NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, January 7, 2011

FIKRA YA IJUMAA: LEO TUTAFAKARI UTAFITI HUU. ATI BINADAMU TUNAZIDI KUWA MAZUZU???

Hoja: Wanasayansi wanasema eti ubongo wa binadamu unasinyaa tena kwa kasi. 

Swali: Binadamu tunazidi kuwa mazuzu? Sasa endelea......

 
Msimbo wa Kiikolojia. Binadamu yupo kileleni!
 • Japo kimaumbile binadamu ni kiumbe dhaifu sana, uwezo wake wa kufikiri, ikiwemo lugha inayomwezesha kuwasilisha mawazo tata dhahnia kumemfanya akifikie kilele cha msimbo tata wa maumbile na kumpa uwezo wa kuwatawala wanyama wengine.
 • Akili na uwezo huu wa kufikiri vinatokana na ukweli kwamba binadamu ndiye mnyama mwenye ubongo wenye ujazo mkubwa zaidi (ikilinganishwa na uzito wake) kuliko wanyama wengine wote. Kwa ujumla kuwa na ubongo wenye ujazo mkubwa ni jambo jema kwa kila kiumbe hapa duniani.
 • Ni kutokana na sababu hizi, wanasayansi wamepigwa na butwaa kugundua kwamba ubongo wa binadamu unazidi kusinyaa na tayari umepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka 20,000 tu iliyopita. 
 • Kulingana na mahesabu ya wanasayansi hawa, asilimia 10 ya ubongo wa binadamu uliopotea katika kipindi hiki kifupi ni sawa na ukubwa wa mpira wa tenisi; na hiki ni kiasi kikubwa sana.
  • Japo wanasayansi hawa hawajui hasa sababu ya ubongo wa binadamu kusinyaa kwa kasi namna hii, wapo wanaodhani kwamba jambo hili si la kushangaza sana hasa ukizingatia kwamba katika dunia ya sasa binadamu hahitaji kutumia akili nyingi ili kuweza kuishi na hata kuzaliana. Kwa hivyo kimsingi, sababu zilizomfanya awe na ubongo mkubwa - mazingira ya kihasama huku akiwa kiumbe dhaifu, sasa zimeanza kupotea na hivyo hakuna sababu tena ya kuendelea kuwa na ubongo mkubwa zaidi. 
  • Je, madhara ya kusinyaa huku kwa ubongo ni yapi?. Inawezekana kwamba binadamu wa leo ameanza kuwa zuzu (zaidi?) pamoja na ukweli kwamba ana Google, Facebook, mtandao na makorokocho mengine ambayo anadhani kwamba yanamsaidia kuendesha maisha yake kwa urahisi zaidi?  Wanasayansi wametatanishwa na bado hawana jibu. 
  • Japo hawajasema utafiti huu umefanyika wapi, mimi nadhani umefanyika katika nchi za Kimagharibi. Kama hivi ndivyo, ningependa kuona kama ubongo wa Waafrika, hasa wale wanaoishi vijijini ambao kimsingi maisha yao hayajabadilika sana, umesinyaa ama la. Wewe una maoni gani? Binadamu!
   • Utafiti huu unapatikana hapa.

    1 comment:

    1. Hii inawezekana kuwa kweli, kwa mtizamo wangu kuwa , mambo mengi yanarahisishwa kwenye mashine, na kwa mfano hesabu ndogo tu mtu anahitaji culculator...ni wazo langu tu mkuu

     ReplyDelete

    JIANDIKISHE HAPA

    Enter your email address:

    Delivered by FeedBurner

    VITAMBULISHO VYETU