NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, February 22, 2011

"SIACHII MADARAKA WALA SIONDOKI, NITAKUFA KAMA SHAHIDI WA LIBYA, WAANDAMANAJI WANAWEWESEKA KUTOKANA NA KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA..." - GADHAFI

 • Huku kiti cha madaraka alichokalia kikiwa kinawaka moto unaochochewa na maovu ya udikteta wa miaka zaidi ya 40 madarakani, Moammar Gadhafi ama ni mgonjwa au hajaelewa kinachoendelea. Katika hotuba yake ya kipayukaji iliyomalizika muda si mrefu uliopita ametoa matamko ya kushangaza - yakiwemo hayo juu. Huku akiwa mwenye hasira na akigonga meza kwa ngumi, amewaita waandamanaji kuwa ni "mbwa" na akawaonya kwamba wakae chonjo kwani bado hata hajatoa amri ya risasi ya moto hata moja kufyatuliwa; na akitoa amri hiyo basi Libya nzima itawaka moto. Ameendelea kusema kwamba yeye ni shujaa na kwamba ataipigania Libya mpaka tone lake la mwisho la damu!
 • Ametoa mwito kwa wanaomuunga mkono kujitoa mhanga kuanzia kesho na kujitosa mabarabarani ili kupambana na waandamanaji wanaoipinga serikali yake. Ili kujipambanua na wapinga serikali, inabidi wavae "bangili" za kijani katika mikono yao.
 • Amewauliza waandamanaji swali la Kitashtiti kwamba "nini kimewapata? Mbona tulikuwa tunaishi katika ustawi?" Kwa habari zaidi soma HAPA.
Sikiliza sehemu ya hotuba hiyo hapa chini

6 comments:

 1. Walibya inabidi watumie nguvu za ziada kulitoa hilo joka pangoni mwake, ni joka lenye sumu kali kwa hivyo zitahitajika mbinu kali kukabiliana nayo. Nadhani hata ndani Libya yapo makundi mengi ambayo bado wanamkubali Gaddafi kwasababu ya misimamo yake dhidi ya nchi za magharibi.

  Lakini pia tukumbuke kama si uroho wa madaraka, Gadaffi kwa takribani miaka 42 ya uongozi wake, sijui kama kweli alishindwa kumwandaa mtu ambaye angeweza kurithi viatu vyake, kama kweli lengo lake ni kulinda utaifa wa Libya.

  ReplyDelete
 2. Pamoja na yote, kipengele cha madawa ya kulevya nacho kina ukweli. Hata kwetu, wengi wanatumia madawa ya kulevya, achilia mbali gongo, wanzuki, na rubisi. Wote hao wako sana mitaani.

  Ikitokea kuna maandamano, nao wanajumuika. Hilo halikwepeki. Na vibaka nao wanakuwepo. Ukweli huo unaelezwa katika usemi kuwa kwenye msafara wa mamba na kenge nao wamo.

  Labda hii inaweza kuwa sababu moja kwa nini polisi wa kwetu wanayaogopa maandamano na wanataka waweze kujihusisha katika kuyapangia utaratibu.

  Kila suala lina vipengele vingi, na pamoja na vile vipengele ambavyo tunavisikia kutoka kwa vyama vya siasa, au matamko ya masheikh au maaskofu, ni muhimu kipengele hiki cha madawa ya kulevya nacho kiwemo katika tafakari na mijadala yetu.

  ReplyDelete
 3. Bwana Matiya. Ni kweli huyu jamaa alikuwa ndiye Fidel Castro wa Afrika kwa tabia yake ya kutotishwa na mataifa ya Kimagharibi; na mawazo yake juu ya Muungano wa Afrika pengine hayakuwafurahisha wakubwa.

  Hata hivyo miaka 42 madarakani ni mingi mno na inasikitisha kuona kwamba hajaweza kusoma alama za nyakati na kuona kwamba mambo yamebadilika.

  Sasa anatumia ndege za kivita kuwatisha raia zake. Kwa nini ni vigumu sana kuachia madaraka na kuondoka kwa heshima? Kama aliyoyasema katika hotuba yake hii isiyoeleweka ni ya kweli basi ni wazi kwamba moto utawaka Libya!

  Profesa Mbele - hili la madawa ya kulevya nilikuwa sijalifikiria kwa kiwango hiki na muktadha huu.

  ReplyDelete
 4. Profesa Matondo, ni kweli kuwa tunapoongelea masuala haya, huwa vitu kama hivi vya madawa ya kulevya hatutaji. Lakini ukweli ndio huo, kwamba mitaani mwetu kuna wavuta bangi, vibaka, na wateja wa ulabu. Ukipita mdundiko, nao wanajumuika. Ikitokea ajali nao wanawahi, si kuokoa majeruhi, bali kusachi mifukoni mwa waathirika. Ikitokea kufukuza mwizi, nao wanajumuika. Yakipita maandamano ya chama cha siasa, hakuna anayewachunguza na na kuwazuia.

  Tatizo ni kuwa taarifa zinapotolewa, kuhusu maandamano ya kisiasa, kwa mfano, tunachoambiwa ni kimoja tu, kwamba wanachama wa chama fulani wameandamana. Inakuwa kama vile wananchi wengine wote wanakuwa wameondoka katika mitaa hiyo, wakati hii si kweli. Wananchi wanaendelea na shughuli zao katika mitaa hiyo hiyo. Ushahidi wa hilo ni kule Arusha, ambako kati ya watu waliouawa na polisi kwenye hayo yaliyoitwa maandamano ya CHADEMA, kulikuwa na raia wa Kenya ambaye si mwana CHADEMA.

  ReplyDelete
 5. Hakutaka kung`atuka mwenyewe ili alinde heshima kiasi maana hana hiyo heshima wala Hekima!.

  ReplyDelete
 6. Halafu huyu baba du, miaka zaidi ya 40,bado hataki kuondoka, halafu anaonekana katili hata ukiangalia sura yake.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU