NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, March 11, 2011

FIKRA YA IJUMAA: PENYE NIA PANA NJIA (MAKALA YANGU YA KWANZA MAREKANI !!!)

 • Ilikuwa ndiyo tu nimefika kuanza shahada ya Uzamili (Isimu) katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Kutokana na misingi legelege niliyokuwa nayo katika uwanja wa isimu (japo kule nyumbani eti nilikuwa ndiyo kipanga!), masomo (hasa upande wa nadharia) yalikuwa magumu sana kiasi cha kukatisha tamaa kabisa (Watanzania wengi waliokuja kusoma shahada za juu moja kwa moja hapa Marekani nadhani wanalitambua hili!).
 • Japo nilikuwa nimeonywa kuhusu jambo hili, kamwe sikutegemea kwamba masomo yangenichachafya kiasi hiki na kuninyima hata muda wa kupumua. Na kama vile sikuwa na matatizo ya kutosha, nilikuwa pia sijui kutumia kompyuta. Kwa hivyo mazoezi yote ya darasani na makala ya muhula ilibidi yaandikwe kwa mkono!
 • Kama hii haitoshi, tofauti za kitamaduni pia zilikuwa zinanihangaisha. Kinyume na kule nyumbani ambako maprofesa wanaogopwa na kuonwa kama vile "miungu wadogo", hapa "wamiliki maarifa" hawa ni marafiki na mwanafunzi una uhuru wa kwenda kukaa nao wakati wo wote na kujadili masuala mbalimbali - ikiwemo alama yako ya mwisho wa muhula na hata masuala mengine ya maisha bila wasiwasi wo wote.
 • Pamoja na vipingamizi vyote hivi, kijana wa Kitanzania niligangamara na kupigana kiume mpaka mwisho. Haya ni makala yangu ya kwanza katika darasa la Fonolojia (tazama pia HAPA) wanafunzi wa shahada ya kwanza. Makala haya ya kitoto ni ya muhimu sana kwangu kwa sababu, mbali na sababu zinginezo, Profesa wa somo hili ni Mwanafonolojia anayeheshimika duniani kote na anajulikana pale idarani kwa "ukali" na uhitaji wake wa kazi zenye kiwango cha juu sana. Yeye huwa hapendi mzaha wala mchezo!
 • Nakumbuka aliponiita ofisini kwake na kuniambia kwamba alikuwa ameyapenda haya makala yangu ya kwanza. Alinihakikishia kwamba hakukuwa na sababu yo yote kwangu kuwa na wasiwasi kwani kulingana na maoni yake baada ya kuisoma makala yangu haya alikuwa amefikia hitimisho kwamba nilikuwa ninahitaji kozi nyingine moja tu ya shahada ya kwanza katika Fonolojia ili kuwa na misingi sahihi ya kufanya vyema sana katika masomo ya shahada zangu za juu.
 • Maisha ni mapambano na kabisa hakuna haja ya kukata tamaa. Na kweli baada ya miaka miwili nilipata shahada yangu ya uzamili; na baada ya miaka mitatu mingine nikaipata shahada ya Uzamifu (Ph.D).
 • Nakumbuka baada ya kutetea tasnifu yangu kwa mafanikio, profesa huyu alinishika mkono na kunikumbusha kuhusu karatasi yangu hii ya kwanza huku akiniambia kwa sauti ya msisitizo "Matondo, nilikwambia!" Aliendelea kuniambia kwamba utetezi wa tasnifu yangu ulikuwa umefanikiwa vizuri na uwasilishaji wa mada yangu ulikuwa umeandaliwa na kupangwa vyema kiasi kwamba hakuwa na maswali mengi. Kilichobakia ilikuwa ni kusherehekea. Na tangu siku hiyo nikaanza kuitwa Dr. Matondo !!! Ati, ningekatishwa tamaa na hekaheka za mwanzo ingekuwaje?
 • Tusikate tamaa na tukumbuke kwamba vitu vyema daima huwa havipatikani kwa urahisi wala kwa njia za mkato! Ukitaka kuyasoma makala haya au kuona alama ambayo nilipata bofya HAPA (pdf).
Tuonane tena wakati mwingineo tukijaliwa!
Tusikate tamaa !!!

***************************

10 comments:

 1. Profesa Matondo, nimeifungua na kuisoma makala yako nzuri. Nimeipenda, hasa ukizingatia kuwa nami kwa kiasi fulani nina kahistoria ka kusomea somo hilo. Makala imenikumbusha nilivyosoma isimu ya lugha pale Chuo Kikuu cha Dar, baadhi ya walimu wakiwa Profesa Trevor Hill, Derek Nurse, na Pauline Robinson.

  Naona umemnukuu Profesa David Massamba na Profesa Kahigi. Hao tulikuwa darasa moja. Profesa Massamba bado yuko Chuo Kikuu Dar na Profesa Kahigi ni Mbunge wa Bukombe (CHADEMA).

  Umemnukuu pia Profesa Batibo. Huyu ndiye kigogo wa siku nyingi wa isimu na lugha ya kiSukuma. Wakati sisi tunasoma pale Chuo Kikuu, yeye alikuwa mwalimu tayari.

  Makala yako nimeiteremsha mtandaoni na nimei-"print." Ulifanya kazi nzuri, tena kuandika kwa mkono. Si mchezo :=)

  ReplyDelete
 2. Prof Matondo, nashukuru kwa bandiko hili. Ni funzo kubwa hususani kwetu sisi vijana ambao wakati mwingine twajiweka katika mazingira ya kuwa sisi ni "delicate" na kusahau kuwa sio wakati wote mafanikio yanakuja kwa mteremko au kwa urahisi pasi na kuweka juhudi binafsi.

  ReplyDelete
 3. Matondo, pamoja na kuwa ukokotoaji wako umenipiga chenga, lakini nivutiwa na jinsi ulivyoweza kutunza kumbukumbu ya kazi zako za tokea 1998 hadi leo hii, hapa nimejifunza kitu juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu kwa manufaa ya kuelimisha jamii.

  ReplyDelete
 4. Hongera sana kaka kwa jitihada hizo zote.

  NB; Jamani wenzenu huku Japan hali ni tete, tsunami imetukumba leo, tuombeane.

  ReplyDelete
 5. Tusikate tamaa na tukumbuke kwamba vitu vyema daima huwa havipatikani kwa urahisi wala kwa njia za mkato!- Umemaliza Mkuu MMN

  @Anony wa Japan: Poleni jamani!

  ReplyDelete
 6. Prof. Mbele:

  Kumbe Derek Nurse alikufundisha? Yeye ameinukia na kuwa Mwanaisimu mashuhuri sana; na ameandika vitabu vingi vya isimu ya lugha za Kibantu. Nilikutana naye katika mkutano kule Oregon miaka michache iliyopita.

  Inaonekana hilo darasa lenu lilikuwa la vipanga tupu. Maprofesa Kahigi, Massamba na Mulokozi - wote mabingwa katika tanzu zao. Kahigi alinifundisha Sintaksia Mlimani na sasa naona amejitosa katika siasa. CCM walimfanyia mizengwe katika kura za maoni akatimkia CHADEMA.

  Nimeshangaa kusikia kwamba Profesa Batibo mlimkuta tayari akiwa Mwalimu. Nilionana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1998 alipokuja kutoa mada kuu katika mkutano tuliouandaa hapa chuoni. Angali bado "kijana" kabisa. Yeye alikimbilia Botswana na amefanya kazi nzuri sana katika uteteaji na hasa uimarishaji wa lugha za kienyeji za huko zilizokuwa katika hatari ya kufa. Hata Kezilahabi pia alikimbilia huko!

  Kama nilivyosema hapo juu, makala hiyo ni ya kitoto na nadhani hata Kiingereza chenyewe kinaonyesha hivyo. Niliitunza kwa ajili ya kujikumbusha tu. Fikiria leo mtu ukiambiwa uandike hata anuani kwenye bahasha eti unaona ni kazi ngumu kwa sababu tumezoea kompyuta. Kumbe miaka si mingi sana iliyopita wengi wetu tulikuwa bado tunaandika makala kwa mkono!

  Kissima - kweli. Kama binadamu ni rahisi sana kujisahau - na hasa kwenu nyinyi vijana wa leo. Mnataka mambo yote yaende kama yanavyopaswa. Mkipoteza hata simu tu au mkishindwa kuingia kwenye facebook siku hiyo chakula hakiliki na dunia nzima itajua.

  Kutokana na harakati zako kupitia katika kibaraza chako, ni wazi kwamba unajua kuwa bila jitihada mafanikio hayaji. Asante sana !!!

  Matiya - hiyo ni isimu ya kitoto kabisa. Huko mbele unaambiwa mambo yanachanganya mpaka na hesabu zinaingia. Ukichanganya isimu, kompyuta na hesabu basi unaweza kupata kazi nzuri sana katika makampuni makubwa ya simu na mengineyo kama vile Google.

  Kutunza kumbukumbu ni muhimu kwani nikiwaonyesha mabinti zangu hawa jinsi nilivyokuwa naandika kwa mkono makala zangu zote basi wanashangaa sana - na kusifia mwandiko wangu kiasi wengine wameapa kuuiga! Ni wazi wanajifunza kitu.

  Anony. wa Japan - poleni sana kwa mkasa uliowapata. Wasiwasi sasa kulingana na CNN ni kuhusu vinu kadhaa vya Nyuklia ambavyo inaonekana vimeharibiwa na tetemeko hili. Mungu na Akawasaidie!

  Mtakatifu - kizazi hiki kipya kimerahisishiwa sana mambo na wakati mwingine kinajisahau na kudhani kwamba mambo yanapatikana kirahisirahisi tu. Kikiona kwamba wengine miaka michache tu iliyopita tulikuwa tunaandika makala nzima kwa mkono naona kitashangaa kidogo kwani sasa mpaka nimeanza kuona laptop ambazo unazungumza tu maneno nayo inakuandikia kila kitu. Inabidi tukikumbushe kwamba jitihada zinahitajika katika kupata mafanikio hapa duniani. Hata mafisadi wanafanya jitihada katika kufanikisha ufisadi wao!

  ReplyDelete
 7. profesa matondo kwa kifupi hongera kwa mambo matatu. Mosi, kwa kuwa kipanga kipanga UDSM. Nimefungua kuona ukipanga wako ingawaje neno kipanga lina ka-ukakasi fulani ingawaje tena sio sana. Pili, kwa kufanya kazi nzuri hii ingawaje mwenye nayo unaiita ya kitoto. Tatu, kwa kuitunza kwa ajili ya kumbukumbu yako ambayo imekuwa tunu kwetu wasomaji.

  nadhani ungesalia UDSM ungenifundisha ama ungekuwa seminar leader wangu. nami nimepita hapo maeneo ya Foreign Langauages and Linguistics. kati ya vitu vigumu huko lingustics ni phonetics na phonology. hapa unamkuta prof Maghway na prof massamba. basi hali inakuwa tete!

  ReplyDelete
 8. Mwaipopo - Pengine siku hizi wanatumia neno jingine pale Mlimani ili kutenganisha vipanga wa darasani na vipanga wa mademu. Hata hivyo tunaweza kuwatenganisha vipanga hawa kwa kutegemea muktadha kwani neno moja kuwa na maana mbili au zaidi ni jambo la kawaida katika lugha.

  Ningebakia hapo na kubahatika kuajiriwa hapo si ajabu ningekufundisha. Prof Maghway na Prof massamba hawakuwahi kunifundisha, lakini sifa zao huwa nazisikia. Prof. Massamba nimezisoma baadhi ya kazi zake. Ni Mwanafonolojia na Mwanaisimu makini sana!

  Mimi nilifundishwa Fonetiki na Profesa Maganga (RIP) na Fonolojia na Prof. Mekacha (RIP). Walinipa misingi mizuri sana na Mungu Awapumzishe salama huko waliko!

  ReplyDelete
 9. Hongera sana kaka Matondo!pia asante sana kwa kututia moyo Mungu awenawe daima!naungana nawe kweli tusikate tamaa!!!!!.

  ReplyDelete
 10. Sasa Professor Matondo kama mkono wako ulikuwa na uwezo wa kuchapa kuzidi "kompyuta" mbona sioni hata haja ya kompyuta kwa wakati huo kwako (mzaha).

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU