NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, April 22, 2011

JELA MWEZI MMOJA KWA KUKOJOA OVYO !!!

 • Naona ile sheria ya usafi wa mazingira iliyopitishwa na serikali kimchezomchezo tu imeanza kuzingatiwa na mkazi mmoja wa Ubungo jijini Dar aitwaye Dismas Geogre (25) amehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kujisaida haja ndogo katika eneo lililokatazwa kisheria. Japo tabia hii ya kukojoa hovyo hovyo inakera, mimi nadhani sheria hii peke yake haitaweza kutatua tabia hii kama kiini chake hasa hakitafahamika. 
 • Ati, ni kwa nini watu wanapenda kukojoa hovyo hovyo? Ni kwa sababu ni wachafu na hawajali? Ni matokeo ya mila na utamaduni wao? Au pengine ni kutokana na ukosefu wa vyoo vya umma vilivyo safi na tayari kwa matumizi? Vyoo vingi vya umma (hata vile vya kulipia) ni vichafu kupindukia, vinanuka sana na havina maji wala karatasi za kujisafishia. Kwa nini basi mtu asijibanze kando ya mti au uchochoroni akamaliza haja yake chapu chapu na kwenda zake? Si budi basi tatizo liangaliwe katika upana wake vinginevyo magereza yatafurika wafungwa wenye makosa ya kukojoa vichochoroni kama kweli serikali imedhamiria kuitekeleza sheria hii kwa hali na mali!
~~~~~~~~~~
Afungwa jela baada ya kukiri kukojoa ovyo

Imeandikwa na Oscar Job
Tarehe: 21 Aprili 2011 

MKAZI wa Ubungo, Dismas Geogre (25) amehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kujisaida haja ndogo katika eneo lililokatazwa kisheria.

Hukumu hiyo imetolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Sokoine Drive (Jiji), William Mutaki baada ya mshitakiwa huyo kukiri kutenda kosa hilo.

Awali Mwendesha Mashitaka, James Munga alidai kuwa Aprili 17 mwaka huu mshitakiwa alikutwa akikojoa katika eneo la Ubungo Kisiwani kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa madai hayo, mshitakaiwa alikutwa na Ofisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Evarist Msigwa akikojoa katika eneo hilo ambalo si rasmi kwa shughuli hiyo na kukaidi agizo hilo lililotolewa na Manispaa hiyo.

Alisema, mshitakiawa huyo alifanya hivyo huku akitambua wazi kuwa kosa hilo ni kinyume na Sheria Ndogo ya Usafi wa Mazingira ya Manispaa ya Kinondoni iliyoanzishwa 2002.

Baada ya mshitakiwa kukiri kosa hilo, Mwendesha Mashitaka alimuomba Hakimu kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Mutaki alimuhukumu mshitakiwa huyo kulipa faini ya Sh. 50,000 au kwenda jela mwezi mmoja kutumikia kifungo na kutokana na mshitakiwa kukosa fedha hizo, alipelekwa jela kutumikia kifungo hicho.

Chanzo: Habari Leo.

4 comments:

 1. Natafakari kuanzia yaliyoandikwa kwenye picha ya kwanza !

  Nukuu``Atakaye kojoa hapa anafanana na MBWA!´´-mwisho wa nukuu

  DUH!

  ReplyDelete
 2. "Dismas George"?

  Hilo jina nimeliangalia kwa makini sana kwani ninandugu zangu kibao huko Ubungo Kisiwani. Mtoto wakwanza kwa baba yangu mdogo yuko hukohuko, ni kaka yangu, George. Na wasije wakanifungia jela watoto waKaka jamaani eti kwa haja ndogo tu?

  Ndani zaidi ya tundu: ni mjadala mkubwa sana huo, Mkuu, tena daima utavutia tu. Kwa hiyo, asante kwa kutujuza hayo mepya!

  Hata huku kwetu Pretoria, mambo ni hayohayo ya kujisaidia saidia hovyo, lakini sijawahi kusikia lipo hata kabila moja Afrika au ulimwenguni mzima lenye desturi ya kutoa HOSEPIPE za suruali mitaani na kumwagilia majani ya watu bila kuombwa!


  Na, kuhusu Dismas George, Pole Sana, Mwanangu. Nafikiri hayo umeyataka mwenyewe! Upande wangu nitayiunga serikali mkono pamoja na kutokuwepo kwa sehemu nzuri jijini kwa watu kujisaidia. Breki zako kijana wa miaka 25 zimeenda wapi mapema namna hii maishani mwako usivumilie mpaka nyumbani au mpaka kazini kwako unakokwenda? Au umekunywa pombe gani yenye kutaka kutoka haraka ikiwa huku inakupa kichwani mwako jazba kwamba ni haki yako ya kuutolea uma kidole chako cha siri hadharani?

  ReplyDelete
 3. Mwalimu,nadhani ni tatizo la kiutamaduni zaidi.Nalinganisha tabia yetu ya kukojoa popote pale "penye nafasi" na ya hawa "wazungu" kuchafua hewa popote pale.Kwao,mtu akibanwa na hamu ya (ashakum si matusi) kujamba basi haijalishi nani yupo jirani.Eti wanadai ni nzuri kiafya.Well,labda afya zao lakini sio kwa akina sie ambao (ashakum si matusi tena) ushuzi ni uchafuzi wa hewa,period!

  Lakini kwa upande wa pili,ni upatikanaji wa huduma za kujisaidia.Hivi kama mtu anabanwa na haja ndogo pale ambapo hakuna sehemu ya kujisaidia afanyeje?Athamini mazingira aishie kuchafua nguo zake,au ajinusuru lakini aharibu mazingira?Yaleyale ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na umuhimu wa kuni kwa ajili ya kupikia chakula.

  Kingine ni ustaarabu tu.Kwa mtu aliyekosa ustaarabu,hata ukimtengenezea choo cha kutembea nacho kwenye begi bado atajisaidia pasipostahili.Sijui kama sheria zitasaidia kubadili kasumba hiyo.San sana zinaweza kuwapatia mgambo ulaji mpya: anakojoa yeye kisha anakugeuzia kibao mpita njia kudai umekojoa wewe.Usipotoa rushwa,jela mwezi mmoja.

  Ijumaa Kuu njema kwako Prof na familia yako

  ReplyDelete
 4. Baba Mtakatifu: Pengine ni suala la utamaduni. Inaonekana huyu jamaa aliyeandika hili tangazo anamwona mbwa kama kiumbe wa hali ya chini kabisa. Kwa wengine, kufananishwa na mbwa yaweza kuwa ni bonge la ujiko!

  Goodman: Isije ikawa kweli Dismas George ni nduguyo. Jaribu kufuatilia uone kama ni kweli. Naona masikini hata hawezi kulipa faini ya 50,000 kwani hizi ni pesa nyingi sana kwa Mtanzania wa kawaida. Ukimlipia hiyo faini mapema anaweza kuepuka mwezi mmoja jela!

  Evarist: Nakubaliana nawe kwamba hili tatizo liangaliwe katika upana wake. Jambo moja la muhimu ambalo umelizua: ulaji kwa wanamgambo na mapolisi. Naamini kwamba sababu kubwa iliyomfanya huyu Dismas George mpaka akafungwa huu mwaka mmoja ni umasikini. Inaonekana hakuwa na pesa za kumhonga polisi au mwanamgambo aliyemkamata. Ndiyo maana hata hawezi kujilipia faini ya 50,000 na matokeo yake inabidi atumikie mwaka mmoja jela. Kama angekuwa na angalau buku tano tu ya kumpa mgambo aliyemkamata yote haya yasingemfika. Inashangaza kidogo kuona kwamba mtu anafungwa kwa kukojoa uchochoroni wakati mifisadi mikubwa inayokwapua maliasili zetu iko huru ikiendelea kutanua. Hata sheria zina makali zaidi kwa baadhi ya watu kuliko wengine ati!

  Ukali huu wa serikali ukiambatana na ujenzi wa vyoo vingi vya umma, vyoo ambavyo vitatunzwa vizuri na kuwa safi wakati wote, vinaweza kuwa hatua nzuri ya mwanzo katika kubadili tabia hii inayokera ya kukojoa hovyo hovyo.

  Asanteni nyote na maandalizi mema ya pasaka - ingawa hapa tupo tunajadili vikojozi:

  NYONGEZA: Niko tayari kumlipia Dismas George hii faini kama itamfanya atoke gerezani. Kama kuna ndugu yake wa karibu tuwasiliane.....

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU