pale wanapomaliza masomo yao. Na kuboresha taaluma ya ualimu pamoja na kuwa na sera imara ya lugha ya kufundishia vinaweza kuwa mwanzo mzuri katika kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wetu wa ualimu.

          Wednesday, December 15, 2010

          KABWELA ALIVYOMKUMBUKA NA KUMUAGA DR. REMMY

          • Mimi nilimwona Dr. Remmy nilipokuwa shule ya msingi alipokuja Bariadi kutumbuiza. Nakumbuka ilikuwa majira ya saa nne asubuhi na alikuwa anatembea mjini na wenzake nasi watoto tulianza kuzunguka naye mji mzima. Pumzika salama Dr. Remmy!

          Tuesday, December 14, 2010

          WATANZANIA WA NJE WALALAMIKAJI - NYALANDU

          Watanzania mlioko nje: Dongo hilo la Mh. Nyalandu. Mnajiteteaje?
          ***************

          Nyalandu: Watanzania wa nje walalamikaji 
          (Sunday, 12 December 2010)

          Na James Magai

          NAIBU Waziri wa Viwanda,  Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu, amesema sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wamekua walalamikaji tu kuhusu taratibu za uwekezaji,  lakini hawachukui hatua.

          Nyalandu alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, wakati akizungumza na Mwananchi  baada ya kuzindua Kampuni ya Ndege ya Bold Air, inayomilikiwa na John Ndunguru, Mtanzania anayeishi Marekani. Uzinduzi wa kampuni hiyo, ulifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,  jijini Dar es Salaam.

          “Watanzania waache kulalamika tu kwenye mablog. Wengi wamekuwa walalamikaji tu, lakini hawachukui hatua,” alisema Nyalandu.

          Naibu waziri huyo aliwataka Watanzania hao, watumie muda wa kukaa kwenye mitandao, kuangalia taarifa zinazohusu fursa za uwekezaji zinazopatikana pia hata kwenye mtandao wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania na kusaidia shughuli za  uwekezaji hapa nchini.

          “Kitendo cha kulalamika bila ya kuchukua hatua ni ishara kwamba wengi wao sio wabunifu. Nampongeza ndugu yangu John Nduguru, kwa kutumia fursa hiyo na kuanzisha kampuni hii,” alisema.

          Nyalandu alimpongeza Ndunguru kwa uamuzi wa kuja kuwekeza nyumbani, jambo ambalo alisema litasaidia katika kuinua uchumi wa Tanzania.

          "Pamoja na kwamba Ndunguru amekuwa akifanya biashara zake nchini Marekani, lakini ameona umuhimu wa kuwekeza nyumbani jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi na kutengeza ajira kwa Watanzania wenzake," alisema Naibu waziri.

          Kwa upande wake, Ndunguru aliishauri serikali iangalie na kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za uwekezaji ukiwemo mlolongo mrefu kuhusu mchakato wa uwekezaji.

          Alisema mchakato wa uwekezaji nchini ni mrefu, jambo linalowafanya Watanzania wengi walioko nje, wakate tamaa, na kwamba hiyo inachangiwa na tatizo la kutakiwa kutumia muda mrefu katika kumilisha taratibu za uwekezaji.

          “Tataratibu zetu bado ni ngumu, maana mtu anatumia muda mrefu na gharama na kubwa, jambo linalowakatisha tamaa Watanzania wengi kuja kuwekeza nyumbani," alisisitiza.

          Alisema ameamua kuwekeza katika usafiri wa anga kwa kuwa kuna nafasi nyingi za kufanya biashara na kwamba wakati umefika kwa watanzania, kuachana dhana kwamba huduma ya usafiri wa ndege ni ya watu maalum tu na wenye fedha nyingi.

          “Zamani biashara hii ilitawaliwa na Wahindi na Waarabu ambao walitujengea hisia na dhana kwamba huduma hiyo ni ya gharama kubwa sana na kwa hiyo ni ya watu maalumu tu. Hii si kweli,  hata Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu gharama za usafiri huu,” alisema.

          Kwa upande wake, Nyalandu alisema ni azma ya Serikali ya Awamu ya Nne, kuwaandalia Watanzania mazingira bora ya uwekezaji kama ambavyo imekuwa ikifanya, ili kila Mtanzania aliyeko nje na mwenye uwezo wa kuwekeza, aje kufanya hivyo.

          Alisema kwa sasa serikali iko katika mchakato wa kuangalia mfumo mzima wa kodi za uwekezaji, ikiwa ni hatua ya kuboreesha zaidi mazingira ya uwekezaji, ili kuwavutia wawekezaji wengi wakiwemo wazawa.

          Kampuni hiyo ya Bold imeingiza ndege mbili kwenye soko, moja ikiwa ni ya aina ya Cessna 310 na nyingine aina ya Seneca 1, zote zikiwa na uwezo wa kuchukua abiria sita kila moja kwa wakati mmoja.
          Chanzo: Mwananchi

          BINADAMU (A.K.A HOMO SAPIENS)



          Monday, December 13, 2010

          VYUO 12 VYENYE MAPROFESA "WABOVU" NA WAZURI KABISA HAPA MAREKANI

           Wamarekani wana rekodi za kila aina; na hii ya sasa inahusu vyuo vyenye maprofesa "wabovu" kabisa kama ilivyoainishwa katika tovuti ya kidakudaku ya ratemyprofessors.com. Tovuti hii hutumiwa na wanafunzi kutolea maoni yao kuhusu madarasa waliyofundishwa na maprofesa wa vyuo vikuu na vyuo vingine hapa Marekani na kwingineko. 

          Kulingana na uchambuzi uliofanywa kwa kuegemea zaidi maoni ya wanafunzi katika tovuti hii, vyuo 12 vyenye maprofesa wabovu kabisa hapa Marekani ni kama ifuatavyo:

          1. US Merchant Marine Academy
          2. US Coast Guard Academy
          3. Tuskegee University
          4. Michigan Technological University
          5. New Jersey Institute of Technology
          6. Milwaukee School of Engineering
          7. Bryant University
          8. Bentley University
          9. St. Cloud State University
          10. Rensselaer Polytechnic University
          11. Minnesota State University, Mankato
          12. Western Michigan University

          Kwa upande mwingine Vyuo 12 vyenye maprofesa bora kabisa ni:

          1. Oklahoma Wesleyan University
          2. US Military Academy
          3. Clarke College
          4. Wellesley College
          5. North Greenville University
          6. Master's College and Seminary
          7. Wabash College
          8. Carleton College
          9. Sewanee - the University of the South
          10. Marlbore College
          11. Corban College
          12. Randolp College

          Nami nimejiangalia huko ratemyprofessors.dom na kujikuta nimeshatathminiwa na wanafunzi wanne tu. Kwanza nilitazama tathmini nyingine na nikagundua kwamba kumbe nilikuwa nasoma tathmini ya Matondo mwingine. Kazi kweli kweli!

          Kwa habari zaidi kuhusu mada hii soma hapa na hapa.

          CHADEMA KUNAFUKA MOSHI ???


          ZITTO AWATIKISA CHADEMA
           (Sunday, 12 December 2010)

          Na Boniface Meena

          KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeunda jopo la wazee wa chama hicho, litakalosikiliza maelezo ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, kuhusu mgogoro kati yake na viongozi wenzake ndani ya chama.Imeelezwa kuwa kamati hiyo pia imemtambua rasmi Rais Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi halali na imewaagiza wabunge wa chama hicho, kushiriki katika shughuli zote za kitaifa.

          Jopo hilo la wazee hao wa Chadema, litaongozwa na Profesa, Mwesiga Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

          Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kupitia tiketi ya Chadema, amekuwa katika mvutano na viongozi wenzake ndani ya Chadema, tangu alipopinga hatua ya wabunge wa chama hicho, kususia hotuba ya Rais Kikwete wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi, uliofanyika mwezi uliopita mijini Dodoma mwaka huu.

          Akizungumzia kukutana na Zitto, Profesa Baregu alisema wameamua kufanya hivyo kwa kuwa Zitto ni kiongozi wa chama na anahitaji kusikilizwa.

          Alisema jopo hilo alikataloliongoza yeye, linawashirikisha pia mzee Nyangaki Shilungushela, Dk Kitila Mkumbo na Shida Salum ambaye ni mama yake Zitto.

          "Tunazungumza ndani ya chama, ili kujenga maelewano na kuweka mambo sawa,"alisema Baregu.

          Alipoulizwa kuhusu msimamo wa kamati kuu kumtambua Rais Kikwete, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa hakutaka kuzungumzia hilo na badala yake, alitaka lisubiriwe tamko rasmi la chama litakalotolewa kesho.

          "Nani kasema hivyo, ni vizuri kwa gazeti makini kama Mwananchi mkasubiri taarifa kamili, itatolewa,"alisema Dk Slaa.

          Dk Slaa alisema ni vizuri kusubiriwa tamko hilo ambalo alisema litatolewa katika mkutano wa waandishi wa habari.

          "Sipendi muandike taarifa zisizo rasmi ningependa usubiri hadi keshokutwa (kesho). Kutakuwa na 'press conference (mkutano wa waandishi wa habari)," alisema Dk Slaa ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita, alikuwa mpinzani wa karibu wa Rais Kikwete.

          Juzi, Kamati ya Wabunge wa Chadema, ilimvua Zitto wadhifa wake wa unaibu kiongozi wa upinzani bungeni, lakini chama hicho 'kikapigwa jeki' baada ya mfanyabiashara maarufu, Mustafa Sabodo kukipa Sh150 milioni kwa ajili ya kujenga chuo cha maadili ya uongozi.

          Matukio hayo mawili pia yaliambatana na kuugua ghafla kwa Zitto na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Amur Arfi, ambao walilazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, kwa matatizo tofauti.

          Katika siku hiyo Zitto, alipigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, hatua iliyofanywa na wabunge wa chama hicho katika mkutano wao uliofanyika mjini Bagamoyo, Pwani.

          Wabunge hao pia walimtaka Zitto ajieleze kufuatia kitendo chake cha kupinga uamuzi wa pamoja wa kususia hotuba ya Rais Kikwete.

          Uamuzi wa wabunge hao kumvua uongozi, ulikuwa ukitarajiwa na wengi baada ya Zitto kupinga hadharani kitendo cha wenzake, kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais, alipoanza kuhutubia.

          Hatua hiyo ilikuwa na lengo la wabunge hao kuonyesha kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais,kushinikiza kuandikwa kwa katiba mpya na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

          Uamuzi wa wabunge hao kususia hotuba ya Rais Kikwete, ulifikiwa baada ya mjadala mrefu uliokwisha kwa kupiga kura.

          Zitto na wenzake tisa hawakuingia ndani ya ukumbi wa Bunge siku Rais, alipolihutubia. Baadaye, aliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza kupinga kitendo cha wenzake.

          Baada ya Zitto na wenzake kutoingia kwenye ukumbi wa Bunge ili watekeleze uamuzi wa kutoka nje wakati Rais Kikwete akianza kuhutubia, Katibu Mkuu wa Chadema (Slaa), alisema waliosusia uamuzi huo, wangechukuliwa hatua na Kamati ya Wabunge wa Chadema.

          Baadaye Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, alitangaza kumwandikia barua Zitto na wabunge wengine tisa ambao hawakuingia kwenye ukumbi wa Bunge, kuwataka wajieleze kwa maelezo kuwa walichofanya ni utovu wa nidhamu.

          Wakati taarifa hizo za kuvuliwa uongozi wa Zitto zikibainika, mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alilkuwa ametoka katika Hospitali ya Aga Khan, alikokuwa amelazwa kwa ugonjwa wa tumbo.

          Jana gazeti la Mwananchi lilichapisha habari zilizomkariri Zitto, akidai kuwa ugonjwa huo ulitokana na kula chakula chenye sumu.

          Taarifa zilisema Zitto alilazwa katika wodi namba 57 iliyoko katika ghorofa ya tatu na alikuwa amechukuliwa vipimo vyote ili kutihibitisha kiini cha ugonjwa wake.

          Hata hivyo madaktari katika hospitali hiyo, walisema hawakuona tatizo na kwamba wanasubiri kipimo kikubwa.

          Akizungumza na gazeti hili akiwa hospitalini, Zitto aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu na kuugua kwake kwa kuwa ni ugonjwa wa kawaida na kuwasihi wamuombee apone haraka.

          "Watanzania wasiwe na wasiwasi na kuugua kwangu. Hii ni kawaida tu, madaktari wananipa matibabu niombeeni nipone haraka," alisema Zitto.

          Kuhusu hatua ya chama hicho kumvua madaraka, Zitto, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hajapata taarifa rasmi kutoka chama chake mbali na kusoma kupitia katika vyombo vya habari.

          Alisema hata hivyo, hakuwahi kuomba kupewa wadhifa huo na kwamba ikiwa watu waliomwona anafaa kufanya kazi na kumpa wadhifa huo, wakiamua kumnyang’anya siyo tatizo kubwa kwake.

          “Kwa sasa nadhani suala la afya yangu ndiyo muhimu zaidi. Ngoja kwanza nitoke hapa na afya yangu iimarike na kama kutakuwa kuna sababu ya mimi kuzungumza, nitazungumza,” alisema Zitto:

          “Lakini ikumbukwe kuwa mimi sikuwahi kuomba wadhifa huu, kwa hiyo kama watu walionipa wameamua kunibadilishia, mimi sidhani kama kuna tatizo.”

          Alipoulizwa kuhusu madai ya Zitto kuvuliwa wadhifa ndani ya Bunge, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe,alisema chama kitatoa taarifa baadaye.

          Chanzo: Mwananchi

          JIANDIKISHE HAPA

          Enter your email address:

          Delivered by FeedBurner

          BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO