NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, March 26, 2011

FIKRA YA IJUMAA: KWA NINI "UDAKU" UNAPENDWA SANA? TENA DUNIANI KOTE ???

 • Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko juu ya tabia ya Watanzania kutopenda kujisomea. Hata hao wachache wanaojisomea, inasemekana kwamba wengi wao huvutiwa zaidi na udaku na kukwepa magazeti na vitabu dhati pevu.
Picha ni kutoka Global Publishers .
 • Tabia hii ya kupenda udaku haipo kwetu pekee. Udaku unapendwa duniani kote! Hapa Marekani kwa mfano magazeti mengi makini (mf. Los Angeles Times, New York Times, Newsweek na Time) yamekumbwa na misukosuko ya kukosa wasomaji hadi kupelekea baadhi yake kupunguza wafanyakazi, kupunguza kurasa, kufungwa na mengineyo kuhamia mtandaoni.
  • Magazeti ya udaku (mf. US Weekely na The Globe) kwa upande mwingine yameendelea kufanya vizuri na hayajakumbwa na msukosuko wa aina yo yote; na yanazidi kujiimarisha. Swali ninalopenda kuuliza hapa ni kwamba kwa nini udaku unapendwa hivi - tena karibu duniani kote? Ati, kupenda udaku ni vibaya? Isome makala ya Padri Karugendo kuhusu suala hili HAPA

   2 comments:

   1. nami hujiuliza swali hilo mara nyingi sana. Wanadamu tunapenda sana kufahamu habari za watu kuliko za vitu. Nakumbuka wakati fulani akizungumza na waandishi wa habari, Mwalimu Nyerere aliwaambia yeye hajakwenda pale kuzungumza watu (ambao ungegeuka kuwa udaku) bali alikwenda kuzungumza vitu (masuala makini)

    Kwa mtazamo wangu, pengine mfumo wa maisha ya sasa unaochangiwa na utandawazi umetuathiri sana kiasi cha kutufanya kutopenda kuumiza kichwa kufikiria vitu serious na badala yake kupenda kufahamu tu juu ya maisha ya wenzetu.

    Huwa najiuliza mara nyingi, mimi kufahamu kuwa Chris Brown (mwanamuziki wa RnB) amepigana na mpenzi wake, kunanisaidia nini chenye thamani kuliko kufahamu utandawazi unaathiri vipi mahusiano baina ya mwajiri na mwajiriwa eneo la kazi?

    Na hii tabia sasa pengine ndiyo inayosababisha plagiarism kwa kiasi kikubwa sana vyuoni. Hatusomi kwa makini mambo makini, tunasoma udaku.

    Naamini nitajifunza mengi kutoka kwa wachangiaji wengine watakaokuja hapa.

    Ahsante sana Prof Matondo kwa kulileta hili.

    ReplyDelete
   2. Bwana Mtanga - nimeupenda mfano wako juu ya Chris Brown. Au sijui jeans alilokuwa amevaa 50 Cent jana lilikuwa ni rangi ya bluu. Hii kweli ni habari? Lakini ndiyo mambo yanayopendwa sana.

    Kuhusu plagiarism vyuoni ni swala linalohitaji kuangaliwa kwa undani zaidi; na mimi nadhani kuwa ni tatizo la mfumo wetu wa elimu kwa ujumla. Mlimani pale ukiwa na "madesa" mazuri na ukajua kukariri basi unaweza kupata A bila wasiwasi. Halafu uje huku kwa wenzetu sasa. Notisi zote za mihadhara, mazoezi ya nyumbani na vitu karibu vyote vipo mtandaoni kwenye tovuti ya Profesa lakini bila kusoma vitabu vilivyopangwa kwa somo hilo kamwe hutafaulu. Swala kwa hawa jamaa siyo kupata jibu sahihi - lakini hilo jibu umelipata wapi (inabidi utoe rejeo kamili) na cha muhimu zaidi, wewe unasemaje kuhusu jibu hilo? Unakubaliana nalo au la na kwa nini? Ni kweli hakuna jibu lingine mbadala? Hiki ndicho kinachokosekana katika elimu yetu.

    Ni miaka zaidi ya 10 sasa tangu nimalize shahada yangu ya kwanza pale Mlimani lakini nakwambia mpaka leo hii madesa yangu bado yapo "yanawasaidia" vijana. Kazi kweli kweli!

    Ninaandika makala kuhusu hili suala la udaku na nilikuwa nategemea kwamba watu wangetoa maoni yao lakini naona mada IMEFULIA, Dah!

    ReplyDelete

   JIANDIKISHE HAPA

   Enter your email address:

   Delivered by FeedBurner

   VITAMBULISHO VYETU