NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, March 7, 2011

HEBU SIKILIZA MASHARTI YA HUYU MGANGA UCHWARA !!!

 • Kimsingi mimi sina ugomvi na waganga wa kienyeji. Wapo waganga wa kweli wanaotibu magonjwa sugu na kusaidia watu hasa masikini kule kijijini (Mf. Tazama kizaazaa hiki kama ni kweli - pia HAPA na HAPA). Na baadhi ya mitishamba wanayotumia imeshathibitishwa kisayansi kwamba ina kemikali zenye kutibu magonjwa mbalimbali. 
 • Ugomvi wangu na waganga hawa unakuja pale wanapoanza kudanganya watu kwa kuwapa njia za mkato maishani kama vile kujipatia utajiri wa haraka haraka, ajira na madaraka. Njia hizi za mkato mara nyingi huambatana na masharti magumu na ya ajabu ajabu kama haya ya zinaa, viungo vya albino, kubikiri vitoto vidogo na kutoa makafara ya binadamu.
 • Inasemekana pia kwamba kuendelea kwa mauaji ya vikongwe hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa kunahusishwa na waganga hawa kuwadanganya watu kwamba ndugu zao wamerogwa; na hivyo kuamua kulipiza visasi.
 • Cha ajabu ni kwamba imani hizi za kishirikina; na watu kuamua kupita njia za mkato maishani kunazidi kujiimarisha katika jamii. Pengine ugumu wa maisha na elimu duni ndivyo vinasababisha tatizo hili. Kama jibu ni ndiyo, utatuzi wa kweli wa tatizo hili basi ni lazima ufungamane na vita vyetu dhidi ya umasikini, vita ambavyo mimi naamini kwamba ni lazima vianzie katika elimu bora!
Nyongeza
 • Mh. Lowassa yeye anafikiri kwamba pengine watu wakimrudia Mungu wataweza kuachana na hizi imani za kishirikina. Cha kushangaza ni kwamba, hata huko kwa Mungu kuna wahubiri ambao pia wanasadikiwa kwamba wanatumia nguvu za giza (tazama HAPA) katika utendaji wao wa kazi. Isome kauli ya Mh. Lowassa HAPA ambapo anasema yuko tayari kusaidiana na wahubiri wa neno la Mungu katika kueneza neno la Mungu! 

   3 comments:

   1. Ni ujinga. Ni matokeo ya umasikini na sera zilizoshindwa za CCM. People don't see any other way out. Kila mmoja anafanya awezalo ili kuishi. Wapo waliogeukia makanisa ili kujitajirisha. Wapo wanaoendeleza ufisadi, ali mradi kila mmoja kula pale alipo. There is no simple solution to this problem and I agree with you that this should be part of our long term agenda to eradicate poverty and educate our people.

    Lowassa anaposema kwamba yuko tayari kushirikiana na hawa wahubiri wa dini ambao nao pengine wanatumia nguvu za ushirikina, ina maana atakuwa mhubiri au? I will join his church in an instant !!!

    ReplyDelete
   2. Mimi huwa naamini kuwa mtu mambo yanakunyookea kutokana na juhudi katika shughuli uifanyayo. Na elimu, ujuzi, na maarifa ni msingi muhimu. Sasa basi, kutokana na imani yangu hii, nimejaribu kwa miaka mitatu mfululizo kuendesha warsha Tanzania, kuhusu masuala ambayo kwa huku Marekani, watu wanayaona muhimu katika dunia ya utandawazi wa leo.

    Mahudhurio kwa upande wa Tanzania yamekuwa hafifu, na mwaka jana hakuhudhuria hata m-Tanzania moja, sehemu nilizoenda kufanya hizo warsha, yaani Tanga na Arusha.

    Sasa nashangaa kumwona huyu m-Tanzania kwenye katuni, ambaye badala ya kuhudhuria warsha yangu, kutafuta elimu, yeye ameenda kwa mganga :-)

    ReplyDelete
   3. Profesa Mbele - kutokana na juhudi yako ya kuzitangaza warsha hizo katika blogu mbalimbali, nilifikiri kwamba zilikuwa zinahudhuriwa na Watanzania wengi ili nao waweze kubadilishana mawazo nawe na kujifunza kutoka kwako kuhusu mustakabali wa utandawazi na mengineyo. Kumbe mambo ni yale yale.

    Hii hata hivyo haishangazi kwani watu wanapenda njia za mkato kama hizi za kwenda kwa waganga wa kienyeji. Watu wanakwenda kwa waganga ili waweze kupandishwa vyeo, waweze kupatiwa uwaziri n.k. Hata hili sokomoko la huyu Mzee wa Loliondo mimi nadhani linaingia katika mkumbo ule ule wa kutafuta njia za mkato katika utatuzi wa matatizo yetu. Ni tamaa hii hii inayofanya watu wawe wepesi wa kutapeliwa na mtu ye yote mwenye ujanja iwe ni kwenye dini (miujiza na kuokoka) au hata siasa. Hatukai chini na kujaribu kuangalia kiini cha tatizo ni nini.

    Mtu unaambiwa nenda ukabake katoto kachanga halafu uende kwenye machimbo ya dhahabu ukatajirike (au eti upone UKIMWI) kweli unatii. Au kalete mguu wa albino...Katika wakati huu na nyakati hizi hili ni jambo la kushangaza sana. Kama asemavyo Mzee wa Changamoto - pengine tuonavyo tatizo ndiyo tatizo lakini ni wazi kwamba jamii yetu imo katika matatizo makubwa.

    Nyongeza: nilipokuwa nyumbani mwaka jana wakati wa hekaheka za uchaguzi, mitaani kulikuwa kumeenea uvumi kwamba vigogo wa chama fulani eti walikuwa wameleta "kamati ya ufundi" kutoka Equatorial Guinea ili kusimamia uchaguzi na kuhakikisha kwamba wanapata ushindi na kuingia Ikulu. Sikupenda kuziamini tetesi hizi kwani haiingii akilini kwamba kweli mtu atataka kuingia ikulu kuwa raisi wa nchi kwa kutegemea ushirikina hasa katika dunia hii tuliyonayo. Lakini inavyoonekana Afrika kila kitu kinawezekana !

    ReplyDelete

   JIANDIKISHE HAPA

   Enter your email address:

   Delivered by FeedBurner

   VITAMBULISHO VYETU