NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, April 5, 2011

LUGHA YA KUFUNDISHIA TANZANIA: TUTAENDELEA KUJICHANGANYA MPAKA LINI ???

 • Mimi nilikuwa nafikiri kwamba mapendekezo ya sera yetu mpya ya lugha iliyotolewa mwaka 1999 yalikuwa yanalenga katika kuanza kutumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi; na kwamba maandalizi ya kiutekelezaji yalikuwa yakifanyika. Ina maana Kiswahili bado kinafikiriwa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za sekondari na elimu ya juu japo ni mpaka kitakapokidhi haja? Kipi kinaendelea hapa? 
 • Yote kwa yote, nikiwa kama mkereketwa wa mambo ya lugha na utamaduni, kauli hii ya Mh. Dr. Nchimbi imenifurahisha. Kumbe mkabala wa Kiswahili si mbaya kama wakati ule wa Mh. Mungai.
 
*****************

Nchimbi: Kiswahili kutumika kufundishia kikikidhi haja

NA HAMIS SHIMYE
Monday, 04 April 2011

SERIKALI imesema ipo tayari kuunga mkono jitihada za lugha ya Kiswahili kufundishiwa elimu ya juu, ikiwa utafiti na machapisho ya lugha hiyo yatakidhi haja. Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana, kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). 

Kilele kitakuwa Oktoba 26, mwaka huu. Dk. Nchimbi alisema dira ya TATAKI ni kuwa kitovu cha ufundishaji, utafiti, maendeleo, ubora na ubobezi katika lugha, fasihi na utamaduni wa Kiswahili.

Chanzo: Uhuru

6 comments:

 1. Unajua mkuu mimi nashindwa kuelewa, najiuliza sana `nini hasa msingi mkuu wa mtu kusoma...' Kwangu mimi nasema ni ili kujua, kuelimika ili kuweza kuyamudu maihs ayke yake `kirahisi'...sasa kama ni hivyo lugha ni nini? Ni jinsi ya kumuwezesha huyu mtu kujua nini anachokisoma(tukiangalia upande wa kusoma)
  Wachina wanasoma katika lugha yao ya kichina, Warusi, halikadhalika Wajerumani, nawataja hawa kwa uchache!
  Sasa kimbembe kwetu, watoto wanapata shida, kwani wamezaliwa katika lugha zao za asili, wajifunze kiswahili, na bado wanaambiwa hicho kiswahili sio lugha ya kusomea...hapo akitoka kwenye lugha ya asili, anapunguza kitu fulani, akitoka kwenye kiswahili kuingia Kiingereza , ndio kabisa anapunguza sehemu kubwa ya kitu fulani kichwani na hata kile `kipaji' alichojaliwa nacho kinampa `walakini'
  Mimi nimewaza tu mkuu, kuwa tujaribu kufikiri `tunatafuta elimi ya namna gani..ili elimu hiyo iwe bora, na isiwe bora elimu!

  ReplyDelete
 2. Mimi bado nitashikilia msimamo wa matumizi ya lugha moja kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. aidha Kiswahili au Kiingereza. Mfumo unaotumika kwa sasa yaani Kiswahili kwa shule za msingi na kiingereza kwa sekondari unaleta mchanganyiko na wala ufanisi wake hautaonekana kamwe. Tujifunze angalau kidogo toka kwa majirani zetu Kenya na Uganda.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Pendekeza kwa hoja nzito ni lugha ipi itumike!

   Delete
 3. Tatizo ni kwamba suala hili ambalo ni muhimu sana limegeuzwa kuwa la kisiasa.

  Ni lazima tuamue ni lugha ipi tunayoitaka. Kama bado tunataka lugha zote mbili kama ilivyo sasa inabidi tufanye mabadiliko makubwa katika mfumo mzima. Kuna tatifi na mapendekezo mengi sana ambayo yameshafanyika kuhusu suala hili na nadhani serikali inalijua hili.

  Ndiyo maana hata niliposikia kwamba serikali ilikuwa imeamua kutumia Kiingereza kuanzia shule za msingi sikuhangaishwa kwani naamini ni bora kuliko mfumo wa kimiujiza tulionao kwa sasa. Ndiyo maana nimeshangaa kumsikia tena waziri hapa akisema Kiswahili kinaweza kutumika kama kitakidhi haja. Isije ikawa bado tunacheza kisiasa tu. Bila mfumo mzuri wa lugha ya kufundishia, elimu yetu itaendelea kudidimia. Japo hili ni suala la "common sense" sijui ni kwa nini linaonekana kuwa gumu kwa wanasiasa!

  ReplyDelete
 4. Bwana Matondo wewe ni msomi tena wa kuhangaikia shahada zako. Inakuwaje unampa heshima kihiyo Nchimbi ambaye anajulikana alivyoghushi?
  Ili kuongea kwa data, hebu chungulia CV ya Nchimbi aliyotoa kwa tume ya uchaguzi ya taifa.
  Angalizo-angalia alivyoweza kufanya shahada mbili yaani Masters na PhD kutoka vyuo vikuu viwili tena kwa wakati mmoja.

  Jina: Emmanuel John Nchimbi
  Nafasi: Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo
  Tarehe ya Kuzaliwa: 24 Desemba, 1971
  Jimbo la Ubunge: Songea Mjini (2005-2010) na ametetea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu

  Nafasi nyinginea alizowahi kushika:
  Naibu Waziri: Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (2008 – 2010), Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana (2006-2008) na Habari, Utamaduni na Michezo (Januari 2006 – Oktoba 2006).
  Mkuu wa Wilaya: 2003 -2005
  Afisa Tawala, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC, 1998 – 2003)

  Elimu:
  CommonWealth Open University PhD (Management) 2001 2003 PHD
  Shahada ya uzamili katika masuala ya fedha na benki (MBA), Chuo Kikuu Mzumbe, (2001 -2003)
  Stashahada ya Juu ya Uongozi, Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe (IDM) (1994- 1997).
  Je Nchimbi ni kihiyo au jiniasi wa kawaida?

  ReplyDelete
 5. Anony - siyo wajibu wangu kupitisha hukumu kuhusu uhalali wa digrii na usomi wa watu. Nadhani kuna mamlaka inayoshughulika na jambo hili. Kwa hivyo sioni ugumu kumuita Mheshimiwa huyu Daktari. Jambo ambalo ninakereka nalo ni hili la hawa wabunge na mawaziri kutaka waitwe waheshimiwa. Hili mpaka leo sielewi mantiki yake hasa ni nini. Wamarekani walijiwahi mapema na kuweka mwongozo wa kutaka rais wao aitwe Mr President tu basi. Nyerere alitaka aitwe Mwalimu ...lakini wakaja hawa vijana wake wakataka waitwe waheshimiwa. Hata sijui ni kwa nini!

  Kusoma digrii mbili kwa mpigo siyo jambo la ajabu hasa ukizingatia kwamba digrii mojawapo ni ya Open University ambayo pengine ilimpunguzia Mheshimiwa ule ulazima wa kuwa sehemu mbili kwa wakati mmoja - jambo ambalo haliwezekani. Na kama mtu ni jiniazi kufanya digrii mbili - hata tatu si jambo la kushangaza hasa kama digrii hizo zinafananafanana au kuhusianahusiana.

  Pamoja na haya, kuna watu ambao wanakitilia shaka hicho Chuo Kikuu cha Commonwealth kwani kimeorodheshwa katika orodha ya vyuo ambavyo havina sifa na kinasemekana kuwa ni mojawapo ya hivi vyuo wenyewe wanaviita "diploma mills" (http://en.wikipedia.org/wiki/Diploma_mills).

  Kwa vile hizi ni tetesi tu na hazijathibitishwa basi tuacheni haya mambo ya ki-ad hominem na badala yake tumakinikie utendakazi na mchango wake kwa jamii.

  http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/41483-mawaziri-wenye-phd-feki-hawa-hapa.html

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU