NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, January 11, 2011

ETI HILI NDILO TAIFA LENYE WATU WANENE KULIKO MATAIFA YOTE DUNIANI !!!

Picha hii inapatikana hapa.
 • Imejulikana kwamba kisiwa kidogo cha Nauru ndicho kinaongoza kwa kuwa na wakazi wanene zaidi kuliko taifa lingine lolote hapa duniani. Kisiwa hiki kidogo kina eneo la mraba la maili 8.1 tu na idadi ya watu wasiopungua 10,000. Hata hivyo, zaidi ya asilimia 95 ya watu wake wazima ni wanene; na asilimia 85 ya wanaume wote ni wanene futufutu (obese). Sasa kisiwa hiki kimebatizwa jina la utani la "kisiwa cha mapandikizi"
 • Kunenepa huku kumetokana na wenyeji wa kisiwa hiki kuacha kula vyakula vyao vya kiasili na badala yake kuanza kufakamia vyakula vya Kimagharibi huku wakiamini kwamba haya ndiyo maendeleo! Matokeo yake sasa karibia nusu ya wakazi wote wanaugua ugonjwa wa kisukari (Tazama pia hapa na hapa).
 • Nilipoisona taarifa hii nikakumbuka nyumbani kwani nasi tumeingia kwenye mkumbo huu na hasa mijini. Sasa tuna supamaketi karibu kila kona na kununua vyakula vya kwenye makopo na nyama zilizotoka viwandani Afrika Kusini ndiyo usasa. Sitashangaa kama baada ya muda tu magonjwa hatari ya Kimagharibi kama kansa na kisukari yataanza kutupukutisha. Japo mimi siyo daktari, huwa nafikiri na kuamini kwamba pengine unene wa mtu anayekula vyakula vya kiasili ni tofauti na ule wa mtu anayekula vyakula vilivyokuzwa na kusindikwa "kisayansi" na kujazwa makemikali kibao.
 • Tazama video hapa ili kuona hali halisi ilivyo kule Nauru. Orodha ya nchi zenye watu wanene zaidi duniani inapatikana hapa na hapa. Marekani imeshika nafasi ya 8,  Misri ni ya 15 na Uingereza ni ya 19.

6 comments:

 1. Matondo kule nyumbani kuna mtori, chapati, supu ya mkia, kitimoto,supu ya ulimi,supu ya kongoro. Hivi vyote vikiambatana na moja baridi moja moto,mwili lazima ufumuke.

  ReplyDelete
 2. Bwana Matiya - Mimi huwa nadhani kuwa pengine kama hiyo mitori, chapati, supu ya mkia, kitimoto,supu ya ulimi na supu ya kongoro yote inatokana na mimea na wanyama waliokuzwa kiasili - bila kushindiliwa makemikali na mahomoni bandia - basi pengine ina uafadhali kuliko ile inayotokana na wanyama wanaozalishwa viwandani. Ndiyo maana pengine unene wa Msukuma au Mbulu wa kijijini anayekula chakula alichokilima mwenyewe bila makemikali unaweza kuwa tofauti na unene wa mdau wa Florida anayefakamia kuku na nyama ya ng'ombe wanaodungwa sindano za homoni na madawa ili wakue kwa wiki sita au miezi mitatu tu.

  Unajua, kwa mfano, wazungu huwa wanashangaa sana kusikia kuwa Wamasai hula mchanganyiko wa maziwa na damu na jamaa wako fit tu bila magonjwa yo yote?

  Vyakula vya Kimagharibi vilivyoenea katika masupamaketi yaliyotanda kila kona mijini kwa sasa ndivyo vitakavyotumaliza kwa kansa, kisukari na magonjwa mengineyo ya Kimagharibi kama hawa jamaa wa kisiwa cha Nauru!

  ReplyDelete
 3. kaka Matondo nasikia sikuhizi nyumbani nako kuku si salama kwani hawa wakizungu wanalishwa madawa hatari na chipsi wanapikia mafuta machafu. Wafanyabiashara wapo kipesa zaidi kuliko utu! Ughaibuni vyakula vya kiafrika bei juu wangu viazi vitamu viwili tu unaambiwa kama $20.000. Je tutafika kweli na tutaweza kuepuka haya yote? Nakubaliana nawe unene wa msukuma wa kijijini si unene wa mtu wa ng`ambo, MUNGU TUBARIKI.

  ReplyDelete
 4. Nauru ipo mahali gani hapa duniani? nisaidieni mwenzenu jiografia imenishinda hapo

  ReplyDelete
 5. Wewe anony wa mwisho. Wakati huu wa google kweli unauliza swali kama hili? Kweli wabongo bado tuko mbali. Basi subiri nitafute ATLASI nije nikuonyeshe hiyo Nauru ilipo. Kweli bado tuna safari ndefu jamani.

  ReplyDelete
 6. hiyo kaka matondo sio hoA SANA, TATIZO SIO CHAKULA BALI LIFE STYLE. SIKU HIZI HATA SERIKALI INAPOTAKA KUWEKA MAKAZI YA WATU HAIZINGATII UWEPO WA ENEO LA WAZI LA WATOTO KUCHEZA NA LA WATU KUFANYA MAZOEZI, SKU HIZI TUNAPANDA GARI MARA NYINGI KULIKO KUTEMBEA KWA MIGUU, SKU HIZI WATU HAWATOKI JASHO NA WANAKWEPA HALI HIYO KWANI INAONEKANA KAMA NI UCHAFU WA MWILI NA NGUO HIVO CALORIES TUNAZOKULA NYINGI HAZITUMIKI KAMA ENERGY BALI ZINAJIKUSANYA NA KUWA CONVERTED INTO FAT,NDIO MAANA TUNA MAJITU MANENE,VILEVILE TUNAKULA VYAKULA VYENYE MAFUTA MENGI TENA NDO VINAAMINIKA KUWA NI VITAMU NA IKITOKEA MTU KAPIKA BILA KUJAZA MAFUTA MFANO WALI ANAONEKANA HAJUI KUPIKA, VILEVILE TUNAMTAZAMO KUWA MTU ANAENENEPA MAISHA YAKE SAFI NA ANAPENDEZA HIVO BASI ILI WATU WASEME UNAISHI VIZURI UNAKULA SANA UNENEPE, MWISHO KUNA WANAWAKE WANANG'ANG'ANIZA WANAUME ZAO WALE SANA KWA KUJIDAI MWANAUME ANAMLO MKUBWA NA IKITOKEA MWANAUME KALA KIDOGO MWANAMKE ANAONA LABDA HAPENDWI AU HAJUI KUPIKA VIZURI HIVO KWASABABU ZA MAPENZI WANAUME WANAISHIA KUWA KULAKULA NA MWISHOWE KUNENEPA HOVYO.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU