NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, March 15, 2011

JAKAYA MRISHO KIKWETE: TUMAINI LILILOREJEA - NA PRINCE M. BAGENDA (PORIS PRESS AGENCY, 2006)


 Angalizo
 • Lengo langu la kukiweka kitabu hiki hapa siyo kuanzisha mashambulizi ya ki-Ad Hominem dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilipokiona maktabani nilivutiwa nacho na niliamua kukisoma mara moja. Prince Bagenda ninayemfahamu ni mchambuzi makini na mwandishi mahiri; na umakinifu na umahiri huu unaonekana bayana katika kitabu hiki hasa katika makala zake nyingi alizowahi kuandika katika gazeti la Rai (lile la zamani!) - makala ambazo zimerejelewa pia katika kitabu hiki. 
 • Ni wazi kwamba kitabu hiki kiliandikwa katika mazingira ya mhemko wa kisiasa na kinaweza kuonekana kama kitabu ambacho kinaegemea zaidi katika propaganda za kumpigia debe mgombea wa wakati ule. Pamoja na ukweli huu, Jakaya Mrisho Kikwete: Tumaini Lililorejea kinaonyesha harakati na mshikeshike uliokuwapo wakati wa uteuzi wa mgombea wa urais mwaka 1995; na baadaye 2005 kwa undani kama vile Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania cha Mwalimu Nyerere kilivyofanya - japo kwa mitazamo tofauti. 
 • Kitabu kinaonyesha sababu zilizomfanya Kikwete ateuliwe kugombea urais mwaka 2005 baada ya kupoteza nafasi hiyo mwaka 1995. Akiwa rais kijana kuliko wote, mchapakazi na mwenye nidhamu ya hali ya juu, uteuzi wake ulifumbata matumaini makubwa kwa Watanzania; na kauli-mbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya ilirindima sawasawa katika masikio ya Watanzania. Pengine hii ndiyo sababu iliyomfanya Bagenda akiite kitabu hiki Tumaini Lililorejea.
 • Sijui Prince Bagenda angetoa tathmini yake sasa baada ya Mh. Dr. Rais Kikwete kumaliza kipindi chake cha kwanza na kuanza cha pili angesema nini kuhusu tumaini hili (WanaChadema tayari wanamtafuta HAPA). Kwa ujumla hiki ni kitabu cha kihistoria kinachofaa kusomwa na watu wote wenye kufuatilia hekaheka za kisiasa nchini mwetu, mapito yetu; na safari yetu ya kujikomboa inavyosonga mbele pamoja na changamoto zake nyingi!
(1) Shukrani
 • Kitabu kimefadhiliwa na Mh.Sabodo, kada wa CCM mkereketwa na mpigania demokrasia ambaye katika siku za karibuni ametoa mchango mkubwa wa kuimarisha upinzani nchini kwa kuwa mfadhili mkubwa wa chama cha Chadema. Mh. Sabodo anatoa ushauri mzuri kuhusu jinsi ya kutokomeza ufisadi, mfumo wa elimu na mengineyo.

(2) Utangulizi


(3) Sifa za JK


(5) Sababu za kushindwa kwa upinzani


Kitabu kina kurasa 289. 
Sina uhakika kama bado kinapatikana katika maduka ya vitabu. Kama nilivyosema hapo juu, kitabu hiki kinafaa kusomwa, japo ni katika muktadha wa kihistoria zaidi. 

3 comments:

 1. katika kitabu hicho, Prince Bagenda kwa kiasi kikubwa sana amejivua uandishi mahiri na uchambuzi makini na kujivika uanapropaganda. Nimeanza kumsoma Bagenda miaka mingi lakini mwaka 2008 nilipokisoma kitabu hiki, i was disappointed kwa kiasi kikubwa tu.

  Si lengo langu kutumia jukwaa hili kuanza kukishambulia kitabu. La hasha. Yapo mambo kadha wa kadha ambayo yameandikwa kwa uhalisia wake. Lakini kuna mambo mengi sana ambayo yameandikwa ili kumpamba mlengwa.

  Lakini ndo mambo ya siasa hayo. Wahusika wa kisiasa shurti wajadiliwe kisiasa.

  ReplyDelete
 2. Bwana Fadhy - ni kweli. Kutokana na makala zake makini katika gazeti la RAI, hata mimi kidogo nilishangaa jinsi mwandishi alivyodadilika katika kitabu hiki. Badala ya kuwa mchambuzi, hapa naona muktadha wa wakati ule ulimwelemea na hatimaye kugeuka kuwa mpiga mbiu tu.

  Yote kwa yote ni kitabu kinachopaswa kusomwa kwani kina mambo mengi ya muhimu kuhusu mchakato wetu wa kisiasa.

  ReplyDelete
 3. Mwalimu Matondo umefanya vema kutundika tabu hili. Nilisoma kitabu kile na kusikitika sana. Kilipaswa akuitwa TUMAINI LILILOPOTEA baada ya CCM kupoteza nafasi ya kumpata mtu ambaye alifaa kuwa rais. Kimsing Bagenda aliyeandika kitabu cha Kikwete si yule aliyekuwa akitoa changamoto kwenye gazeti la Rai. Huyu ni Bagenda nepi ambaye aliweka kando maadili ya taaluma ya uandishi huku akitumia tumbo kufikiri badala ya kichwa. Bagenda ni mmojawapo wa wana kwaya wazuri waliowatukana wagombea wengine makini ili mtu wao apite wapete wasijue wengine atawageuka. Zilifumka shutuma na tuhuma kuwa alikuwa akimpigia debe Kikwete sambamba na Salva Rweyemamu ili ateuliwe kuwa balozi nchini Uganda. Hili halikuwa maana JK alistuka baada ya kushinda na kutulia na kusoma kile kitabu. Aligundua uhovyo na uongo wa Bagenda kiasi cha kuachana naye huku akimlipa fadhila Rweyemamu ambaye naye pia alijigeuza nepi akisaliti yale aliyosimamia tangu akiwa kijana.
  Nangoja kusoma kitabu kingine cha Kikwete kilichoandikwa na profesa Nyang'oro ambaye naye ataishia kuwa kama Bagenda. Wapo wengi. Jiulize wako wapi akina Dk Gideon Shoo aliyeshirikiana na Rweyemamu kutaka kuisafisha Richmond? Njaa ikipanda kichwani ni hatari kuliko hata ukoma na ukimwi. Kwa ufupi ni kwamba ingawa hasemi, kama amerudia kusoma kitabu chake, Bagenda amejishangaa, kujilaumu na kujiona wa hovyo.Na hii ndiyo dhambi kubwa aliyoitenda kitaaluma katika maisha yake. Aliaminika kama nguli wa kufikiri lakini akaishia kufikiri vibaya.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU