NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, February 11, 2011

NAKUMBUKA SIKU MADAKTARI NA WAHUDUMU WALIPOKUSANYIKA KWA MSHANGAO ILI KUANGALIA MENO YA MTU MZIMA MBAYE ALIKUWA HAJAWAHI KWENDA KWA "DENTIST "!!!

Hapa ni zamani kidogo enzi zileeee !!!
 • Ilikuwa ndiyo kwanza tu nimefika kuanza shahada yangu ya Uzamili (Masters) katika Isimu (Linguistics) kutoka katika Chuo kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Baada ya kugundua kwamba bima niliyokuwa nayo ilikuwa inaruhusu mpaka matibabu ya meno basi niliamua kwenda katika kliniki ya meno.
 • Katika fomu mojawapo niliyotakiwa kujaza pale ofisini ilikuwa inauliza ni lini kwa mara ya mwisho nilipata kusafishwa meno na daktari. Niliiacha nafasi hiyo wazi kwani katika maisha yangu yote nilikuwa sijawahi kwenda kwa daktari wa meno eti kwa ajili tu ya kusafishwa meno!
 • Basi wakati nimelazwa tayari kwenye kiti, na daktari tayari yupo anakagua meno yangu yaliyokuwa yamepigwa X-ray, niliulizwa tena kama nilikuwa nimeshawahi kwenda kwa daktari wa meno ili kusafishwa meno. Nilimwambia daktari yule kwamba "nyumbani kwetu" yaani vijijini Afrika watu huenda kwa madaktari wa meno kama jino linauma na kama linataka kuong'olewa. Nilimwambia kwamba siye huwa hatuendi kwa madaktari wa meno eti kusafishwa meno!
 • Basi madaktari wote na wahudumu waliitana na kuanza kuonyeshana meno yangu katika X-ray. Wengi walishangaa sana baada ya kugundua kwamba meno yangu hayakuwa na mianya (cavity) wala matatizo mengine makubwa mbali na madoa doa tu ya kawaida. Waliniuliza chakula ambacho nilikuwa nakula, vinywaji, mvinyo na vinywaji vingine ambavyo nilikuwa natumia.
 • Basi daktari yule alinisafisha meno yangu na akaniambia kwamba alikuwa na bahati ya mtende kwa kusafisha meno ya mtu mzima ambaye ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda kwa daktari wa meno kwa lengo hili. Mpaka leo huwa nawaza mara mbili mbili kama kweli ni lazima niende kusafishwa meno yangu kila baada ya miezi sita. Na ndiyo maana huwa nazitilia shaka tafiti nyingi zinazofanywa katika nchi za Kimagharibi kama kweli zinaakisi hali halisi katika jamii zetu za Kiafrika (mf. hatari za unene).
 • Ati, kama wewe ni mtoto wa mkulima, ni lini ulienda hospitalini kwa ajili tu ya eti kusafishwa meno ambayo wala yalikuwa hayakuumi? Na inawezekana ni kweli unafikiri kwamba wakati mwingine kutojua tatizo yaweza kuwa sehemu ya suluhisho la tatizo ama!

5 comments:

 1. Duuh, kusafisha meno...huku bwana mpaka liume na unakwenda pale unaona ni la kuong'oa...!

  ReplyDelete
 2. Ndugu yangu Matondo unanikumbusha kitambo kidogo.
  Hata mimi yalinitokea kama ya kwako. kisa changu ni baada ya jino langu kuanza kunisumbua, niliamua kwenda kumuona daktari wa meno katika zahanati binafsi London. baada ya kuingia kwenye chumba cha mganga ambaye alikuwa mzungu na kusalimiana naye, aliniuliza nina tatizo gani, nami nikamwelezea kwamba jino langu linanisumbua sana na sikupata usingizi kabisa, naye akaniambia nilale kwenye kiti ili akague meno yangu. baada ya kuangalia meno yangu, akaniuliza ni lini mara ya mwisho nilisafishwa meno yangu. sikulielewa swali lake kwa vile nilikuwa sijui kama unaweza kwenda kwa daktari kusafishwa tu meno. nikamuuliza ana maana gani, baada ya kunifafanulia swali lake, nilimwambia sijawahi toka nizaliwe. aliniangalia kwa macho ya mshangao na simanzi na mimi nikajiuliza kwa nini anashangaa. Nilimwangalia pia kwa macho ya mshangao na kumweleza kuwa sisi kijijini kwetu watu wanakwenda kumuona daktari pindi wanapokuwa na matatizo ya meno na ni mala yangu ya kwanza kusikia kama ninatakiwa kusafisha meno mara kwa mara.
  Bada ya kunitibu akanishauri baada ya miezi sita niende tena kusafisha meno yangu, niliondoka nikijisemea ama kweli kutembea kuona mengi. kwa sasa kila baada ya miezi sita ninapata barua ikinikumbusha lakini sijawahi kurudi tena.
  Tafiti nyingi hasa zinazohusu miili ya binadamu huwa hazitoshelezi, badala yake zinaweka ''blanketi'' kwa kila binadamu kama ni mmoja bila kujali tabaka na mazingira aliyopo au aliyokulia yanavyoweza kuathiri mwili wake. Huwa sishangai sana nikiona kila mara serikari ikipiga marufuku utumiaji wa madawa fulani baada ya kugundulika yana athari au hayana nguvu za kutibu magonjwa baada ya kipindi fulani kwa vile mara nyingi tafiti zinakuwa zimefanyika kwa watu wa tabaka au mazingira fulani tofauti na nyumbani.

  ReplyDelete
 3. haaaaa kama halijauma utaenda kutafuta nini?na tulikuwa tuishi na wanaishi mpaka leo!tena walipoanza mchezo wa kuyachokonoa ndiyo wameniletea ubovu!!!!
  kaka hiuyo picha ulipiga ilala au magomeni?

  ReplyDelete
 4. Ni kweli hatuna taratibu za kuwaona madaktari wa meno ambao kwa nchi za wenzetu ni watu muhimu sana na kazi yao inalipa san. Mimi nikiwa mwanafunzi chuo kikuu mlimani nilikwenda Mhimbili kwa ajili ya tatizo la jino, lakini huko nilikutana na dokta mwanafunzi toka Uganda ambaye aliniambia kwamba meno yangu yalihitaji kusafishwa, alinisafisha japokuwa shida yangu ya mwanzo haikuwa kusafishwa meno. Huduma hii hata kwetu ipo isipokuwa kwakuwa huwa hatucheck afya zetu na tunakwenda hospital tunapokuwa wagonjwa basi tunaishi kwa kudra za Mungu.

  Ikiwa memo hayakusafishwa vizuri basi huweka utando fulani ambao huwa mgumu kama cement ambao husababisha upigapo mswaki meno kutoa damu na kinywa kutoa harufu mbaya.

  Tatizo lingine ni uduni na uchache wa huduma za afya pengine pia kipato uchangia na watu kulazimika kufanya mambo mengine ambayo wanafikiri ni muhimu. Bima ya afya ndo usiseme kwani hata huduma ya meno na macho haipo

  ReplyDelete
 5. Ng'wanaMwamapalala - kisa chako kinafanana na changu. Yapo mambo mengi ambayo hawa jamaa wanafikiri kwamba ni ya muhimu sana kumbe kwetu sisi wala hatuyajali sana - na watu wapo tu wanaendelea kuishi - pengine kwa kudra za Mwenyezi Mungu kama alivyosema anony. wa mwisho.

  Swahili na Waswahili - "tena walipoanza mchezo wa kuyachokonoa ndiyo wameniletea ubovu!!!!" Oh, pole. Au tuseme pengine wakati mwingine kujua tatizo pia yaweza kuwa tatizo!

  Hii picha ni ya Uswahilini Temeke Mwisho enzi zile nikisoma Mlimani. Maisha!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU