NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, March 28, 2011

SERIKALI INAPOKIMBILIA LOLIONDO KUPATA KIKOMBE CHA BABU....

 • Ati, hii tabia ya "serikali" kukimbilia Loliondo "kutibiwa" inatoa taswira gani kwetu kama jamii? Na leo hii, baada ya kufanya utafiti wake, serikali imetoa tamko lake rasmi ikisema kwamba dawa hiyo haina madhara kwa binadamu; na kwamba inaendelea kuifanyia uchunguzi. Serikali pia itaboresha huduma kule Loliondo ili kupunguza vifo vya wagonjwa. Mungu Aendelee kuibariki nchi yetu!
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, akipata kikombe cha tiba ya babu, katika Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro juzi. (Picha na Lilian Joel)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa bunge ), William Lukuvi (wa pili kulia) na Rosemary Nyerere wakipata kikombe cha babu Loliondo. Picha kutoka kwa Mjengwa.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Teresya Huvisa akipata kikombe cha Babu Loliondo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk Yohana Balelel wakipata tiba ya mchungaji Ambilikile Mwasapile wa kijiji cha Samunge, Loliondo.


  Huyu bila shaka wamjua!

Hapa chini ni kikombe kipya cha Mama wa Tabora !

9 comments:

 1. Ndugu yangu, hapa hata mimi nimeshindwa kuelewa. Sikuwa na habari ya kuwa wanene wote hawa wameshafika kwa babu, tena inaelekea vikombe vya babu ndio hivyo hivyo vinatumika kwa watu wote. Sina uhakika na usalama wake kwenye masuala ya usafi. Ama kweli.... imani kweli huponya na wakati mwingine kumfanya mtu kuwa kipofu na kiziwi.

  ReplyDelete
 2. Kinachodhihirisha hapa ni ombwe la fikra na kutapatapa. Pia huu ni ushahidi kuwa watanzania ni wagonjwa kuliko watu wote. Ugonjwa wao mkubwa ni imani haba na kutofikiri sawa sawa. Hawa wakubwa wanaowenza kuamini kila upuuzi ni hawa hawa wanatumiwa na matapeli wa kimataifa kutuibia kwa njia ya mikataba tata. Matapeli wamefanikiwa kutokana na kujua udhaifu huu wa kufikiri na kuamini kila upuuzi. Kesho mtamuona rais na mkewe wakienda kupata kikombe. Ajabu wakubwa hawa ambao ni public figures hawatwambii wanaumwa nini na kwanini wanatumia pesa zetu nyingi kwenda kutibiwa ulaya.
  Hii licha ya kuwa kashfa na aibu kwa taifa, ni pigo la ajabu. Kesho ataibuka mwingine na upuuzi mwingine tutapwakia. Na huu ni ushahidi tosha kuwa hata wale matapeli wa makanisani wanavumiliwa kutokana na kuwa na watawala wasiofikiri sawa sawa na waumini wa ushirikina na kila upuuzi.
  Badala ya kukimbilia kwa babu boresheni huduma za afya kwa kupambana na ufisadi.
  Yaani tulishindwa kujifunza toka kwa akina Kibwetere, Kolesh na wengine?
  Ujiko anaopata babu ndio unawaowatoa roho akina Kakobe, Mwingira na matapeli wengine.
  Kesho mtasikia shehe akitangaza kuoteshwa dawa ili awatibu waumini badala ya kazi hii kufanywa na makafiri. Hiyo ndiyo Tanzania yenu ya Nyerere.
  Kwanini Tanzania siyo nchi nyingine? JE sisi ni wacha Mungu sana au wepesi wa kuamini kila kitu hasa ushirikina? Maswali ni mengi kuliko majibu. Wakubwa kapimeni badala ya kujihadaa na miigizo. Pia wananchi rudini kwenye hoja za kupambana na ufisadi badala ya kuzugwa na umaarufu wa soda wa babu.

  ReplyDelete
 3. jamani mimi sipingani na maoni ya mtu bali kama watu wamepona je kunaswali hapo wewe unayesema selikali nayo kwani sio binadamu nafikiri watu waliopona ndo wanaojitangaza na wala si babu hakuweka bango lolote hivi huwa unafyatilia mkasa huu vzr au umekurupuka from no where mimi nafikiri suala hapa ni kumuacha babu aponye watanzania na unasema watanzania je hujaona waganda na wakenya wakimiminika kwa babu tena hata boda hawapitii wanachanja mbuga kwenda kwa babu mwenyewe hapo usikute ndugu zako wengi wameenda who knows haya mambo kama unaimani duni bora kuyaacha kama babu muongo atakuja kuumbuka na kama ni kweli wewe utauficha wapi huo uso

  ReplyDelete
 4. nilichogundua ni kwamba watu wanaumwa sana magonjwa mengine ni ya kutia huruma. cha kufanya hapa ni watu kuwa makini na chakula tulacho ili tuweze kuwa imara

  ReplyDelete
 5. NJIA NYEMBAMBA NI YA UZIMA NA NJIA PANA NI YA KUZIMU

  ReplyDelete
 6. Chib - kweli imani ni imani. Tunaambiwa kwamba kama tungekuwa na imani basi tungeweza hata kuhamisha milima!

  Mwalimu Mhango - Loliondo imesaidia kututoa katika mijadala ya mambo mengine muhimu yaliyokuwa yanarindima. Leo hii husikii tena kuhusu mambo ya katiba mpya wala mambo mengine muhimu. Kila kitu ni Loliondo - utafikiri kwamba Loliondo ndiyo utatuzi wa matatizo yetu yote mengi yanayotukabili.

  Anony. wa kwanza: Naona umenirarukia tu hata bila kusoma vizuri na kuzingatia hasa lengo la post yangu hii. Nakuomba usome tena hiyo mistari yangu michache hapo juu kisha urudi tena kutoa maoni.

  Kimsingi sina ugomvi na Mzee wa Loliondo kwani masuala ya imani wakati mwingine huwa hayaelezeki Kisayansi. Mimi mwenyewe nilishawahi kutokewa na muujiza na naamini katika nguvu zilizo kuu - ama kutoka kwa Mungu au kwingineko - na wakati mwingine ndani yetu wenyewe. Pamoja na ukweli huu, hata hivyo, ninachohoji ni kwamba serikali hapa inatoa taswira gani kwa watu wake nayo inapokimbilia kwenye miujiza hii ya kiimani? Ndiyo, waheshimiwa hawa nao ni watu lakini pia ni wawakilishi wetu na tunawategemea watuonyeshe njia ya utatuzi wa matatizo yetu mengi yanayotukabili - mojawapo ni hili la huduma za afya zisizoridhisha hasa kwa watu masikini kule vijijini. Pengine nawaza kwa sauti tu, lakini ni kweli wanataka kutuaminisha kwamba katika wakati huu tulionao tunaweza kutegemea miujiza hii ya kiimani kama utatuzi wa matatizo yetu yanayotukabili?

  Sitaki kuuhamishia mjadala unaorindima kule kwenye blogu ya Mjengwa (mjengwa.blogspot.com) kuhusu jambo hili hapa. Au maoni na mjadala wa kina ulioanzishwa na mdau katika blogu ya Da Chemi (http://swahilitime.blogspot.com/2011/03/maoni-ya-mdau-kuhusu-mjengwa-blog-na.html) - kwani itakuwa ni kurudia hoja zile zile kutoka pande zote mbili.

  Pia kama unafuatilia habari vizuri, tayari tuna watoa vikombe watatu sasa - mmoja yupo kule Mbeya (yeye kaoteshwa dawa na marehemu mamake) na mwingine kaibuka kule Tabora. Kule Rombo pia mtoa kikombe mmoja ilibidi apigwe marufuku (sijui kwa nini!). Cha ajabu ni kwamba kote huko watu wanamiminika kwenda kupata hizi tiba. Wewe unalionaje hili? Serikali inalionaje? Tazama hapa:

  http://www.wavuti.com/4/post/2011/03/mwingine-aibuka-tabora-na-tiba-ya-kikombe.html?utm_source=feedburner&utm_medium=feed&utm_campaign=Feed%3A+wavuti+%28Wavuti%29#axzz1HyhHih1k

  Miujiza ipo,imani zinaponya lakini sitaki kuamini kwamba huu ndiyo mkabala ambao serikali yetu inataka tuuchukue kutatulia matatizo yetu mengi yanayotukabili!

  Kamala - Ni kweli kwamba magonjwa mengi tunayapata katika mazingira tunamoishi - vyakula vibovu, mipombe, sigara, ngono zembe n.k. Pengine miujiza hii ndiyo itatuokoa ati!

  Anony. wa mwisho - Loliondo ni njia nyembamba au pana? Tufafanulie!

  ReplyDelete
 7. Ndugu yangu Matondo swala la tiba halina taswila na wala halihitaji msukumo kutoka kwa watu wanaoitwa ‘’public figure’’, unapougua hasa ugonjwa usiokuwa na tiba au tiba ambayo haipatikani kwa urahisi kutokana na gharama au umbali, huhitaji msukumo wowote kwenda kupata tiba unayoamini itakuponya na upatikanaji wake ni rahisi. Ikumbukwe kuwa hakuna mtu hai anayependa kufa na katika hili binadamu hawapendi kulifikilia kama linaweza kutokea ndiyo maana ‘’Dr Remmy Ongalla’’ katika wimbo wake wa kifo alisema kama kifo angejua alipo angempatia ruswa ili aishi milele pamoja na kujua rushwa ni adui wa haki na ni kosa kisheria. ‘’Dr Remmy Ongalla’’ ujumbe wake ni kuwa binadamu anapokumbwa na gonjwa atafanya lolote ili apone.
  Ninakubaliana na Ndugu NN Mhango anaposhauri ‘’serikali’’ kuboresha huduma ya afya , labda kama ingekuwa imeboreshwa, tusingeshuhudia maelfu kwa maelfu ya watu wakienda kwa ‘’Babu’’ kupata kikombe.
  Sikubaliani kidogo na Ndugu NN Mhango anaposema Watanzania wana imani haba na kutofikili sawasawa akiwa na maana ya watanzania wanaoenda kwa ‘’Babu’’. kama hii ndiyo fikra yake basi hata waumuni katika madhehebu yote wana imani haba na ukosefu wa fikra kwa kuwa hakuna ‘’tangible evidence’’ inayoonyesha kama wanachokiamini kipo. Ninachojua ni kwamba, Imani haipimiki na fikra huendana na imani. Mpaka leo kuna misuguano ya mawazo, imani na ushahidi kati ya creation na evolution. Hii haitupatii haki kusema upande mmoja una imani haba na haufikili sawasawa. Dawa ya ‘’Babu’’ imejikita zaidi katika imani, Ikumbukwe kuwa hawa ‘’serikali’’ ni binadamu kama binadamu wengine na kuna ushuhuda wa watu ambao wamepata ‘’kikombe’’ wakapata nafuu au wamepona.
  Sikubaliani pia pale Ndugu Mhango anaposema hii ni kashfa, aibu kwa Taifa na upuuzi, kwangu naona kama ametoa hitimisho mapema kabla ya utafiti. Ninatanguliza samahani yangu kama nitakuwa nimemnukuu kimakosa na kama sivyo basi hii siyo dalili nzuri ya utoaji maamuzi hasa nikizingatia yanatoka kwa mwanazuoni. Sina uhakika kama binadamu wa kawaida watashangaa kumuona rais na mkewe wakienda kupata ‘’kikombe’’ kwa ‘’Babu’’ kwa sababu nao ni binadamu wa kawaida. Ndiyo, hii ni Tanzania ya nyerere aliyoitaka iwe katika msahafu wa Azimio la Arusha sehemu ya kwanza, Imani ya TANU katika kipengele (a-i) Kwamba binadamu wote ni sawa... (Rejea kwenye blog ya Matondo katika sehemu ya pata nyaraka mbalimbali kipengele cha Azimio la Arusha kupata maelezo zaidi.
  Nitashangaa kama nikiona au kusikia kiongozi wa serikari akiwahimiza wananchi waende kwa ‘’Babu kupata ‘’kikombe’’ lakini natumaini mpaka sasa hilo halijafanyika na kwa maana hii, serikali haijavua wajibu wake wa kuboresha sekta ya kiafya kwa wananchi wake.

  ReplyDelete
 8. Salma na Mrisho wameshakunywa kikombe hata kama hayo hayakuwekwa wazi. Hata kama ningekuwa ni rais na nina uwezo wa kubadili damu kama nguo ya ndani, ikiwa kuna ushahidi toka kwa wanene wenzangu kwamba LOLIONDO upo ufumbuzi kwanini nisiende?

  Watu kwenda LOLIONDO si kwamba ni wapuuzi, miaka yote mtu kahangaika huko mahospitali na kisukari au gonjwa lolote lile linalomsumbua halina ufumbuzi kwanini asiende?

  Mimi nimekwenda huko na nimekunywa kikombe hicho, huko tulikuwa kwenye foleni moja na the so called wazungu ambao ni werevu, but who knows labda wamekwenda kule out of curiosity ama na wao pia wako kwenye utafiti wao. Kabla ya babu wa LOLIONDO tiba za miti shamba zilikuwepo na watu walikunywa si ajabu hata hao wanojifanya kushangaa watu kunywa kikombe kwa babu walishakunywa, kufukizwa au hata kuogea madawa. Yashangaza nini mtu kuchemsha majani ya mlonge, mpera au muarubaini kutibu tatizo alilonalo?

  Watu washekula vinyesi vyao na kunywa mikoja ili kutatua matatizo yao vipi kikombe kiwe issue? Eti ni umati mkubwa wa watu wanatumia niambie ni wapi tunatembea na vikombe na vijiko vyetu tunapotaka kupata huduma ya chakula? Kule vikombe vipo na vinaoshwa kama ambavyo unapokwenda kwa mama/baba lishe au hata huko mahotelini.

  Watu ni wagonjwa na wanataka tiba, kwani nani anahaja ya kumeza mavidonge mpaka uhai umtoke? Hata huko kuliko na maendeleo pamoja na huduma zao nzuri kwani wamefunga hospitali zao? Si watu wanaugua kila siku? Kama ufumbuzi upo LOLIONDO kwanini tusiende? Mwenye imani na aende asiyekuwa nayo na abaki kwani babu kafunga watu kamba na kuwaburuza LOLIONDO?
  Kwani matangazo ya wanganga wa kienyeji kwamba wanatibu nguvu za kiume na UKIMWI si yapo siku nyingi na hospitali zipo? Ni kwanini watu hunywa MKUYATI na nyinginezo? Ni kwakuwa wana matatizo. Hapa yatasemwa mengi lakini LOLIONDO aende mwenye imani yake kama huna kaa, na sasa hospitali hakuna foleni au na madaktari nao wako huko?

  Matatizo mengine ya akina DOWANS na mengine yapo huenda watu wanakwenda kujitibia ili wasizirai hovyo na kuyakabili.

  CIAO.

  ReplyDelete
 9. Kama kutakuwa na mgonjwa hata mmoja tu atakayethibitishwa na madaktari kwamba amepona ugonjwa wake baada ya kunywa dawa hii basi wote wenye mashaka na dawa hii watafunga midomo.

  Tuwe huru kuwaza na kuhoji - hasa kwa mambo mazito kama haya yanayohusu mwelekeo wetu kama jamii - Jamii ya miujiza, jamii ya vikombe ! (Loliondo, Rombo, Mbeya, Morogoro, Tabora, Magu ....)

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU