NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, January 29, 2011

SHULE ZA KATA ZINAHITAJI MSAADA WA HARAKA !!!

 • Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne (Tazama pia HAPA) yaliyotolewa juzi yanasikitisha. Yanasikitisha kwa sababu, mbali na kuonyesha kwamba kiwango cha kufaulu kimepungua kwa asilimia 22, matokeo hayo yanaonyesha kwamba shule za serikali ndizo zimeongoza kwa kuboronga. Ni kwa sababu hii wasomi na wadau wengine wa elimu, wametoa kauli na kusema kwamba matokeo haya ni janga la kitaifa!
 • Na katika shule hizi za serikali zilizoboronga, shule za kata (mimi huziita majengo ya kata kwani nyingi hazina hata sifa ya kuitwa shule) ndizo zimeongoza kwa kuboronga zaidi. Nimeangalia shule za kata za nyumbani kule Wilayani Bariadi na kusikitika sana. Katika shule nyingi, hakuna mtahiniwa hata mmoja aliyepata daraja la kwanza, la pili na wakati mwingine hata la tatu. Unakuta watahiniwa wachache wamepata daraja la nne, na waliobaki wameambulia "FAILED"
 • Hali hii inaonyesha mambo mawili: Kwanza wanafunzi wa shule za binafsi (ambazo ni ghali sana kwa Mtanzania wa kawaida) ndiyo wamefanya vizuri. Pili - shule za serikali zilizoko mijini zimefanya vizuri ikilinganishwa na nyenzake zilizoko vijijini.  Kwa hivyo, watoto wa masikini - na hasa wale wanaoishi vijijini (ambako ndiko kuna wakazi wengi) ndiyo wanazidi kuachwa nyuma kielimu na kuendelea kuwa tabaka la kudumu la kilalahoi.
 • Hali hii nayo inaibua maswali mengine mazito zaidi. Matabaka haya tunayoyapalilia na kuyaengaenga kwa wakati huu yatakuwa na madhara gani huko mbele ya safari? Kwa kuwanyima elimu bora hawa watoto wa masikini ambao ndio wengi, tunajenga jamii ya aina gani?
 • Ni nani hasa anayetoa amri ya shule hizi za kata kufunguliwa na kuanza kupokea wanafunzi wakati inajulikana wazi kwamba hazina walimu, vitabu, nyumba za waalimu, maabara na vifaa vingine vya muhimu? Naamini mtoa amri huyu (ambaye pia aliniathiri mimi mwenyewe), watoto wake si ajabu wanasoma shule za Kimataifa ndani au nje ya nchi. Ati, kulikuwa na mkakati wo wote kuhakikisha kwamba shule hizi za kata zinapatiwa waalimu na vifaa vya kutosha kabla hazijafunguliwa? Inasikitisha sana kwani hapa tunaongelea maisha ya vijana wetu walio wengi - vijana ambao inaonekana kama vile jamii haiwataki na inawapiga teke na kuwafukuzia mbali. Kuna hata anayejua wanakwenda wapi? Kwa mtindo huu, kwa hakika tunakoelekea zi kuzuri kwani hawa masikini siku wakiamka na kuanza kukariri yale maneno ya Azimio la Arusha..."tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumedharauliwa kiasi cha kutosha...na sasa basi...", hata hawa wafanya maamuzi wanaosomesha watoto wao katika "akademi" za kimataifa hawatakaa wafaidi matunda ya elimu ya watoto wao pendelewa. Na kama hatuwekezi katika elimu, basi tujiandaeni kuwekeza katika magereza!
 • Ni taifa gani linalokaa na kukenua meno huku zaidi ya nusu ya vijana wake wakishindwa kuendelea na elimu ya juu - huku likiwa limekazana kuilipa mabilioni ya pesa  kampuni tata ya kifisadi? Kweli tuko siriazi na maendeleo yetu kama taifa????
 • Ni wakati sasa wa kukaa chini na kufanya upembuzi yakinifu ni kwa nini elimu yetu inazidi kudorora. Kwa vile hatuwezi kuendelea bila kuwa na elimu bora, nguvu zetu zote inabidi tuzielekeze katika kuwapatia elimu bora vijana wetu wote. Badala ya kuilipa Dowans (na upuuzi mwingine), pengine ni vizuri tukazitumia pesa hizo kwa kuanzisha programu maalumu kwa ajili ya walimu watakaokwenda kufundisha katika hizi shule za kata vijijini. Tuwape posho maalumu, tuwajengee nyumba nzuri za kuishi na kuwapatia vifaa ili wachape kazi.

 • Wazazi pia tuhakikishe kwamba watoto wetu wanasoma katika shule zenye angalau mahitaji ya msingi. Inabidi tufike mahali tusimame na kuhakikisha kwamba watoto wetu hawaendi kusoma katika majengo haya ambayo kimsingi yanawaandaa kupata hizi "FAILED!". Inabidi tuwe tayari hata sisi wenyewe kujinyima na kuchangishana; na kuhakikisha kwamba angalau watoto wetu wana vitabu au madawati. Ni wakati wa kuamka na kuwa siriazi na elimu ya watoto wetu!!!

 • Na kwa upande wa serikali, ni vizuri ianzishe mikakati maalumu ya kuzisaidia shule za kata na mahali pa kuanzia ni katika upendeleo katika mgao wa walimu. Elimu ni suala nyeti mno na halipaswi kutazamwa kama suala la kisiasa. Hili ni suala la uhai wa taifa letu!

1 comment:

 1. Matondo, kwa mtindo kwa kilimo kwanza badala ya Elimu kwanza unadhani tutafika mahali tukawa na elimu yenye kukidhi haja na mahitaji ya watanzania wa karne hii!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU