NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, March 5, 2011

DR. SLAA AFANANISHWA NA SAVIMBI. CCM WAITAKA DOLA IWADHIBITI CHADEMA !

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati...

“Hatutaki usavimbi hapa. Dk. Slaa akubali ameshindwa uchaguzi na ajipange kwa uchaguzi ujao kwa kuboresha sera za chama chake si uchochezi na uzushi dhidi ya Rais aliye madarakani,” alisema Chiligati. 

Alisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuenzi urithi ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambao ni amani na utulivu. 

Chiligati alitumia nafasi hiyo kuiomba dola iwadhibiti Chadema akidai kwamba wanataka kuifanya nchi isitawalike.

********************************
 • Pamoja na mikakati hii ya CCM ya kutaka dola iwadhibiti wapizani wao hawa, inabidi pia (CCM) wakae chini na kujiuliza kwa makini sana ni kwa nini Chadema kimegeuka na kuwa "tishio" namna hii.  Ati, ni kwa nini wananchi wanajitokeza kwa maelfu na maelfu kwenda kuwasikiliza hawa Chadema? Kwa nini Chadema wameibuka kuwa na mvuto sana hasa kwa wananchi wa hali ya chini? Je, kutumia nguvu za dola ndiyo njia sahihi ya kuzima vuguvugu hili? CCM inabidi wafikirie kwa makini sana kero zinazowakabili wananchi na wapambane nazo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. 
 • Mimi nadhani kwamba "tatizo" hapa siyo Chadema bali wananchi ambao wamechoshwa na ugumu wa maisha unaowakabili. Wanakerwa sana na ufisadi unaoitafuna nchi waziwazi wakati hawaoni mabadiliko yo yote chanya katika maisha yao. Wanakerwa na huduma mbovu za msingi kama vile afya, elimu na umeme. Wanakerwa na ahadi hewa nyingi wanazopewa na wanasiasa wakati wa uchaguzi. Wamechoshwa na uzembe, wamechoshwa na.....
 • Njia nzuri na bora kabisa ya kupambana na Chadema ni kusikiliza kero za wananchi hasa hawa wa tabaka la chini na kuzitatua. Kufanya vinginevyo ni kujidanganya tu. Na itakuwa vizuri sana kama CCM watasikiliza mapendekezo ya kutumia hoja za kisiasa badala ya nguvu za dola kama ilivyopendekezwa na Mh. Sumaye HAPA.
Heri yule asomaye alama za nyakati na kuzielewa.

Mungu Ibariki Tanzania !!!
************************

Huu ni muda mzuri kwa CCM kujitathmini.

6 comments:

 1. Slaa ni Savimbi wa Ufisadi, hivyo huyu kapteni wa jeshi mstaafu bwana Chiligati hajakosea kabisa. CCM lazima waelewe kuwa huu wimbo wa amani si njia mbadala ya kuwatuliza wana mageuzi.Wavunjaji amani wakuu Tanzania ni vyombo vya dola na wala siyo Chadema.

  ReplyDelete
 2. Chiligati anafanya dhihaka au usanii kumtaja Mwalimu Nyerere kwa namna anavyofanya, kwani CCM hii hii ilimpa taabu sana Mwalimu Nyerere, hadi akatutahadharisha wa-Tanzania kuhusu CCM. Soma hapa.

  ReplyDelete
 3. Watamuita majina yote watayamaliza lakini ukweli utasemwa, mambo ya kuwadanganya wananchi kuwa eti nchi ina amani wakati watu wanashindia mlo mmoja,hawana pesa za matibabu,hawana umeme,hawana maji ,shule hazina walimu,madarasa hayana viti watoto wa masikini wanasoma huku wamekaa chini,ujambazi unaongezeka,rushwa imetawala kila kona watu wananunua haki zao. Tena sasa CCM inajaribu kutuchonganisha kwa kusingizia Dini, kila jambo linamwisho,wananchi wamechoka. Walisema tupuuze yote yanayosemwa na CDM sasa kwanini wanaanza kuogopa. kumekucha hatudanganyiki tena watanzania tumeamka usingizini.

  ReplyDelete
 4. Asante Prof.Mbele kwa kututoa matongotongo kwa kutuelezea wazi jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa mtabiri, nimetembelea blog yako,ila nimeshindwa kutuma huu ujumbe, hakika Baba huyu alikuwa na unabii wa hali ya juu. Tunaona wazi kabisa Kansa hii inavyotafuna nchi yetu kwa kasi kubwa, Kumbe na Mwalimu alitamani kuwepo na chama mbadala wa CCM,ilimradi tu kiwe thabiti, aliyosema yote muda si mrefu yatatimia.

  ReplyDelete
 5. Penye ubovu shurti wenye upeo, uelewa, ujasiri na kujali maslahi ya taifa tuseme. Hivi tujiulize mtaji wa chama cha siasa ni nini. nadhani ni watu. watu watapatikanaje? watapatikana kwa kuwavutia kwa sera. tujiulize zaidi wale watu katika mikutano ya chadema nani anawalazimisha kwenda. Je TLP, APPT-Maendeleo na UDP wakiitisha mkutano utajaa vile. sidhani. Naamini kuwa umati katika mikuno ya chadema ni matokeo ya sera mbadala na nzuri ambazo kwa hivi sasa chadema wanaziuza kwa wananchi ili inshaalah siku moja wafanikiwe kukamata dola. huwezi ukawa na chama cha siasa chenye lengo la kukamata dola siku moja halafu unalala usingizi dar es salaam ukitegemea kushinda uchaguzi.

  hiyo tisa, kumi je katika mikutano ya chadema na dk slaa kuna jambo baya linalosemwa? hapa naomba kujulishwa.

  ninavyosikia ni kuwa wanaongelea mambo hayahaya ambayo sasa yameshakuwa kero kuu na mzigo wa misumari kwa mwananchi wa kawada. mambo hayo ni kupanda kwa petroli, sukari, sembe, mchele na juu ya yote umeme.

  ReplyDelete
 6. Kwa mliosoma logic:

  Kwa vile Savimbi hatimaye aliuawa na serikali, huyu Savimbi mpya nawe atauawa??? Au masikini Chiligati yeye anajiropokea tu. Japo mimi ni mwanaCCM tena wa tangu enzi na enzi, nina wasiwasi sana na chama hiki kwa sasa. Hakina dira kabisa na inavyoonekana hata viongozi wenyewe wa ngazi ya kitaifa hawana mshikamano.

  Naomba tu kwamba waweze kurekebisha kasoro hizi kabla ya mwaka 2015 vinginevyo nimeanza kuamini kwamba nchi hii yaweza kuingia katika matatizo. Ni wakati sasa wa kuacha lelemama na kuwasikiliza wananchi hasa walalahoi.

  Kidumu Chama cha Mapinduzi!!! CCM daima!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU