NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, March 10, 2011

MWANAUME AUAWA KWA KUZUIA MVUA !!!

 • Kama jamii, bado tuna safari ndefu ya kwenda. Ni haki kweli katika karne hii na wakati huu bado tunauana kwa sababu ya kuzuia mvua? Imani hizi za kishirikina zinazozidi kujiimarisha zinatupeleka wapi lakini? Tatizo hasa ni nini? Ni umasikini? Ni ugumu wa maisha? Ni mfumo mbovu wa elimu? Ni nini? Tufanye nini?
*************************
Mwanamume auawa kwa kuzuia mvua 
(Wednesday, 09 March 2011)

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

EREST Khamis (45), mkazi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kushiriki kumuua baba yake mzazi wakimtuhumu kuzuia mvua kunyesha mkoani humo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zellothe Stephen, amesema tukio hilo limetokea jana saa 2 usiku wilayani humo.

Amesema mtuhumiwa huyo alimshambulia baba yake, Khamis Hussein (70), kwa kumpiga kwa madai kuwa ndiye aliyesababisha mvua isinyeshe katika mkoa huo.

Ameongeza kuwa kulikuwa na taarifa za muda mrefu kuwa marehemu alikuwa akihusika katika uzuiaji wa mvua ambapo baadhi ya wanakijiji walimfuata mtoto wake huyo na kumuelezea kero hiyo.

Kutokana na kitendo hicho, mtoto huyo aliamua kumpiga baba yake kwakuwa ndiye anayejua ukweli wa madai hayo na polisi watamfikisha mahakamani.

Chanzo: Dar Leo 

Mzunguko wa Maji - Kwa mtazamo wa "wanasayansi"

5 comments:

 1. Hili ni tatizo, ni tatizo kubwa sana kwani adui ujinga katuzunguka kila kona. Namkumbuka profesa Mbele kwa nasaha zake,....kuwa Watanzania hawataki kusoma, hawataki vitabu, wanataka nini...`pick-up', wanataka nini...`maisha bora' wanataka nini...
  Je tutavipata hivyo kirahisi rahisi tu...kwa imani tu...sio siri imani za kishirikina zinazidi kuongezeka badala ya kupungua. ...
  Jamani hii sio LAANA , TENA LAAA KUBWA!

  ReplyDelete
 2. Kama kweli baba yake alikuwa anazuia mvua au la tutajuaje, Jamaani? Mbona wengine wanaamini mtu aliyekufa miaka 2000 iliyepita atafufuka siku moja nakuja kututawala miaka 1000 na hamna anayedai "huo ni ujinga"?


  Ni kweli kwamba ujinga mwingi. Lakini tusishambulie aina moja ya ujinga lakini aina ingine tubariki. HUO UBAGUZI WA IMANI ZA KIAFRIKA NDIYO ITAKUWA UJINGA HALISI!

  Afrika Kusini hapa tunayo imani nasi (hasa makabila ya Wapedi labda na Wavenda kaskazini na nchi mpakani waZimbabwe) kwamba mvua inategemea sana maombi ya binadamu. Tunaye hata mwanamama anayechaguliwa kuwa RAINQUEEN!


  Mimi binafsi naheshimu sana hizi imani za watu ikiwa ni zile za Marehemu Miaka 2000 au wenye kuzuiya au kuombea mvua. NINACHOKATAA KOTEKOTE NI UMWAGAJI WA DAMU!

  ReplyDelete
 3. Bwana Manyanya;

  Asante sana kwa maoni yako ya kufikirisha ambayo umekuwa ukiyatoa katika blogu hii na nyinginezo. Asante sana!

  "Mbona wengine wanaamini mtu aliyekufa miaka 2000 iliyepita atafufuka siku moja nakuja kututawala miaka 1000 na hamna anayedai "huo ni ujinga"

  Hili nawaachia wenyewe "wakereketwa" wajitetee.

  KWINGINEKO

  Hata sisi Wasukuma tulikuwa na watu ambao waliaminika kuwa walikuwa na uwezo wa kuleta mvua. Nakumbuka nilipokuwa darasa la nne kulikuwa na ukame mkubwa sana na wanakijiji walichangishana na kwenda kumleta mtaalamu wa kuleta mvua kutoka Musoma. Mleta mvua huyu alitoa wiki mbili na mvua ingeanza kunyesha. Wiki mbili zilipita hakuna mvua, mwezi mzima, miezi mitatu hakuna mvua. Ikabidi aondoke huku akidai kwamba pengine wanakijiji walikuwa hawatimizi masharti aliyokuwa amewapa - mojawapo likiwa ni kutokula Masangu (makande!) - chakula cha kawaida kwa Wasukuma, na watoto wa kike kutonyoa nywele! Aliwaacha wanakijiji wakilaumiana na kunyosheana vidole kama mmoja wao pengine alithubutu kupika Masangu, au kunyoa nywele za mtoto wa kike kinyume na masharti ya "mleta mvua yule"

  Baadaye ikagundulika kwamba miti yote ilikuwa imekatwa na kampeni kubwa ya HASHI (Hifadhi Ardhi Shinyanga) ikaanzishwa kwa msaada wa serikali ya USWIDI. Miti ikapandwa na hali ikaanza kubadilika.

  Mimi ni Mkereketwa mkubwa wa utamaduni wa Mwafrika na sikatai wala kupinga imani zetu zote. Pia kuna mambo mengi tu kutoka utamaduni wa Kimagharibi ambayo sikubaliani nayo. Ukisoma kwenye blogu yangu hasa kile kipengele cha utafiti utaona ushahidi kuhusu imani yangu hii.
  Najua pia kwamba sayansi bado haijaweza kueleza mambo yote yanayotokea katika jamii zetu lakini nahisi kwamba inabidi tuanze kuziangalia baadhi ya mila zetu kwa jicho kali na kuzifanya zishabihiane na wakati tulionao.

  Wakati dunia nzima inapiga makelele kuhusu "Global Warming" na madhara yake kwa hali ya hewa, sisi bado tunalaumiana na kuuana kwa kuzuia mvua. Wataalamu wanaonya kwamba nchi za ulimwengu wa tatu ndizo zitakazoathirika zaidi na mabadiliko haya ya hali ya hewa. Pengine ukame unaokumba sehemu kubwa ya nchi za Kiafrika ni tokeo la mabadiliko haya ya hali ya hewa.

  Siamini kwamba kuna mtu anaweza kuzuia wala kuleta mvua. Na hili nililitambua miaka mingi iliyopita nilipokuwa darasa la nne wakati mleta mvua yule alipoondoka na ng'ombe wa wanakijiji na kuwaacha wakilaumiana na kunyosheana vidole kwa kupika Masangu na kunyoa nywele watoto wao wa kike!

  Badala ya kulaumiana na kuuana kwa kuzuia mvua pengine ni vizuri tukahamasishana kupanda miti na au kuanzisha kilimo cha umwagiliaji maji - kama hili linawezekana (Dodoma ni nusu jangwa !!!)

  Hebu mjadala huu na UKARINDIME !!!

  ReplyDelete
 4. Bwana mdogo Matondo, mimi ninakushangaa sana unaposhangaa ni kwa vipi mtu katika jamii yetu ya Kitanganyika anashambuliwa eti kwa kuzuia mvua isinyeshe! Mbona wabunge wakiwamo na maprofesa waheshimika kama wewe na wao huenda kwa mafundi (waganga)ili kusafisha nyota zao wapate ushindi katika kura? Wabunge karibia wote wa Tanzania wameenda shule tunategemea kwamba wametoa tongotongo katika macho yao na kwa hivyo wana fursa ya kuwa na upeo wa hali ya juu sana katika kutengeneza falsa nzuri ambazo zinaweza kuifanya nchi yetu kuwa na muskabali mzuri. Nadhani mimi ninatofautiana na wewe na kwahiyo sishangazwi sana na huyo mtu kuuawa eti kazuia mvua isinyeshe; kitendo hiki kiko ndani ya kiunzi cha imani. Ushirikina nao ni imani kama ulivyo Ukristo au Uislamu na dini zinginezo nyingi.

  Nadhani nikipata muda wa kutosha nitazungumzia vya kutosha juu ya swala hili. Labda tu ni kwamba, kwa mtizamo wa Kikristo au Kiislamu huyu mtu aliyeuawa yuko upande wa shetani. lakini nakuomba ujibu swali hili:

  "Kama kuelimika (kuwa na elimu katika mfumo rasmi)ni kuwa na mfumo mpevu na mpana kijamii, mbona wasomi wengi huenda kuangalia mambo yao kwa masangoma?"

  ReplyDelete
 5. The Shashulas

  "Kama kuelimika (kuwa na elimu katika mfumo rasmi) ni kuwa na mfumo mpevu na mpana kijamii, mbona wasomi wengi huenda kuangalia mambo yao kwa masangoma?"

  Kuna mikabala mingi ya kuliangalia swali hili - mojawapo ni kuhusu kiini na misingi ya elimu yenyewe, elimu ambayo wewe umeiita rasmi! Au tuanze na swali ambalo niliwahi kuliuliza hapa: "Msomi" ni nani????

  http://matondo.blogspot.com/2010/02/fikra-ya-ijumaa-ati-msomi-ni-nani.html

  Kama wanavyodai wanaharakati wengi (mf. Walter Rodney, Paulo Freire na Julius Nyerere), elimu hiyo rasmi ilikuwa na lengo la jumla la kumtenga Mwafrika na utamaduni wake na hivyo kumfanya ajidharau. Na ukimfanya mtu ajidharau na kumshinda kisaikolojia basi utaweza kumfanyia cho chote unachotaka (The most potent weapon at the hand of the oppressor is the mind of the opressed - Steve Biko!)

  Napenda kusema kwamba lengo hili la jumla la elimu ya kikoloni lilishindwa au pengine tuseme lilifanikiwa nusunusu. Japo watu walizikana imani na utamaduni wao, hawakufanya hivyo kwa asilimia 100. Ndiyo maana wako huku na huku. Unakuta mtu ni "msomi" au mchungaji/shekhe lakini pia anakwenda kwa masangoma.

  Mtazamo huu ulisisitizwa na Placide Tempels, mmishenari wa Kibelgiji aliyeandika kile kitabu mashuhuri cha Bantu Philosophy. Mojawapo ya dai lake kuu katika kitabu hiki ni kwamba Mwafrika hata 'asome" namna gani, huwa hawezi kuutupilia mbali utamaduni na falsafa yake ya msingi - ambayo kwa upande mmoja inajumuisha kuamini katika mzunguko wa maisha usio na kikomo (maisha -> kifo -> mizimu -> miungu -> maisha -> kifo ->->->->).

  Kwa hivyo kwenda kwa masangoma siyo tatizo la msingi na wala la kushangaza. Imani zinaweza kuhamisha milima na kama "wasomi" hawa wanakwenda huko kusafisha nyota zao binafsi na wanaamini kwamba kweli nyota zao zimesafishika, ni nani wa kuwapinga? Japo ni hivi, inabidi tuzishabihishe imani hizi za kijadi na hali na mazingira halisi tunamoishi - na ukiangalia vizuri vitu hivi vinaweza kwenda pamoja na si lazima viwe katika ukizani. Si ajabu basi "msomi" kwenda kwa mganga wa kienyeji kutafuta tiba ya kienyeji Loliondo au kwingineko!

  Inabidi tuliangalie suala hili kwa upana wake na tupinge mambo ambayo kama yakiachwa yanaweza kutuletea madhara makubwa. Hatuwezi kukaa kimya wakati maalbino wanauawa kwa sababu eti mtu kaenda kwa mganga na kupewa masharti ya utajiri yanayojumuisha mguu wa albino, kubikiri mtoto mdogo na mambo mengine kama hayo. Na badala ya kuhamasishana kuhusu kupanda miti na kutunza mazingira yetu ili kuzuia ukame, mbona tuendelee kukazania waleta mvua ingawa tuna ushahidi kwamba watu hawa hawaleti mvua; na ndiyo maana tuna ukame? Vipi tukibadilisha na kusema kwamba waleta mvua wanaweza kuleta mvua kwa urahisi kama tutapanda miti kwa wingi, kuzuia mmomonyoko na kutunza vyanzo vya maji?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU