NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, February 28, 2011

WAZIRI WA ELIMU AZUNGUMZIA SEKONDARI ZA KATA

Nimefurahi kusikia kwamba angalau kuna mikakati mizuri ya kuziimarisha shule za Sekondari za Kata. Fuatilia kauli za Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Dr. Kawambwa hapa chini.

**********


Dk Kawambwa akiri sekondari za kata kuchangia matokeo mabaya

Venance George, Morogoro

SERIKALI imekiri kuwa matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu unaozikabili sekondari za kata.

Akizungumza kwenye mahojiano na Mwananchi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alikiri matokeo hayo kutoifurahisha serikali.

Dk Kawambwa alisema kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na changanoto zilizoko sekondari za kata. Alisema sekondari za kata zilizoanza kujengwa mwaka 2006, zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, miundombinu, walimu, maabara na vifaa vingi vya utendaji kazi.

“Matokeo yake tunafika mahali wanafunzi wanamaliza kidato cha nne, kwa sababu ya upungufu mbalimbali ambao umejitokeza shule zetu hasa za kata ambazo ni idadi kubwa, tukapata matokeo ambayo sio mazuri, asilimia 49 ya vijana wamefeli kabisa,” alisema Dk Kawambwa.

Dk Kawambwa alisema kuwapo kwa upungufu wa walimu na vitendea kazi, matokeo yake ni kutopata matokeo mazuri kama ilivyojitokeza mwaka jana, serikali ilijikita zaidi ujenzi wa shule.

Alisema hatua ya kwanza ilikuwa kuhakikisha ujenzi wa shule hizo unakamilika, inayofuata ni kuimalisha madarasa ambayo yalikuwa hayajakamilika.

Waziri Kawambwa alisema programu ya serikali iliyoanza mwaka 2010 mpaka 2015, itahakikisha lengo linatimia la kuwa na vifaa, maabara, vitabu, maktaba na kuajiri walimu wa kutosha.

Alisema hivi sasa wanakabiliana kumaliza upungufu wa walimu 43,000 na kwamba, kupitia programu hiyo serikali imeanzisha kozi za ualimu vyuo vikuu, huku vingine vikibadilishwa kuwa vyuo vya ualimu.

Aliongeza kuwa kila mwaka vitakuwa vikizalisha wastani wa walimu 10,000 hadi 15,000, hivyo kuweza kumaliza tatizo la walimu ndani ya miaka mitano.

Kuhusu tatizo la vitabu vya shule, Dk Kawambwa alisema tayari serikali imesambaza vitabu 800,000, huku 2,250,000 vikitarajiwa kupokelewa na kusambazwa kwenye sekondari nchini.

Alisema serikali imekopa dola 1,050,000 za Marekani kutoka Benki ya Dunia (WB) kuboresha miundombinu ya elimu sekondari za kata na kuweka vitendea kazi.   

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU