NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, April 7, 2011

NYUMBANI BARIADI KUNA NJAA MWAKA HUU !!!

Mvua mwaka huu hazijanyesha kabisa Wilayani Bariadi; na kwa vile kilimo chetu bado ni cha kutegemea maji ya mvua, matokeo yake ndiyo haya: njaa! Hata hivyo wilaya hii ina bahati ya kuwa na wabunge machachari na wenye uwezo mkubwa wa kifedha na kiushawishi (Mzee wa Vijisenti na Bwana Mapesa). Natumaini kwamba wabunge hawa watashirikiana vyema na serikali pamoja na wananchi ili kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi wa Bariadi anayekufa kwa njaa. Naamini kuna maeneo mengine nchini ambayo yana tatizo hili lakini hatuyasikii kwa sababu kwa kawaida vyombo vyetu vya habari havina tabia ya kuripoti mambo ya vijijini (isipokuwa kama ni habari za kusisimua kama mauaji na ajali za kutisha). Kwa sasa hali ni mbaya zaidi kwani juhudi zote zimeelekezwa Loliondo. 
*********************

Wananchi Bariadi Walia Njaa

Jumatatu, 04 Aprili 2011
Zulfa Mfinanga,  Bariadi

SERIKALI imeombwa kuwapelekea chakula wananchi wa Kata ya Kinangw’eli, Gilya na Mwaumatondo wilayani Bariadi mkoani Shinyanga ili kuwanusuru wananchi hao kupoteza maisha kwa kukosa chakula kutokana na mazao yao kukauka kwa  jua.

Ombi hilo lilitolewa juzi kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hizo kwa nyakati tofauti kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga  ambaye yuko katika ziara ya wiki moja ya kutembelea kata za wilaya hiyo kujionea hali ya chakula sanjari na kukagua vocha za kilimo zilizotolewa na serikali kama zimewafikia walengwa.

Kilio hicho cha wananchi kilifuatia siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza kusambazwa kwa chakula cha msaada katika kukabiliana na tatizo la njaa maeneo mbalimbali hapa nchini.

Baadhi ya wananchi hao, Paul Jilumbi na Pambalu Lufungulo wote wakazi wa Kijiji cha Kinang'weli, walisema kuwa ni vema serikali ikapeleka chakula cha msaada chenye bei nafuu ili wananchi wenye uwezo wanunuwe kabla hawajamaliza kuuza mifugo na akiba ya pesa walizoweka na hivyo chakula kuishia kwa baadhi ya watu wasio na uwezo kabisa.

“Kilio chetu kikubwa wananchi wa kata hizi hatuna chakula, mazao yetu yamekauka na jua, tunaiomba msikie kilio chetu, tupatiwe mapema chakula cha msaada la sivyo njaa itatuua”, walisema.

Naye mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga alisema kuwa tayari tathimini imeshafanyika ili kujua hali halisi ya upungufu wa chakula katika wilaya hiyo na kupeleka takwimu hizo Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kwa ajili ya kusaidia  maeneo yaliyokumbwa na njaa kali.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU