NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, February 13, 2011

SERIKALI YAPOTEZA SH. BILIONI 24 ZA MADINI KWA MWAKA MMOJA !!!


Ati, shilingi 24,000,000,000 zingetusaidia kutatulia matatizo mangapi yanayowakabili watu wetu na hasa kule vijijini? Ati, shilingi 24,000,000,000 zingeweza kuchimba visima vya maji vingapi? Ati, shilingi 24,000,000,000 zingeweza kununua madawati mangapi? Ati, shilingi 24,000,000,000 zingeweza kujenga nyumba ngapi za walimu? Ati, shilingi 24,000,000,000 zingeweza kujenga vituo vingapi vya afya? Ati, shilingi 24,000,000,000 zingeweza ku........Kwa hakika matatizo yetu mengi ni ya kujitakia tu !!!

****************************
Serikali yapoteza Sh24 bn za madini mwaka mmoja

Friday, 11 February 2011 20:57

(Fidelis Butahe na Hussein Issa)

RIPOTI ya kuchunguza ulipaji kodi serikalini kwa kampuni za madini (Teiti), iliyofanywa na Kampuni ya BDO ya Afrika Mashariki, imeonyesha kipindi cha mwaka mmoja, serikali imepoteza Sh24 bilioni.

Fedha zinazoonyeshwa kuwa zimekusanywa kutoka kampuni 13 kuanzia Julai 2008 hadi Juni 2009. Baadhi ya kampuni hizo za madini, ni Geita, North Mara, Buzwagi, Bulyanhulu, Tulawaka, Tanzanite One, Williamson Diamonds Ltd,  El- Hillal na Pan Africans Energy.

Ripoti hiyo imetolewa baada ya Tanzania kujiunga kwenye umoja wa nchi zinazofanya uchunguzi wa kodi sekta ya madini (Teiti), huku Mwenyekiti wa tawi la Tanzania (MSG), Jaji Mark Bomani, akisema uchunguzi huo umefanyika kutokana na kuwepo kwa hisia kuwa, sekta ya madini haichangii kwa kiasi kikubwa pato la taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa BDO, Jovinal Betambira, alisema kipindi hicho cha mwaka mmoja, kampuni hizo zinadai zililipa Sh89 bilioni kama kodi, huku serikali ikisema imekusanya Sh64 bilioni. Awali, akipokea ripoti hiyo, Bomani alisema lengo kubwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye usimamizi wa sekta ya madini, mafuta na gesi asilia nchini.

Jaji Bomani alisema mpango huo wa kufuatilia mapato yote yanayopatikana kutoka sekta hizo, ulianza rasmi mwaka 2009 Tanzania ilipojiunga na umoja huo ambao unajumuisha nchi zisizopungua 30.

Alisema malengo ya mpango huo, ni kuwajibika kikamilifu kufuatilia malipo yote yanayopatikana kwenye sekta hiyo kama yanafika sehemu husika. Alisema lengo jingine ni kutizama upungufu kwenye ukusanyaji kodi na kuongeza kuwa, sehemu ambazo zitaonekana kuwa na tatizo zitafuatiliwa ili kupata ufumbuzi.

“Serikali ilianzisha MSG, chombo hiki kimepewa jukumu la kuhakikisha kinatekeleza yote yanayotakiwa na Teiti, MSG ina wajumbe watano kutoka serikalini, watano kutoka kampuni za madini na watano kutoka vyombo mbvalimbali,” alisema Jaji Bomani. Jaji Bomani alisema kupitia mpango huo sheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka taratibu.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU