NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, April 17, 2011

BAKITA LAWASHUKIA WABUNGE: NI KUHUSU KUCHANGANYA LUGHA BUNGENI

 • Huwa unajisikiaje unapomsikia mbunge wako akitoa hoja bungeni huku akichanganya Kiswahili na Kiingereza? Huwa unamwelewa? Kama huwa unamwelewa basi ni wazi kwamba unafahamu Kiingereza. Ingekuwaje kama ungekuwa hufahamu Kiingereza? Wabunge hawa wanapochanganya lugha namna hii, huwa wanafikiria kwamba kuna watu wanaowawakilisha ambao Kiingereza hawakifahamu (vizuri)? Kuna ulazima wowote kwa "waheshimiwa" hawa kuchanganya lugha namna hii? Wewe nawe huwa una tabia ya kuchanganya lugha katika mazungumzo yako? Kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini huwa unafanya hivyo? 

****************
BAKITA lawashukia wabunge
(Alhamisi, 14/4/2011)

*Wadaiwa kuwaacha wananchi hewani
*Latamani kuwafunda
*Lugha yatajwa tatizo

Na Simon Nyalobi, Jijini

BARAZA la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) limewakumbusha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumia Kiswahili pekee badala ya kuchanganya na Kiingereza kwani linawafanya wananchi kutoelewa vizuri hoja zao.

Akizungumza juzi na Dar Leo Ofisini kwake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bakita, Noel Karekezi, alisema wabunge wanatakiwa kulitambua hilo kila wanapochangia hoja zao ili waeleweke na wananchi.

“Malalamiko yetu tangu awali ni uchanganyaji wa Kiswahili na Kiingereza. Unakuta wanajisahau kuwa wanazungumza wenyewe kumbe wanasikilizwa na wananchi wengi,” alisema.

Amesema kuchanganya lugha hizo kunawafanya wananchi kushindwa kuelewa hoja wanazozitoa na hivyo kuwataka kujifunza kutumia Kiswahili wakati wakitoa hoja zao.

Amekiri suala la uchanganyaji wa lugha hizo ni la kitaifa kutokana na mazoea yaliyojengeka katika jamii.

“Wakati mwingine tatizo la kuchanganya lugha ni gumu kuliacha kwa sababu unakuta Kiswahili unatumia nyumbani na Kiingereza unatumia ofisini,” alisema.

Ameongeza kuwa BAKITA ina azma ya kuwapa semina wabunge hao, lakini kutokana ufinyu wa bajeti wameshindwa kutimiza azma yao lakini bado wataendelea kuwakumbusha juu ya matumizi ya Kiswahili.

Katika hatua nyingine, Kaimu Katibu Mtendaji huyo amesema wahisani wengi toka nje ya nchi wamekuwa wazito kukubali kufadhili uenezwaji wa lugha ya Kiswahili kwa kile alichodai kuwa wengi wanataka lugha na tamaduni zao ziendelezwe.

Chanzo: Dar Leo.
 • Ni kutokana na kikwazo hiki cha lugha kwamba serikali imeamru muswada tata wa katiba uandikwe katika Kiswahili kwanza ili uweze kusomwa na Watanzania walio wengi. Pengine huu ni ushahidi kwamba Kiingereza kimeshatushinda na inashangaza kidogo kuona kwamba hatufanyi lolote la maana katika kurekebisha sera yetu kengeufu ya lugha. Hata Profesa Mbele alishawahi kuombwa kuandika kwa Kiswahili kwa sababu Kiingereza hakieleweki!
 • Msikilize Anna Makinda hapa akitoa ufafanuzi kuhusu suala la lugha katika muswada wa sasa wa katiba. 

8 comments:

 1. Mimi binafsi hali hii inanikera sana. Sio wabunge, sio Raisi, kiswakinge kama kawaida.

  Wasanii wa filamu za kiswahili Tanzania ndio wananikera zaidi. Natambua kuwa kila kionekanacho katika kazi hizi zina maana kifasihi. Lakini kwa mchanganyo huu katika filamu, ninakosa tafsiri kabisa. Mtu anapokwambia "nimekuona live" au "tutoke out", au "tukaspend" kwa kweli kwa kazi ya fasihi, huwa nashindwa kutafsiri kuwa wanafasihi hawa huwa wanakusudia kuifunza ama kuiambia nini hadhira hususani ya Tanzania. Hata muongea kimombo ataelewa kweli?

  ReplyDelete
 2. Kwa vile Kiingereza kinachukuliwa kama lugha ya wasomi na wabunge wetu wengi hawaamini katika usomi wao kutokana na sababu wazijuazo, wanajaladia kwa kuchanganya kimombo na kiswahili. Hii ni dalili na ishara mojawapo ya kutojiamini au kutoiva vilivyo kisomi.
  Hii haina tofauti na watu kupenda kuitwa madaktari au maprofesa ili waonekane wasomi. Msomi hategemei cheo wala vikorombwezo bali mchango wake kwa jamii na kwake binafsi.
  Akina Socrates, Heraclitus, Sophocles, Plato, Demacritus na wengine wengi hawakuwa na shahada hata moja lakini bado ni wasomi wa kupigiwa mfano. Shaaban Robert aliishia darasa la nne. Lakini ni msomi wa kupigiwa mfano. Hivyo, kwa ufupi ni kwamba kuchanganya Kimombo na Kiswahili ni njia nzuri ya kujifunua kwako ili uwatathimini vilivyo. Ni hao hao wanapata kigugumizi ima kupitisha kiingera au kiswahili kama lugha ya taaluma. Hamkumbuki baadhi ya wachangiaje walivyowahi kumsakama mwenye blogu hii kwa kudai lugha si ngumu au yenye maana ikilinganishwa na sayansi? Maskini wajinga hawa walisahau kitu kimoja-bila hiyo lugha hiyo sayansi utaiawilisha vipi? Kusoma na kuelimika vilivyo ni suala la kuwa makini na unavyotumia akili ya kawaida na unavyojitambua kama mtu binafsi tofauti na wengine wanavyokutambua au unavyotaka wakutambue. Elimu ya kuaminisha kuwa mhusika kaelimika au anayo si elimu kitu bali aina nyingine ya ujinga unaofichwa kwenye 'elimu'.

  ReplyDelete
 3. Mwalimu Matondo - I can't believe your blog was found. Katrina found it and posted it on my Facebook page. I was one of your students at UF. You were such a great teacher and made a lasting impression. I hope things are going well.

  Cassandra Brown

  ReplyDelete
 4. Wapendwa, nilikuwa nimepotea kidogo. Nimerudi tena. Asanteni kwa maoni yenu. Hili suala la lugha za hawa waheshimiwa na sisi sote pengine linaakisi kwa uwazi hata sera yetu nzima ya lugha. Kwenye Kiswahili hatuko na kwenye Kiingereza hatuko pia ali mradi vurugu tupu. Sijui ni lini mkombozi atasimama na kuamua moja kuhusu lugha tunayopaswa kuifuata. Naamini kwamba kiinimacho hiki tulichonacho siku moja kitafikia ukomo.

  Cassandra: I am happy to hear that you still remember me; and that I made a lasting impression on you. This is what teaching is all about: making last impressions and positively influencing students' lives. Where are you now? Have you taken your first flight yet? You can write to me through profesamatondo@gmail.com. Tell Katrina that I said hi!

  ReplyDelete
 5. Tulipata uhuru wa kisiasa (japo hata kwenye hilo kuna utata) lakini kwa kiwango kikubwa tumeendelea kuwa chini ya ukoloni wa kifikra na kitaaluma.Kiswahili kina nafasi nzuri kimataifa lakini kinaishia kupuuzwa kwa vile wenye lugha yao wanataka kuongea lugha za wenzao.Ukienda huko twitter,unakuta kila mswahili "anatwiti" kwa kimombo.Lakini tweets za waarab ni kwa kiarabu,za wachina kwa kichina,za warusi kwa kirusi,nk lakini akina sie ni kimombo tu.

  Na hao wanasiasa wetu vihiyo ndio tatizo kabisa.Kuongea kiinglishi mahala panapohitaji kiswahili si vema,lakini kuongea kiingilishi fyongo ni ufisadi wa kilugha.Wanasiasa wetu na vyeti vyao vya kufoji wanajitutumua kuongea kimombo ilmradi tu waonekane tofauti na wanaotutawala.

  Naamini kuna siku tutampata Kiongozi mwenye kupenda kiswahili,atapokwenda nje ya nchi ataongea kiswahili,na si ajabu akapiga marufuku matumizi ya kiingereza bungeni.Hadi kufikia hapo,tutaendelea kuwa chini ya ukoloni wa kujitakia kwenye kimombo

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU