NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, February 4, 2011

FIKRA YA IJUMAA: "KAMA HAWANA MIKATE SI WALE KEKI?" SWALI: KAMA HAWANA KEKI WALE NINI ???

Mmachinga wa kike akiburuzwa na wanamgambo wa jiji la Dar. 
Picha kutoka Mzee wa Sumo
************************ 
 • Ulikuwa ni mwaka 1789 nchini Ufaransa. Wafanyakazi wa kawaida na watu wengine wa tabaka la chini walikuwa wamechoka na utawala mbovu wa mfalme wao Louis XV. Maisha yalikuwa magumu sana, wengi hawakuwa na kazi na kulikuwa na upungufu mkubwa wa chakula.
 • Wananchi hawa wa tabaka la chini waliamua kuandamana na lalamiko lao kuu mojawapo lilikuwa ni ukosefu mkubwa wa chakula (mikate) na uongozi mbovu na dhaifu wa mfalme wao. Inasemekana kwamba mke wa mfalme Louis XV, Malkia Marie Antoinette, alipowasikia waandamanaji hawa alishangazwa sana na madai yao ya chakula; na inasemekana alitamka kwa kejeli "kama hawana mikate si wale keki?"
 • Kauli hii ya dharau ya malkia huyu (ambaye yeye pamoja na mume wake baadaye waliuawa kwa kunyongwa), imekuja kuwa kielelezo kizuri cha viongozi "vipofu" wanaoishi peponi wakati watu wanaowaongoza - umma wa wakulima na wafanyakazi, ukiishi katika jehanamu ya ukosefu wa ajira, maji safi na salama, elimu bora, huduma bora za afya, miundo mbinu na matatizo mengine mzomzo. 
 • Ukipita vijijini na kuona umasikini wa kutisha uliotamalaki huko daima hutakosa kujiuliza kama kweli watawala wetu wanayaelewa kwa undani matatizo ya wananchi wao. Utazidi kuchanganyikiwa zaidi utakaposikia kashfa mbalimbali za kifisadi, kashfa zinazotafuna mabilioni ya shilingi ambayo kama yangetumiwa vizuri yangeweza kuinua maisha ya wananchi hawa waliosahaulika na kutatua baadhi ya kero zao za msingi.
 • Watawaliwa hawa masikini hufika mahali wakachoka na kusema liwalo na liwe. Hivi ndivyo alivyofanya Mohamed Bouazizi, mmachinga wa Tunisia aliyewasha moto wa mapinduzi ya Jazmine  yaliyomfurusha rais wa nchi hiyo na hatimaye kusambaa katika nchi nyingine za Kiarabu. Baada ya kunyang'anywa bidhaa zake na wafanyakazi wa halmashauri, mmachinga huyu alibakia na deni la zaidi ya dola 200 na hakuona njia nyingine isipokuwa kujichoma moto ili kuelezea kukata tamaa kwake.
 • Naamini kwamba watawala wa bara la Afrika wamejifunza kitu katika kisa hiki cha Mohamed Bouazizi na kilichofuatia baadaye. Ni lazima wajibidishe kuyatambua matatizo ya wananchi wanaowaongoza na kujaribu sana kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Ni lazima waache dharau, kutojali, kujiamini kupita kiasi na kuepuka ufisadi na ufujaji wa mali za umma kama vile ni zao binafsi. Inabidi watambue kwamba mtu asiye na mkate wala keki, mtu aliyefikia hatua ya liwalo na liwe, mtu ambaye hawezi kumsomesha mtoto wake, mtu ambaye hana matumaini ya maisha huwa haogopi risasi ya moto, mabomu ya kutoa machozi, mipira ya maji, bakora, pingu wala silaha yo yote ile!!!

1 comment:

 1. Wanamgambo wenyewe hawa ni darasa la saba. Masikini hawajui kwamba na wenyewe ni victims wa system kama huyu mwenzao wanayemburuza.

  Huyu binti anajaribu kujitafutia ridhiki kwa njia ya halali anafanyiwa hivi kama jambazi. Pengine wanataka awe changudoa.

  Huyu mwendesha baiskeli ya miguu mitatu naye kavaa chupi ya arsenal. Duh!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU