NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, February 5, 2011

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) KIMEFIKISHA MIAKA 34 LEO. KARIBUNI TUSHEREHEKEE + HOTUBA YA J.K. KUHUSU MAFANIKIO YA CCM NA DOWANS


Chama cha Mapinduzi leo kimefikisha miaka 34. Kwako wewe, yapi ni mafanikio makuu ya chama hiki kikongwe nchini mwetu? Chama hiki kinaelekea wapi? Tuna haja ya kusherehekea?

Mwana CCM  wa kesho

(1) Wapo wanaodhani kwamba chama hiki kwa sasa kimepoteza mwelekeo (tazama katuni ya Fede hapa chini). Nadhani hisia hizi zinachangiwa na visa vya kifisadi kama Dowans na Richmond.


(2) Wengine (wakiwemo makada wa CCM wenyewe) wanafikiri kwamba chama hiki kinapita katika kipindi cha misukosuko na hali hii haipendezi; na kushindwa kwa CCM katika majimbo mengi ya ubunge katika uchaguzi uliopita ni ushahidi wa jambo hili. Baadhi ya sekta za muhimu kama elimu na huduma muhimu kama umeme zinazidi kuzorota.

 
(3) Wengine wanasema kwamba chama hiki kimegawika na kuna magenge na mitandao mbalimbali ndanimwe. Pesa ndiyo chanzo kikuu cha migogoro hii. 


(4) Wengine wanadhani kwamba chama hiki kinapita katika misukosuko ya kawaida tu na hakuna haja ya kuweweseka kwani CCM bado hakijapoteza mwelekeo na bado kiko ngangari kama kawaida.


(5) Kwa kuwa chama hiki ndicho kipo madarakani, natumaini kwamba kinatambua kuwa kinayo dhamana ya kuleta maendeleo ya kweli kwa waTanzania wote. Natumaini kwamba kinatambua kwamba hali ya hewa ya kisiasa nchini imeshabadilika na kitaacha tabia yake ya dharau, kujiamini kupita kiasi, kutojali na badala yake kianze kusikiliza kwa makini matakwa ya wananchi wa kawaida, na kuyatimiza. Bado kinayo nafasi ya kujirekebisha wakati kingali na muda madarakani. Vinginevyo......Happy birthday Chama cha Mapinduzi !!!

************************************
Sehemu ya Hotuba ya J.K. Dodoma leo

Kuhusu mafanikio ya CCM

Ni ukweli ulio wazi, tena wa kujivunia, kwamba katika miaka 34 ya uhai wake, Chama chetu kimepata mafanikio makubwa. Kimeendela kukua na kimezidi kuimarika kwa kila hali. Wanachama wameongezeka sana na kufikia takriban *milioni 5.7*. Wanachama wake ni watu wenye umoja, mshikamano na ushirikiano wa hali ya juu pamoja na kuwepo kwa changamoto za hapa na pale kwa nyakati fulani fulani.  

Kwa sababu hiyo, Chama cha Mapinduzi kimeweza kufanya mambo mengi mazuri na ya kujivunia katika nchi yetu. Tumejenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maendeleo yanazidi kupatikana mwaka hadi mwaka. Najua wapo wenzetu wanaopenda ukweli huo usionekane kwa kukuza changamoto za hapa na pale. Hata changamoto hizo tuna uwezo nazo, suala lililopo ni kuwa huwezi kufanya mambo yote wakati mmoja. Hata Mwenyezi Mungu asiyeshindwa na lolote aliumba dunia kwa siku sita na siyo siku moja. Hii inatufundisha kuwa na subira na kupanga vizuri mipango yetu.

*Ndugu Zangu Wana-CCM Wenzangu na Ndugu Wananchi;*

Tembeeni kifua mbele, acheni unyonge, tupo na tutakuwepo. Tutamaliza miaka yetu mitano kwa salama na heshima na tutashinda kwa kishindo mwaka 2015 kwa nafasi zote. Wakati mwingine ninapoona wana-CCM mnakuwa wanyonge kwa matokeo ya uchaguzi uliopita huwa nashangaa sana. Najiuliza kwa nini? Tumemsikia Katibu Mkuu akitueleza kuwa katika uchaguzi wa Rais, mgombea wetu alipata kura *5,276,827* aliyemfuata alipata kura *2,271,942*. Tofauti ya kura *milioni 3* zisizokuwa na ubishi. Kwa upande wa Ubunge wa Majimbo kati ya viti *239*, CCM ilipata viti *187 (78.2%)*, wenzetu wamegawana viti *52* *(21.8%)* kama ifuatavyo:- CUF viti *24 (10%)*, CHADEMA viti *22 (9%)*, NCCR –Mageuzi viti *4 (1.7%)*, TLP na UDP walipata kiti kimoja kimoja *(0.4%) *kila kimoja. Katika Viti Maalum *102*, CCM imepata viti *67* wenzetu wamegawana viti *45*. Katika jumla ya *viti 341*, CCM inavyo *viti 254* na wenzetu wana *87*. Nani mwenye nguvu kubwa?

Kwa nini tujisikie wanyonge baada ya kupata ushindi mnono kiasi hicho? Nadhani tunatishwa na kelele na propaganda za Chama fulani na Bwana fulani ambazo zinajenga hisia kama vile wako wengi sana na wamepata ushindi mkubwa sana hata kuliko CCM. Hilo si kweli, ingawaje safari hii wamepata viti vingi kuliko uchaguzi uliopita. Ukweli ni kwamba Chama hicho kimepata *asilimia tisa tu* ya viti vyote vya Majimbo. Chama chetu, kwa maana ya Viongozi, wanachama na makada, lazima tujipange vizuri kukabiliana na propaganda hizi za wachache. Hali kadhalika, tujipange kimkakati ili uchaguzi ujao viti tulivyowaazima tuvichukue tena wenyewe. Lazima tuazimie sasa kufanya hivyo na kujiandaa kisawasawa kwa ajili hiyo. Wakati wote tusisahau kanuni muhimu ya siasa kwamba *“mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa matayarisho ya uchaguzi mwingine”*. Ndugu zangu huu ndiyo wakati wa kujipanga kwa ajili ya 2015.

Kuhusu Dowans

Jambo ninalotaka kulizungumzia sasa sikutaka kulizungumza kwa sababu Waziri Mkuu alishalifafanua baada ya semina ya Wabunge wa CCM na hata Mheshimiwa John Chiligati, Katibu wa Siasa na Uenezi Taifa alishalizungumzia. Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu hao wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha Wabunge wa CCM.
 
Lakini, yapo maneno mengi ati mbona Rais yupo kimya sana, hatujamsikia kusema chochote? Niseme nini zaidi na hao wote wameshasema kwa niaba yangu. Wapo wanaosema nipo kimya kwa sababu nahusika na Downs na ati ndiyo mwenyewe hasa. Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika. Nawalinda. Kwa sababu hiyo, nikaona nami nisema angalau watu wanisikie lakini sina la ziada ni yale yale yaliyokwishasemwa.

Kwanza niseme wazi kwamba ule msemo wa wahenga wa akutukanae hakuchagulii tusi hapa umetimia. Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu kuwa sina uhusiano wowote wa kimaslahi kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans. Sina hisa zozote wala manufaa yoyote yale. Pia sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama angekuwa ndugu yangu kahusika. Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya Chama ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uogozi wangu. Ni uthibitisho tosha wa ukweli huo. Waliokuwepo kwenye vikao hivyo wanajua ukweli wa haya ninayosema. Ningekuwa na maslahi au hofu tusingefanya uamuzi ule.

*Wana-CCM Wenzangu na Wananchi Wenzangu;*

Kama mtakavyokumbuka tulipoingia madarakani nchi ilikuwa na tatizo kubwa la ukame mkali sana ambao haujawahi kutokea. Mavuno ya chakula yalikuwa mabaya tukawa na njaa kali na watu 3,776,000 walilazimika kuhudumiwa na Serikali. Aidha, mito mikubwa na midogo ikapungukiwa sana maji na mingine kukauka kabisa. Matokeo yake ni mabwawa yetu yote ya kuzalisha umeme yakakosa maji hivyo uzalishaji wa umeme ukaathirika vibaya sana na nchi ilikuwa gizani.

Ili kukabiliana na tatizo hilo ushauri ulitolewa na TANESCO nasi tukaukubali kuwa wakodishe mitambo ya kuzalisha umeme kutoka nje. Serikali tukaombwa kugharamia ukodishaji huo. Taratibu za kisheria zikafanywa, tenda zikatangazwa na washindi wakapatikana Aggreco, Richmond na Alstom. Kampuni za Aggreco na Alstom zilileta mitambo yao kwa wakati lakini kampuni ya Richmond ikawa inasuasua. Wakati huo huo maneno mengi yakawa yanazagaa kuhusu Richmond kutostahili kupewa tenda kwa sababu ya kutokuwa na uwezo kwa kampuni hiyo na kampuni hiyo kutokuwa hai. Ikadaiwa kuwa wamepewa tenda kwa sababu ya kubebwa na baadhi ya viongozi Serikalini. Maneno hayo yalifanya Wizara ya Fedha wasite kutoa fedha za kuanzia kwa kampuni hiyo. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati ule alipokuja kuniomba niingilie kati ili kampuni hiyo ilipwe malipo ya awali (*down payment) *nikataa na kumwambia Waziri aachane nao kwani kampuni hiyo ni ya mashaka. Hivyo kampuni ya Richmond haikulipwa down payment, wakashindwa kutimiza mkataba. Maneno
yakazidi kadri makali ya kukosa umeme yalivyoendelea kuuma.
 
Baada ya hapo kampuni ya Richmond ikauza mkataba wake kwa kampuni ya Dowans ambayo ilileta mitambo na uzalishaji wa umeme ukafanyika na kupunguza kabisa makali ya mgao. Tuhuma kuhusu Richmond ziliendelea kulindima mpaka hatimaye Tume ya Bunge ikaundwa na kugundua kuwa Kampuni iliyouziwa haikuwa hai na ni ya mfukoni. Hatima ya Tume hiyo tunaijua sote. Aliyekuwa Waziri Mkuu na Mwawaziri wawili waliwajibika. Zile tuhuma za yeye kuwa ndiye mwenye kampuni hazikuthibitika lakini aliwajibika kwa sababu yeye ndiye aliyetoa kauli ya kukubali ipewe tenda ili kuepusha nchi isiwe gizani.
 
Miezi kadhaa baadaye, likazuka sakata la Dowans ifutiwe mkataba kwa hoja kuwa wamerithi mkataba na kampuni ambayo haikupata kihalali mkataba wake. Kamati ya Bunge ilisema hivyo na wanasheria wa TANESCO pia walishauri hivyo. TANESCO ikavunja mkataba. Dowans hawakuridhika, wakashitaki kwenye Baraza la Usuluhishi kama yalivyo masharti ya mkataba waliotiliana sahihi. Madai yamesikilizwa na TANESCO imeonekana ni mkosaji hivyo wakatozwa fidia ya Dola za Marekani 64 milioni.  Taarifa hiyo imetushtua wengi. Niliuliza na kupewa ushauri mbali mbali. Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria. Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka katika kulipa. Ndiyo maana ya taarifa ya Mheshimiwa Chiligati na ile ya Waziri Mkuu. Ni mzigo mkubwa mno kwa TANESCO kubeba, hivyo tufanye kila tuwezalo tuepuke kulipa. Tumewataka wanasheria wetu wasaidiane na wale wa TANESCO kuhakikisha hilo halitokei. Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka TANESCO ilipe, hivyo kauli za kuhusika na Dowans inanishangaza maana nisingeamua hivyo katika Kamati Kuu na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi. 

Unaweza kuisoma hotuba yote HAPA

4 comments:

 1. Swali: Mbona hawa viongozi wa CCM hapa wanajiita ndugu wakati everywhere else wanataka waitwe Waheshimiwa?

  Bwana Matondo, hivi na wewe ni CCM? Mbona huelewekieleweki? Nitashangaa sana kama nawe utakuwa CCM.

  ReplyDelete
 2. "Bwana Matondo, hivi na wewe ni CCM? Mbona huelewekieleweki? Nitashangaa sana kama nawe utakuwa CCM"

  Anony: nini cha ajabu kama mi ni mwanachama wa CCM? Nitakuwa nimevunja sheria ya nchi ama? Nifafanulie. Si kila mtu ana uhuru wa kuamini dini anayotaka na kujiunga na chama cho chote cha kisiasa akipendacho? Vipi tena mi nishangawe kwa kuwa mwanachama wa chama kikongwe cha CCM?

  Hata kama ni mwanachama wa CCM, sioni sababu ya kkujitetea!!!

  ReplyDelete
 3. Ndugu yangu Matondo sikutegemea kama ungepata muda wa kuweza kujibu hoja za huyu Anonymous. Tatizo la Tanzania ya leo ina wasomi wengi ambao hawakuelimika, na hii yote ninaamini inachangiwa zaidi na elimu inayopatikana katika shule za sekondari za kata ambazo viongozi waliozianzisha watoto wao wengi wamesoma au wanasoma katika shule nzuri nchini au nje ya nchi. Katika mada zako nyingi, ambazo pia nakubaliana nazo ndio maana unapinga sana kuwepo kwa shule hizi ambazo nyingi hazielimishi bali zinadumaza kizazi cha baadaye kwa kutoa elimu isiyofikia kiwango cha kumjenga kijana ili aweze kukabiliana na dunia ya karne iliyopo na ijayo.
  waswahili wanasema ukibishana na mpumbavu na wewe utaonekana ni mpumbavu au labda umeamua kujibu hoja kwa vile ndiyo taaluma yako katika kuelimisha.
  CCM ya leo siyo CCM ya jana. Kwa maana nyingine, uongozi wa CCM wa sasa unamapungufu zaidi ukilinganisha na uongozi wa CCM ya jana(waanzilishi wa CCM) na kutokana na hili, hata uongozi wa serikali ya sasa unakuwa pia na mapungufu mengi.
  Tanzania ya sasa inahitaji viongozi siyo tu waadilifu bali pia lazima wawe ni wakali katika utekelezaji wa majukumu ya taifa kwa sababu nchi kwa sasa imejaa mapapa wa ufisadi kama Bwana Reginald Mengi alivyodai.
  Mwalimu nyerere alishasema, Tanzania ya sasa ukiona kiongozi ananunua kura lazima tu naye atakuwa amenunuliwa na kiongozi akishanunuliwa, hata utekelezaji wa majukumu ya kitaifa unakuwa umenunuliwa na hapo ndipo mwanzo wa chimbuko la rushwa.
  Ninaamini Mwenyekiti wa CCM na Waziri Mkuu ni watu waadifu, tatizo walilonalo ni kutokuwa wakali na hii inanipelekea kuamini kuwa labda midomo na mikono yao imefungwa.
  Ninaamini CCM ya sasa itakuwa na watu au viongozi waliojaliwa uwezo wa kusoma nyakati ambao ndiyo watakaoinusuru isibomoke kutokana na nyufa zinazoendelea kutokea siku baada ya siku.
  Inanishangaza kuona bado kuna watu au viongozi ndani ya CCM wanaodiliki kuandika hotuba wakidai wamevikopesha vyama vya upinzani viti ya ubunge. Kweli!!!
  Mwalimu Nyerere alinyambulisha haya yote katika kitabu chake cha uongozi wetu na hatima ya Tanzania.

  ReplyDelete
 4. Ng'wanaMwamapalala. Blogu ni shule na kuna mambo ya muhimu sana ambayo nimeshajifunza tangu nianze kublogu. Niliamua kumkumbusha tu huyu mdau kuhusu haki za kikatiba za kila Mtanzania - kuamini dini anayotaka na kufuata itikadi yo yote aitakayo ali mradi havunji sheria. Na hili ni jambo la muhimu kukumbushana mara kwa mara.

  Kama kawaida yako, maoni yako hapa ni ya kina na yenye kufikirisha. Baada ya kuisoma hotuba ya J.K. mimi nadhani bado CCM haijakaa chini na kufanya tathmini ya kina kuhusu sababu zilizoisababishia msukosuko katika uchaguzi uliopita. Bado hakijasikia kilio cha wananchi hasa wanataka na wamechoshwa na nini. Kuna mambo yaliyosemwa katika hotuba hii ambayo kidogo yanashangaza. Kuhusu hoja zaidi juu ya jambo hili tazama makala na maoni ya wadau mbalimbali katika blogu ya gazeti la Majira:

  http://majira-hall.blogspot.com/2011/02/jk-achochea-moto.html

  Wabeja!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU