NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, March 18, 2011

JK: MAPROFESA WANANISIKITISHA

Maprofesa mpo? Wito huu mzuri kutoka kwa J.K.

JK: Maprofesa wananisikitisha

Na Jane Mihanji

RAIS Jakaya Kikwete amewataka maprofesa na wasomi nchini kutunga vitabu ili kukabiliana na tatizo la kushuka kiwango cha elimu, kunakochangiwa na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada.

Amesema anasikitishwa na kitendo cha maprofesa na wasomi chini kulalamikia upungufu wa vitabu katika fani mbalimbali, huku wakikwepa kutoa mchango wa kutatua tatizo hilo.

Rais Kikwete amewata kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anafanya jitihada za kuboresha elimu ili kuwa na kizazi kilichowiva kitaaluma.

Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Taarifa ya wizara iliyosomwa na waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, ilieleza uhaba wa vitabu ni moja ya matatizo yanayokwamisha sekta ya elimu.

Dk. Kawambwa alisema shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vitabu na katika baadhi, wanafunzi hutumia vya tofauti, tatizo linaloweza kupatiwa ufumbuzi kwa wasomi kujikita katika uandishi wa vitabu.

"Hili ni tatizo, wakati tunasoma Msoga kitabu cha Bulicheka, mwanafunzi aliyekuwa akisoma Lindi alikisoma, lakini siku hizi mambo yamebadilika," alisema rais Kikwete na kuiagiza wizara kutoa kipaumbele katika uchapishaji vitabu vya kiada na ziada.

"Lazima tupange kila mwaka bajeti ya kuchapisha vitabu vya watoto wetu, hatuwezi kuacha waendelee kuchangia vitabu kwa kuwa hili ni la kwetu, na hatuwezi kusubiri wafadhili," alisema.

Alionya fedha za vitabu, maabara na ujenzi wa nyumba za walimu zisipelekwe katika matumizi mengine.

Kwa upande wake, Dk. Kawambwa alisema wizara inakabiliwa na upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari, hususan katika mikoa ya pembezoni.

Alisema pia kuna tatizo la kiwango kidogo cha ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na ualimu, hususan masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza.

Waziri Dk. Kawambwa alisema ufinyu wa bajeti katika utekelezaji programu za elimu  na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu pia ni tatizo kubwa.

Akizungumzia kiwango cha ufaulu, rais Kikwete aliwataka walimu wanaotunga mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo, kuacha kutunga migumu kupita kiasi, kwa kuwa yawezekana kuwa ndicho chanzo cha matatizo.

"Changamoto ya ufaulu mdogo kama mnavyodai katika masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza pengine inatokana na ugumu wa mitihani... lakini msitunge rahisi sana," alisema na kuongeza ni lazima wahitimu wawe na viwango vinavyostahili.

Chanzo: Uhuru

16 comments:

 1. hili la vitabu hili....hili la maprofesa hili.
  nitalisemea la kwanza, la vitabu.

  kwanza, niliposoma leo juu ya malalamishi ya Rais, nilijaribu kutafakari sana. nilitafakari kwa kiwango cha uelewa wangu juu ya sikitiko la Rais. nami nikajaribu kuutazama uandishi wa vitabu Tanzania ingawa mie siyo Profesa (ewe Mwenyezi Mungu ninakuomba unijaalie nifike huko)

  mie nadhani kuna matatizo yanayowakatisha tamaa waandishi wa vitabu. si kwa maprofesa tu, bali hata sisi wananchi wa kawaida tunaopenda kuandika vitabu, viwe vya kiada ama ziada.

  Rais anasema kiwango cha elimu kinashuka ikiwa moja ya sababu ni uhaba wa vitabu. ngoja nami leo niseme.

  1. Tatizo ninaloliona ni serikali kutokuwa na msimamo kuhusu sera ya elimu. Kubadilishwa badilishwa kwa mitaala nadhani ni moja ya vitu vinavyokatisha sana tamaa. hebu fikiria unatumia muda mrefu sana kufanya utafiti wa kitabu chako, muda mrefu kukiandika, kukihariri, hatimaye kukichapa. lakini baada ya muda mfupi, unaambiwa kuwa mtaala umebadilika, kitabu chako hakitumiki tena. hadi leo sielewi kwa nini serikali inabadilisha badilisha mara nyingi mitaala. labda nikieleweshwa hilo.

  2. Tatizo jingine lipo kwa wachapishaji wa vitabu. Kama hujajulikana kwenye uwanja wa uandishi, kazi yako haiangaliwi kwa undani sana na mhariri katika shirika la uchapishaji. Mswaada huchukua muda mwingi kutathiminiwa. Hali hii hukatisha sana tamaa. unaweza kujituma kuandika kazi yako, lakini ukifika kwa mchapishaji unajikuta unagonga mwamba.

  3. Tatizo jingine mie naliona lipo kwenye mfumo wa uteuzi wa vitabu vya kiada na ziada kwa mamlaka zinazohusika. kumeshawahi kuwa na lawama kadha wa kadha kuwa mfumo wa uteuzi huangalia zaidi majina ya waandishi badala ya kile kilichoandikwa kiasi cha kuwakatisha tamaa waandishi wengu hususani wale wachanga.

  4. gharama za uchapaji kuwa kubwa. hata wachapaji wamelalamika mara kadhaa juu ya gharama kubwa katika karatasi cha kuchapia. gharama hizo zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya vitabu. waandishi hukatishwa tamaa na gharama hizi.

  5. malipo duni kwa kazi. wakati fulani mwandishi anaamua kuondokana na wazo la kuchapa kazi akifikiria gharama kubwa anayoitumia kufanya tafiti kulinganisha na maslahi atakayoyapata. mwandishi anatarajia kazi yake pamoja na kuleta mabadiliko ya kifikra katika jamii, pia kazi hiyo iweze kumwinua kiuchumi. kama alivyosema Robert (1966: 82) kwamba "Mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye, kama watu wengine wa desturi hafarijiwi na hasara".

  wakati Rais anawalalamikia maprofesa (mie nadhani ni wasomi wote) wao pengine wanayo malalamiko kama nilivyoyasema hapo juu.

  Ama, kama alivyoyasema Mallya (1994:24), "Popote pale duniani mwandishi wa kitabu anapoketi chini kuandika anategemea vitu vitatu. Kwanza, kitabu chake kitoke vizuri na haraka iwezekanavyo; pili, kisomwe na watu wengi iwezekanavyo; na tatu, apate chochote kutokana na jasho lake. Hivi vikikosekana lazima mwandishi yeyote yule alalamike".

  Kwa kumalizia, serikali (rais ndo serikali) iache kulalamika, bali iyafanyie kazi malalamiko ya waandishi.

  Naomba kutoa hoja.

  ReplyDelete
 2. Profesa Matondo, shukrani kwa kuileta taarifa hii. Nami, baada ya kuiona hapa kwako, nimeiweka kwenye kiblogu changu.

  Mimi ni mmoja wa hao maprofesa, ila najikongoja katika uandishi wa vitabu vya aina anayoongelea Mheshimiwa Rais. Baadhi ya vitabu nilivyochapisha hadi sasa ni hivi hapa, na vingine kati ya hivi vinatumika vyuoni huku ughaibuni.

  Lakini hata hivi vichache haviko mashuleni Tanzania, kwa sababu sina uwezo kifedha wa kuvinunua na kuvipeleka kwenye vyuo na shule zinazofundisha masomo haya ninayoshughulika nayo, au kama vitabu vya ziada kwenye vyuo na shule zingine.

  Pamoja na uwezo wangu mdogo, huwa kila ninapoenda Tanzania nachukua nakala mbili tatu za hivi vitabu vyangu, na huwa nanunua vitabu vingine pia, na nimeshavigawa kwenye vyuo kadhaa. Moyo ninao, ila uwezo ni finyu sana.

  Ndugu Mtanga ametoa changamoto nzuri. Napenda tu kusema kuwa kuhusu matatizo ya uchapishaji, mimi nimejikwamua kwa kutumia uchapishaji wa mtandaoni, ambayo ni tekinolojia ya kisasa, isiyo na usumbufu.

  Tatizo lake ninavyoona ni kuwa bei ya vitabu inakuwa juu kiasi kuliko inavyokuwa kwa uchapishaji tuliozoea. Na vile vile, kwa sasa, si waTanzania wengi wenye uwezo wa kununua vitu mtandaoni. Lakini naamini kuwa miaka inavyopita, tatizo litaendelea kupungua.

  Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO nimeelezea uchapishaji wa aina hii, kwa kutumia uzoefu wangu. Ni mchango wangu kwa waandishi wengine.

  ReplyDelete
 3. Bwana Fadhy:

  Umegusia karibu mambo yote ambayo nilikuwa na dukuduku nayo. Hivi ni waziri gani katika serikali ya awamu ya tatu ambaye alifurumua mitaala yote, akafuta masomo mengine na kurundika mengine pamoja? Ni Mungai? Uamuzi huu ulileta misukosuko na sijui kama ulifanywa kwa kuwashirikisha wataalamu wa mitaala na elimu au la. Sitashangaa kama ni mtu mmoja tu (ambaye suala la elimu na mitaala inawezekana wala siyo uwanja wake) kaamka vibaya na kuanza kufuta masomo na kuparaganya mitaala. Ndiyo Tanzania yetu hiyo. Waziri aliyefuatia naye akaanza kupanga mitaala upya na kurudisha masomo yaliyofutwa. Kumbe ni afadhali enzi zetu za Juma na Rosa; na mwanasesere wao. Suala la elimu ni muhimu na linapoingiliwa na maamuzi ya kisiasa basi matokeo yake ndiyo hayo.

  Pengine sasa mambo yameshabadilika lakini enzi zile hata kama ungeandika kitabu kizuri namna gani bila kumfahamu mtu katika mamlaka zinazohusika na upitishaji wa vitabu na upangaji wa mitaala, kitabu chako kisingeingizwa katika mitaala ya shule. Ni ule ule wimbo wa kawaida: kujuana, urafiki, udugu na kupendeleana badala ya kuangalia utaalamu wa mtu na kazi aliyofanya. Pengine mambo yamebadilika sasa.

  Kama ulivyosema, waandishi wakilipwa vizuri kutokana na kazi zao, na vitabu vyao kuchapishwa katika wakati unaotakiwa bila shaka watu wataandika vitabu tena sanatu. Kwa Tanzania sasa uandishi wa vitabu umedorora na vitabu vingi - hasa vya Kiswahili- sasa vinatoka Kenya. Sijui kuna nini huko Kenya kinachowafanya waandike vitabu vingi namna hii.

  Asante sana kwa changamoto zako hizi.

  Prof. Mbele. Bado nakumbuka ule mkasa wako wa kurudi nyumbani na vitabu badala ya pick up kama wengi walivyotegemea.

  Suala linalokatisha waandishi wengi - ambalo pia Mtanga amelizungumzia hapo juu - ni ukosefu wa wasomaji. Soko la kuaminika ni huko huko mashuleni ambako nako mpaka kitabu chako kikubaliwe na kuingizwa katika mitaala ni kizungumkuti kweli. Ya nini basi mtu unandike kitabu, uingie gharama ya kukichapisha na usipate cho chote? Jambo hili linakatisha tamaa sana. Kama kukiwa na utaratibu mzuri na unaoeleweka kuhusu uteuzi wa vitabu vya mashuleni pamoja na malipo mazuri kwa waandishi naamini kwamba vitabu vitaandikwa tena vingi sana.

  INAENDELEA...

  ReplyDelete
 4. Mimi nadhani pia kwamba hata suala la lugha nalo linachangia. Ukiandika kitabu cha Kiingereza na kwa bahati mbaya kisichaguliwe kutumika mashuleni basi hapo umeula wa chuya kwani wasomaji wa Kiingereza pengine ni wachache zaidi kuliko wale wa Kiswahili. Na naamini kwamba si maprofesa wote wanaweza kuandika vitabu katika nyanja zao kwa Kiswahili. Kuna mzunguko fulani hapa pia kuhusu suala hili la lugha.

  Ndiyo maana watu wengi wanaamua kupita njia ya uhakika zaidi na kuamua kuandika vitabu vinavyotoa mwongozo wa jinsi ya kujibu maswali ya mitihani. Vitabu hivi vinanunuliwa sana na ndiyo maana watu kama akina Nyambari Nyangwine (sasa mbunge wa Tarime) wamajiwahi na kuanzisha makampuni ya uchapishaji ya vitabu vya kujibu maswali tu basi na wameweza kutajirika kwa haraka.

  Profesa Mbele - huo mwongozo wako wa Things Fall Apart ukiupeleka Tanzania utanunuliwa sana hasa kama kule mwishoni utaongezea mwongozo na mifano bora ya jinsi ya kujibu maswali ya fasihi ya kidato cha nne. Watoto watakuwa hawana tena haja ya kuisoma riwaya ya Things Fall Apart yenyewe na badala yake watasoma tu huo mwongozo na kutegemea kupata A katika mitihani yao. Ndiyo elimu yetu hiyo ilipofikia!

  Kwa hiyo inawezekana ukawa umekalia utajiri na huo mwongozo wa Things Fall Apart.

  Kuhusu hivyo vitabu vyako vingine hata kama angetokea mtu akakusaidia kuvipeleka Tanzania, nani atavisoma? Pengine mtu avilipie kabisa na wewe ukavigawe bure mashuleni. Au uwe na bahati vipendekezwe kama vitabu vya kiada mashuleni na vyuoni. Vinginevyo hakuna kitu.

  Mwaka huu nategemea kuchapisha vitabu vitatu - viwili vya isimu na kimoja cha sayansi kwa ajili ya shule za msingi Tanzania. Hiki cha shule za msingi nitakipeleka mwenyewe laivu kwa JK nikampe mkononi akisome ili aone mawazo na mapendekezo yangu kuhusu jinsi ya kuimarisha na kuwafanya watoto wetu wavutiwe na masomo ya sayansi. Huu ni mchango wangu kwa nchi yangu na hata kisipopendekezwa mashuleni ni sawa lakini nitakuwa nimeridhika na juhudi zangu za kujaribu kusaidia!

  ReplyDelete
 5. Nashukuru Mhe. Rais kutoa changamoto hii.
  Lakini tulishamsihi mapema alipompongeza Prof aliyemuandikia kitabu kuwa NI YEYE ALIYETAKIWA KUANDIKA KITABU CHA MAISHA YAKE (japo kwa kuanzia tu).
  Nadhani ni wakati ambao SIASA zastahili kuwa kando na wanaSIASA wazungumze ukweli. Naona ule mchezo wa "fanyeni nyinyi" unaendelea hapa.
  Nina hakika Mhe Rais ana mengi mema ya kuandika na angekuwa wa kwanza kuandika kwa manufaa ya wananchi. Kwa kufanya hivyo ANGEKABILIANA NA UGUMU WANAOPATA WAANDISHI WENGINE na pengine ingesaidia kuwatatulia matatizo yao.
  Sina hakika kama sasa hivi anakumbuka alichosema kwani siamini kama alisema akimaanisha.
  BARAKA KWENU

  ReplyDelete
 6. Profesa Matondo, nilisahau kumalizia ujumbe wangu kwa kusema kuwa hivi vitabu unavyopangia kuvichapisha mwaka huu usikose kutupa taarifa zake.

  ReplyDelete
 7. Mzee wa Changamoto - angalizo zuri. Wapo viongozi waliokuwa na tabia ya kuandika vitabu. Nyerere ni mmojawapo. Nakumbuka pia niliposoma kitabu cha mashairi ya Augustino Neto wa Angola (Risasi Zianzapo Kuchanua?) - mashairi mazuri na ya kimapinduzi. Kwame Nkrumah na wengine wachache pia waliwahi kuandika vitabu vya maisha yao wenyewe: Facing Mount Kenya (Kenyatta), Long Way to Freedom (Mandela). Marais wa Marekani pia wana tabia ya kujiandikia vitabu wenyewe. JK naona alitoa wito wa wasomi kuandika vitabu vya viongozi wakati ule akikabidhiwa kile kitabu cha maisha yake na Profesa Nyang'oro. Naamini kwamba hata yeye mwenyewe anaweza kujiandikia chake kama akitaka.

  Na kwa mtu msomi na mwandishi wa habari aliyebobea kama Mkapa kweli anashindwa kuandika kitabu cha kina kuhusu maisha yake? Si utamaduni wetu pengine sijui.

  Mimi sina ugomvi na wito huu kama kweli rais atakuwa amedhamiria kuwasaidia waandishi kupambana na changamoto zilizoibuliwa na Mtanga hapo juu. Na sitashangaa pia kama hizi ni siasa tu mtindo mmoja.

  Profesa Mbele - vitabu hivyo vikitoka bila shaka vitakuwa hapa kibarazani - na kama kawaida wewe utapata kopi zako zilizosainiwa na kutumwa moja kwa moja kutoka Bariadi!

  ReplyDelete
 8. Nimeulizwa swali na Koero kama naunga mkono vitabu vya akina Nyambari Nyangwine kule kwa Profesa Mbele. Nimetoa jibu lifuatalo:

  Koero - vitabu vya akina Nyambari Nyangwine, kwa maoni yangu vinadumaza elimu badala ya kuiimarisha. Badala ya kusoma vitabu (riwaya, tamthiliya na ushairi) vilivyopendekezwa wanafunzi wanapita njia za mkato na kusoma mwongozo wake na majibu waliyotafuniwa. Ndiyo maana nikasema kwa kejeli kwamba "ndipo elimu yetu ilipofikia!"

  Mimi nilifundisha katika shule za sekondari za Jitegemee, Mwanza na Mwadui wakati ule nikisoma pale Mlimani. Wakati ule Mbunda Msokile ndiye alikuwa akitamba. Watoto walichokuwa wanafanya ni kusoma miongozo ya Mbunda Msokile na kukariri majibu yake kwisha. Hawana tena haja ya kuvisoma vitabu vyenyewe.

  Nilipokuwa nyumbani mwaka jana pia nilitembelea vijana fulani hivi waliokuwa wakijiandaa kufanya mitihani ya kidato cha nne. Hawa walikuwa na vitabu vya Nyangwine vya kila aina. Nao waliniambia yale yale: kusoma riwaya nzima ni kupoteza muda tu kwani kila kitu wameshatafuniwa na Nyangwine. Cha kushangaza ni kwamba wote wamefeli. Mmoja tu katika kundi lile la watu sita amepata divisheni 4 ya point 28! Sasa sijui hawawezi kukariri, hawakukariri vizuri au pengine majibu ya Nyamgwine ndiyo yana matatizo. Kuna hata anayechunguza na kuyahakiki majibu yaliyotolewa katika vitabu hivi na kuona kama yanaendana na yale ya baraza la mitihani au? Kama majibu ya Nyangwine ni tofauti na yale ya baraza la mitihani basi sishangai kwa nini vijana wale wameambulia patupu.

  Kupendekeza kwangu kwamba Profesa Mbele aongeze majibu ya fasihi katika mwongozo wake wa Things Fall Apart kulikuwa ni uchokozi tu ili nimwone atasemaje. Ndiyo maana ukisoma vizuri utaona kwamba kuna utani utani hivi katika maelezo yangu!

  Hili ni suala la muhimu, tuendelee kubadilishana mawazo.

  ReplyDelete
 9. Wanaosikitisha si maprofesa wala waandishi na watunzi bali serikali isiyowajibika wala kuwa na sera ya kila kitu zaidi ya ufisadi.
  Badala ya kulaumu watunzi na waandishi, Jakaya Kikwete angejilaumu mwenyewe kwa kutokuwa na visheni wala sera ya elimu na mambo mengine.
  Nyerere alionyesha mfano wa uandishi na uongozi. Yeye Kikwete zaidi ya kukodisha watu wa kumwandika vizuri ameandika au kutunga nini?
  Kuondokana na hili nashauri. Rais aondokane na ufisadi wa kiakili ambapo madili yamefunika maadili.Mie kama mtunzi huwa nashauri watunzi watunge si kwa ajili ya soko la leo bali kuacha urathi kwa jamii hapa watakapokuwa wameondoka. Shaban Robert alifanya hili.

  ReplyDelete
 10. Hivi ni kweli mtu mwenye kariba ya Profesa kama Mbele anaweza kutueleza kwamba hana uwezo wa kifedha wa kuchapisha vitabu na kuvisambaza? Ninapata tabu kidogo ikiwa wale ambao wanapaswa wawe na 'uwezo wa kuwaelekeza wasion upeo' kuna kundi moja na hawa wasio na upeo. Je, Profesa anataka kutuambia mabenki, hayafahamu? Kiu kubwa Tanzania kwa sasa ni mikopo katika mabenki, SACCOs, and Microfinance. Ikiwa tayari umefanikiwa kuandika kitabu, sidhani ikiwa kuchapisha au kusambaza utashindwa. Ninavyofahamu mimi, mabenki yapo tayari kukubali hata mkataba wa ku-supply (order), kama moja ya ushahidi wa uhitaji wako wa fedha na uwezo wako wa kulipa. Hapo ndipo usomi wetu unapotushinda, kwamba vitu ambayo asiye msomi aliye na tenda ya kusambaza chakula mashuleni (kwa kutumia mkataba tu) anapata mkopo na anasonga mbele. Wasomi wetu tutabaki tunalia hadi lini?
  Kuhusu suala la pick-up ninakubaliana sana na waliompa changamoto hiyo Profesa. Kwa upande wangu wapo sahihi, kwani wakati huo ambao maisha yalikuwa ni magumu, hakuna usafiri, magari ya wagonjwa, aliyeweza kuleta pick-up alikuwa amefanya jambo la maana kwani aliweza kuokoa maisha ya akina mama wajawazito vijijini kuliko vitabu! Sio kila lilijema kwa mmoja ni jema kwa wote. Kila mtu upo sahihi katika hili.

  ReplyDelete
 11. Nakupongeza Prof Mbele kwa juhudi zako za kujaribu kuinua elimu ya Tanzania pasipo kukata tamaa, japo mazingira yanakatisha tamaa. Mimi ni muumini wa usemi wa kwamba, usikate tamaa kamwe. Nilikuwa naamini hivyo na ninaendelea kuamini hivyo hasa baada ya kufanya kazi huko umasaini na kwa wamng'ati vijijini kwa zaidi ya miaka 2.
  Nakusifu pia Prof Matondo kwa juhudi za kutunga kitabu kunufaisha watotot wa kitanzania.
  Nyumbani tuna matatizo makubwa 4
  1. Hatuna sera za elimu, tunadandia tu
  2. Ubinafsi, na kukubali kuhujumiwa na waandishi fulani ili wauze vitabu nchini na wizara kubadili mfumo na vitabu vinavyotumika ili mradi kukidhi asilimia kumi mtu aliyopokea
  3. Watendaji wetu hawana upendo au sijui niiteje, I mean they are not proactive and serious .... kuhusiana na kiwango cha elimu na ubora wake
  4. Watanzania wengi hawana utamaduni wa kupenda kusoma chochote, labda magazeti ya udaku, kwa sababu hakuna misingi imara ya watotot kufunzwa na kuelewa umuhimu wa kusoma vitabu au majarida ya kimaendeleo.
  Wenzetu wakienda kutembea na watotot wakirudi nyumbani, wanawaambia waandike matukio yote waliyo yaona njiani na baadaye kuja kuwasomea wenzao ni nini walifanya wakati wakiwa mapumzikoni. Hii inajenga upendo na hamu ya kusoma.

  ReplyDelete
 12. Anony wa March 20, 2011 3:08 PM;

  Umezisoma hizo changamoto za Mtanga na wengineo hapo juu? Je, Prof Mbele akichukua huo mkopo na kupeleka hivyo vitabu katika mashule Tanzania, ataurudishaje huko mkopo? Au unataka Profesa aingie mkenge na mwisho wake waje wataifishe nyumba na magari yake?

  Tuwe siriazi na hii ishu kwani ni muhimu sana. Tukiacha mambo ya nepotism na kupat attention kwenye uwezo wa watu na what they can give us tutafika mbali sana.

  Blessings !!!

  ReplyDelete
 13. Binti Kombo,
  Ninashukuru sana ikiwa hoja ya anonymous imekugusa. Ukweli ni huu hapa. Tuondokane na fikra za zamani za kudhani kwamba watu fulani ndio wa kupata hasara au ndio wa kuuziwa nyumba walizoweka reheni benki. Tufike pahali tumwonw huyu anayetafuta mafanikio ana uthubutu wa kuweka nyumba yake reheni benki akiwa mtizamo chanya wa kufanikiwa.Hilo ni la kwanza.

  La pili, kwa nini kutaki kufahamu kuwa uandishi wa vitabu ni business venture kama nyingine? Kwa nini wenngine wajaribu, either kwa kupata faida au hasara, lakini huyu wa vitabu asiwe na uthubutu huo kuwa sio kuandika vitabu tu ni pamaoja na marketing pia? Wanaofanikiwa katika fani nyingi ni pamoja na kuwa uwezo wa kuthubutu kuweka rehani nyumba zao. Hii ni kutokana na kufahamu fika kuwa kitabu chako ni kizuri na kina thamani zaidi hata ya nyumba yake na kitapata soko. Sioni kwa nini uwe mwoga wa kukopa Benki wakati hukuwa mwoga wa kukiandika! Lakini pia yawezekana hujanielewa sawa sawa, nimeandika hivi, ikiwa kitabu chako kimekubalika kitumike kama kitabu cha kiada, basi peleka ushaidi huo benki ukionyesha wazi kuwa soko tayari unalo. Sijasema uchukue mkopo benki halafu uchape vitabu uviweke Kariakoo sokoni au Msimbazi.Ukiwa mwelevu wa kuandika ni lazima uwe mwelevu na mbinu za kuuuza. Tufike sehemu tukubali kwamba uandishi au ualimu sio wito, ni fani kama fani nyingine. Vinginevyo tutabaki kusubiri huruma ya serikali tu. Tuendako, hayo hayapo tena.
  Mdau wa elimu

  ReplyDelete
 14. Anony - naomba urudi tena ukasome maoni ya mwanzo kabisa kuhusu changamoto kuhusu suala la vitabu Tanzania, maoni ya wadau waliofuatia, na ya Profesa Mbele mwenyewe. Yasome kwa makini halafu rudi tena utoe maoni yako upya.

  ReplyDelete
 15. Kwa ndugu Anonymous anayesema uandishi vitabu ni biashara kama biashara zingine, napenda kusema kuwa mimi ni mwalimu ambaye najali maadili na misingi ya ualimu kwa namna ambayo ni kama dini kwangu.

  Ninaandika vitabu kwa lengo la kuelimisha vijana na jamii. Ni kazi inayonifanya nitumie muda mwingi ili kuhakikisha kuwa ninawatendea vijana haki kwa kulingana na viwango vya taaluma.

  Siwezi kuihujumu shughuli hii kwa kuifanya ni biashara. Kitabu changu kimojawapo kuna jamaa walinishauri nikiwekee masuali na majibu ili kitumike kwenye "tuition." Walinihakikishia kuwa hapo nitauza sana na kujipatia hela.

  Sikufuata ushauri wao, kwa sababu kitu kinachoitwa "tuition" nakiona ni hujuma dhini ya elimu. Elimu ninavyofahamu mimi ni utaratibu wa kumfanya kijana afikiri, apanue mawazo, si kukariri mambo au kutafuniwa na kuwekewa mdomoni kama kifaranga. Elimu inamjengea mtu akili ya kuwa na duku duku ya kujua na kutafuta elimu.

  Siwezi kuwatumia watoto au vijana wetu kama fursa ya kufanyia mradi wa pesa. Ingekuwa natafuta pesa, ningeshaandika vitabu vingi sana. Lakini mimi hutumia muda sana kuandika kitabu kimoja. Kwa mfano kitabu cha "Matengo Folktales" kilinichukua miaka yapata 23 ya kuandika, kurekebisha na kutafakari, hadi nikachapisha.

  Yawezekana kuna vitabu ambavyo ni sawa vikiwa ni vya biashara. Lakini mimi sijui ni namna gani nitaandika vitabu vya aina hiyo. Kila nikiwazia kitabu nakiwazia kwa misingi ya manufaa yake kwa msomaji.

  Mimi naona wajibu wangu ni kufanya utafiti, kufundisha na kuandika. Nikishaandika kitabu na kukichapisha, nahitaji kuendelea na uandishi wa kitabu kingine. Naamini ni juu ya wengine, ambao wanafanya biashara ya vitabu, kama hao wenye maduka ya vitabu, kutafuta hiyo mikopo ya kununulia vitabu vyangu na kuvisambaza. Hiyo ndio kazi yao.

  Mimi mwalimu sipaswi kuacha kazi ya ualimu na kuwa nahangaika na mikopo ya biashara, halafu nitafute magari ya kusafirishia, nigombane na dreva na utingo, nifuatilie mahesabu, na kadhalika. Kazi yangu ya ualimu itadorora.

  Tuwe na mgawanyo wa kazi, ndipo tutapata mafanikio makubwa kwa pande zote.

  ReplyDelete
 16. Profesa,
  Ninaheshimu sana mawazo yako. Nimefurahishwa na majibu yako ambayo yapo wazi mno kwamba tatizo kumbe sio fedha, bali ni mgawanyo wa kazi katika jamii. Naam, na huo ndio mtizamo wa soko huria, maana huko ndiko tulikotoka enzi za Mwalimu ambapo Kiwanda cha sukari kiweza kuzalisha bidhaa na kuhakikisha infika hadi kwnenye duka lake lililopo Songea. Matokeo yake ni kwamba tulikuwa uchumi usio na ushindani kwa kukosa creativity and productivity maana huwezi tumikia mabwana wawili, ni lazima mmoja utampoteza (Watu wa gender samahanini msije nishukia kama mwewe).

  Ningaliendelea kupata tabu kidogo ikiwa unauwezo wa kufanya utafiti unaokuchukua miaka 23, ambayo kwangu mimi ni sawa na ng'ombe mzima kumla, halafu ushindwe kumalizia mkia. Kimsingi hiyo ndio hoja iliyonipelekea kuzidi kushangaa. Pia, nimefurahishwa mno kwa kugusia kwamba uandishi au sekta ya vitabu ni biashara kwa upande mmoja, ingawa sio kwako maana unayo majukumu tosha. Lakini, Nimekuelewa zaidi pale ulipogusia kuwa huandiki ili upate pesa au utajiri utokanao na kazi yako, bali ni huduma kwa jamii. Nami ninatoa wito kwamba, kwa mlengo huo, ni vizuri basi watu wenye mtizamo wako mkajaribu kuwatafuta wahusika (nadhani mnawafahamu na uwezo wa kuwafikia mnao) mkianza na Mh. Rais kuanzisha mjadala wa namna gani watu wenye nia kama yako, mnaotaka kujitolea ili nayo serikali ione namna gani ya kuwaongezea nguvu au kuwawezesha. Kwani baada ya kila siku kuona picha za waheshimiwa wakipokea misaada ya vitabu kutoka Marekani na Uingereza, sasa ifike mahala, tuone musanyiko wa waheshimiwa wetu wakipokea kazi kuotoka kwa Watanzania na wazalemdo hasa ambazo serikari hiyo hiyo imechangia kuifanikisha. Hapo naliona ni jukumu la serikali kwa watu wenye mtizamo wenyu kuwasaidieni.
  Asante Prof. kwa majibu yako kila kheri na wito wa kusaidia.
  Mdau katika elimu

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU